Showing posts with label MAKALA. Show all posts
Showing posts with label MAKALA. Show all posts

Thursday, May 29, 2014

Ni sisi wenyewe wa kujitosa au kujikomboa

 
KATIKA mfululizo huu nilieleza kiundani jinsi ambavyo siasa ya ndani ya nchi yo yote ni lazima itajionyesha katika diplomasia yake.
Siasa iliyopangiliwa vyema itazaa diplomasia iliyopangwa vyema. Misingi ya maisha ya nyumbani itajionyesha pia katika maisha yetu nje.
Imekuwa ni rai yangu kwamba diplomasia yetu imekwenda mrama. Sisemi kwamba tawala zilizoiendesha nchi yetu tangu kuondoka serikalini kwa Julius Nyerere ndizo pekee zilizopotosha diplomasia yetu. Kwa uhakika nimeandika katika makala zilizopita jinsi chini ya uongozi wake, Mwalimu aliruhusu, baadhi ya nyakati, mambo ya kipuuzi yakafanyika.
Mfano mmoja ni ule uliohusiana na Angola na jinsi Tanzania ilivyoyumba vibaya tukikaribia tarehe 11 Novemba 1975.
Ninachosema ni kwamba katika mazingira yale ya mwaka huo tunaweza kusema kwamba Mwalimu aliteleza, au aliruhusu washauri wake wamfanye ateleze, ama kwa sababu waliweza kumdanganya, ama kwa sababu yeye mwenyewe alikuwa na mitazamo iliyokuwa rahisi kumfanya akubali kuyumbishwa.
Hivi sasa tunachokishuhudia ni kwamba diplomasia yetu inakwenda hovyo, na haina mwelekeo. Nimesema katika makala zilizopita kwamba hali hii imekuwa ikiendelea, chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi, na baadaye Rais Benjamin Mkapa, halafu akafuatia Rais Jakaya Kikwete.
Wote hawa wamekuwa wakiendesha diplomasia ya hovyo kwa sababu hawakuelekea kuelewa wanatakiwa wafanye nini kwa maslahi ya Watanzania. Na msingi wa hayo ni kwamba siasa za ndani zilikwisha kuvurugwa, na leo hii bado zinaendelea kuvurugwa.
Kama nilivyosema mara kadhaa, siasa ya ndani ikiisha kuvurugwa ni lazima na siasa ya nje, yaani diplomasia, itavurugwa. Kama kuna mikanganyiko ndani ya nchi, na nje ya nchi mikanganyikao itajitokeza tu. Nitoe mifano michache.
Nchi kama Central African Republic (CAR) imekuwa katika vurugu za ndani kwa zaidi ya mwaka sasa. Raia wake wanashambuliana kwa mishingi ya itikadi za kidini, na sasa hivi ndiyo nchi inayojulikana kama nchi ya dola iliyokufa.
Ni nani anaweza kutarajia kwamba nchi kama hiyo inaweza kuwa na diplomasia inayoeleweka? Misingi ya diplomasia hiyo itakuwa ni ipi? Ni mambo gani itakayoyaunga mkono, na yapi itakayoyapinga, na kwa msingi upi?
Zipo nchi nyingi barani Afrika zinazofanana na hii, nazo zina mikanganyiko kama hiyo, ama tofauti na hiyo, lakini muhimu ni kukumbuka kwamba kwenye mikanganyiko ya nyumbani kutazaliwa mikanganyiko ya nje.
Mikanganyiko ya ndani hutokea kimsingi kwa sababu watawala wameshindwa kuwa viongozi na kuonyesha njia. Watawala hushindwa kwa sababu mbalimbali. Mojawapo ni kwamba wengi wao  si viongozi, na wala hawajawahi kuwa viongozi wa wananchi wao, au wa kitu cho chote.
Ni watu walioingia madarakani kwa sababu waliona kwamba ni nafasi ya kujineemesha, wao na familia zao, na wala hawakuwa na dhamira ya kufanya lo lote kuinua maisha ya wananchi wao, au kuwalinda dhidi ya hatari zinazowakabili.
Hili si tatizo la Tanzania pekee. Afrika nzima imejaa watu kama hawa. Wanakumbukwa kwamba walipitapita katika maeneo ya nchi zao wakiahidi hili na lile. Wakati mwingine ahadi hazikuwa na sababu yo yote; wangeweza wakajikalia kimya juu ya ahadi (wasiahidi lo lote) na bado wakapata kura walizozitaka.
Tatizo wakati mwingine ni kwamba wanasiasa uchwara  huamini kwamba mchezo wa siasa maana yake ni kutoa ahadi ambazo unajua tangu awali kwamba hazitekelezeki. Kwa maneno mengine, kuna imani iliyojengeka kwamba siasa ni kusema uongo.
Katika ngwe hii inayoanza wiki hii ninayo nia ya kurejea masuala makuu ya siasa zetu na uchumi wetu, na jinsi ambavyo tumekuwa tukienenda katika nyanja hizi. Kusema kweli, napenda kuchunguza ni jinsi gani tunajenga mahusiano baina ya maeneo na sehemu mbalimbali katika nchi yetu kwa njia ambazo zinahatarisha uhai na usalama wa Taifa letu.
Ili kuyajadili masuala haya, bila shaka itanilazimu kuangalia kwa undani iwapo bado tunaendelea na juhudi za kujenga utaifa au tunababaisha ujengaji wa miundombinu ya unyonyaji ambayo umuhimu wake wa kweli ni kwa waporaji wa nje na wasaidizi wao wa ndani katika uporaji wa rasilimali za nchi na watu wake.   
Haitawezekana kujadili masuala haya bila kuzungumzia kashafa tuliyoishuhudia katika kile kilichoitwa mchakato wa kuandika katiba mpya kwa ajili ya nchi yetu. Kashfa ambayo imewaacha watu wengi wakijiuliza iwapo kile tulichokishuhudia ndiyo hali halisi ya nchi yetu, na iwapo uozo uliotugubika umefikia viwango vya kutisha kama vile tulivyovishuhudia kwenye televisheni na kwenye redio.
Nia yangu ni kuibua mjadala mpana wa hali juu ya hali ya nchi yetu, na kuufanya mjadala huo kuwa wa kudumu. Hatuwezi kujiwekea ukomo wa kufikiri na kusemezana kuhusu nchi yetu na kisha tukataraji kwamba tutakuwa salama.
Najua kwamba hali yetu ya sasa, na hasa tukiangalia kile tulichokiona na kukisikia wakati wa mijadala ya Dodoma, inatoa taswira ya watu waliodidimia katika upuuzi na ujinga kiasi kwamba labda waletewe mwokozi kutoka kwa Mwenyezi Mungu ndipo wataweza kupona. Mimi siamini hivyo.
Naamini kwamba ukombozi wetu u mikononi mwetu, na kwamba jinsi ambavyo tutafanya kazi kwa weledi ndivyo tutakavyopata ahueni katika maswahibu tunayoelekea kukumbana nayo leo.
Kinyume chake, jinsi ambavyo tutaendeleza upuuzi na ujinga, kama tunavyofanya leo, ndivyo tutakavyozidi kudidimia katika lindi la upuuzi na ujinga, hatima yetu ikiwa ni kuwa kama nchi hizo ambazo nimekuwa nikizijadili.
Najua kwamba tumezoea kujisalimisha au kujipatia manufaa kwa kutoa rushwa ili tuepukane na majukumu yetu, ama tuchaguliwe, ama tupate tenda bila kuistahili, na kadhalika. Bahati mbaya kwa watoa na wapokea rushwa, rushwa ya kumuhonga Mwenyezi Mungu ili atuepushe na athari za upuuzi wetu, bado haijajulikana ni mapesa kiasi gani.
  src
Raia mwema
Rai ya Jenerali

Tuesday, May 27, 2014

TASNIA YA UTANGAZAJI SASA IMEINGILIWA!


KWENU,
Watangazaji wa kike Bongo. Poleni na kazi za kila siku na hongereni kwa namna mnavyojituma kuhakikisha gurudumu linasonga mbele.
Nimeona leo ni vyema niwakumbuke kwa barua yenye lengo la kukumbushana kuhusu weledi wa kazi yenu ya utangazaji. Nianze kwa kusema kwamba, kiukweli baadhi yenu ni kama mmevamia fani!
Heshima ya utangazaji iliyokuwepo zamani imeanza kupotea! Kuna watangazaji wanatia kinyaa. Yaani wamegeuza runinga kama mahali pa matangazo.
Mavazi ya baadhi yenu si ya staha. Nimekuwa nikitazama vipindi mbalimbali vinavyoendeshwa na wanawake, mavazi ni ya hovyo.
Kwanza yanaacha sehemu kubwa ya miili nje, lakini mbaya zaidi kuna wengine bila haya, kwenye taarifa za habari, utakuta ameacha sehemu kubwa ya matiti nje, uso ameupara kupitiliza! Ya nini yote hayo?
Kinachotakiwa ni mtangazaji kuonekana nadhifu na asome vizuri habari. Sasa hayo mambo ya kuanika matiti nje ni kwa faida ya nani?
Wanaokera zaidi ni wale ambao wanajifanya wamevaa kiheshima lakini kifuani wanapandisha matiti juu na kuyaminya ili yaonekane! Sijui ndiyo staili mpya?
Hata kama ni staili, kwenye runinga si mahali pake. Fanya hivyo nje ya runinga, siyo sehemu ambayo inafuatiliwa na watu wengi. Kwa nini usijiheshimu?
Ukiachana na habari kuna vipindi vinavyoongozwa na wanawake, baadhi yao hawana maadili, achilia mbali mavazi wanayovaa lakini hata maneno wanayotumia si ya kistaarabu.
Mnatakiwa kufahamu kuwa runinga ni chombo cha habari, ambacho kinapaswa kuheshimiwa. Watu wanaokuwa wamekaa nyuma ya runinga wanategemea kupata kitu sahihi kutoka kwenu.
Si kujianika! Hapo si mahali pa kujianika. Inafikia mahali mpaka mtu unaweza kujiuliza; hao wenye tabia hizo, wanakuwa wanatafuta nini  zaidi ya kutoa taarifa kwa jamii?
Maana isije kuwa mna yenu. Manenomaneno mengi sana kuhusu wasanii wa sanaa mbalimbali nchini. Wanaonekana kama wahuni kutokana na mavazi yao. Vipi kuhusu ninyi?
Mnatakiwa kujitambua na kuthamini utu wenu, mfahamu kuwa mmepewa dhamana kubwa ya kubeba vyombo vya habari. Ukiwa mbele ya kamera, maana yake ujue wewe ni chombo cha habari.
Lindeni maadili ya Kitanzania, msivunje miiko  ya utangazaji habari. Viongozi wa vituo mko wapi? Wekeni sheria zinazolinda maadili.
Nasisitiza, siyo wote ila wapo ambao wameingilia fani wakiwa na malengo yao vichwani mwao! Wapo wenye staha na wanaojitambua. Mfano mzuri ni Rehema Salum, Fatma Almasi Nyangasa, Grace Kingalame na wengine wengi wanaojitambua.
Wenye tabia hizo hebu jiangalieni upya.
Yuleyule,
Mkweli daima,
Joseph Shaluwa

Tuesday, May 13, 2014

UKIZINGATIA VIDOKEZO HIVI NA UKAVIFANYIA KAZI MAFANIKIO KATIKA MAISHA KWAKO SIYO NDOTO TENA


Mwenyekiti Mtendaji Wa Makampuni Ya IPP Media Ltd,  Dk. Reginald Mengi
KILA mara nimekuwa nikiwaeleza watu wangu wa karibu kuwa maisha yako ya baadaye yanaanza na kile unachokifanya leo. Kama wewe unatamani maisha ya kitajiri, basi msingi wake unakutegemea jinsi utakavyoanza kuujenga hivi sasa.
Wapo baadhi ya watu wana ndoto za maisha mazuri na ya kitajiri kwa kutegemea yaje kama wanavyoota. Wengine utawasikia ipo siku watakutana na wanawake au wanaume wenye fedha, ambao watawapa maisha wanayohitaji kirahisi.
Kuishi kwa matumaini hayo ni kupoteza muda, lakini amini nikuambiayo, unaweza kuishi maisha unayoyataka kama utaanza kujiandaa kuanzia hivi sasa, kwani hata umaskini walionao wananchi wengi, ni wa kujitakia, ingawa baadhi yao, miundombinu duni ya nchi yetu imechangia.
Hapa chini, nimekuwekea baadhi ya vidokezo kadhaa, ambavyo kama utavizingatia, vinaweza kukusaidia kukupatia maisha yenye mafanikio na hivyo kutimiza ndoto zako za muda mrefu.

Kinachobakia katika matumizi yako ni mtaji
Watu wengi wamekuwa hawajui kuwa kila senti inayobaki baada ya matumizi yako basi ni mtaji mkubwa wa kukusaidia kufikia malengo. Staili ya maisha ya wengi yanawafanya wajiandae kuwa maskini au watu wa daraja la kati badala ya utajiri.
Kuna watu wana maisha mazuri kiasi kwamba wanajimudu kutengeneza bajeti zao za vyakula na matumizi muhimu kwa mwezi mzima kwa fedha za mishahara yao au biashara wanazofanya.
Baada ya bajeti ya vitu muhimu kukamilika na kutekelezwa, kinachobakia huwa ni matumizi mengineyo kwa fedha zote zilizobakia kwenye mishahara yao.
Wapo pia ambao akiba yao huitunza benki au hununulia vitu vya bei kubwa kama vitanda, makabati, televisheni, magari na kadhalika.
Katika hesabu za kuelekea kwenye mafanikio, unahimizwa kutopenda sana kuweka hela ‘iliyokufa’. Hela hii ni ile unayohifadhi benki au kununulia vitu ambavyo haviwezi kukupa faida.
Watu wa uchumi na wajasiriamali waliofanikiwa, wanakushauri kuwa akiba unayopata kuwekeza katika kupata vyanzo vipya vya mapato yako.

