KWA mujibu wa gazeti la Fahamu, toleo Na. 288 la Jumanne Machi 25 – 31, 2014 katika ukurasa wa nane, Profesa Ibrahim Lipumba, kupitia makala yake ya ‘Jicho la mwanachuoni’ amedai kwamba katika kuelezea maoni ya wananchi kuhusu mfumo wa Muungano, Rais Jakaya Kikwete kwa makusudi ametumia takwimu za ujumla bila kutenganisha maoni ya Zanzibar na Tanzania Bara.
Anasema asilimia 76.3 ya maoni yaliyotolewa Zanzibar yalihusu mfumo wa Muungano wakati Tanzania Bara ilikuwa asilimia 5.6 na kwamba suala la mfumo wa Muungano ndiyo lililoongoza Zanzibar. Kwa bahati nzuri kwenye hotuba ya Jaji Warioba kwenye Bunge Maalum la Katiba takwimu hizo zinazotenganisha Zanzibar na Tanzania Bara zilitolewa kwa msingi huo anaodai Lipumba.
Hivyo ni vyema sasa tukizifanyia uchambuzi wa kisheria na kitakwimu ili tubaini ukweli uko wapi. Aidha baada ya hapo tutaonesha pia ni jinsi gani uchambuzi huo unahusiana na takwimu za Rais ambazo Lipumba kwa namna ya kushangaza anadai ni za usanii. Sheria ya kuandaa Katiba mpya imesisitiza katika kifungu cha 9(2) na imetoa mwongozo kwa Tume kuzingatia mambo kadhaa ya msingi.
Kati ya mambo hayo ni kuendelea kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano, kuwepo kwa Serikali, Bunge na Mahakama na kuendelea kuwepo kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Hata hivyo, mara baada ya kuanza kwa mchakato wa kuandaa Katiba mpya yalijitokeza makundi ya watu, Bara na Zanzibar, yaliyotaka mjadala ujikite pia katika suala la muundo wa Muungano.
Isitoshe Kulingana na hotuba ya Jaji Warioba bungeni alikubali na kueleza kuwa sheria ya Mabadiliko ya Katiba kifungu cha 9(2) imetoa mwongozo kwa Tume kuzingatia mambo kadhaa ya msingi. Kati ya mambo hayo ni “kuendelea kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano, kuwepo kwa Serikali, Bunge na Mahakama na kuendelea kuwepo kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.”
Lakini alidai kuwa mwongozo huo ulikuwa ni kwa Tume tu, sio kwa wananchi. Hivyo Mheshimiwa alibainisha kuwa Tume isingezingatia agizo hilo la sheria. Kisingizio alichotoa cha kutozingatia mwongozo huo eti ni maoni ya wananchi. Swali kubwa la kujiuliza ni je wananchi katika maoni yao walikataa kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano yenye serikali mbili?
Takwimu zilizotolewa katika hotuba ya Mwenyekiti wa Tume, Jaji Warioba katika Bunge Maalumu la Katiba kuhusu Tanzania Bara ni kama ifuatavyo. Watu wote Bara waliozungumzia Muungano ni 39,000 na kati ya hao walioukubali muundo wa serikali mbili mapema kwa maana ya kuacha kuuhoji ni watu 12,000 sawa na asilimia 30.
Halafu waliouhoji na kuuchambua ni 27,000. Katika hawa waliouchambua na kutaka serikali mbili ni asilimia 24 ya hao 27,000 ambao idadi yao ni watu wapatao 6,480. Waliotaka serikali moja ni asilimia 13 ya hao 27,000 ambao kiidadi ni watu wapatao 3,510. Waliotaka serikali tatu ni asilimia 61 ya hao 27,000 ambao kiidadi ni watu 16,470.
Mpaka hapa Tume ikajifanya haina habari na wale watu 12,000 wa Tanzania Bara walioukubali Muungano mapema bila kuuhoji. Kwa hivyo tukijumlisha watu 12,000 walioukubali Muungano bila kuuhoji pamoja na watu 6,480 waliouhoji na kuukubali idadi yao ni watu 18,480. Idadi hii ni kubwa kuliko ile ya watu 16,470 ya watu waliotaka serikali tatu.
