DHANA ya utawala bora ni dhana pana kwa tafsiri yake.
Kiuchumi dhana hii inajumuisha hali ya utengemavu wa kudumisha amani na utawala wa haki ili kutoa mazingira wezeshi yanayoweka misingi muhimu ya kuwezesha uzalishaji mali, uwekezaji, ukuaji wa uchumi na maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Kiuchumi, matunda ya kuwa na utawala bora ni mapana, mojawapo ni kuweza kupunguza umaskini wa kipato na kuongeza ubora wa maisha ya wananchi.
Kwa kutambua hili, moja ya misingi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, kati ya misingi minne ya utekelezaji wake, inahimiza uimarishaji wa utawala bora na uongozi wa haki na kisheria ikiwa ni pamoja na jamii kukataa rushwa, kuimarisha mifumo ya uongozi na utawala ili kuweza kufikia malengo makuu ya dira hiyo.
Misingi mingine mitatu ya dira hiyo ya maendeleo ni pamoja na kudumishwa kwa utulivu wa uchumi kwa kuzingatia misingi ya uchumi kama vile kudhibiti mfumuko wa bei, kuhakikisha ukuaji endelevu wa uchumi, na ujazi sawia wa fedha; na kuzingatia ufuatiliaji wa masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabia nchi yanayoongezeka kutokana na ukuaji wa miji na utekelezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu. Pamoja na kuhakikisha matumizi bora ya ardhi kwa makazi ya binadamu na uzalishaji.
Akitilia mkazo umuhimu wa utawala bora wakati akiwasilisha Bungeni Taarifa ya Hali ya Uchumi kwa Mwaka 2012 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2013/14, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu Stephen Wasira alisema kuwa katika kuhakikisha kasi ya ukuaji wa uchumi katika viwango vya juu na endelevu, kuimarisha utawala bora na uwajibikaji kwa kila mwananchi kutii sheria bila shuruti na kufanya kazi kwa bidii na maarifa ni suala lazima.
Kwa kuzingatia umuhimu wa utawala bora katika ukuaji wa uchumi, Serikali imekuwa ikihuisha mikakati yake ya kuhakikisha inafikia vigezo vya kimataifa vya utawala bora. Kwa kutambua hili tarehe 26 Mei 2004, Tanzania ilisaini mkataba wa awali wa makubaliano ya kujiunga na mchakato wa APRM na kuridhiwa rasmi Julai 08, mwaka huo huo.
Lengo la msingi la APRM ni kuhimiza utumiaji wa sera, viwango na miendeno inayokubalika kitaalamu ili kujenga utengamano wa kisiasa, ukuaji chanya wa uchumi, maendeleo endelevu na kuharakisha ushirikiano wa kiuchumi wa kikanda na hatimaye bara zima.
Pia, APRM inatoa fursa ya kuchangia katika kudumisha utengamano, kuleta maendeleo pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kikanda kwa njia ya kubadilishana uzoefu na kuiga mifano bora ikiwa ni pamoja na kutambua udhaifu na kutathmini mahitaji ya kuongeza uwezo wa serikali na nchi.
Hivi karibuni Katibu Mtendaji wa Mpango huu (APRM) nchini Tanzania, Bibi Rehema Twalib alitoa taarifa kuwa Tanzania ni moja ya nchi zinazofanya vizuri katika utawala bora Barani Afrika. Kwa mujibu wa Bibi Twalib, Tanzania imepata mafanikio katika maeneo ya Usimamizi wa Uchumi, Maendeleo ya Uchumi- Jamii Demokrasia na Utawala Bora, Siasa, Uendeshaji wa Kampuni na Masuala Mtambuka kama Afya.
Bibi Twalib aliongeza kuwa Tanzania kupitia APRM, imefanya tathmini yake katika maeneo hayo na kuwasilisha ripoti yake mbele ya wakuu wa nchi wanachama na kujadiliwa. Akizungumzia mikakati iliyopo katika kuhakikisha kuwa malengo ya APRM yanakuwa chachu ya kukuza uchumi wa nchi.