Mipango yako ya matumizi ni dhahabu
Wote tunajua kwamba dhahabu ni jiwe lenye thamani ambalo kila mmoja angetamani kulipata, hasa likiwa ni kubwa. Mipango yetu ya matumizi ni sawa na madini haya yenye thamani. Ukitaka kujua uimara wa mtu kifedha, angalia jinsi mipango yake ya matumizi ilivyo.
Chukulia mipango ya watu wawili tofauti ifuatayo
Mtu wa kwanza: Anachangia kwa wasiojiweza. Anajiwekea akiba. Ananunua vitabu vya uwekezaji. Semina ya mashamba. Muda wa mazoezi.
Mtu wa pili: Bia sita kila siku.
Ananunua viatu vipya.
Nunua TV mpya. Tiketi za soka. Bia zingine sita.
Mfano huu mdogo unakuonyesha aina mbili tofauti kabisa ya watu. Mmoja hafikirii kabisa kuhusu kesho yake. Unachogundua ni kwamba wakati mmoja anawekeza na kujiandalia kuhusu kesho, fedha za mwingine zinaonyesha zinatoka tu mfukoni zikiwa hazina mrejesho.
Ili kujua kama unaandaa kesho yako iliyo nzuri, angalia mipango yako ya matumizi ya fedha, ndipo utakapojua jinsi unavyoipa thamani dhahabu uliyoishika au unavyoifuja bila wewe mwenyewe kujua.
Tumia ulichonacho kwa ukomo
Kila siku, watu wanaotafuta mafanikio katika maisha yao hawaishi na wala hawaridhiki na walipo. Wanaamini katika kuwekeza, kwa kuwa kutawawezesha kutimiza kila ndoto waliyonayo.
Lakini lipo tatizo la baadhi ya watu kuanza kuridhika na mafanikio madogo yanayojitokeza mbele yao. Badala ya kuendelea kuwekeza, tena na tena, wao huanza kutapanya mali zao kana kwamba wanazo nyingi kiasi hazitakwisha.
Huku ni kujidanganya. Mtu anayesaka mafanikio, hata kama atatamani kununua kitu kizuri, hatauza mali aliyonayo ili anunue, bali atatafuta mbinu zaidi za kufanya ili apate anachokitaka.
Atatafuta vyanzo zaidi vya mapato ambavyo kwa vyovyote, vitaongeza kiasi cha fedha anachoingiza kila mwezi na kwa maana hiyo, baada ya muda atajikuta amepata kile alichokitaka bila kupoteza mali yoyote aliyokuwa nayo kabla. Hivyo ndivyo walivyofanya akina mzee Reginald Mengi, Rostam Azizi, mzee Saidi Bakhresa na wengine wengi waliotajirika


src
bongoswaggz

Monday, May 12, 2014

WABUNGE, NINI FAIDA YA RIPOTI YA MKAGUZI MKUU KAMA HAMFANYII KAZI?


Nianze kwa kumuomba Mungu atuzidishie amani katika nchi yetu huku akitupa afya njema ili tuweze kumtukuza na kumsifu daima kwa wema wake kwetu.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Bw. Ludovick Utouh.
Baada ya kusema hayo niingie katika mada ya leo ambapo nitazungumzia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka wa fedha wa 2012/13 iliyofichua madudu ya ajabu, ambayo bila shaka yatakuwa yameondoa matumaini ya wananchi ya kukua kwa uchumi na kuwaondolea umaskini uliokithiri.
Ni kawaida kila mwaka ripoti za CAG ya ukaguzi wa fedha za umma huwa zinafichua mambo mazito ya ubadhirifu wa pesa za serikali lakini hakuna hatua zinazochukuliwa ili iwe fundisho kwa watu wanaotafuna fedha hizo kama mchwa.
Lakini ni jambo la kusikitisha kwamba ripoti iliyotolewa ufafanuzi na CAG mwenyewe, Ludovick Utouh  wiki iliyoopita mjini Dodoma imeonyesha dhahiri kwamba serikali haijawa na dhamira ya kweli ya kudhibiti matumizi haya mabaya ya fedha za umma na kupambana na vitendo vya ufisadi na ubadhirifu wa mali za nchi.
Tunajua kuwa lipo Bunge na mifumo mingine kadhaa ya umma ya kuhakikisha kwamba serikali inakuwa na nidhamu katika kusimamia mapato na kudhibiti matumizi yake, bado hakuna mabadiliko wala dalili za uwajibikaji katika matumizi ya fedha hizo za umma nchini.
Ripoti ya CAG inaonyesha kwamba matumizi hayo mabaya yanaendelea kufanywa na maofisa wa serikali pamoja na hali mbaya ya uchumi inayolikabili taifa. Kwa mwenendo huo, inaonekana hakuna uwezekano wa kupunguza Deni la Taifa ambalo tumeambiwa limefikia shilingi trilioni 21.20, ambalo ni ongezeko la shilingi trilioni 4.23 sawa na asilimia 25, ikilinganishwa na shilingi trilioni 16.98  katika mwaka wa fedha wa 2011/12.
Ndani ya serikali umekuwamo utamaduni wa ufujaji wa fedha za serikali  ambao umechangia kupanda kwa deni la ndani kutoka shilingi trilioni 4.55  mwaka 2011/2012 hadi shilingi trilioni 5.78 mwaka wa 2012/13, likiwa ni ongezeko la shilingi trilioni 1.23, sawa na asilimia 27.
Haya ni mambo mazito ambayo mwananchi wa kawaida ni vigumu kwake kuyajua lakini wabunge ambao ndiyo wasimamizi wa serikali, watakuwa ni waajabu sana kama watakaa kimya wakati ubadhirifu huu unafanywa na wenzetu wachache tuliowapa dhamana ya kutuhudumia.
Mwenendo huo ni hatari kwa uchumi na maendeleo ya taifa letu. Baya zaidi ni pale serikali inapoendekeza mikopo kutoka katika benki za biashara nje ya nchi.
Ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), inasema kwamba serikali imekuwa ikikopa wastani wa shilingi bilioni 360 kwa mwezi kutoka nje. Kutokana na hali hiyo, Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia (WB), vimeonya dhidi ya mwenendo huo kwamba utahatarisha uchumi wa nchi.
Miradi mingi ya maendeleo imekuwa ikikwama kutokana na fedha zake kuingizwa katika michepuko isiyofaa, mbali na wizi na ubadhirifu wa baadhi ya wanasiasa, watendaji wa serikali na taasisi zake.
Ripoti ya CAG imebaini ufisadi mkubwa katika maeneo mengi ya mapato na matumizi ya fedha za serikali.
Kwa mfano, magari mapya 11 yenye thamani ya mamilioni ya shilingi yalinunuliwa lakini anasema yaliishia katika miliki za watu binafsi. Mdhibiti wa fedha za serikali anasema hayo lakini Bunge linakaa kimya, sasa kuna faida gani mzee Ludovick na timu yake kuwafanyisha kazi isiyozaa matunda?
Katika ripoti yake anasema mamilioni ya shilingi yalitumika kulipia mishahara kwa watumishi hewa, hili nalo kweli linafumbiwa macho au mpaka amri itoke kwa rais wa nchi?
Kama hilo halitoshi tukaambiwa kuwa kuna misamaha ya kodi ambayo imefanya taifa likose mapato ya shilingi trilioni 1.52!
Hizi ni fedha nyingi sana. Wabunge mnakaa kimya bila kujua kuwa fedha hizo zingeweza kujenga shule za sekondari za kisasa zaidi ya 300 nchini, nini faida ya ukaguzi wa CAG?.
Nilitegemea baada ya ripoti ya CAG wabunge wangeungana kutaka waliofanya ubadhirifu huo wa fedha za umma kuwajibishwa lakini ajabu sijasikia ukemeaji wowote. Wananchi siyo vipofu, wanaona kinachofanyika.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.


src
GPL

Thursday, May 8, 2014

UTAISHI KWA KUUNGAUNGA, KUPIGA MIZINGA HADI LINI?


MPENZI msomaji, leo nimedhamiria kuwazungumzia watu ambao Mungu amewapa afya njema na nguvu za kutosha lakini bila kuona aibu, wanaishi maisha ya kuungaunga kwa kupiga mizinga ikiwa ndiyo utaratibu wao wa kila siku.
Ukweli ni kwamba kuna umuhimu mkubwa wa wale waliofanikiwa katika maisha kuwakumbuka na kuwasaidia wasiojiweza lakini kwa wale wazima, wenye afya na nguvu za kutosha hawastahili kusaidiwa bali wanatakiwa kutumia vile walivyojaaliwa na Mungu kuhakikisha wanaendesha maisha yao bila kuwa tegemezi.
Wengi wa waliobahatika kuwa na mafanikio walichagua mafanikio, waliuchukia sana umaskini kiasi cha kulazimika kupambana vilivyo ili kuhakikisha wanaondokana na maisha duni na ya utegemezi.
Hiyo inaonesha kwamba kila mtu kama atachagua mafanikio na kuchukia maisha ya utegemezi anayo nafasi ya kubadili maisha yake na kuondokana na maisha duni.
Hata maandiko matakatifu yanaeleza kwamba miongoni mwa yale yanayomchukiza Mungu ni pamoja na kitendo cha mtu ambaye ana uwezo wa kutafuta na akapata kwa kufanya kazi na kujikimu mahitaji yake lakini kabweteka na kutegemea msaada kutoka kwa wengine.
Wapo watu huko mtaani ambao eti kwa sababu mmoja kati ya ndugu zao ana uwezo kifedha basi hawataki kabisa kujishughulisha huku wakiweka akilini kwamba ‘flani yupo, atanisaidia.’
Ni sawa, mtu yeyote kama anao uwezo ana haki ya kusaidia ndugu zake pale inapobidi lakini si vibaya kwanza wewe ukajiuliza, umejisaidiaje kwa nguvu na akili ulizopewa na Mungu na umeshindwa wapi?
Usikae tu ukabweteka na kutegemea fulani atakusaidia, fahamu na huyo fulani ana majukumu yake.
Si kwamba kwa sababu ana uwezo basi kila siku atakuwa akiangalia nani ana tatizo amsaidie, kuna kipindi atakuwa hana uwezo wa kukusaidia, je utaishije kama wewe mwenyewe hujajiwekea msingi imara wa maisha yako?
Waliobahatika kuwa katika nafasi nzuri kimaisha ni mashahidi wa usumbufu wanaoupata kutoka kwa watu wa karibu yao ambao hawataki kujituma kufanya chochote katika maisha yao.
Wao wanategemea tu kusaidiwa licha ya kwamba wakiamua kujituma kwa bidii wanaweza kuondokana na hali duni waliyo nayo.
Tusijaribu kuutengeneza ugumu kwenye maisha. Kwani hao ambao maisha yao ni mazuri wana akili ya aina gani? Je, wao wana vichwa viwili na mikono minne? Hapana! Naamini ni watu wa kawaida tu kama mimi na wewe.
Kikubwa ambacho kimewafanya waishi maisha hayo ni kuuchukia umaskini.
Anza leo kuchukia maisha ya kupiga mizinga watu, ona aibu! Pambana kutafuta maisha yako na hata pale utakapokuwa umekwama, watu watakusaidia. Unatakiwa uanze kujisaidia mwenyewe kabla hujafikia hatua ya kusaidiwa.
Kwa kumalizia nishauri tu kwamba, ukitaka kufanikiwa katika maisha chukulia mafanikio ya wengine kama changamoto kwako. Unapoona mwenzako kafanikiwa, kaa chini na uumize kichwa. Jiulize kama wengine wanakula bata kwa nini wewe uishi maisha ya kuungaunga?
Wapo wanaosema wamejaribu lakini wameshindwa, sawa lakini kumbuka hakuna kushindwa wala kukata tamaa katika kutafuta maisha mazuri. Hivyo kuwa tayari kupambana mpaka siku unaingia kaburini.