Kwa hivyo ukweli ni kwamba kati ya watu 39,000 waliotaka serikali moja Bara ni watu 3,510 sawa na asilimia 9; waliotaka serikali mbili ni watu 18,480 sawa na asilimia 48; na waliotaka serikali tatu ni 16,470 sawa na asilimia 43. Kinachoshangaza ni kuwa ilitarajiwa Tume izingatie msingi wa wengi (asilimia 48) wape, lakini badala yake wakawapa wachache wenye asilimia 43 na kuwanyima haki walio wengi wenye asilimia 48.
Kwa upande wa Zanzibar Tume ilihoji watu 38,000. Kati ya watu hao 19,000 sawa na asilimia 50 waliukubali Muungano wa serikali mbili mapema na hivyo hawakuhoji muundo wake.
Nusu ya pili iliyobaki ya watu 19,000 ndio waliohoji na kuuchambua. Katika hiyo nusu ya pili ya watu 19,000 waliouhoji muundo huo na kukubali ule wa serikali mbili ni watu 6,460 sawa na asilimia 34; Waliotaka serikali ya mkataba ni 11,400 sawa na asilimia 60 ya waliouhoji.
Halafu waliotaka serikali moja ni watu 1,140 sawa na asilimia 6 ya waliouhoji. Mpaka hapa Tume ikajifanya tena haina habari na wale watu 19,000 wa kwanza kutoka Zanzibar walioukubali Muungano mapema bila kuuhoji. Kwa hivyo tukijumlisha wale watu 19,000 walioukubali Muungano wa serikali mbili toka mwanzo bila kuuhoji pamoja na watu 6,480 waliouhoji na kuukubali Muungano wa serikali mbili idadi yao ni watu 25,460.
Idadi hii ni kubwa kuliko ile ya watu 11,400 waliotaka mkataba. Hivyo kwa Zanzibar ukweli ni kwamba kati ya watu wote 38,000 wale waliotaka serikali moja ni watu 1,140 sawa na asilimia 3; waliotaka mkataba ni watu 11,400 sawa na asilimia 30 na waliotaka Muungano wa serikali mbili uendelee ni watu 25,460 sawa na asilimia 67.
Idadi hii ni kubwa na hivyo ya watu wengi zaidi kuliko ile ya watu waliotaka mkataba. Hivyo kwa Zanzibar ilivyokuwa wengi wape (asilimia 67) inashangaza Tume iliwapa wachache (asilimia 30) na kuwanyima wengi (asilimia 67) waliozidi na hivyo walioshinda. Hiyo ndio picha ya kwanza ambayo msingi wake ulizitenganisha takwimu za Bara na Zanzibar.
Hata hivyo msingi huo haukuitazama Tanzania kwa ujumla wake. Hebu sasa tuitazame Tanzania kwa ujumla wake na tuone takwimu zote walizopokea Tume zilikuwa na taswira ya namna gani. Kwa kunukuu maneno ya Rais Kikwete ya tarehe 21 Machi 2014 alipolihutubia Bunge Maalumu la Katiba alisema, na ninanukuu, “Tume imetoa sababu mbili kubwa za kupendekeza muundo wa serikali tatu.
Sababu ya kwanza ni kwamba ndiyo matakwa ya Watanzania wengi kote Zanzibar na Tanzania Bara.Inaeleza kuwa idadi kubwa ya Watanzania waliotoa maoni, yaani asilimia 60.2 wa kutoka Zanzibar wanaunga mkono muundo wa serikali ya mkataba, na asilimia 61.3 wa kutoka Tanzania Bara wanaunga mkono muundo wa serikali tatu.
Sababu ya pili ni kwamba muundo huo unatoa majawabu ya uhakika na endelevu kwa changamoto za muundo wa sasa wa serikali mbili zinazonung’unikiwa na watu wa pande zetu mbili za Muungano.
