KONA ya Kivazi, leo imeamua kuja kivingine, ambapo inawageukia wasanii wa kiume wanaong’aa kutokana na upangiliaji mzuri wa mavazi, unaokwenda kulingana na wakati uliopo na hivyo kuwafanya kuvutia kila wanapoonekana.
Wasanii hao wameelezwa kwa nyakati tofauti na wadau mbalimbali kuwa wanapigilia nguo na mitindo yao tofauti tofauti hadi kusababisha baadhi ya wasanii wengine kuiga mitindo hiyo kutoka kwao.
Diamond
Ni kati ya msanii ambaye kila anapokuwa na onyesho, mashabiki wanakuwa na hamu kutaka kujua atapanda na vazi gani.
Ni kati ya wasanii ambao wamekuwa wakipangilia mavazi kutokana na sehemu husika, ambapo hata kama ni msibani bado anaonekana kuwa nadhifu.
Ama kwa hakika, naweza kumwita ni mbunifu, pia anayeumiza kichwa kwa kufikiri kabla ya kuvaa. Na kama haitoshi, hivi karibuni anatarajia ‘kupaisha’ nguo zenye nembo ya WBC.
Hemed Suleiman ‘PHD’
Huyu si mwanamuziki tu, bali pia ni mwigizaji ambaye ama kwa hakika, akivaa nguo hupendeza na anaonekana kuvutia.
Msanii huyu, mara nyingi hupenda kuvaa makoti ya kifungo kimoja yanayobuniwa hapa nchini na mbunifu wa mavazi, Martin Kadinda na kumfanya kupendeza wakati wote.
Hemed amezidi kuonekana kung’aa kutokana na rangi ambazo amekuwa akizichagua, ambazo ni za kung’aaa, na hivyo hata kama mahali kuna watu wengi, yeye hujikuta akionekana zaidi.
Huyu naye anastahili sifa ya pekee, hasa katika kujiweka nadhifu na mwenye kupangilia mavazi kulingana na wakati aliopo.
Jux
Msanii huyu ambaye anatamba na kibao cha ‘Uzuri Wako’ kilichopigwa ‘stop’ na Basata hivi karibuni, amekuwa kati ya wasanii wanaofuatiliwa mavazi yake na watu mbalimbali.
Kutokana na rangi yake na urefu alionao, kila nguo anayoivaa anaonekana kupendeza.
Kinachomuongezea nakshi zaidi, ni pale anapotupia na urembo wa ziada kama saa, cheni za mkononi na shingoni.
Gelly wa Rhymes
Gelly ambaye ni mwigizaji na pia mwanamuziki, amekuwa akivutia katika mavazi yake kiasi cha kutumiwa na wanamitindo mbalimbali katika shoo za mavazi.
Msanii huyu ambaye alijaribu kuingia kwenye muziki wa miondoko ya mduara na baadaye kurudi kwenye Bongo fleva, watu wamekuwa wakimsifia uvaaji wake, hasa anapokuwa ametupia pensi au jinzi na fulana.
src
Tanzanai DAIMA