Friday, May 2, 2014

Tuache ukasuku wa Serikali mbili au tatu

 
  • Tunaweza tukawa na serikali nyingi, nchi moja
SASA ni dhahiri kwamba mchakato wa Katiba Mpya umekwama ndani ya Bunge Maalumu la Katiba. Na hakuna dalili kwamba tuna uwezo wa kutoka katika huu mkwamo.
Ni dhahiri pia kwamba waliokwamisha mchakato huu ni wabunge wa Bunge Maalumu la Katiba. Nina shaka vile vile kwamba Bunge hili, kwa muundo wake, lina uwezo wa kujitoa katika mkwamo huu.
Kwa maoni yangu Bunge hili limekwama kwa sababu kubwa mbili. Mosi, ni ukweli kwamba viongozi wetu wengi tulio nao, na ambao ndio wamejaa bungeni, ni zao la kuzuka.
Kwa namna walivyokuwa wanachangia hoja bungeni ni wazi kwamba hawa ni viongozi ambao hawakuwahi kujiandaa wala kuandaliwa kuwa viongozi.
Wamezuka tu na kujikuta wamo katika nafasi walizonazo. Hawa si watu waliowahi kupitia katika utamaduni wa mijadala angalau walipokuwa shule.
Hawana uzoefu wowote wa kupambana na hoja kinzani. Ni wazi pia kwamba wengi wa wabunge wetu ama hawaelewi au hawajaukubali utamaduni wa mfumo wa vyama vingi.
Pili, Bunge hili limekwama kwa sababu ya kujaza wanasiasa na ambao wamekaririshwa misimamo ya vyama vyao.
Ni mwendelezo ule ule wa siku zote wa kudhani kwamba katika nchi hii watu pekee wenye akili ni wanasiasa, kwa hivyo ni lazima washirikishwe katika kila jambo.
Jambo hili liliwahi kuonywa mapema na wataalamu wa kuandika Katiba. Walionya kwamba ni vizuri wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wasiwe wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kwa sababu wangehamishia utamaduni wao wa kusimamia misimamo ya vyama vyama vyao ndani ya Bunge Maalumu. Wakubwa hawakusikiliza na sasa tunavuna aibu.
Sambamba na hili, ni wazi kwamba tulifanya makosa makubwa kuruhusu jambo zito kama la Muungano liwe jambo la kisera kwa vyama vya siasa.
Matokeo yake sasa kila chama kimeibuka na msimamo wake wa kisera na wabunge wa kila upande wamekaririshwa misimamo ya vyama vyao. CCM wamekariri Serikali mbili, na wapinzani nao wamekariri Serikali tatu.
Wote wameng’ang’ania walipo. Hawasogei. Pamoja na kwamba wapinzani wanajifanya kuunga mkono maoni ya wananchi kama yalivyopendekezwa na tume, ukweli ni kwamba imekuwa bahati tu kwamba tume imekuja na maoni yanayoendana na misimamo yao.
Laiti Tume ingekuja na mapendekezo ya Serikali mbili, kwa mfano, wapinzani wangekuwa kama CCM katika kuwaporomoshea wajumbe kashfa
. Tukumbuke wapinzani waliwahi kusema kwamba Tume hii ilikuwa haina weledi wowote na baadhi yao wakataka wajumbe wake wajitoe katika tume hiyo.
Bahati nzuri akina Profesa Mwesiga Baregu wakaweka msimamo, wakaamua kuchagua nchi badala ya chama.
Ni kwamba wanasiasa wetu, wa pande zote, hawana utamaduni wa kuheshimu taaluma na wao hudhani kwamba wana akili kuliko watu wengine wasio wanasiasa. 
Sasa ni lazima tukubaliane kama nchi mambo fulani fulani yanayoashiria uhai wa nchi yasiruhusiwe kuwa sehemu ya sera za vyama vya siasa.
Haya ni lazima tuyawekee wigo kwamba ni mambo ambayo tunakubaliana kama taifa na hakuna chama cha siasa kitakachoruhusiwa kutungia sera.
Kwa maoni yangu jambo la Muungano ni moja ya mambo hayo kwa sababu linahusu uhai wa nchi na hatupaswi kuruhusu mwanasiasa yeyote akafanyia propaganda jambo nyeti linalohusu uhai wa taifa. 
Wanaofahamu maana ya mijadala ni kwamba inabidi unapoingia katika mjadala wowote uwe huru katika kufikiri ili uweze kufungua milango ya usikivu.
Tatizo la kuingia kwenye mijadala ukiwa na msimamo wa kichama ni kwamba unakuwa umeziba ufahamu wa kutambua mantiki ya hoja kinzani na unabaki kuimba kama kasuku msimamo ambao unakuwa umekaririshwa na chama chako.
Na hiki ndicho kilichotokea ndani ya Bunge letu Maalumu. Wajumbe wa pande zote mbili za CCM na upinzani wamekaririshwa misimamo ya vyama vyao na wanaiimba kama kasuku.
Na pale hoja zao za kukaririshwa zinapoelekea kuzidiwa wanahamia kwenye kuporomosha matusi na kutoa vitisho visivyo na kichwa wala miguu, kama wale waliotishia kwenda msituni na wale waliotishia kwamba jeshi lingeingilia kati.
Hawa ni watu ambao wana dhamana kubwa lakini inaelekea hawajui wala kuthamini maana na ukubwa wa dhamana walizo nazo.
Wanaongea kama vijana wanavyopiga ‘stori’ kwenye vijiwe vya pombe za kienyeji na bado wanataka waendelee kuheshimiwa kwamba ni viongozi.
Kwa mwenendo huu ni wazi kwamba tumekwama mno kama taifa na tumekwamishwa na watu tuliowakabidhi dhamana kubwa ya kiungozi.
Sasa, kwa maoni yangu, ili tutoke hapa tunahitaji kufanya mambo mawili makubwa na magumu. Jambo la kwanza ni kwamba ni lazima tukubali kutoka nje ya sanduku ili tuweze kufikiri zaidi ya serikali mbili au tatu kwa maana kwamba tuna uwezo wa kuunda serikali zaidi ya hizi zilizopendekezwa na Rasimu ya Tume na ile Rasimu ya CCM iliyopo mafichoni.
Kwa mfano tungeweza kuiboresha Rasimu ya Tume. Badala ya kuwa na Serikali tatu kama zilivyopendekezwa, tungeamua kuwa na Serikali ya Zanzibar kama ilivyo leo na tukaunda Serikali ya Tanganyika yenye Waziri Mkuu na yenye kufuata mfumo wa kibunge.
Kwa hiyo tunapoenda kwenye uchaguzi tunachagua wabunge tu na chama kinachoshinda uchaguzi ndicho kinachotoa waziri mkuu ambaye atateuliwa na Rais wa Jamhuri.
Waziri Mkuu angeshughulikia mambo ya kawaida ya maendeleo kama vile elimu ya msingi, maji, barabara za halmashauri, kilimo, ufugaji na mengine kama hayo, wakati mambo mazito kama ardhi, elimu ya juu, kodi yakibaki kuwa shughuli za Muungano.
Kwa kufanya hivi tutakuwa tumedhibiti uwezekano wa ubabe ambao ungetokana na ukubwa wa Tanganyika.
Tungeweza kuamua vilevile kuendelea kuwa na serikali ya Zanzibar kama ilivyo lakini kwa upande wa Tanganyika tungeweza kuunda serikali kadhaa kwa mtindo wa kanda au majimbo kama ilivyo Afrika Kusini.
Serikali hizi nazo zitakuwa na mamlaka kamili katika mambo kadhaa lakini chini kidogo ya mamlaka iliyo nayo Serikali ya Zanzibar.
Hizi serikali zingeongozwa na mawaziri wakuu ambao wangeteuliwa na Rais ambaye ndiyo mkuu wa nchi na mkuu wa Serikali ya Jamhuri.
Ndio kusema tunaweza tukawa na majimbo au kanda kati ya tano hadi saba kwa Tanganyika, kila kanda ikiwa na watu kati ya milioni mbili hadi tano, ambayo ndiyo idadi ya watu katika nchi nyingi za Ulaya zinazotupa misaada.
Kisha tunakuwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano itakayokuwa na mamlaka kwenye mambo makubwa kadhaa lakini zaidi ya yale yaliyopendekezwa katika Rasimu ya Tume.
Kimsingi Serikali ya Muungano lazima iwe na fursa ya kushughulikia mambo kadhaa yanayohusu maendeleo ya wananchi, vinginevyo ni Serikali ambayo itakuwa haina mvuto kwa wananchi wa kawaida.
Serikali ya majimbo au kanda ndio imekuwa sera ya CHADEMA kwa muda mrefu, lakini sijui ni kitu gani kimewapata na sasa hakuna anayeongelea tena jambo hili wakati mimi nadhani ndio ilikuwa wakati mwafaka wa kulipigania.
Tukishaandika Katiba mpya hakuna chama cha siasa kitakachokuwa na uhalali wa kuibuka na sera kuhusu mambo nyeti kama haya.
Mapendekezo yanaweza yakawepo mengi. Muhimu ni kwamba lazima tuwe wabunifu na tutoke katika sanduku. Tatizo ni kwamba huwezi kuwa mbunifu kama umekaririshwa msimamo wa kivyama kama kasuku.
Ndio maana siamini kwamba hili Bunge la Katiba lililojaa misimamo ya kukaririshwa lina uwezo wa kutuandikia katiba mpya.
Jambo la pili kuhusu namna ya kutoka katika huu mkwamo ni kuangalia uwezekano wa kisheria wa kulivunja Bunge Maalumu la Katiba na kuliunda upya.
Tukiamua kuliunda upya Bunge hili kuna haja ya kuzingatia mambo kadhaa ya msingi. La kwanza, pengine kuna haja ya kuacha kuwajumuisha wabunge wa sasa katika bunge hili.
Nchi nyingi zilizoandika Katiba Mpya kwa mtindo wa Bunge la Katiba hazikujumuisha wabunge wa kawaida. Jambo la pili ni kuangalia uwezekano wa kutunga sheria itakayowapiga marufuku wale wote wanaowania kugombea katika uchaguzi mkuu ujao ili kuepuka mgongano wa maslahi.
Kuna nchi kadhaa ambazo zilifanya hili kwa kutambua uwezekano wa mgongano wa kimaslahi kwa sababu wajumbe ambao wanawania uongozi katika uchaguzi ujao watafanya kazi kubwa ya kujiuza watakapokuwa bungeni.
Ni kwa sababu hii wanasiasa wetu waling’ang’ania kwamba lazima Bunge lionyeshwe ‘live’ ili waonekana kwa wapiga kura. Tunahitaji wajumbe wa Bunge la Katiba ambao hawana haja ya kuonekana wanapotoa michango yao ili wafanye kazi yao kwa utulivu bila mbwembwe.
Bado tuna nafasi ya kujikwamua kwenye mkwamo. Cha msingi ni dhamira na nia. Rais Kikwete bado ana nafasi ya kulinda heshima yake. Auvae tena ujasiri kama alivyofanya awali kwa kuanzisha mchakato huu bila chama chake kutaka.
Namshauri amuagize Mwanasheria Mkuu apeleke marekebisho ya sheria katika Bunge la Bajeti linaloanza ili, pamoja na mambo mengine, apate nguvu ya kulivunja Bunge Maalumu la Katiba.
Muundo wa Bunge Maalumu jipya lazima uzingatie kupunguza wanasiasa ili wasiwe zaidi ya theluthi moja na kwamba wale wote wenye nia ya kugombea katika uchaguzi mkuu ujao wapigwe marufuku kuwa wajumbe wa Bunge Maalumu.

Kitila Mkumbo
src
Raia mwema

Tanzania ya 9 duniani kwa uwezo mdogo wa kufikiri?

 
  • Kama ni kweli, haishangazi nchi kukosa mwelekeo
WIKI iliyopita niliandika kuhoji iwapo mambo kwenda shagalabagala hapa Tanzania, ni kwa sababu ya werevu wa chama tawala CCM au ni kwa sababu ya ujinga wetu Watanzania.
Nilipata mrejesho wa sms na barua pepe wa ajabu kidogo – wako waliokubaliana nami, na wako ambao si tu hawakukubaliana nami, lakini walinilaumu kwa kuwaita Watanzania ‘wavivu wa kufikiri’; kana kwamba wamesahau kuwa wa kwanza kutamka hivyo alikuwa Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa!
Lakini kabla sijaenda mbali, nichukue fursa hii kusahihisha kosa nililolifanya katika makala hiyo. Nilitaja jina la Rais wa Zanzibar aliyesimamia mchakato wa mwaka 2010 kuirekebisha Katiba ya Zanzibar kwa kuingiza vifungu vilivyoudhoofisha Muungano kuwa ni Dk. Mohamed Shein wakati jina nililokusudia kuandika ni Amani Karume. Namuomba radhi sana Dk. Shein na wasomaji wangu kwa kosa hilo.
Nikirejea kwenye sms nilizotumiwa, kuna moja ilinisisimua kidogo; nayo inatoka kwa msomaji wangu mwenye simu namba 0754532797 ambaye aliandika hivi: 
“Tatizo letu kubwa hapa Tanzania na mkuu wa maadui wetu kama taifa ni COLLOSAL MASS IGNORANCE. Ukweli ndugu yangu Mbwambo, hatutoki hapa tulipokwama labda miaka 50 ijayo.”

