KILA mmoja anapaswa kutamani kuwa kiongozi ili aweze kujenga uwezo wa kuwa na maendeleo binafsi, pasipo kutamani maendeleo ya mtu mwingine, kwa sababu hakuna atakayemlazimisha mtu mwingine kupata mafanikio.
Lakini kwa upande mwingine, suala la mafanikio ni jambo linalotokana na muda uliopo, kujitoa na kufanyia kazi mambo mbalimbali unayoyapanga.
Hakuna mtu atakayekulazimisha kupata mafanikio, bali inakupasa kufanya bidii binafsi ili ufikie matarajio ya juu uliyojipangia.
Haya yakizingatiwa, kila mmoja atakuwa na ari ya kujisimamia kufanya kazi kwa bidii katika mipango mbalimbali ya maendeleo ya ukuaji wa uchumi.
Sasa basi ili uweze kukua na kupata maendeleo, inakupasa kila jambo unalolipanga uweze kulitekeleza.
Ni vema kuanza kufanya jitihada binafsi za kupata maendeleo, pamoja na kufanya tathmini ya hapo ulipo na ulipotoka, taratibu utajikuta unapiga hatua siku baada ya siku.
Kwa kuwa tayari unayo maabara iliyosheheni kila hitaji la mwanadamu, unayotakiwa kuichunguza na kuifanyia kazi, ni vema kujibidiisha ili uweze kukitumia kila kifaa kilichopo ndani yake, kwa ajili ya maendeleo.
Hakuna kikwazo chochote katika maabara hiyo kinachoweza kukukwamisha, kama utajitambua kama wewe ni mhusika mkuu katika maabara hiyo, ni wazi utapenda kujua kazi ya kila kifaa.
Kwa kuwa ndani ya maabara hiyo hakuna kitu cha kununua, kodi ya kulipa, wala ada ya aina yoyote, unaweza kuitumia vile unavyopenda bila malipo yoyote.
Kama wewe ni msimamizi katika maabara yako mwenyewe, utapenda kufanya vile wanasayansi wengine wanavyofanya.
Unaweza kushangaa kwanini watu wengi wana uelewa mdogo wa kufikia mafanikio, wakati wanazungukwa na wenye mafanikio makubwa.
Hii ni kwa sababu watu wengi hawafuatilii mambo yanayofanywa na wengine ili kufikia malengo makubwa.
Kuna uchaguzi wa aina mbili wa kukusaidia ili uweze kufanikiwa; mojawapo ni kupenda kujifunza kwa kuchunguza kila kitu unachokiona na kuamini kuwa kinaweza kukupatia maendeleo.
Pia unaweza kuchagua mifano ya watu wawili unaoweza kuwatumia kwa ajili ya kujifunza katika kupata mafanikio yako.
Unatakiwa kuwachagua watu ambao mmoja wao, amefanikiwa na mwingine ambaye hajafikia mafanikio, ambao unawajua vema.
Anza kufuatilia kila jambo wanalolifanya, utapata somo litakalokufumbua macho.
Kila unachojifunza kwa watu hao, kinakuwezesha kupiga hatua zaidi, lengo lako likiwa ni kuangalia kanuni za kufikia mafanikio.
Pia kwa kutumia mifano ya watu hao, ndivyo utakavyopata mbinu mpya za kukabiliana na changamoto za maisha kufikia mafanikio.
Ni jambo la kufurahisha unapokuwa na ujasiri na kufanikiwa kila unachopanga, kujiangalia unavyokuwa siku baada ya siku na mwezi baada ya mwezi.
src
TD