Tuesday, April 1, 2014

Wajumbe Bunge Maalumu la Katiba changanyeni akili

WAPO wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) walioambiwa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wasigombee ubunge kwa tiketi ya chama hicho cha upinzani bali wajiunge na CCM ili wawe na uhakika wa kuupata ubunge.
Baada ya kuutafakari ushawishi huo, wabunge hao waliamua kuchanganya akili zao na zile za kuambiwa na kubaki CHADEMA ambako walifanikiwa kuupata ubunge.
Wapo baadhi yao waliamua kutumia akili za kuambiwa bila kuchanganya zao na matokeo yake waliusikia ubunge kwenye bomba, hawa walipoingia CCM waliondolewa kwenye kura za maoni.
Wagombea hao sasa hawana tofauti na karai la zege ambalo kazi yake ni kujenga nyumba lakini mwisho linatupwa nje kama takataka.
Kwa kawaida akili za kuambiwa usipochanganya na zako ni maafa, lakini ukichanganya na zako mara nyingi huwa na manufaa makubwa sana.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) hivi sasa kinatumia nguvu na fedha kuwalazimisha watu waamini kuwa muundo wa serikali tatu ni balaa au laana.
Wanataka watu waendelee kuwa kwenye mfumo wa serikali mbili ambayo kwa miaka mingi sasa wananchi wanalalamikia kile kinachoitwa kero za muungano na kufutika kwa taifa la Tanganyika lililoungana na Zanzibar kuzaa Tanzania.
CCM wanawalazimisha wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba waunge mkono serikali mbili na kura ya wazi, badala ya Rasimu ya serikali tatu  na kura ya siri, kama wajumbe hawa wasipo changanya akili za kuambiwa na zao taifa linaelekea kubaya.
Simba mmoja anayeongoza kundi la kondoo 100 katika vita, ana ushindi mkubwa kuliko kuni la simba 100 wanaoongoza kondoo mmoja.
Simba hao ni pamoja na wale Wana CCM wasiokubali kutekeleza matakwa ya chama chao ilhali hawayaamini. Hawa wanataka Tanganyika yao na kamwe hawaogopi vitisho.
Ingawa wako kondoo 100 wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) wenye wajumbe wengi wa kutoka upinzani wanapambana na CCM wanaoongozwa na hisia mbaya juu ya muundo wa serikali tatu.
CCM hawataki kusikia jina la Tanganyika, sijui jina hili limewakosea nini wakati Zanzibar wanaendelea na jina lao tena sasa wameamua kuandika Katiba yao inayowatambua kama ni nchi na si sehemu ya Jamuhuri ya Muungano kama ilivyo kwenye Katiba ya 1977.
Mbunge wa Kahama na Mwenyekiti  wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli (CCM), yeye si miongoni mwa wasioitaka Tanganyika, amepaza sauti yake kulilia taifa lake.
Wanachokifanya wajumbe wengini kutoka CCM ni sawa na aliyekimbilia mjini na kuanza kuwakataa wazazi wake waliomzaa, eti kwa sababu tu amekutana na waliomshauri kwa kumwambia fanya hivi na fanya kile bila kuchanganya na akili yake.
Ni wakati muafaka sasa Watanganyika tusimkatae baba na mama yetu, Tanganyika aliyetuzaa na kutukuza, eti kwa sababu Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeamua kufia kwenye hoja yake ya muundo wa Muungano wa serikali mbili.
Vikao vya juu vya chama hicho – Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na Kamati Kuu (CC) – vilivyofanyika mwezi uliopita mjini Dodoma, vimesisitiza umuhimu wa kuendelea na muungano wa serikali mbili, kwa madai kuwa hiyo ndiyo sera ya chama hicho.
Hata andishi la CCM, lililowasilishwa kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba, limepinga mapendekezo ya kuwapo kwa serikali tatu ndani ya Jamhuri ya Muungano.
Andishi linasema, mwarobaini wa matatizo ya Muungano si kuwapo kwa serikali tatu bali serikali mbili.
Katika kutetea mfumo wa serikali mbili, chama hicho kimejikita kwenye hoja tatu:
Kwanza, muundo wa muungano wa serikali tatu ni kinyume cha makubaliano yaliyofikiwa Aprili 1964 na waasisi wa Muungano, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Aman Karume.
Pili, Muungano wa serikali tatu utaongeza gharama serikalini; utaingiza nchi kwenye umaskini na utasababisha Zanzibar kushindwa kuchangia uendeshaji wa serikali ya pamoja. Hoja inayojengwa ni kwamba mapato ya Zanzibar ni madogo ukilinganisha na Tanganyika.
Tatu, mfumo wa Muungano wa serikali tatu, si sera ya chama hicho tawala. Kinasema sera ya CCM ni serikali mbili kuelekea serikali moja. Inadai kuwa mfumo wa serikali tatu unahatarisha uhai wa Muungano.
Ukichunguza hoja hizi za kupinga muungano wa serikali tatu na utetezi wa serikali mbili, waweza kuona jinsi chama hiki kinavyozeeka kwa kasi; kinashindwa kufikiri, kuchambua na kutafiti.
Sioni sababu kwa wajumbe wa Bunge Maalumu, kuendelea kusikiliza ngonjera za wakubwa bila kuchanganya akili zao, Katiba tunayoitengeneza sasa si ya chama chochote cha siasa.

src
Tanzania Daima