Anatamba na kibao ‘Skelewu
Kwa hapa Tanzania, amemuwezesha msanii Nassib Abdul ‘Diamond’ kutamba katika vituo mbalimbali vya redio na televishani nchini Nigeria na Channel O, kwa kupitia kibao alichomshirikisha cha ‘My Number One’.
Jina la Davido kwa hapa nchini limepata umaarufu zaidi baada ya kutoka na wimbo wake unaokwenda kwa jina la ‘Skelewu’ ambao umefanikiwa kupendwa na wapenzi na mashabiki lukuki wa burudani.
Davido alionesha kwamba hakubahatisha kazi hiyo, ambapo kwa sasa ameachia nyingine inayofanya vema ikijulikana kwa jina la ‘Aye’.
Pamoja na kwamba wengi wanadhani jamaa huyo ni msanii mpya, lakini mwenyewe anasema kuwa fani ya muziki aliianza tangu mwaka 2009, lakini akakaza zaidi mwaka 2011.
ALIKOTOKA
Davido ambaye alizaliwa Novemba 21, 1992 Atlanta, Georgia, Marekani, anaeleza kuwa historia yake ya muziki ilianzia katika kundi lake la KB International nchini Marekani, lakini hakuweza kufanya nalo kazi muda mrefu kutokana na familia yake kurejea nchini Nigeria.
Davido aliyezaliwa na baba, Chief Deji Adeleke ambaye ni mfanyabiashara mkubwa na mama yake ambaye ni marehemu, Dk. Vero Adeleke, aliyekuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu, hakubahatika kufuata nyayo za wazazi wake.
Kielimu, Davido ni msomi wa Shahada ya Biashara na Utawala aliyohitimu Chuo Kikuu cha Oakwood nchini Nigeria na amefanikiwa kuishi na familia yake katika miji mbalimbali Marekani, Uingereza na Nigeria.
Anasema kuwa wakati aliporudi Nigeria akitokea Marekani, alikuwa kijana mdogo aliyekuwa mikononi mwa wazazi na kuendelea kufanya muziki.
Alipenda kuwa karibu na wasanii wakubwa, kiasi cha wengi kufikiria kwamba alikuwa akitokea kwenye kundi la kina Wande Coal na Don Jazzy.
“Nimekuwa nikiulizwa kuhusu wasanii hao na jibu langu huwa nawaeleza kuwa wasanii hao wamekuwa washauri wa kazi zangu,” anasema.
Anaongeza kuwa kwake Wande Coal ni sawa na kaka yake mkubwa, kwani alimfahamu miaka minne iliyopita, kabla hata ya kuachia kazi yake ya kwanza.
Pia anamtaja msanii Shank, kama ndugu yake wa karibu, kwa sababu amekuwa miongoni mwa wale waliomtambulisha katika sanaa ya muziki.
Davido anakiri kwamba pamoja na kuanza muda mrefu muziki, lakini ameanza kung’aa mwaka 2011, baada ya kuachia kazi yake ya kwanza katika studio za HKN Music iliyojulikana kama ‘Dami Duro’, akiwa ameshirikiana na kaka yake, Adewale Adeleke.
Uwezo wake wa kuimba vizuri ulimsaidia kupata ‘dili’ kibao, ikiwamo Aprili 2012 ya kusaini kufanya kazi na Kampuni ya MTN Nigeria.
Mwaka uliofuata, alifanya onyesho kabambe akiwa ameshirikiana na Kampuni ya Guinness ambalo lilipewa jina la Guinness World of More.
Ubora wake katika muziki umemuwezesha kutwaa tuzo kibao ikiwamo ya Kora, Channel O, Nigeria Music Video, tuzo tatu za Headies, tuzo nne za Nigeria Entertainment, na tuzo mbili za Dynamix All Youth na nyingine kibao.
Mwaka 2012 ulikuwa mzuri kwake kwani ndipo aliachia albamu yake ya kwanza iliyokwenda kwa jina la ‘Omo Baba Olowo’ ikiwa na kazi kama ‘Back When’ aliomshirikisha Naeto C, ‘Dami Duro’, ‘All of You’, ‘Overseas’ akimshirikisha Sina Rambo, ‘Ekuro’, ‘Gbon Gbon’ na ‘Feel Alright’.
Kwa sasa yuko katika maandalizi ya albamu yake ya pili ambayo ameshatoa kazi zake za utangulizi.
Mwaka 2013, Davido alianza mikakati ya kuachia albamu hiyo na wimbo wake wa utangulizi ni ‘Gobe’ ambao video yake imetengezwa nchini Afrika Kusini.
Davido aliachia wimbo mwingine uliojulikana kama ‘One of a Kind’ ambao video yake imetengenezwa na muongozaji wa Afrika Kusini wa studio za Tebza of Godfather.
Wimbo wake wa tatu wa ‘Skelewu’, umefunika kabisa kwa kushika nafasi ya kwanza katika chati za nyimbo 100 za Afribiz.
Februari 2, 2014, Davido ameachia kazi yake ya nne inayokwenda kwa jina la ‘Aye’ , iliyotengenezwa na T Spice.
Katika moja ya mafanikio yake makubwa aliyoyapata ni pale Aprili 6, 2012 aliposaini dili la Naira milioni 30 (fedha za Kinigeria) na Kampuni ya luninga ya MTN na Oktoba 24, 2013 alisaini mkataba na Kampuni ya Guinness.
MIKASA
Agosti 12, 2012 Davido aliingia kwenye matatizo na dereva teksi mmoja anayejulikana kama Femi Ajibola, aliyemlalamikia kumpiga akimtuhumu kutembea na ‘demu’ wake.
Ajibola alisimulia mkasa huo akisema kuwa siku moja alipigiwa simu na binti mmoja aliyekuwa akitaka teksi na alipofika, alikuta hali ya kutoelewana kati yake na Davido.
Mwanadada huyo alipoingia garini, alisababisha apigwe na Davido kibao kisha kipigo kikahamia kwa dereva huyo aliyepigwa na wapambe wanne wa msanii huyo.
Dereva huyo alikwenda kulitolea taarifa polisi tukio hilo akidai pia kupoteza kiasi cha Neira 100,000 garini zilizokuwa makusanyo ya siku.
Ajibola anasema kuwa alishangazwa na dada huyo kukana kupigwa na Davido.
Davido alijibu tuhuma hizo kwa kusema kuwa malalamiko hayo hayakuwa ya msingi zaidi ya kuwa na nia ya kumuharibia na kulenga kumshusha
src
Tanzania Daima