Kilichonisisimua kwenye ujumbe wake huo ni mambo mawili. Kwanza, ameliita tatizo letu hilo kuwa ni ujinga wa kihalaiki, lakini pili; amesema kwamba hatutoki hapa tulipokwama labda miaka 50 ijayo? Mambo hayo mawili yanatafakarisha. Je, ni kweli wetu ni ugonjwa unaoitwa COLLOSAL MASS IGNORANCE? Na kama ndiyo, je, ni kweli hatuna namna tunaweza kutoka hapo labda mpaka baada ya miaka 50? Tafakari!
Hilo pembeni, kuna msomaji wangu mwingine alikubaliana na nilichokiandika, na hasa kile kilichosemwa na Profesa Kabudi kuhusu ujinga wa kizazi hiki cha sasa cha Watanzania, na kauli ya Rais Mstaafu Benjamin Mkapa kwamba Watanzania tu wavivu wa kufikiri.
Msomaji huyo alikwenda mbali na kunifahamisha ya kwamba Tanzania tunashika nafasi ya tisa duniani katika orodha ya mataifa yenye wananchi wenye bongo zenye viwango vya chini vya kufikiri – wenyewe huita IQ - yaani Intelligence QuotientIQ hupimwa kwa kuangalia uwezo wa ubongo wa kupembua aina mbalimbali za taarifa.
Msomaji wangu huyo alinipa changamoto niitafute kwenye tovuti
External Links icon
  nijisomee mwenyewe jinsi Tanzania tunavyofahamika duniani kuwa tu taifa lenye wananchi wenye IQ za viwango vya chini.
Kwa shauku kubwa niliifungua linki hiyo na nyingine ya http/www.statisticbrain.com, na ndipo nilipokutana na ripoti yenye kichwa kinachosomeka: The Top 10 Countries With the Lowest Population IQ. Katika orodha hiyo sisi Tanzania tunashika nafasi ya tisa tukiwa na wastani wa kiwango cha IQ  72. Nafasi ya 10 inashikiliwa na Sudan ambayo pia kiwango chake ni 72.
Kwa mujibu wa orodha hiyo, Ghana inashika nafasi ya 8 kwa wananchi wake kuwa na kiwango cha chini cha IQ yaani 71. Nafasi ya saba ni Nigeria (67), nafasi ya sita ni Guinea (66), nafasi ya tano ni Zimbabwe (66), nafasi ya nne ni DR Congo (65), nafasi ya tatu ni Sierra Leone (64), nafasi ya pili ni Ethiopia (63) na nafasi ya kwanza ni Equatorial Guinea (59).
Mpenzi msomaji, sina hakika na ukweli wa utafiti uliofanywa ulioibuka na orodha hii, na wala sina sababu ya kuuamini kwa asilimia 100, lakini ninachotaka kusema ni kwamba tuna kila sababu  Watanzania na Waafrika kwa ujumla kujadili suala hili na kujiuliza kulikoni? Ni kweli IQ zetu  Watanzania (na Waafrika kwa ujumla) ni za viwango vya chini?
Kitu muhimu cha kufahamu ni kwamba upimaji IQ hauzingatii namna mtu anavyojibu maswali ya ujumla (yawe ya siasa, jiografia, sayansi nk); bali huzingatia upembuaji wa ubongo wa aina mbalimbali za taarifa na ujengaji hoja. Waingereza wanaita  abstract reasoning.
Kama ni hivyo, je; ni kweli ukimchanganya Mtanzania na Mnyarwanda, Mkenya, na Mganda, na kisha kuwafanyia vipimo vya kisasa vya IQ kama vile Raven’s Progressive Matrices au kile cha Wechester Adult Intelligence Scale, Mtanzania atashika nafasi ya mwisho kwa kuwa na kiwango cha chini?
Nauliza hivyo; maana nchi hizo tatu majirani zetu – Kenya, Uganda, Rwanda, na hata Zambia na Burundi hazimo kwenye orodha hiyo ya nchi 10 duniani ambazo watu wake wanaongoza kwa kuwa na viwango vya chini vya IQ. Na hiyo maana yake ni kuwa, tunazidiwa na nchi hizo kwa viwango vya kufikiri. Hicho ni kitu cha kutafakari.  Natukitafakari basi ili kupata maelezo yenye mashiko.
Mwaka 2007 niliandika katika safu hii kulijadili suala hili baada ya mtafiti na mwanasayansi maarufu wa Marekani, Dk. James Watson, kutoa kauli inayoonyesha kuwa bongo zetu sisi watu weusi ni za viwango vya chini ikilinganishwa na bongo za Wazungu – kauli ambayo alikujashutumiwa nayo dunia nzima kwa kuitwa mbaguzi wa rangi.
Dk. Watson alisema hivi: Bara la Afrika halitoi matumaini ya kusonga mbele kimaendeleo kwa sababu sera zetu zote za kijamii zimewekwa katika msingi wa imani kwamba bongo zao (Waafrika) ni kama zetu Wazungu; ilhali vipimo vyote vya vinasaba vinaonyesha kuwa si sawa, hazifanani na zetu.”
Hivyo ndivyo alivyosema mtafiti na mwanasayansi huyo. Kwa ufupi, anachosema ni kwamba bongo zetu sisi weusi ni dhaifu ukilinganisha na za Wazungu. Sasa, maneno hayo yangesemwa na Mzungu tu wa kawaida, tungeyapuuza moja kwa moja na kumwita mbaguzi wa rangi.
Lakini huyu Dk. Watson si Mzungu wa kawaida. Yeye ndiye aliyevumbua muundo wa chembechembe za nasaba (DNA) za binadamu, na pia ni mshindi wa tuzo inayoheshimika mno duniani ya Nobel, na kwa hiyo huwezi kumpuuza moja kwa moja bila kwanza kuwa na hoja nzito za kisayansi za kumpinga. Huo ndiyo ukweli mchungu kwetu sisi weusi.
Vyovyote vile, hicho alichokisema Dk. Watson miaka saba iliyopita sasa kimeungwa mkono na ripoti hiyo ya nchi 10 zinazoongoza duniani kwa wananchi wake kuwa na viwango vya chini vya IQ ambayo Tanzania tumo.  Katika orodha hiyo, nchi zote 10 ni kutoka bara la Afrika.
Labda niijadili kidogo ripoti hiyo. Kwanza, ripoti hiyo inasema ya kwamba ni makosa kuhusisha viwango vidogo vya IQ moja kwa moja na suala la rangi ya mtu (mweusi au mweupe, Mzungu au Mwafrika nk).
Pili, ripoti hiyo inasema pia kwamba ni makosa kuhusisha moja kwa moja viwango vidogo vya IQ na suala la elimu tu, kwa sababu, mbali ya uduni wa elimu, IQ ndogo pia huchangiwa na mambo mengine kadhaa yakiwemo genes za wazazi, tamaduni, viwango vya lishe na afya za wahusika.
Kama hivyo ndivyo, swali la kujiuliza ni hili: Kama kiwango kidogo cha IQ hakihusiani na suala la rangi ya mtu, ni kwa nini Waafrika ndiyo tunaoongoza kwa kuwa na viwango vya chini vya IQ duniani?
Nadhani jibu lipo katika mseto wa mambo hayo mengine yaliyotajwa yanayochangia bongo zetu kuwa na IQ ndogo – yaani genes za mababu zetu, elimu duni, tamaduni zenye mila hovyo, viwango vidogo vya lishe, afya duni nk.
Kama mambo hayo ndiyo yalikuwa sehemu ya maisha ya babu zetu karne na karne zilizopita, haishangazi, basi, vizazi vya leo kuwa bado na IQ ndogo; maana si tu kwamba tuna genes zao katika miili yetu; lakini bado tumeendelea kuwa na elimu duni, afya duni na lishe duni ikilinganishwa na wenzetu Wazungu.
Kwa maneno mengine, ili isituchukue miaka mingine 50 kuondoka hapa tulikokwama kwa sababu ya uvivu wetu wa kufikiri na ujinga wetu, kama alivyoeleza msomaji wangu yule katika sms yake, ni muhimu kizazi cha sasa kupambana na mambo hayo yanayofanya sisi na wanetu na wajukuu na vitukuu vyetu kuwa na IQ ndogo – yaani tupambane na elimu duni, afya duni, lishe duni, mila duni nk!
Kwa mtazamo wangu, tusipofanya hivyo, tutaendelea kurithisha wanetu, vijukuu na vitukuu vyetu bongo zetu zenye IQ hafifu. Na tutaendelea kukasirika kila tafiti za Wazungu zitakapoibuka na “mapya” kuhusu uwezo wetu sisi Waafrika wa kufikiri.
Kwa bahati mbaya sana, tunawakasirikia watafiti wa kizungu wanapoibuka na tafiti hizo zinazotilia shaka uwezo wetu sisi weusi wa kufikiri, lakini kwa upande mwingine, ni hulka, matendo  na mienendo yetu sisi wenyewe, na ya watawala wetu inayowajengea Wazungu (kina Dk. Watson)  hoja kwamba uwezo wetu wa kufikiri una mushkeli!
Chukua mfano wa hapa Tanzania. Kwa miaka karibu 50 tumekuwa tukipokea misaada ya maendeleo ya mabilioni ya fedha kutoka kwa nchi za Scandnavia, lakini mpaka leo tumeshindwa kuzitumia fedha hizo kujiendeleza. Bado tunawaomba misaada hata ya kujenga choo!
Na hii inanikumbusha kauli iliyopata kutolewa na mama mmoja mwanaharakati wa Sweden. Mama huyo alisema kwamba alipokuwa akinyonyesha mwanawe wa kwanza, Serikali ya Sweden ilikuwa ikiipa Tanzania sehemu ya mapesa ya walipakodi ili iyatumie kujiendeleza.
Mama huyo akaendelea kusema ya kwamba, sasa mwanawe huyo amekuwa mkubwa - naye amezaa mtoto wake, lakini bado Serikali ya Sweden inaendelea kuipa Tanzania misaada ya maendeleo ya mabilioni ya fedha za walipokodi, na akahitimisha kauli yake kwa kuhoji: Ni nchi gani hii Tanzania isiyoweza kusimama yenyewe na kutembea yenyewe hata baada ya miaka 50 ya kusaidiwa? 
Jibu la mama huyo liko katika aina ya watawala tulionao, na pia limo katika aina ya bongo tulizonazo watawaliwa. Unapokuwa na Rais anayefurahia kusafiri kila mara kwenda Ulaya kuomba misaada (tena daraja la kwanza) huku akiwa na msafara mkubwa, unatarajia nini kutoka kwake kuhusu dhana ya kujitegemea?
Unapokuwa na watawala wanaoigeuza nchi kuwa “shamba la bibi” kwa wawekezaji wa kigeni, na huku mikataba wakiifanya siri, na wakati huo huo wananchi wakiona ni sawa tu, na kwenye uchaguzi wanakichagua chama chake kwa sababu tu wanapewa pilau, kofia kanga, na vijisenti kidogo, kwa nini Wazungu wasiibuke na tafiti zinazotilia shaka uwezo wetu wa kufikiri?
Tunapokuwa na maliasili za kila aina – maji, madini, misitu, gesi asilia nk, lakini bado wanetu wanakalia mawe shuleni na wajawazito hospitalini wanajifungulia chini, kwa nini tusiamini tunapowekwa katika orodha ya nchi 10 duniani ambazo wananchi wake wana viwango vya chini vya IQ?
Tunapopiga makofi na kushangilia bila kutafakari (abstract reasoning) kila watawala wanapopanda majukwaani na kupiga blah blah za kisiasa; licha ya kufahamu kwamba walijiuzia kwa bei poa nyumba za serikali na mashirika ya umma, kwa nini kina Dk. Watson wasihoji uwezo wetu wa kufikiri?
Babu wa Loliondo anapoibuka na tiba yake ya ‘kuoteshwa ya kikombe’ na kudai inatibu ukimwi na kisukari, na sisi tunakimbilia kwake kwa mamilioni tukiongozwa na mawaziri wetu, kwa nini tushangae tafiti za kisayansi za kina Dk. Watson zikihoji ubora wa bongo zetu?
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anapokaa kimya wakati Katiba ya Zanzibar inarekebishwa kwa kuweka vifungu vinavyokiuka Katiba ya Muungano, na kisha Rais huyo huyo katika hotuba zake ajinadi kuwa ni ‘mpenda Muungano’ na ataulinda kwa uwezo wake wote, vipimo vya IQ zetu vitaonyeshaje kama sisi wananchi tunamshangilia katika hilo bila abstract reasoning?
Ndugu zangu, nihitimishe tena kama nilivyohitimisha wiki iliyopita kwa kusema kwamba; Profesa Palamagamba Kabudi alikuwa sahihi kabisa alipowatahadharisha hivi watawala wetu kuhusu mfumo wa Muungano unaotakiwa na wananchi katika Katiba mpya:
"Ujinga wa kizazi hiki tusidhani utakuwa ujinga wa kizazi cha kesho. Vizazi vijavyo vya Tanzania vitakuwa na ujinga wake. Ni vyema kuwawekea misingi lakini waje kuishi na ujinga wao kuliko kulazimisha ujinga wetu, kwa sababu ujinga wetu ndiyo amali yetu lakini kwa wengine siyo amali."

