WATANZANIA wengi hasa waliopo vijijini wanakunywa sana pombe za kienyeji kuliko zinazotengenezwa viwandani.
Takwimu za Shirika la afya Duniani (WHO) zinaonesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zenye wanywaji wengi wa pombe za kienyeji ukilinganisha na nchi nyingine.
Miongoni mwa nchi 55 za Afrika zilizo chini ya uangalizi wa WHO, Tanzania inashika nafasi ya tatu kwa kuwa na wanywaji wengi zaidi wa pombe baada ya Niger na Uganda.
Hata hivyo licha ya takwimu hizo kuonesha Tanzania ni nchi yenye wanywaji wengi wa pombe, takwimu hizo ziliweka wazi kuwa asilimia kubwa ya Watanzania hao wanakunywa pombe za kienyeji zenye majina kibao kama mataputapu, wanzuki, ayoga, chibuku, rubisi, komoni, gongo na mbege.
Inasemekana asilimia 10 ya wanywaji wanakunywa bia na asilimia moja wanakunywa mvinyo, asilimia tatu wakinywa pombe nyingine kali zilizotengenezwa viwandani na asilimia 86 wanakunywa pombe za kienyeji.
Ingawa Tanzania kuna sheria isemayo kuwa pombe haiuzwi kwa mtu mwenye umri chini ya miaka 18, lakini sheria hii haitekelezeki huko vijijini ambapo ndio kuna wanywaji wengi zaidi, inasemekana huko mtoto wa miaka 10 tayari anakuwa mlevi.
Unywaji wa pombe unashamiri zaidi vijijini kwakuwa sheria nyingi zianatekelezwa mijini, lakini vijijini sheria hizo hazifuatiliwi.
WHO inaeleza kuwa takriban watu milioni 2.5 duniani kila mwaka hufa kutokana na madhara ya kiafya yasababishwayo na pombe ambapo kati yao vijana ni 320,000 wenye miaka 15 hadi 29.
Pia pombe inaelezwa kuwa ni sababu kuu ya tatu kusababisha maradhi, pia ni chanzo cha matatizo mengi ikiwemo uvivu, mashambulizi, kutelekeza familia, ngono zisizo salama na mengine mengi.
Ni muda wa saa nne asubuhi napita katika Soko la Sovya la vyakula katika Wilaya ya Kasulu, mkoani Kigoma, natupia ‘jicho’ upande wangu wa kulia wa soko naona wananchi wa rika mbalimbali wakiwa wameketi chini ya miti ya miembe wakishirikiana kunywa kopo lililojaa pombe ya kienyeji maarufu kwa jina la kayoga.
Ninaamua kusogea karibu yao ambapo wananikaribisha kwa kuniambia: “Karibu, karibu, binti karibu unywe kayoga, njoo ukae hapa usiogope, wewe mama fanya haraka lete lita moja hapa mrembo asije akaondoka.”
Ndivyo nilivyopokewa katika klabu cha pombe za kienyeji Sokoni Sovya.
Lengo la safari yangu hiyo katika klabu cha pombe za kienyeji ni kufanya uchunguzi ni jinsi gani pombe za kienyeji zinachangia maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).
Muuzaji wa pombe hiyo ya kienyeji katika klabu hiyo ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini anasema wanywaji wengi wa pombe za kienyeji hushindwa kuzuia tamaa za mwili na kujikuta wakiingia katika vitendo vya ngono bila ya kinga.
“Kipindi cha mavuno pombe za kienyeji (kayoga) huwa nyingi ambapo huuzwa kwa kipimo kuanzia shilingi 300 hadi 1,000, hicho sasa ndicho kipindi cha ngono kuwa nje nje, ndiyo maana msimu wa mavuno, ukiisha wanawake wengi huwa na mimba zisizotarajiwa,” anasema mama huyo muuzaji huku akicheka.
Wanywaji wengi wa pombe za kienyeji wanakiri kuwa pombe hiyo inachangia kuongezeka kwa maambukizi ya VVU.
“Kipindi cha mavuno pombe za kienyeji huuzwa bei nafuu sana na hakuna anayeshindwa kununua, hivyo watu hulewa sana. Ni rahisi kufanya ngono isiyo salama kwani wanakuwa hawajajiandaa na wanawake wengi wakishanunuliwa pombe, huwa si rahisi kukataa kufanya ngono,” anasema Elisha Muka, mnywaji wa pombe za kienyeji.
