TANZANIA ni moja ya nchi ambayo haina wachezaji wanaocheza soka la kulipwa kwenye nchi kubwa zenye ligi ya kiushindani kama vile England, Hispania, Italia, Ujerumani, Uholanzi, Ufaransa na nchi nyingine zilizoendelea kisoka hasa zile za Ulaya.
Yaelekea Ulaya ni kugumu kwa wachezaji wa Kitanzania kupata nafasi ya kucheza soka la kulipwa kwenye ligi hizo zenye majina makubwa na mapesa lukuki.
Nakumbuka mwaka 2009 wakati kiungo mshambuliaji wa timu ya Yanga na timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Mrisho Ngasa alipopata nafasi ya kwenda kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa kwenye timu ya West Ham United ya Mashariki mwa London, ilikuwa ni shangwe kwa kila Mtanzania ila baadaye shangwe hiyo ikaingia nyongo baada ya kuikosa nafasi ile.
Shangwe hiyo ya wapenda soka wa Tanzania waliona nafasi hiyo ni kama ingefungua mlango kwa wachezaji wengi wa Kitanzania kama yeye angefanikiwa kuipata na kuonesha ulimwengu kuwa hata Tanzania wapo wachezaji wazuri kama nchi nyingine za Afrika.
Sasa lazima tuwe wawazi na wa kweli, ni ngumu tena ngumu kwa wachezaji wa Kitanzania kupata nafasi ya moja kwa moja kwenda kucheza soka kwenye klabu hizo za kwenye ligi ya ushindani kama vile England na sasa basi mimi naona tuangalie pande zingine ambazo zitakuwa rahisi kwao kwenda kucheza soka ya kulipwa na pia inaweza ikawa njia yao ya kwenda barani Ulaya kusaka mafanikio.
Pande hiyo ni pande ya nchi za Mashariki ya Mbali kama vile China, Japan na hata Korea Kusini au kwa ujumla niseme barani Asia, ambako hivi sasa ligi zake zimeanza kujijengea jina tayari na ninaposema hivi tayari wachezaji lukuki kutoka nchi za Afrika Magharibi wameshaanza kumiminika kutafuta nafasi kwenye klabu mbalimbali za Mashariki ya Mbali hasa kwenye nchi za China, Japan na Korea Kusini.
Licha ya hao, wapo pia wachezaji kutoka Amerika ya Kusini kwenye nchi kama vile Argentina na Brazil nao tayari wameanza kuingia kwenye nchi hizo kwa ajili ya kucheza soka na kwa hili, ujue kwamba hivi sasa huku nako ni sehemu nzuri la kucheza soka la kulipwa.
Kwa mfano, kwenye ligi ya soka ya China (Chinese Super League (CSL), tayari majina makubwa kwenye soka duniani yameshaanza kuingia na kama mnakumbuka tayari wachezaji kama Didier Drogba na mwenzake Nicholaus Anelka walishatua kwenye Jiji la Shanghai kuichezea timu ya Shanghai Shenghua kabla ya kutimka zao kurejea Ulaya.
Drogba aliondoka kwenye timu ile baada ya kutokea kutokuelewana na wakuu wa timu hiyo pia kwa namna nyingine tunaweza kusema ligi ya China si ya kiwango chake ila ligi hii ni ya kiwango cha wachezaji wale wanaotaka kujijengea jina na kujiimarisha zaidi na baadae kwenda kutimkia Ulaya kwenye timu kubwa na ligi kubwa za huko na wachezaji hao ni kama wachezaji wetu wa Kitanzania ambao wengi wao wapo nyumbani wakicheza kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara na ile Ligi Kuu ya Zanzibar.
Kwa hiyo inabidi wachezaji wetu waanze kutupia macho huku Mashariki ya Mbali kuliko barani Ulaya, huku ninaweza kusema kutatoa maana hata baadhi ya klabu kubwa Ulaya zimeanza kutupia macho huku na kwa nyakati tofauti zimekuwa zikija kwa ajili ya maandalizi yao kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi.
Lakini kwa wao dhumuni lao kubwa si la kisoka sana, bali ni la kibiashara na kujitangaza kimataifa hiyo inatokana na nchi zake kuwa na uchumi mzuri hivi sasa kuliko hata baadhi ya nchi za Ulaya na Amerika.
Kiukweli kabisa huku Mashariki ya Mbali ni kuzuri kwa maslahi ya wachezaji wenyewe maana malipo yao ni mazuri tofauti na malipo wanayoyapata kwenye klabu za hapo nyumbani Tanzania na hata soka lake kiukweli kwa sasa limebadilika tofauti na fikra za watu kuwa soka la nchi za Asia ni la kiwango cha chini.
Kwa mfano, ligi ya hapa China ndio imetoa bingwa wa michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Asia kwa mwaka 2013, bingwa ni timu ya Guangzhou Evergrande inayofundishwa na kocha wa zamani wa timu ya Taifa ya Italia, Marcello Lippi.