Tafakari.
Johnson Mbwambo

src
Raia mwema
-

Thursday, April 24, 2014

UKAWA watakawia sana

Viongozi wa UKAWA

            DEMOKRASI yetu ni ya aina gani kama hatuamini katika kupewa nafasi kwa mawazo ya wengi. Demokrasia hii ni ya aina yake ambapo wachache hatuna uvumilivu pale inapothibitika kuwa wapinzani wetu wametuzidi kwa wingi unaotokana na uchaguzi za kidemokrasia na hivyo wanahaki ya kupitisha wanachoamini? Msingi mmoja muhimu wa demokrasia ni kukubali mawazo ya wengi. Usahihi wa hoja mara nyingi sio jambo muhimu kuliko wingi wa ufuasi. Msingi mwingine muhimu wa demokrasia ni utawala wa sheria. Ni uelewa wangu huo wa demokrasia unaonishawishi nisikubaliane na mantiki ya msimamo wa kundi linalojiita Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) lililoamua kususia Bunge la Katiba wiki iliyopita. Chama cha Mapinduzi (CCM) kina wajumbe wengi katika Bunge la Katiba. Msingi wa wingi wao ni ushindi walioupata katika uchaguzi halali wa kisheria na kidemokrasia. UKAWA wanalijua hilo na hawawezi kuhoji uhalali wa Bunge hilo sasa, baada ya kuingia bungeni na kuanza kushiriki maana maji ukiyavulia nguo, sharti uyaoge. Kadhalika, ni dhahiri kuwa UKAWA hawabishi kwamba Bunge la Katiba lina uwezo wa kubadili vifungu katika rasimu kama mabadiliko hayo yanaungwa mkono na wabunge wengi. Hata hivyo, ni jambo la ajabu kuwa UKAWA hawataki CCM watumie wingi wao kubadili vifungu hivyo. CCM walipofanya hivyo, UKAWA wakalalamika kuwa CCM wamepindua rasimu na kupuuza maoni ya wananchi. Lakini, kwa kufanya hivyo je, CCM wanakiuka sheria? Ni dhahiri kuwa CCM wana uhalali wa kisheria kubadili vifungu vya rasimu. Akilijua hili, Zitto Kabwe aliandika katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Facebook: “Majadiliano ya upande mmoja yanaweza kuwa halali kisheria (legal legitimacy) lakini yanakosa uhalali wa kisiasa (political legitimacy)”. Katika nukuu hiyo ambapo Zitto anasema huenda upo uhalali wa kisheria, kwa upande mwingine anatilia shaka uhalali wa kisiasa. Hata hivyo, uhalali wa kisiasa utakosekana vipi kama hakuna hoja nzito zinazohalalisha ususiaji? Kimsingi, kwa mujibu wa Ismail Jussa, sababu tatu za uamuzi wa UKAWA kususia Bunge aliouita uamuzi wa hekima na busara ni pamoja na kile alichoita CCM kupindua Rasimu ya Katiba ya Wananchi na kupenyeza rasimu yao yenye lengo la kuwalinda watawala na mafisadi. Kwamba, kinachopendekezwa na CCM ni rasimu ya kuwalinda mafisadi, ni maoni ya UKAWA lakini je, sheria inawakataza kubadili vifungu vya rasimu vile waonavyo kama wana wingi wa wajumbe? Sababu ya pili ya UKAWA ya kutoka bungeni ni Waziri William Lukuvi kutumia kanisa kupandikiza chuki na kuchochea vurugu kwa kurejea kauli ya Rais Jakaya Kikwete, kwamba ukipitishwa muundo wa Muungano wa Shirikisho la Serikali tatu, jeshi litachukua madaraka na kwamba Zanzibar itaunda dola ya Kiislamu dhidi ya Wakristo. Lukuvi kama alifanya hivyo bila shaka alikosea. Lakini Lukuvi ni mmoja kati ya wajumbe wengi wa Bunge la Katiba na wala si mwenyekiti au kiongozi wa Bunge hilo. Pili, hatua sahihi ilikuwa ni kupeleka malalamiko rasmi kwa uongozi wa Bunge hilo na mamlaka iliyomteua kuwa Waziri. Vinginevyo, kama kila matamshi ya uchochezi yakitumika kuhalalalisha kususa, hakuna shughuli zinazoweza kuendelea mbele. Lakini Profesa Ibrahim Lipumba ambaye analamlalamikia Lukuvi naye hayuko nyuma katika siasa za misikitini. Siku mbili baada ya kususia Bunge, video ikawekwa Facebook ikimuonyesha Profesa Lipumba akihutubia Waislam msikitini. Yaliyomo humo sitaki kuyataja hapa au kuyatafsiri. Sababu ya tatu iliyosukuma UKAWA kususia Bunge la Katiba ni kile walichodai kuwa mjadala wa Bunge la Katiba umegeuzwa jukwaa la kuhubiri matusi, chuki, ubaguzi wa rangi na ukabila. Kama UKAWA wanakimbia kauli za ubaguzi, wanadhani wapi na lini watapata jukwaa lao peke yao kuzungumza? UKAWA walipaswa kuendesha mapambano yao dhidi ya kauli za ubaguzi ndani ya Bunge, na sio nje. Mikutano watakayoifanya na wananchi haitowabadili wajumbe wa CCM katika Bunge la Katiba na baada ya kumaliza mihangaiko yao, wakirudi watawakuta wenzao vile vile. Kutokana na mazingira haya, mjadala wa upande mmoja utakaoendelea bungeni ni halali, hata kama UKAWA wakiendelea kususia. Kwa maoni yangu, uamuzi wa UKAWA wa kususia Bunge sio wa busara kabisa. Katika siasa za ushindani unaweza kushinda au kushindwa. Kama ambavyo UKAWA wanaamini sana katika Serikali tatu, wapo wengine wanaoamini sana katika Serikali mbili au moja na tupo baadhi ambao hatuutaki hata huo Muungano. Lakini haiwezekani mifumo yote mitatu itumike ndio maana kila upande unapong’ang’ania msimamo, mnapiga kura za kuamua. Dhana kuwa CCM hawana hoja nayo haina mashiko. Tumeshuhudia hata miongoni mwa jamii ya wasomi, wanaoangalia mambo kwa ushahidi wa kitaaluma, baadhi wakiunga mkono Serikali mbili, sembuse wanasiasa ambao hawatumii vipimo vya kisomi katika kujenga hoja? Bila upendeleo, mtu yeyote anayetumia vigezo vya kitaaluma ni rahisi kutilia shaka takwimu za Tume ya Katiba kama kweli zinathibitisha kuwa wengi wanataka Serikali tatu. Hili limezungumzwa sana, na ni bahati mbaya kuwa UKAWA wanajaribu kuonyesha kuwa ukosoaji huu ni kumdharau Jaji Joseph Warioba na tume yake iliyojaa baadhi ya watu wenye heshima kubwa ndani na nje ya nchi. Kwa upande mwingine, hata bila ya hoja za Serikali mbili, Muungano wa UKAWA ni rahisi kumtisha mtu yeyote kwa sababu kinachowaunganisha watu wa UKAWA ni upinzani dhidi ya Serikali mbili tu. Ukiacha hilo, kila moja katika kundi la UKAWA linahitaji mfumo tofauti, baadhi wakidai Muungano wa mkataba, wengine wakidai Serikali tatu za marais watatu na wengine wakidai Serikali tatu chini ya rais mmoja na mawaziri wakuu wawili. Kadhalika, wote tunajua historia ya minyukano kati ya vyama vinavyounda UKAWA hususan CUF na CHADEMA. Binafsi, sina imani na UKAWA kwa sababu ni muungano wa maslahi ya muda mfupi ambao huenda zikikubalika Serikali tatu tusishangae kukaibuka UKAWA- asili na UKAWA - mpya! Hata hivyo vyovyote iwavyo, kwa maslahi ya demokrasia na utawala wa sheria, UKAWA wanapaswa warudi bungeni wakaendelee kupambana. Wakishindwa tutasema wamekufa kiume ingawa demokrasia na utawala wa sheria vimefuata mkondo wake. Kabla ya kurudi bungeni, UKAWA wanapaswa kujipanga vizuri zaidi kwa hoja, walifanya makosa kadhaa ikiwemo kung’ang’ania hoja ya uhalali wa Muungano, ambayo haina maana yoyote na ilisukuma kutajwa kwa udhaifu wa watu wanaochukuliwa kama nembo ya taifa hili, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Aman Karume. Halikuwa jambo zuri kuhoji uhalali wa Muungano wenyewe na waliyoyafanya waasisi hao katika miongoni mwa taratibu za kuunganisha nchi hizi kwa sababu wazee hao waliishi katika zama tofauti, tena wakiendesha taifa changa. Kama walifanya makosa ya makaratasi na vikao, hayawezi kuharamisha Muungano tuliouishi miaka 50 sasa. CCM hawawezi kuwapa UKAWA Serikali tatu. Lakini upo uwezekano wa kuandaa kura ya maoni ili wananchi wapate nafasi ya moja kwa moja ya kusema wanautaka au hawautaki Muungano na kama wanautaka uwe wa mfumo gani. Hiyo ndio hoja ambayo UKAWA wanapaswa kuisimamia. Hilo likipita hakuna mshindi wa moja kwa moja, lakini utatuzi wa kudumu wa mfumo wa Muungano utapatikana. Wazo la kura ya maoni likikataliwa, bado UKAWA wanayo nafasi ya kushawishi wananchi waikatae Katiba katika kura ya maoni. Kadhalika, Uchaguzi Mkuu ni mwakani tu, wajipange na kwa kuwa kama wanavyojinasibu wao ndio wawakilishi wa wananchi, watashinda na kuanzisha mchakato mwingine wa uuundaji

src
Raia mwema
Njonjo Mfaume

Tutengeneze Katiba ya Serikali mbili zisizonung’unikiana

 
 