Elizabeth Mondwa, mkazi wa Kasulu anasema pamoja na pombe za kienyeji kuchangia VVU pia zinarudisha maendeleo nyuma kwani nafaka wanazovuna badala ya kutumia kama chakula hutumika kupikia pombe.
“’Mara nyingi pombe hizi za kienyeji hutengenezwa kwa kutumia nafaka tunazolima shambani kama vile mahindi, muhogo, ndizi miwa na ulezi ambavyo vingetumika kama chakula pia, hali hiyo huhatarisha uwepo wa vyakula hivyo baadaye,” anasema mama huyo.
Baadhi ya wananchi wameitaka serikali kupitia Jeshi la Polisi kuendeleza msako wa kuwakamata watengenezaji wa pombe za kienyeji hasa zile haramu kama gongo.
Mfamasia wa Hospitali ya Mkoa wa Kigoma, Samson Masaka, anasema kwa kawaida pombe za kienyeji hutengenezwa kwa kusindika nafaka na nafaka hizo zinapochachushwa hutengenezwa vilevi (alcohol).
Anasema kiwango cha ‘alcohol’ hutofautiana kulingana na aina ya nafaka iliyotumika, kiwango cha joto kilichotumika kusindika na muda uliotumika kuchachusha pombe hiyo.
Mfamasia huyo anasema tatizo jingine linalosababisha madhara kwa wanywaji wa pombe za kienyeji kuwa ni aina ya unywaji na upikaji.
“’Kuna wapishi wengine wa pombe za kienyeji hupika huku wakiwa wamezichanganya na hamira, hamira zenyewe hazina kipimo, huwezi kujua hamira hiyo inaweza kuleta madhara gani kwenye mwili wa binadamu,” anasema.
Anasema unywaji wa pombe ya kienyeji pia mbali ya maambuki ya VVU pia huweza kusababisha magonjwa ya kuambukiza kama Kifua Kikuu (TB), kwa sababu kopo moja hutumiwa na wanywaji zaidi hata ya kumi kwa mtindo wa kupokezana.
“Lakini kuna wakati maji wanayotengenezea pombe huwa na vijidudu vya amoeba au minyoo, wanywaji wengi hupata madhara ikiwemo kuharisha,” anasema.
Naye Mganga Mkuu wa Hospitali ya Maweni, Dk. Leonard Subi, anasema kuwa pombe zinachangia sana ngono zembe hivyo kusababisha kuchangia kwa kiasi kikubwa maambukizi ya VVU.
Dk. Subi anasema watu 31,910 waliojitokeza kupima VVU kwa hiari kwa mwaka 2010 hadi Desemba 2011; kati yao 1,271 sawa na asilimia nne ya watu hao waligundulika kuwa na maambukizi ya VVU ambayo ni sawa na asilimia 1.7.
“Utafiti unaonesha kuwa Kigoma maambukizi ya ukimwi yamepanda na kuwa juu na waathirika wakubwa wakiwa ni wanawake na watoto,” anasema Dk. Subi.
Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Dahn Mkanga, anasema Wilaya yake ya Kasulu wakazi wake wanapenda kunywa pombe za kienyeji lakini mazao hayo yanatumika kutengenezea pombe hulimwa sana katika wilaya hiyo.
“Sidhani kama tunaweza kupata njaa katika wilaya hii kwani kwa kupungua kwa chakula sababu ya kutengenezea pombe wilaya hii wanalima sana hayo mazao ya kutengenezea pombe.
“Unywaji pombe si maadili yetu Watanzania, wimbi kubwa la wanywaji wa pombe ni vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa, mtu yeyote atakayeoneka ana kunywa pombe wakati wa saa za kazi, saa za masomo tutamchukulia hatua za kisheria, huo ni muda wa kufanya maendeleo, kama ni pombe wanywe nyakati za jioni,” anasema mkuu huyo wa wilaya.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa makala hii katika vijiji vya Heru Juu, Heru Shingo, Muyama na Mnyegela katika Wilaya ya Kasulu unaonesha kuwa ni utamaduni wa kawaida kwa watu wa rika zote kunywa pombe, hasa za kienyeji ingawa wanywaji wengi wana miaka 16 hadi 40
src
Tanzania Daima