WIKI iliyopita Rais wetu, Jakaya Kikwete, alikuwa jijini London pamoja na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, (naambiwa ni marafiki wa karibu) kuhudhuria mkutano wa kimataifa wa namna ya kukomesha biashara haramu ya pembe za ndovu duniani.
Rais alitumia fursa hiyo ya kuwepo Uingereza ‘kujisafisha’ dhidi ya habari zilizoandikwa na gazeti la Sunday Mail la nchi hiyokwamba serikali yake hajachukua hatua zozote kupambana na biashara hiyo haramu nchini.
‘Kujisafisha’ huko pia kulifanywa na Nyalandu kwa kuzungumza na vyombo vya habari vya hapa nchini kabla ya safari hiyo ya London. Kwenye mkutano huo Nyalandu alisema lengo la gazeti hilo lilikuwa ni kuchafua jina la Tanzania kabla ya mkutano huo wa London.
Ni kwa lengo hilo la ‘kujisafisha’, Rais Kikwete aliweza kupata fursa ya kuzungumza na mwandishi maarufu wa CNN, Christine Amanpour na pia Idhaa ya Kiswahili ya BBC.
Sina hakika iwapo ni yeye Kikwete aliyeomba mwenyewe kuhojiwa na CNN na BBC kuhusu suala hilo au ni vyombo hivyo viwili vyenyewe vilivyoomba kumhoji.
Hilo, hata hivyo, si la msingi katika tafakuri yangu ya leo; bali la msingi ni kuangalia iwapo ripoti hiyo ya gazeti la Uingereza, ambayo imemkera Kikwete na Serikali yake ina ukweli wowote au ni “upotoshaji mtupu na upuuzi”kama Kikwete mwenyewe alivyoiambia BBC.
Labda nianze na takwimu. Sensa ya tembo iliyofanywa na Serikali mwaka jana inaonyesha kuwa idadi ya tembo nchini imepungua kwa asilimia 66 ikilinganishwa na idadi ya sensa ya mwaka 1990. Selous -Mikumi wamebakia tembo 13,084 tu wakati Ruaha - Rungwe wamebakia 20,000 tu! Kwa wastani tembo 11,000 huuawa nchini kila mwaka na majangili.
Kama nilivyoeleza mwanzo, gazeti hilo liliandika kuonyesha kwamba Serikali ya Tanzania haijachukua hatua zozote kupambana na biashara ya pembe za ndovu nchini, na ndiyo maana idadi ya tembo inazidi kupungua. Je, ni kweli Serikali haijachukua hatua zozote? Jibu langu ni ‘si kweli’.
Jibu langu ni hilo kwa sababu Serikali imechukua hatua kadhaa na sote tunazijua; huku ya hivi karibuni kabisa ikiwa ni kuanzisha Operesheni Tokomeza.
Kama jibu ni ‘si kweli’, ukweli ni upi? Kwa mtazamo wangu, ukweli ni kwamba Serikali imechukua hatua kadhaa kupambana na tatizo hilo, lakini hatua hizo hazijaleta matokeo yoyote makubwa, na ndiyo sababu biashara hiyo bado imepamba moto hata sasa nchini.
Katika hali hiyo, usahihi wa ripoti ya Sunday Mail ungekuwa kwamba; Serikali ya Tanzania inachukua hatua mara kwa mara kupambana na biashara haramu ya pembe za ndovu, lakini hatua hizo zimeshindwa, mpaka sasa, kuleta matokeo makubwa. Huo ndiyo ukweli usiopingika.
Ni kwa nini hatua hizo za Serikali zimeshindwa, mpaka sasa, kuikomesha biashara hiyo hapa nchini? Swali hili nitalijibu baadaye, lakini kwa sasa tukubaliane tu kwamba serikali – kuanzia ya Mwalimu Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa, na sasa ya Jakaya Kikwete, zimekuwa zikichukua hatua kukabiliana na hali hiyo, lakini ujangili bado umepamba moto.
Tukirejea kwenye suala la habari hiyo ya Sunday Mail, mimi nadhani Kikwete na waziri wake Nyalandu walikasirishwa nayo sana bila kwanza kuzingatia maudhui ya jumla ya ripoti hiyo ya gazeti hilo la Uingereza ambayo ni kwamba ujangili bado ni tatizo kubwa Tanzania.
Natambua wazi wajibu wa rais, waziri na kwa hakika kila Mtanzania, wa kuonyesha hisia za kizalendo kila nchi yetu inapoguswa kwa mabaya na vyombo vya habari vya nje, lakini hiyo haihalalishi kauli za kupitiliza (over reacting) kwenye suala lenye ukweli fulani ndani yake.