Hii timu ya Guangzhou Evergrande ipo kusini mwa China kwenye mji maarufu wa kibiashara wa Guangzhou ambao huko nyumbani Tanzania ni mji maarufu (Gwanzu) kutokana na Watanzania wengi kuja kufanya manunuzi ya kibiashara.
Kwa kweli hii timu ni moja ya timu kubwa barani Asia ambayo imewekeza kwa mabilioni ya Yuan (Fedha ya China) na ina wachezaji hadi kutoka Ulaya. Kwa mfano, mchezaji wa zamani wa timu ya West Ham United ya England na Bologna ya Italia na timu ya Taifa ya Italia, Alessandro Diamanti amejiunga na timu hii ya Guangzhou Evergrande kwa msimu huu wa Ligi Kuu ya China ulioanza mwanzoni mwa mwezi huu.
Hapo ndio utajionea jinsi ligi ya hapa China inavyozidi kujijengea jina na kujiimarisha, kwa hiyo kama wachezaji wetu wakipata nafasi ya kucheza soka hapa, watapata uzoefu mkubwa kutoka kwa wachezaji wengine kutoka kwenye mataifa yaliyoendelea wanaocheza soka China.
Jambo kubwa hapa la kufanya ni kwa mawakala wetu kutupia jicho upande huu mwingine kuweza kuwatafutia soko wachezaji wetu maana huko Ulaya imeshaonekana kabisa hawawezi, hivyo ni wakati wa kugeukia Asia sasa. Kitu kingine ni kwamba ni rahisi kuonekana na timu kubwa za barani Ulaya akiwa anacheza soka kwenye ligi za hapa China au Japan hata Korea Kusini kuliko kutoka kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo haijajijenga na haijulikani kama ligi ya China.
Hapo nina maana kuwa, tunaweza kutumia hii kama njia ya kwenda kwenye timu kubwa barani Ulaya kama tumeshindwa kupeleka wachezaji wetu moja kwa moja kutoka hapo nyumbani. Kwenye ligi ya China, kuna mchezaji mmoja tu mwenye asili ya Tanzania anayeitwa Eddy Francis au wenyewe Wachina wanamwita Aidi.
Yeye baba yake ni Mtanzania na mama yake ni Mchina ingawa hajawahi kufika Tanzania na hajui lugha ya Kiswahili. Anazungumza Kichina tu na hata kwenye timu yake ya Dalian Aerbin, wenyewe wanamchukulia kama mchezaji wa Kichina.
Alipohojiwa na Kituo cha Televisheni cha CCTV mwaka 2012, Aidi alisema alizaliwa kwenye mji wa Shanghai na alikulia huko ila hakuweka wazi kuhusu baba yake mzazi ambaye ni Mtanzania kama bado yupo hapa China au yupo huko nyumbani Tanzania na hadi leo wanapozungumza kuhusu yeye, wanaishia kusema tu baba yake ni Mtanzania ila mama yake ndio anaelezwa kuwa ni Mchina na yupo jijini Shanghai.
Tatizo lingine ambalo lazima niseme kwenye kutafuta soko la kuuza wachezaji ni mawakala. Bado Tanzania haina mawakala wa maana wa kuwatafutia soko wachezaji wetu. Nafahamu kama wakifanya kazi ya maana hapa China, wachezaji wetu watapata tu timu za kucheza na sio China tu, hata kwenye timu zingine za Mashariki ya Mbali.
Wenzetu wajanja kutoka Afrika Magharibi tayari wameshalijaribu hili soko la soka la kulipwa la huku Mashariki ya Mbali hasa hapa nchini China. Ndio maana Drogba alipotoka Chelsea alikuja hapa, ilikuwa ni kujaribu kete inakuwaje huku na wakagundua kuwa hapa sio kwa kiwango cha akina Drogba ila ni njia ya wale wanaotafuta mafanikio ya kwenda kucheza Ulaya.
Nilifanikiwa kuzungumza na mwandishi mmoja wa michezo wa hapa China, aliniambia kitu kimoja tu kama tukiwa na mawakala wa kufanya kazi hiyo, basi wachezaji wetu wanaweza kabisa kupata timu ya kucheza kwenye ligi ya China na mimi ninaamini huku ndio kwenye kiwango chetu kuliko kupigania kwenda Ulaya ambako tayari kumeshatushinda tangu kitambo.
Na kama unakumbuka hivi karibuni, Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) lilitoa taarifa iliyosema kuwa kwenye Lgi ya Mabingwa barani Asia msimu uliopita, ilikuwa na wachezaji wengi kutoka Afrika, lakini hakukuwa na mchezaji hata mmoja kutoka nchi hiyo. Hiyo ni changamoto kubwa kwetu kuwatafutia soko wachezaji wetu Mashariki ya Mbali hasa nchini China.
Mwandishi wa makala haya ni mwanafunzi Mtanzania anayesoma China na anapatikana kwa simu ya mkononi +8615180191494, Instagram: mo1188 au evancemhando@ gmail.com.