“Mheshimiwa Mwenyekiti; Sababu hizi mbili kuu zilizotolewa na Tume zimezua mjadala mkali katika jamii. Wapo wanaokubaliana na Tume na wapo wasiokubaliana nayo. Wapo wanaosema Tume imesema kweli kwamba Watanzania wengi wanaunga mkono muundo wa serikali tatu, hivyo muundo wa Serikali tatu hauepukiki. Ndiyo matakwa ya wengi hivyo msemo wa Kiswahili usemao wengi wape uheshimiwe.
“Lakini wapo wanaodai kuwa takwimu za Tume hazioneshi ukweli huo. Wanasema kuwa taarifa ya Tume imeonesha kuwa Watanzania waliotoa maoni yao kwa Tume kwa mdomo na maandishi walikuwa 351,664. Kati yao ni wananchi 47,820 au sawa na asilimia 13.6 ndiyo waliokerwa na muundo wa Muungano hivyo wakauzungumzia.
Wananchi 303,844 au sawa na asilimia 86.4 muundo wa Muungano kwao halikuwa tatizo, ndiyo maana hawakuuzungumzia kabisa (yaani wanataka huu wa serikali mbili uendelee). Wanahoji kuwa iweje leo asilimia 13.6 ya Watanzania wote waliotoa maoni wageuke kuwa ndiyo Watanzania walio wengi?
“Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasema pia, kwamba mbona Taarifa ya Tume yenyewe, kuhusu takwimu (uk. 66 na 67), inaonesha kwamba kati ya hao watu 47,820 waliotoa maoni kuhusu Muungano, ni watu 17,280 tu ambao ni sawa na asilimia 37.2 ndiyo waliotaka muundo wa Serikali tatu, asilimia 29.8 walitaka Serikali mbili, asilimia 25.3 walipendekeza serikali ya mkataba na asilimia 7.7 walipendekeza serikali moja.
Hii hoja ya Watanzania wengi kutaka serikali tatu msingi wake upi? “Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu za Tume (uk. 57) zinaonesha, vilevile kuwa Tume ilipokea maoni 772,211. Kati ya hayo asilimia 10.4 tu ndiyo yaliyozungumzia muundo wa Muungano na asilimia 88.6 hayakuzungumzia Muungano bali mambo mengine.
Hivyo basi wanahoji pia kwamba kama muundo wa Muungano ungekuwa ni jambo linalowakera Watanzania wengi, lingedhihirika kwenye idadi ya watu waliotoa maoni na kwenye idadi ya maoni yaliyotolewa. Yote hayo hayakujitokeza. Waliouzungumzia Muungano walikuwa asilimia 13.6 tu ya watu wote waliotoa maoni na maoni yanayohusu Muungano yalikuwa asilimia 10.4 ya maoni yote.
Hivyo basi, wanauliza “usahihi wa hoja ya Watanzania wengi kutaka serikali tatu uko wapi?” Kutokana na uchambuzi huo ni dhahiri kuwa kisheria Tume haikuzingatia sheria mara mbili kwa pande zote mbili za nchi yetu. Kwanza ilipuuza sheria kwa kuwanyima wengi haki yao na kuwapa wachache.
Pili, Tume ilikataa kufuata mwongozo wa sheria ulioitaka izingatie kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano na kuwepo kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo kimuundo huendeshwa kwa msingi wa serikali mbili. Hivyo inaelekea Tume iliteleza na hivyo kupotosha wananchi kwa kutoa takwimu zisizo sahihi.
Lakini jambo kubwa na la maana zaidi linahusu mkabala wa mwanachuoni, Profesa Lipumba ambaye anafikiri kuwa watu hawajui mahesabu na kwamba hawazijui takwimu zilizotenganisha Zanzibar na Tanzania Bara kama zilivyotolewa na Jaji Warioba kwenye Bunge la Katiba.
Hivyo baada ya maelezo hayo, je msanii sasa ni nani baina ya Lipumba na Rais wetu na hasa baada ya Lipumba kudai katika makala yake kwamba eti ni hatari kuwa na Rais Msanii? Kutokana na hali hiyo kitendawili chetu sasa kinakuwa hivi: “Ni hatari kubwa kuwa na Profesa wa Uchumi Msanii.”
Makala haya yameandikwa na Mtanzania anayejiita Mzalendo.
Anapatikana kwa simu namba +255 778 101 047