TAIFA liko kwenye mjadala mkubwa wa kijamii na kisiasa katika mchakato muhimu wa kuandika upya Katiba.
Mchakato huu umetokana na malalamiko kutoka kwa watu kadhaa kuwa Katiba, ambayo imelilea Taifa tangu mwaka 1962, imezeeka, imejaa viraka na hivyo iandikwe upya.
Baada ya kauli ya Rais Jakaya Kikwete ya Desemba mwaka 2011 kwamba angeanzisha mchakato wa kuandika upya Katiba, Bunge lilitunga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, sura 83 mwaka 2012 na mchakato ukaanza kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kukusanya maoni na kuwasilisha Rasimu ya pili ya Katiba bungeni mapema Machi, 2014.
Bunge Maalumu la Katiba sasa linaendelea na vikao vyake Dodoma. Mjadala mkali umezuka na unaedelea, kuhusu muundo wa serikali baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kupendekeza kuundwa kwa shirikisho la serikali tatu, kinyume na Katiba ya sasa (Katiba ya mwaka 1977) yenye serkiali mbili.
Je, Katiba yetu imezeeka na hairekebishiki?
Japo swali hili halina umuhimu tena kwa sasa kwani mchakato wa kuandika Katiba mpya unaendelea, mazingira na mijadala inavyoendelea inalazimu wadadisi kurejea swali hili.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliandikwa mwaka 1977, miaka 37 iliyopita. Tangu wakati huo, imefanyiwa marekebisho kwa nyakati na sababu tofauti mara 14. Katiba hii iliandikwa baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964 ambapo ilikubaliwa kwamba Katiba ya Jamhuri ya Tanganyika ya mwaka 1962 ifanyiwe marekebisho ili kuipa sura ya Muungano na kuifanya kuwa Katiba ya Mpito.
Marekebisho hayo yalifanyika mwaka 1965 na hivyo kuifanya Katiba ya mpito hadi mwaka 1977 ilipoandikwa Katiba ya Kudumu inayotumika hadi hivi sasa.
Tanzania, ambalo ni Taifa la Muungano wa Nchi Mbili za Tanganyika na Zanzibar, ni Taifa changa kwani lina umri wa miaka 50 tu. Ziko nchi zenye umri zaidi ya Taifa letu ambazo zimeendelea kutumia na kurekebisha katiba zao.
Marekani, kwa mfano, inatumia katiba yenye umri wa zaidi ya miaka 200 na ambayo imefanyiwa marekebisho zaidi ya mara 100.
India, kwa upande wake, iliandika katiba yake ya Uhuru mwaka 1945, miaka 70 iliyopita, mwaka 2012 iliifanyia marekebisho katiba yake, marekebisho ya 94 Katika yake hiyo ya mwaka 1945.
Hivyo, madai kwamba Katiba yetu ya sasa imezeeka na kujaa viraka (kwa kufanyiwa marekebisho mara 14) na hivyo iandikwe mpya ni madai yanayoacha mjadala.
Msingi wa malalamiko kuhusu Katiba ya sasa (ya Mwaka 1977)
Kwa mujibu wa taarifa na nyaraka mbalimbali zilizoambatishwa na Rasimu ya pili ya Katiba ‘mpya’ iliyowasilishwa bungeni na Jaji Warioba, Machi 2014, madai ya kuandikwa upya kwa Katiba yetu ni kwamba;
Muungano, ambao umedumu kwa mika 50 sasa, umeghubikwa na malalamiko mengi kutoka kila upande, hasa Zanzibar kulalamika kwamba Tanzania Bara, inanufaika zaidi kiuchumi kwa kuwa Serikali ya Tanzania Bara ndiyo hiyo hiyo ya Muungano wa Tanzania, na hivyo, Bara ‘kuvaa koti la Muungano’.
Madai hayo ya Zanzibar, yameufanya upande huo wa Muungano kuwa na majaribio na maombi ya mara kwa mara ya kudai ‘uhuru zaidi’, hasa kwa lengo la upande huo kunufaika zaidi kiuchumi na kijamii na mahusiano ‘ya nje’.
Kwa upande wa Bara, malalamiko machache yaliyopo ni kwamba ‘upande wa Zanzibar unanufaika zaidi na fursa na faida za Muungano’, wakati huo huo, kutokana na mazingira yake (ya udogo kieneo na kwa idadi ya watu), Zanzibar kuchangia kidogo au kutochangia kabisa ‘gharama za Muungano’.
Mabadiliko ya Kisiasa na Kijamii ambapo Katiba ya sasa, licha ya kufanyiwa mabadiliko, kwa mfano, mwaka 1992 kuruhusu Mfumo wa Vyama vingi, bado Katiba imekuwa ni kikwazo kwa vyama vya siasa vya Upinzani kufanya vizuri katika chaguzi kwa madai kwamba Tume ya Uchaguzi, na vyombo vingine vya demokrasia vimebanwa kikatiba kuegemea upande wa chama tawala hasa kwa kuwa viongozi wake wanateuliwa na Rais ambaye ndiye kiongozi wa chama tawala.
Kuwepo kwa umasikini mkubwa miongoni mwa Watanzania, umasikini ambao hauendani na utajiri wa Taifa wa Maliasili; hali inayoashiria kwamba Katiba ya Sasa haijaweka mifumo mizuri ya kusaidia wananchi wanufaike na kuendelezwa na maliasili na utajiri wa asili wa Taifa letu.
Hali hii imeelezewa kusababishwa na mifumo dhaifu ya uwajibikaji wa viongozi; kukoseka kwa dira ya Taifa baada ya Azimio la Arusha kufutwa mwaka 1991 na misingi dhaifu ya Haki za Binadamu.
Ukweli na uhalali wa sababu au madai ya Katiba mpya na jinsi madai hayo yalivyozingatiwa Katika Rasimu ya Pili ya Katiba inayojadiliwa bungeni.
Kama ilivyoelezwa, msingi mmojawapo wa sababu za kuandika upya kwa Katiba ni malalamiko kuhusu ‘manufaa, hasa ya kiuchumi na kijamii’ ya Muungano.
Nitalizungumzia zaidi eneo hili kwa sasa, na maeneo mengine ya ‘uhuru wa tume ya uchaguzi na vyombo vingine vya kukuza demokrasia’ pamoja na eneo la ‘udhibiti na usimamizi wa rasilimali za Taifa kwa manufaa ya wananchi’, nitayazungumzia katika makala zitakazofuata.
Muungano wa Tanzania, na hasa muundo wake, limekuwa ni eneo la mjadala mpana na mkali sana wakati huu wa mjadala wa Rasimu ya Pili kwenye Bunge Maalumu na nje ya Bunge.
Kwa kutambua umuhimu wa Muungano, Bunge la Jamhuri ya Muungano, lilipopitisha Sheria ya Mabadiiko ya Katiba, sura 83, katika kifungu 9(2), liliweka maeneo ambayo yanapaswa kulindwa na kuzingatiwa katika Mchakato na hatimaye kuandikwa kwa Katiba mpya.
Kati ya maeneo hayo, ni uwepo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Katika kufanya kazi yake, Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ilizingatia eneo hilo kwa mtazamo kwamba ‘eneo hilo linapaswa kulindwa na kuimarishwa’, na hivyo tume kujipa uhuru wa ‘kupendekeza marekebisho’ ambayo Tume inaamini yataboresha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa utafiti wa aina za Muungano, Tume inasema, Muungano wa nchi zaidi ya moja huleta ama serikali moja (yaani Muungano uitwao unitary union), au serikali mbili au zaidi (katika mfumo wa shirikisho, yaani federation) au serikali tatu zinazoshirikiana kimkataba (yaani confederation).
Katika aina zote hizo za muungano, bado uwezekano wa muungano kuvunjika upo (bila kujali idadi ya serikali zinazoundwa baada ya muungano).
Kwa maoni ya Tume, uimara wa muungano hautokani na idadi ya serikali zinazoundwa, bali ‘dhamira ya kisiasa’ kusimamia na kumaliza ‘malalamiko kuhusu muungano yanayotoka kwenye nchi washirika’.
Kwa tafsiri hiyo ya kifungu hicho cha sheria, Tume, kwa kuamini kwamba inaboresha na kwa kuzingatia tafiti kadhaa ambazo ilifanya na kwa kusikiliza maoni ya wananchi kadhaa kuhusu jambo hilo (la Muungano) na kwa kutambua hatua ambazo zimekuwa zikichukuliwa na upande mmoja wa Muungano, hususan Zanzibar kujitafutia ‘uhuru zaidi’ (hasa kupitia marekebisho ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984 yaliyofanywa mwaka 2010) , ilipendekeza ‘kuivua Tanzania Bara koti la Muungano’, na hivyo kupendekeza kuwepo kwa serikali ya ‘kati au ya Ushirika au ya Washirika wote wawili’, serikali ya Tatu, ya Shirikisho, sambamba na ile ya Tanganyika inayoanzishwa kutoka Tanzania Bara iliyokuwa ndani ya Muungano.
Utafiti wa tume kwa nchi mbalimbali zilizoungana, unaonyesha kwamba, ipo miungano iliyodumu ya serikali moja, na mingine ya serikali mbili au zaidi (yaani ya shirikisho), na pia ipo mifano ya nchi zilizokuwa za muungano zilizokuwa za serikali moja na nyingine zaidi ya serikali mbili ambazo miungano yao imevunjika.
Hii inathibitisha ukweli kwamba, idadi ya serikali pekee, hailindi muungano. Nchi za Somalia (Somalia na Somaliland); Ethiopia (Ethiopia na Eritrea), Sudan (Sudan Kusini na Kaskazini) zote zilikuwa na muungano wa serikali moja (unitary union), lakini miungano hiyo imevunjika.
Zipo pia nchi za shirikisho, kama Urusi (USSR), Chekoslovakia na Yugoslavia zilizokuwa za shirikisho nazo zimesambaratika! Aidha, zipo nchi zenye mashirikisho (serikali zaidi ya moja) ambazo zinaendelea kudumu kama vile Canada, India, Brazil, Marekani na hata Ujerumani.
Kwa hiyo, kwa maoni ya Tume, dawa ya kulinda muungano wetu ni kubadilisha muundo wa muungano huo kutoka muundo wa serikali mbili wenye malalamiko lukuki yasiyokoma, na kuunda shirikisho la serikali tatu ambazo mipaka yake ya kiutendaji inaeleweka vizuri.
Kwa mtazamo wa Tume na baadhi ya watu, kuitenganisha Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Muungano, kutapunguza malalamiko, hasa kutoka upande wa Zanzibar kwamba Tanganyika imevaa koti la Muungano na hivyo kunufaika zaidi kiuchumi na Muungano.
Malalamiko ya Zanzibar, ambayo yamekuwa kichocheo kwa mshirika huyo katika Muungano kuchukua hatua za ‘kujitafutia uhuru zaidi’ na hivyo kunufaika zaidi kiuchumi, yasiporekebishwa yanaweza kusababisha Muungano kuvunjika, jambo ambalo Tume imeagizwa kisheria kwamba iweke mazingira ya kuzuia lisitokee.
Hali ya Muungano ikoje kwa sasa, nani ananufaika zaidi?
Ukiuliza swali hili kwa kila upande wa Muungano, kila upande utasema upande mmoja unanufaika zaidi. Tuanze na upande mmoja baada ya mwingine.
Upande wa Zanzibar unatuhumu Bara kunufaika zaidi hasa kwa misingi ifuatayo:-
Tanzania Bara, ambayo iko ndani ya Serikali ya Muungano, ndiyo msimamizi mkuu wa vyanzo vya mapato vya Muungano. Mapato hayo ya vyanzo vya Muungano, ambayo yanapaswa kutumika kugharimia shughuli za Muungano pekee na kiasi kinachobaki kikipaswa kugawanywa kwa washirika kwa ajili ya maendeleo, hayatumiki yote kwa lengo hilo.
Kwa miaka mingi sasa, kiasi cha mapato yatokanayo na vyanzo vya Muungano ambacho kimekuwa kikitumika kugharimia shughuli za Muungano ni chini ya 35% tu ya mapato yote, na hivyo, Zanzibar inaituhumu Tanzania Bara, kwamba kiasi kinachobaki cha 65% hutumika kwa shughuli za maendeleo zisizo za Muungano za upande wa Tanzania Bara. Huu ndio msingi mkuu wa madai ya Tanzania Bara kunufaika na ‘koti la Muungano’.
Tanzania Bara, ambayo iko ndani ya Serikali ya Muungano, ndiyo msimamizi wa Sera za Nje za Taifa na ndiye Mwakilishi wa Tanzania kwenye vyombo mbalimbali vya kimataifa.
Kwa kutumia nafasi hii, Tanzania Bara, imekuwa ikipata mikopo na misaada kutoka nje kwa niaba ya washirika wote wawili, lakini misaada hiyo na mikopo imekuwa ikitumika zaidi katika miradi ya maendeleo ya Tanzania Bara.
Kwa kutumia fursa hii, Tanzania Bara, katika ‘koti la Muungano’, imeweza kuingia katika taasisi mbalimbali za kimataifa Kama SADC; EAC; FIFA; WHO; UNESCO nk, na manufaa ya ushiriki wa Tanzania kwenye taasisi hizo yamekuwa hayagawanywi kwa usawa baina ya washirika wote wa Muungano.
Tanzania Bara, ambayo iko ndani ya Serikali ya Muungano, ndiyo msimamizi mkuu wa fedha, sera za uchumi na utumishi katika Wizara za Muungano. Kwa kutumia nafasi hiyo, Tanzania Bara imekuwa haigawi sawia manufaa ya ajira na fedha kwenye taasisi hizo. Zanzibar, bila kujali hali yake halisi ya udogo kieneo na uchache wa wakaazi, inadai manufaa ya Muungano kama ajira, yagawiwe sawa baina ya Washirika hao wawili.
Kwa matazamo wa Zanzibar, ajira kwenye taasisi za Muungano kama uteuzi wa mabalozi nje, ajira katika vyombo vya ulinzi na usalama vinapaswa vigawiwe sawa!
Aidha, manufaa ya kifedha kama scholarships na mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu yanapaswa yagawanywe kwa washirika wote wawili kwa usawa!
Aidha, uongozi katika taasisi za Muungano kama nafasi za waziri, katibu wakuu, wakurugenzi na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama utolewe kwa kupokezana baina ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Tanzania Bara, ambayo iko ndani ya koti la Muungano, ndiyo msimamizi na mtungaji wa sera nyingi za kijamii kwa Tanzania, kwa kutumia fursa hiyo, Tanzania Bara imekuwa ikiinyima Zanzibar uhuru wa kujiamulia mambo yake ya kijamii na kiimani.
Upande wa Tanzania Bara, unaituhumu Zanzibar kunufaika na ‘kudai manufaa zaidi’ kutokana na Muungano, wakati huo huo kuendelea kuomba ‘isiwajibike’ kuchangia Muungano kwa kuwa uchumi wake eti ni mdogo’, kinyume na ukweli halisi kwamba Zanzibar inaeneo dogo (2,600km2, sawa na Jimbo la Uchaguzi la Mwibara, Bunda!) na watu wachache (watu 1,300,000 tu), sawa na wakazi wa Wilaya mbili za Mkoa Shinyanga za Kahama na Shinyanga)!
Baadhi ya Mifano ya manufaa hayo ‘yaliyopita kiasi’ kwa Zanzibar kwa muono wa Tanzania Bara ni yafuatayo:-
Zanzibar, ambayo ni sehemu ya Tanzania yenye wakazi 1,300,000 (sawa na 3% ya Watanzania wote ambao ni 45,000,000), ina wabunge zaidi ya 80 kwenye Bunge la Muungano lenye wabunge 357!
Wabunge hawa, ambao wanalipwa zaidi ya Tshs 10bn kila mwaka kupitia mishahara, posho na marupurupu mengine ukiwamo mfuko wa jimbo, hushiriki kwenye mijadala bungeni ambayo zaidi ya 80% ya mijadala hiyo inahusu Mambo yasiyo ya Muungano ya Tanzania Bara.
Zanzibar, ambayo ni sehemu ya Tanzania, imekuwa na mfumo wake wa utambuzi wa raia wake, na hivyo, kwa sheria yake, kuweza kuwatenga Watanzania Bara kwenye fursa za ajira na umiliki wa ardhi Zanzibar, wakati huo huo wao wakinufaika na fursa hizo upande wa Tanzania Bara.
Zanzibar kiuchumi iko vizuri kuliko Bara, kwani kwa bajeti yake ya Tshs 740bn kwa watu 1,300,000 ni sawa na wastani wa kutenga Tshs 540,000 za kumhudumia kila raia kwa mwaka. Kwa upande wa Tanzania Bara, wastani wa kibajeti kwa raia ni Tshs 330,000 kwa kila raia kwa mwaka, ambayo ni chini kuliko Zanzibar! Pamoja na hali hiyo, Zanzibar imekuwa ikiomba na kusaidiwa na Muungano (ambamo ndani yake imo Tanganyika kwa zaidi ya 90%) kwenye shughuli za kawaida za kimaendeleo.
Kwa kupitia mfumo huu, Zanzibar imefanikiwa kufanya yafuatayo:-
Kutoa huduma za afya bure, wakati Tanzania Bara haifanyiwi hivyo, kutoa elimu ya masingi hadi sekondari bure, wakati Tanzania Bara haifanywi hivyo, kufikia malengo ya kuunganisha wilaya zote 10 na kata zote za Zanzibar kwa Barabara za Lami, wakati Tanzania Bara wilaya zilizounganishwa kwa lami ni kama 70% tu, kufikisha huduma ya maji salama kwa Wanzanzibari kwa uwiano wa kila kaya tatu kuwa na bomba la maji, kuwezesha kujenga hospitali nzuri za kisasa za wilaya na mikoa wakati Tanzania Bara wilaya na mikoa yenye hospitali za wilaya na mikoa ni 60%, kufikisha huduma ya umeme kwenye kata zote za Zanzibar, kuondoa kabisa tatizo la madawati mashuleni.
Zanzibar, ambayo ni ndogo na ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imekuwa ikitoa viongozi na watumishi kwenye wizara zisizo za Muungano. Mfano, mawaziri kadhaa kutoka Zanzibar wanaongoza wizara zisizo za Muungano.
Zanzibar kubaki na utambulisho wake, kama vile Bendera, Wimbo wa Taifa, Rais, Baraza lake la Wawakilishi, wakati Tanzania Bara imepoteza vyote hivyo kupitia Muungano.