Bibi Twalib anasema kuwa APRM kupitia Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania inaendelea kuendesha tathmini ya utendaji wake na vyombo vyake kwa uwazi, ukweli na umakini, kulingana na vigezo vilivyowekwa kwenye Mpango wa Kujipima kwa kutumia Vigezo vya Utawala Bora.
“Kwa kutambua umuhimu katika kuimarisha utawala bora, Sekretarieti inaendelea kutekeleza Mpango kazi wa kitaifa wa kujitathmini katika masuala ya utawala bora (African Peer Review Mechanism - National Plan of Action, APRM-NPoA),” aliongeza Bibi Twalib. Kwa mujibu wa APRM-NpoA, moja kati ya manufaa ya ya utekelezaji wa Mpango huu ni kubaini mambo mazuri juu ya utawala bora nchini Tanzania hali inayoongezea imani (confidence) wawekezaji toka nje ya nchi na wabia wa maendeleo.
Hili moja ya mafanikio ya APRM, maana kwa mujibu wa takwimu kutoka Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC) mpaka kufikia mwezi Desemba, 2013 kilifanikiwa kusajili miradi 9,442. Akizungumzia nafasi ya wananchi katika Mchakato huu, Bibi Twalib anasema kuwa, kwa kuwa APRM ina njema ya kupanua wigo wa demokrasia, na kuwapa wananchi kauli katika maamuzi yanayohusu mustakabali ya nchi yao.
“APRM Tanzania inategemea kuwa wananchi watatumia kikamilifu, nafasi inayotolewa ili kutoa tathmini yao ya kweli, kuhusu yale wanayoyaona kuwa ni mapungufu ya utendaji serikalini na mapungufu ya utawala bora nchini kwa ujumla, ili kuiwezesha serikali nayo kuyabaini mapungufu hayo na kuyachukulia hatua muafaka” anasihi Bibi Twalib.
Anaongeza kuwa ikiwa wananchi watatumia vyema fursa hizi vizuri, ndipo malengo ya kuanzishwa kwa Mchakato huu yatakapotekelezwa.
Kama alivyowahi kusema Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad kuwa matokeo ya Mpango huu yatakuwa na mafunaa zaidi kwa wananchi wa Tanzania, pale yatakapogusia kwa kina maendeleo ya kukuza demokraisa na haki za raia, ikiwemo yale yanayozua mashaka na kuwepo dhana kwamba baadhi ya watu wanakosa haki zao.
Kwa mujibu wa Maalim Seif, kuwashilikisha wananchi na wataalamu wengine katika Mchakato ni muhimu kwa utulivu na amani ya Tanzania katika siku zijazo, hivyo, ni lazima wananchi wapewe nafasi ya kujadili na kutoa ushauri juu ya mambo hayo, na baadaye serikali na wadau wote waweze kuchukua hatua zinazofaa.
Hivyo basi, kwa kuzingatia umuhimu wa Mchakato huu katika kufikia lengo la msingi la Dira ambalo ni kuiwezesha Tanzania kufikia hadhi ya nchi zenye kipato cha kati (Middle Income Country) ifikapo mwaka 2025, ni muhimu kudumisha utengamano, ili kuleta maendeleo pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kikanda kama njia ya kubadilishana uzoefu ili kuiga mifano mizuri kutoka nchi zilizopiga hatua kiuchumi.
Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ilikamilika kuandaliwa mwaka 1999, kama chombo cha kutuongoza katika kufikia maendeleo ya uchumi na ustawi wa jamii kwa robo karne ya kwanza ya karne ya 21. Malengo mahsusi ya TDV 2025 ni pamoja na kumwezesha kila Mtanzania kuishi maisha bora na mazuri, pamoja na kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kuwa na amani, utulivu na umoja.
Malengo mengine mahsusi ya Dira hiyo ambayo inatekelezwa kwa kupitia Mipango ya maendeleo wa miaka mitano mitano ni pamoja na kujenga msingi wa utawala na uongozi bora, kujenga jamii iliyoelimika na inayopenda kujifunza, kujenga na kuendeleza uchumi imara, unaoweza kuhimili ushindani.
src
Habari Leo