Kwa kuwa Tanzania Bara iko ndani ya Serikali ya Muungano, mapato yake kutokana na rasilimali zake lukuki kama madini, gesi nk zinaingizwa kwenye mfuko mkuu wa Muungano, na hivyo kunufaisha washirika wote, wakati rasilimali za Zanzibar si za Muungano na hukusanywa na serikali ya Zanzibar na kutumika Zanzibar pekee.
Hali hii inaleta ule usemi maarufu kwa Watanzania Bara kwamba kuwalenga Wazanzibari kwamba ‘chetu, chao; na chao, chao’!
Kuvipa hadhi sawa vyombo vya Utawala, Utungaji Sheria na Utoaji Haki vya Muungano na Zanzibar, jambo ambalo si sawa. Kwa mfano, katika maeneo yafuatayo:-
Katika majadiliano ya kuondoa kero za Muungano, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano hukutana na Makamu wa Pili wa Zanzibar, ambaye ki hadhi, si saizi yake. Hii ni kushusha hadhi ya Waziri Mkuu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano hulazimika kushauriana na Rais wa Zanzibar katika mambo mengi ya utawala, mfano, katika uteuzi wa wajumbe wa Tume ya Katiba na hata wajumbe wa Bunge la Katika, wakati Rais wa Muungano ni mkubwa kwa wa Zanzibar.
Aidha, Rais wa Muungano huwa nyuma kiitifaki kwa  Rais wa Zanzibar kwenye Sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar, wakati Zanzibar ni sehemu ya Tanzania.
Spika wa Bunge la Muungao kupewa hadhi iliyo sawa kiitifaki na Spika wa Baraza la Wawakilishi, wakati wawili hawa hawana hadhi sawa, kwani Spika wa Muungano ni wa wote (Bara na Zanzibar).
Mwanasheria Mkuu wa Muungano kupewa hadi sawa na Mwanasheria MKuu wa Zanzibar, na mifano mingine mingi.
Tume imependekeza nini katika haya kwenye Rasimu ya Katiba?
Ili kurekebisha matatizo haya, Tume ya Marekebisho ya Katiba, imependekeza kuunda mfumo mpya wa muungano wa shirikisho, la serikali tatu, ambazo mipaka yake ya kiutendaji itakuwa wazi zaidi.
Katika Ibara ya 1 ya Rasimu ya Katiba, imependekezwa kwamba Tanzania itambuliwe kuwa ni Shirikisho.
Katika sura ya 6 ya Rasimu ya Katiba, mgawanyo huu wa serikali tatu umeelezewa katika ibara kama ifuatavyo:-
Ibara ya 60, inaelezea kuwa Muundo wa Muungano utakuwa wa serikali tatu, za Muungano, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Tanganyika. Aidha, ibara hiyo inaanzisha Bunge na Mahakama za Muungano na za Tanganyika. Hii inaivua rasmi Tanganyika ‘koti la Muungano’. Ibara ya 62(3), inaruhusu serikali ya Muungano kusaidia serikali yoyote baina ya ile ya Tanganyika na ile ya Zanzibar  kama itahitajika na kuombwa hivyo. Hii inaweka uhalali wa pande zote mbili za Muungano kusaidiwa na serikali ‘ya pamoja, yaani ya Muungano’.
Ibara ya 64 inazitambua Nchi Washirika na majukumu yake. Hivyo, kuweka mipaka ya kiutendaji iliyo wazi baina ya Tanganyika, Zanzibar na Muungano. Aidha, ibara ya 64(5), inaweka wazi kuwa Nchi Washirika zitakuwa na ‘hadhi na haki’ SAWA ndani ya muungano. Ibara hii, kwa kutoweka matakwa ya ‘wajibu sawa kwa washirika, na kuweka usawa wa Haki na Hadhi pekee’, inatoa fursa kwa mbia mmoja, hasa Tanganyika kulalamika kwani, kwa vyovyote vile kwa kuzingatia hali halisi ya ukubwa na wingi wa rasilimali Bara, basi Tanganyika ITAWAJIBIKA ZAIDI, lakini Washirika hawa wawili watapata HAKI na HADHI SAWA!! Hii ni kasoro kubwa katika rasimu kwenye eneo hili.
Ibara ya 65, inaweka Mamlaka ya Washirika kwa maeneo yao, lakini pia kuweka misingi ya HAKI na USAWA katika ushirikiano baina ya Washirika. Aidha, kila mshirika anaruhusiwa kuanzisha mashirikiano na nchi au taasisi za nje kivyake, hii inaondoka malalamiko ya Zanzibar kwamba Tanganyika inanufaika peke yake kupitia mashirikiano hayo!
Mapendekezo ya walio wengi katika Bunge Maalumu la Katiba
Wajumbe walio wengi katika Bunge Maalumu la Katiba, wamependekeza mfumo wa serikali mbili, kwa kufanya hivyo, walio wengi wamependekeza marekebisho kwenye rasimu kama ifuatavyo:-
Bila kusisitiza msingi wa Usawa katika HADHI na HAKI baina ya Washirika wa Muungano, Serikali zitakazokuwepo Mbili za Muungano na ya Zanzibar zitakuwa na ushirikiano. Ibara ya 60 inapendekezwa kuwapo serikali mbili za Muungano na Zanzibar.
Ibara hiyo pia inapendekeza kuanzishwa kwa Bunge na Mahakama za Muungano na Zanzibar. Hata hivyo, Ibara hii, bado haijaainisha UTOFAUTI WA HADHI NA HAKI baina ya vyombo hivyo. Kwa pendekezo hili, bado viongozi wa mihimili ya Dola toka Zanzibar wataendelea kuwa na hadhi sawa na wale wa Muungano, jambo ambalo ni kero, hasa upande wa Bara.
Ibara ya 62 ya mapendekezo ya walio wengi, inaweka misingi ya ushirikiano baina ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar.
Aidha, ibara ya 62(2), inaelekeza kwamba ‘serikali ya Muungano’ itaisaidia Zanzibar kwenye mambo ya maendeleo yasiyo ya Muungano ili kuleta uwiano wa kimaendeleo katika pande mbili za Muungano.
Pendekezo hili, pamoja na kutotambua ukweli kwamba Zanzibar tayari ‘iko vizuri kimaendeleo kuliko Bara’ hasa kwa sababu ya udogo wake, bado linaweka misingi ya Zanzibar kusaidiwa, tena bila kuweka uwezekano wa Muungano kusaidiwa na Zanzibar, jambo ambalo linawezekana kabisa, kwani endapo Zanzibar ikapata mafuta kwa mfano, kwa udogo wake, uchumi wake unaweza kuimarika ghafla na hivyo kuwa na uwezo wa kusaidia Bara na hata Muungano.
Kwa kuweka msingi wa ‘msaada kwa Zanzibar pekee toka Muungano, ambayo kimsingi ni Bara, tayari linaleta ‘kero kwa siku za usoni kwani Zanzibar haijahitajika kikatiba kusaidia Bara hata pale mambo yake yatakapokuwa safi, ingawa hata sasa yako safi!
Kwa ampendekezo ya walio wengi, Ibara ya 65 inatoa Uhuru kwa Zanzibar kujiunga na taasisi za kimataifa na hivyo kupata misaada na mikopo kwenye maeneo yasiyo ya muungano. Pamoja na uzuri wa jambo hili katika kupunguza malalamiko kwa Zanzibar, ibara hii inaweza kutoa mwanya kwa Zanzibar kuendelea kujitambulisha kimataifa kama nchi, hali inayoweza kutumika hapo baadaye kuifanya Zanzibar kutaka kuwa mwanachama wa UN, walau kama mtazamaji (observer) kama ilivyo Palestine. Jambo hili linahitaji kuangaliwa kwa umakini.
Maoni ya Mwandishi
Kwa maoni yangu, napendekeza, mfumo wa serikali mbili ambao wengi wamependekeza uendelee, lakini unahitaji kuboreshwa zaidi katika maeneo yafuatayo:-
Haki, hadhi na wajibu usiwe sawa bali uwe wa uwiano
Kwa ujumla, walio wengi wamependekeza kuendelea kwa Muundo wa Serikali Mbili, hata hivyo, bado masuala ya HAKI, WAJIBU na HADHI katika kuhudumia na kunufaika na Muungano ambayo ndiyo msingi wa malalamiko mengi yanahitaji kuboreshwa zaidi.
Ni vema kwa wakati huu, tukaweka misingi ushirikiano inayotambua ukweli kwamba Zanzibar ni ndogo, na hivyo ipate WAJIBU, HAKI na HADHI kidogo kuliko Tanzania Bara. Si sawa, kwa mfano, kutoa fursa za ajira kwa usawa. Kutoa fursa za malipo ya mikopo ya elimu ya juu kwa usawa.
Kwa kutambua hali ya Zanzibar, inaweza kufaa kuipa mgao wa wajibu unaolingana na uwezo wake na huo ndio uwe msingi wa Haki kwa ZANZIBAR. Jambo hili liwekwe bayana kwenye KATIBA.
Kama Zanzibar inachangia, kwa mfano, 25% ya mapato ya Muungano, basi ipate haki katika ajira na fedha kwa uwiano huo.
Aidha, kwa kuwa ardhi si suala la Muungano, basi raia wa Tanzania wanaotokea Zanzibar, wapate hadhi tofauti na wale wa Tanzania Bara katika kupata na kumiliki ardhi Bara. Kwa hali ilivyo sasa, ardhi ya Tanzania Bara ni ya Muungano, wakati ile ya Zazibar ni ya Wazanzibar, na hii ni kero!
 Namna nyingine ya kurekebisha suala hili la ardhi ni kufanya ardhi kuwa suala la Muungano, na hii itatoa fursa zaidi kwa Wazanzibari kuhamia Bara pale ardhi Zanzibar itakapokuwa imekwisha, lakini wakati huo huo, Wabara wenye uwezo waweze kupata ardhi Zanzibar, na kwa kuwa Zanzibar ardhi ni ndogo, basi hakika bei yake itakuwa ni kubwa na hivyo Wazanzibari wataweza kuuza ardhi yao kwa bei ya juu na kuja kununua ardhi Bara bila vikwazo kwa upande wowote. Hili limetokea kwa Wazaramo wa Kariakoo bila matatizo yoyote.
Aidha, ni muhimu kupata namna ya kuweka hadhi ya Muungano na vyombo vyake vya Dola kuwa kubwa kuliko ile ya Zanzibar. Kwa mfano, kutomlinganisha Spika wa Muungano na Spika wa Zanzibar; Kutomuweka Rais wa Muungano, kwa namna yoyote na mazingira yoyote, kuwa nyuma au sawa kiitifaki na Rais wa Zanzibar; Kutomuweka Waziri Mkuu wa Muungano sawa na Waziri Kiongozi au Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar nk.
Kuwepo Misingi ya Kusaidiana kwa pande mbili
Ni vema pia kutambua misingi iliyoko kwenye Hati ya Muungano, na hivyo, kutokuweka kwenye Katiba ulazima wa Zanzibar kusaidiwa na Bara au Serikali ya Muungano kwenye mambo yasiyo ya Muungano.
Namna nyingine ya kulifanya jambo hili, kama ni lazima, basi ni kuweka msingi wa KUSAIDIANA kwa wote (Zanzibar, Bara na Muungano), kwani hali za kiuchumi zinabadilika na kwa kuwa, Katiba tunayoiandika ni ya kudumu, hata miaka 100, na hivyo kuwapo uwezekano kwa ‘mnyonge/masikini’ sasa kuwa tajiri kesho, jambo linaloweza kuleta mgogoro hapo baadaye kwa kuwa litakuwa ni la kikatiba.
Kuwepo na mabunge mawili katika Bunge la Jamhuri ya Muungano
Ili kuwatendea haki Watanzania Bara wakati wa kujadili mambo ya Bara yasiyo ya Muungano na kupunguza gharama, ni vema Bunge la Muungano likawa na sehemu mbili, za Bunge la Juu na la Chini.
Bunge la Juu, ambalo linaweza kuitwa senate, liwe ni la Muungano. Liwe Bunge Dogo lenye viongozi wawakilishi wenye uzoefu na elimu ya juu na lizungumzie mambo makubwa ya Kitaifa na kusimamia Wizara na Masuala ya Muungano. Mawaziri wa Wizara za Muungano wawajibike huko. Liwepo pia Bunge la Chini litakaloshughulikia mambo ya Tanzania Bara yasiyo ya Muungano.
Bunge hili linaweza kuwa kubwa zaidi ya lile la senate kwa kutambua ukubwa na wingi wa watu Tanzania Bara. Mawaziri wa wizara zisizo za Muungano wawajibike katika Bunge hili.
Muungano wa SERIKALI MBILI uwe “sera ya Taifa”, si sera ya chama kimoja cha siasa
Uzoefu katika mchakato huu wa Katiba unaoendelea umeonyesha na kuchocheya mgawanyiko mkubwa baina ya Watanzania, kati ya wale wanaounga mkono Mpendekezo ya Tume ya ‘’Muungano wa shirikisho la serikali tatu’’ na mpendekezo ya CCM ya ‘’Muungano wa serikali mbili’’.
Msingi wa mapendekezo ya CCM, bila kujali uwezo wa mfumo huo  wa serikali mbili kutatua kero za  Muungano, ni imani kwamba Muungano wa serikali mbili utalinda Muungano na ni matakwa ya Hati ya Muungano iliyosainiwa na Waasisi wa Taifa hili mwaka 1964. Aidha, kwa kuunganishwa kwa vyama vya TANU na ASP mwaka 1977 na hivyo kuzaliwa kwa CCM, serikali mbili imeendelea kuwa SERA muhimu ya CCM.
Maelezo haya kuwa Muungano wa serikali mbili ndiyo sera ya CCM yamekuwa yakisemwa na viongozi kila wakati, na yalipata kusikika sana mwaka 1993 pale Zanzibar ilipojiunga na OIC na hivyo kupelekea wabunge 55 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wanaotokea Tanzania Bara, kudai kuundwa kwa serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano.
Madai hayo ya wabunge yalizimwa na Mwalimu Nyerere, kwa hoja kwamba serikali mbili si SERA YA CCM na hivyo kwa ukali kabisa, Mwalimu katika kitabu chake cha ‘Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania’, kilichochapishwa mwaka 1994, akawataka wasiounga mkono SERA HIYO YA CCM, basi waondoke CCM.
Msimamo huo umeendelea kuwa moja ya sera muhimu ya CCM.
Hata hivyo, kwa uzoefu wa nchi mbalimbali duniani zenye mfumo wa vyama vingi, masuala muhimu kama Sura ya Nchi (ikimaanisha, eneo la nchi, mipaka yake, kuwepo kwa desturi na makabila mbalimbali miongoni mwa raia wa nchi); Muundo wa Serikali na Dola; Sera za Nje za Nchi na Sera za Kiuchumi (kama ni kibepari au ujamaa) huwa ni TUNU za mataifa hayo, na hivyo, hakuna chama kinachoyahodhi au hakuna chama kinachoweza kuyabadilisha au kutoyaweka katika sera zake.
TUNU ZA TAIFA hazibinafsishwi kwa itikadi za kisiasa, kidini, kikanda au kwa kundi lolote dogo ndani ya jamii ya Taifa husika.
Ni kwa msingi huu, mataifa kama Uingereza, Marekani, India, Australia nk, ambayo ni ya Shirikisho lakini yenye demokrasia ya vyama vingi, hakuna chama kinachoweza kuanzishwa na kushinda katika uchaguzi katika mataifa hayo kwa sera za kubadilisha mambo hayo.
Uingereza imeendelea kuwa UNITED KINGODOM, bila kujali chama kinachoshinda uchaguzi kama ni Labour, au Conservative au chama kingine.
Marekani imeendelea kuwa taifa la shirikisho la UNITED STATES OF AMERICA bila kujali kama ni Democrats au Republican walioshinda.
Kuna mataifa kama ISRAEL, yameweka hata LUGHA ya Taifa na makao makuu ya nchi kama mambo ambayo ni TUNU ZA TAIFA ambazo hazibadiliki kutokana na vyama vya siasa.
Katika katiba yake, Israel imesema, “… Israel is a sovereign Jewish Republic, whose Headquaters shall be UNDIVIDED JERUSALEM…”. Na imeendele kuwa hivyo kwa kuheshimiwa na kulindwa na vyama vyote vya Siasa.
Ili kufikia hatua hiyo ya kupata TUNU na SERA ZA KITAIFA mataifa hayo yalifanya hivyo kwa njia ya KURA YA MAONI KWA WANANCHI WAKE WOTE.
Hivyo, ni vema, suala kama UWEPO WA MUUNGANO na MUUNDO WAKE, likaamuliwa na wananchi wote kwa NJIA YA KURA YA MAONI, na kisha litakavyokubaliwa, litakuwa ni SERA YA TAIFA na si sera ya chama kimoja cha siasa.
Kwa mfumo tulionao wa siasa ya vyama vingi na kwa kufanya suala la muungano wa  SERIKALI MBILI kuwa ni sera ya CCM, basi tunaliweka jambo hili muhimu katika hatari ya kupotea siku CCM itakapoondoka madarakani.
Kwa kutambua uwepo wa vyama vingi na uwezekano wa vyama hivyo kushinda siku moja, ndiyo maana Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilifanyiwa marekebisho mwaka 1992 kwa kumfanya Rais wa Zanzibar asiwe makamu wa Kwanza wa Rais wa Muungano, badala yake, awepo MGOMBEA MWENZA wa urais ambaye atatoka upande wa pili wa Muungano.
Mabadiliko haya, kwa wahafidhina, walipaswa kuyakataa kwani, Hati ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1964 ilianzisha nafasi ya Makamu wa Wawili wa Rais, na ilikuwa hivyo tangu 1964 hadi 1992.
Mabadiliko hayo ya Katiba ya mwaka 1992, yalikuwa pia ni fursa ya kuweza kuweka mabadiliko mengine ya kulinda Muungano na Muundo wake wa SERIKALI MBILI kuwa TUNU ZA TAIFA na si SERA YA CHAMA KIMOJA.
Kwa kuwa fursa hiyo ya mwaka 1992 haikutumika, basi fursa tuliyonayo sasa, na haina budi itumike ili kutouweka Muungano na muundo wake kwenye mashaka ya kuvunjika kwa kuwa eti tu CCM imeshindwa katika uchaguzi.
Kufanyika kwa jambo hili pia kutafanya sera hii ikubalike na Watanzania wote. Kwa hali ilivyo sasa, hata kama SERA YA MUUNGANO WA SERIKALI MBILI NI NZURI, vyama vya siasa tofauti na CCM vitaipiga vita kwa kuwa ni SERA YA ADUI YAO KISIASA!!
Ezekiel Maige ni Mjumbe wa Bunge la Katiba
 src
Raia mwema

Ni werevu wa CCM au ujinga wa Watanzania?

Profesa Palamagamba Kabudi

Profesa Kabudi yu sahihi alichosema Zanzibar
WIKI iliyopita Profesa Palamagamba Kabudi – mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Katiba, alitoa kauli huko Zanzibar inayofikirisha.
Ni kauli inayogusa jambo ambalo limekuwa likinitatiza kwa muda mrefu kupata jibu; maana kila ninapotafakari kulikoni naishia kujiuliza swali lile lile:
Ni werevu wa chama tawala CCM au ni ujinga wa Watanzania?
Akizungumza katika kongamano la kujadili Miaka 50 ya Muungano, Profesa Kabudi aligusia kuhusu kinachoendelea kwenye Bunge la Katiba mjini Dodoma.
 Profesa Kabudi, miongoni mwa mambo mengine mazito yaliyosababisha hata TBC 1 imkatie matangazo, alisema hivi kuhusu suala la shinikizo linaloendelea la kukubaliwa kwa mfumo wa serikali mbili kinyume cha matakwa ya wananchi ya mfumo wa serikali tatu:
“Ujinga wa kizazi hiki tusidhani utakuwa ujinga wa kizazi cha kesho. Vizazi vijavyo vya Tanzania vitakuwa na ujinga wake. Ni vyema kuwawekea misingi lakini waje kuishi na ujinga wao kuliko kulazimisha ujinga wako kwa sababu wewe ujinga wako ndiyo amali yako lakini kwa wengine siyo amali.”

Maneno hayo ya Profesa Kabudi kuhusu ujinga wa kizazi chetu hiki yalinikumbusha kauli nyingine iliyopata kutolewa na Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa ya kwamba Watanzania ni wavivu wa kufikiri.
Mara nyingi (kama sio zote) mjinga ndiye huwa mvivu wa kufikiri. Kwa hiyo, kauli hizo mbili – ya Profesa Kabudi na ya Rais mstaafu Mkapa zinafanana kwa namna fulani.  Zinafanana; maana zote zinazungumzia ujinga na uvivu wa kufikiri wa kizazi hiki cha Watanzania!
Huko nyuma nilipokuwa nikitafakari mustakabali wa taifa letu, niliishia kwenye swali lile lile: Ni werevu wa chama tawala CCM au kweli ni ujinga wa Watanzania unaotokana na uvivu wao wa kufikiri?
Vyovyote vile, sasa naamini pasipo shaka yoyote kwamba, Watanzania tu wavivu wa kufikiri, na kwa sababu tu wavivu wa kufikiri, tu wajinga! Vinginevyo, mambo yasingeenenda katika nchi yetu kama yanavyoenenda, na bado mambo yakaendelea kubaki sawa tu kama yalivyo.
Chukulia mfano wa Bunge la Katiba linaloendelea na kikao chake mjini Dodoma. Watu wengi tu – wasomi na wasio wasomi wamezungumza na wameandika tena na tena na tena ya kwamba, kinachofanyika huko, hivi sasa, ni kutengeneza Katiba ya nchi inayotokana na maoni na msimamo wa CCM, na si wa wananchi.
Wameandika na kuzungumza tena na tena ya kwamba, huwezi kuyaweka pembeni maoni ya wananchi kwenye Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na iliyokuwa Tume ya Katiba kwa kuwahoji wananchi sehemu mbalimbali nchini, na kisha ukaibuka na Katiba utakayoiita  “ni ya wananchi”.
Hiyo ni hadaa. Ni hadaa kwa sababu Katiba ya wananchi haiwezi kutengenezwa na chama kimoja tu cha siasa. Ni hadaa kwa sababu Bunge la Katiba limesheheni wajumbe wa CCM tu, na mbaya zaidi wajumbe hao wameamua kuyatosa pembeni maoni ya wananchi kama yalivyowasilishwa kwenye rasimu.
Lakini kwa sababu ya ujinga wetu huo, sisi wananchi wa kawaida hatuioni hiyo kuwa ni hadaa. Maana, kama Watanzania tungekuwa ni werevu na si wajinga, tungalimshinikiza Rais Kikwete kusitisha Bunge hilo la Katiba na kuyaokoa mabilioni ya fedha za walipakodi yanayoteketea bure.
Kwa mtazamo wangu, ni mabilioni  ya pesa za walipakodi yanayoteketea bure kwa sababu, mwisho wa yote, Katiba itakayotengenezwa Dodoma katika mazingira hayo, kamwe haiwezi kuwa ni Katiba ya wananchi. Na kwa maana hiyo, haiwezi kudumu hata miaka 20 tu kabla haijatupiliwa mbali.
Kwa hakika, naweza kwenda mbali zaidi na kusema ya kuwa ingalikuwa ni katika nchi nyingine zenye demokrasia iliyokomaa na wananchi wasio wavivu wa kufikiri na wabunge wasioweka mbele maslahi yao binafsi, Rais Kikwete angelikwishapigiwa kura ya kutokuwa na imani naye, kwa sababu ya kushindwa kuilinda Katiba ya Jamhuri ya Muungano aliyoapa kuilinda wakati akiapishwa urais.
Lakini kwa sababu ya uvivu wetu wa kufikiri, hatuelewi au hatujui ya kwamba Rais Kikwete ameikosea Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kukaa kimya na kuiruhusu Zanzibar kuifanyia marekebisho Katiba yake mwaka 2010 – marekebisho ambayo yamepora mamlaka ya Rais wa Muungano (mamlaka yake), na kumfanya asiwe na nguvu zozote Zanzibar.
Kama tungekuwa si wavivu wa kufikiri (wajinga), tungelikwishadai maelezo kutoka kwa Rais Kikwete kuhusu hilo. Tungalikwishamuuliza: Alikuwa wapi mwaka 2010 wakati Zanzibar ikirekebisha Katiba na kuweka vifungu vinavyokiuka Katiba ya Muungano?
Miaka 30 iliyopita aliyekuwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamhuri, Aboud Jumbe, alishinikizwa na kikao maalumu cha NEC ya CCM, mjini Dodoma, kuachia nyadhifa zake zote kwa kosa kama hilo la Kikwete la kuudhoofisha Muungano.
Nilikuwepo mjini Dodoma mwaka huo wa 1984 nikiwa ripota wa magazeti ya CCM ya Uhuru na Mzalendo kuripoti habari za kikao hicho maalumu cha NEC ya CCM, na hivyo nafahamu mjadala uliendaje hadi Mzee Jumbe kung’olewa nyadhifa zake zote.
Katika hicho kilichoitwa “kuchafua hali ya hewa ya kisiasa”, maskini Mzee Jumbe wala yeye hakufikia hatua ya kubadilisha Katiba ya Zanzibar kama alivyoanya Rais wa sasa wa Zanzibar, Dk. Shein mwaka 2010 kwa “baraka” za Rais Kikwete, lakini bado mzee wa watu alikwenda na maji kwa kudai serikali tatu!
Leo hii, si Dk. Shein wala Kikwete ambao wamehojiwa na NEC ya CCM kuhusu mabadiliko hayo ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010 yenye vifungu vinavyodhoofisha Muungano.
Lakini hata sisi ambao si wana CCM, kwa ujinga na uelewa wetu mdogo, hatudai maelezo hayo kutoka kwa Rais wetu Kikwete na kwa Rais wa Zanzibar, Dk. Mohamed Shein.
Na mbaya zaidi, tunaukubali kirahisi uamuzi wao mwingine na wa chama chao cha CCM wa kuyatosa maoni ya wananchi katika rasimu ya Katiba yanayotaka muundo wa serikali tatu, na tunakubali kushinikizwa muundo wa serikali mbili kinyume na matakwa yetu wananchi.
Katika hoja yake ambayo ameirudia hivi karibuni, Rais Kikwete anadai ya kuwa idadi ya waliohojiwa na Tume ya Warioba haihalalishi kuhitimisha kuwa Watanzania wengi wanataka muundo wa serikali tatu.
Kwa maneno mengine, anaupigia debe mfumo wa serikali mbili ambao wala wananchi hawakuwahi kuhojiwa kama ndio wanaoupenda – mfumo ambao umekuwa ukilalamikiwa kote nchini, na hasa Zanzibar kwa karibu miaka 40 sasa!
Lakini hata kama Rais Kikwete ana hoja nzito kwamba Tume ya Warioba haikuhoji wananchi wengi, na hivyo haina haki ya kusema kuwa Watanzania wengi wanataka mfumo wa serikali tatu, bado busara si kushinikiza Bunge la Katiba liukubali mfumo wa serikali mbili.
Kwa mtazamo wangu, busara ingekuwa ni kuirejesha tena kazini tume hiyo ya Warioba na kuipa muda zaidi wa kuwahoji wananchi wengi zaidi (idadi yoyote ile anayoona yeye inatosha), lakini si kushinikiza Bunge la Katiba liukubali mfumo wa serikali mbili, na wala si kuikejeli rasimu hiyo na maoni hayo ya wananchi wanaotaka serikali tatu kama anavyofanya sasa.
Huko nyuma, Jenerali Ulimwengu alipata kuandika ya kwamba Katiba si jambo la haraka haraka, na kwamba tunaweza kuiandaa hata kwa miaka mitano.
Aliandika pia ya kwamba yale mapungufu tuliyonayo (mathalan kutokuwepo kwa tume huru ya uchaguzi) ambayo yanahitaji kutatuliwa haraka, yanaweza kushughulikiwa kwa njia za kawaida kama vile kutungiwa sheria nk; huku wakati huo huo tukiendelea na mchakato wetu wa muda mrefu wa kuandaa Katiba imara ya nchi itakayodumua miaka 100 na zaidi!
Nakubaliana naye (Jenerali) kabisa. Hakuna uharaka wowote katika kuandaa Katiba imara. Hakuna u-fastafasta katika kuandaa Katiba ya nchi.
Na ikizingatiwa utata na maajabu yaliyojitokeza mpaka sasa ya maoni ya wananchi yaliyomo katika rasimu kutoswa pembeni, sioni mantiki ya kikao hicho cha Bunge la Katiba, mjini Dodoma,  kuachwa kiendelee. Kufanya hivyo, ni kuteketeza bure mabilioni ya pesa za walipakodi nchini.
Mantiki ninayoiona mimi ni ya kurudi nyuma – yaani mchakato uanze upya; hata kama utatuchukua miaka mingine mitano kuukamilisha.
Na tena mchakato huo ukianza upya uanzie kwenye kuirekebisha Sheria yenyewe ya Mabadiliko ya Katiba – sheria  ambayo, kama sote tunavyofahamu, inampa rais mamlaka makubwa isivyo lazima na isivyo haki.
Lakini ni nani wa kumshinikiza Rais Kikwete aione mantiki hiyo ya kuvunja kikao hicho cha Bunge la Katiba linaloendelea mjini Dodoma?
Ni hawa Watanzania walio wavivu wa kufikiri, na ambao kwao mijadala kuhusu mechi za Yanga na Simba au Manchester na Chelsea ina maana kubwa kwao kuliko suala la Katiba mpya ya nchi yao?
Vyovyote vile, Rais Kikwete na CCM yake wanaweza kutumia ujinga huo wa wananchi na hatimaye kutengeneza Katiba wanayoitaka wao. Hata hivyo, tumkumbushe kwamba Katiba ya namna hiyo haitadumu miaka mingi kabla ya kutoswa; maana ujinga wa Watanzania wa leo siyo ujinga wa Watanzania wa kesho!
Nihitimishe kwa kurudia kusema ya kwamba Profesa Kabudi yu sahihi kabisa kwa tahadhari yake ile aliyoitoa Zanzibar juu ya upuuzaji huo wa maoni ya wananchi kuhusu aina ya Muungano wanaoutaka. Profesa yu sahihi alipotahadharisha
“Ujinga wa kizazi hiki tusidhani utakuwa ujinga wa kizazi cha kesho. Vizazi vijavyo vya Tanzania vitakuwa na ujinga wake. Ni vyema kuwawekea misingi lakini waje kuishi na ujinga wao kuliko kulazimisha ujinga wetu, kwa sababu ujinga wetu ndiyo amali yetu lakini kwa wengine siyo amali”!

src
Raia mwema