Kwa mtazamo wangu, Kikwete kuiita ripoti ile ya Sunday Mail kuwa ni “uzushi na upuuzi mtupu” ni ku-over react kwa jambo lenye ukweli fulani ndani yake.
Kwa ufupi, Serikali haikuwa na sababu yoyote muhimu ya ku-over react,na haina ushahidi kwamba gazeti hilo lilikuwa na ajenda ya kuichafua sifa ya Tanzania zaidi ya kuieleza dunia hali ilivyo hapa nchini ya mauaji ya kusikitisha ya tembo wetu.
Nasema Serikali haikuwa na sababu yoyote nzito ya ku-over react kwa sababu ya mambo mawili makubwa. Jambo la kwanza ni kwamba hoja kuwa taarifa hiyo ya Sunday Mail ililenga kuichafua Tanzania haina mashiko kwa kuwa jina la Tanzania lilishachafuka kwa muda mrefu sasa kuhusu biashara hiyo haramu ya meno ya tembo, na ushahidi upo.
Lakini pili, maudhui ya ujumla ya ripoti ile ya Sunday Mail ni sahihi. Ni sahihi kwa sababu ujangili bado umeshamiri sana katika Tanzania, na watawala wetu japo wanachukua hatua, lakini hatua hizo hazijaleta mabadiliko yoyote makubwa, na ushahidi wa kitakwimu upo, na unaonyesha kuwa idadi ya tembo wanaouawa kila mwaka sasa imefikia 11,000.
Labda nitoe mfano kuthibitisha kwamba sifa ya Tanzania kwenye suala la biashara ya pembe za ndovu duniani ilishachafuka muda mrefu uliopita, na kwa maana hiyo, gazeti hilo la Uingereza haliwezi kuwa na ajenda ya kuchafua jina la nchi ambayo tayari limeshachafuka!
Mwaka 2010 katika mkutano wa mwaka wa CITES (Convention on International Trade in Endagered Species) ambayo Tanzania ni mwanachama, ombi la Tanzania kutaka kuuza shehena ya meno ya tembo iliyoyakamata iliyofikia tani takriban 90 lilitupiliwa mbali kwa sababu kuu nne.
Moja ni kwamba kama ruhusu hiyo ingetolewa kulikuwa na wasiwasi kuwa meno ambayo yangeuzwa si yale tu yaliyokuwepo Ivory Room (Dar es Salaam) kwa wakati ule bali wajanja wangepenyesha na mengine yaliyopatikana kupitia ujangili.
Sababu ya pili ilikuwa ni kwamba Tanzania ilikuwa “imeruhusu” nchi yake kuwa njia ya biashara haramu ya meno ya tembo kutoka nchi za Kusini zikiwemo Zambia na Malawi. Sababu ya tatu ni kwamba Tanzania ilikuwa haifanyi jitihada za kutosha kulinda tembo wake hasa katika mbuga za hifadhi kama Selous.
CITES iliona kwamba Tanzania ilikuwa na uwezo wa kulinda tembo wake lakini haikutekeleza jukumu hilo kwa dhati na hivyo kusababisha ujangili kushamiri.
Na sababu ya mwisho ni kwamba Tanzania haijachukua hatua madhubuti kupambana na biashara haramu ya meno ya tembo na kwamba serikali haijadhamiria kukomesha biashara hiyo.
Hiyo ilikuwa ni miaka minne iliyopita. Yaani, kwa ufupi, CITE ilikuwa inasema kuwa sifa ya Tanzania ya kulinda tembo wake ni mbaya, na ndiyo maana ombi lake lilikataliwa.
Sasa, kuaje leo Rais Kikwete na Waziri Nyalandu walijie juu gazeti hilo la Uingereza kuwa linachafua jina la Tanzania; ilhali jina hilo, katika suala hilo la kulinda tembo wasitoweke duniani, lilishafuka?
Mfano wa pili ni wa Machi mwaka jana ambapo mkutano mwingine wa mwaka wa CITE uliingiza Tanzania katika orodha iliyoitwa “GENGE LA NCHI NANE” (Gang of Eight). Orodha hiyo ni ya nchi zilizokubuhu kwa biashara haramu ya pembe za ndovu duniani. Nchi nyingine katika orodha hiyo ni Kenya, Uganda, China, Thailand, Malaysia, Vietnam na Phillipines.
Sasa, nchi ambayo tayari ilishaingizwa katika orodha ya dunia ya Gang of Eight ya nchi zinazoongoza kwa biashara haramu ya pembe za ndovu yawezaje kulalamikia gazeti hilo kuwa linachafua sifa ya jina lake kimataifa? Sifa gani ya kulinda katika biashara hiyo ya pembe za ndovu kama tayari jina la nchi limo katika orodha hiyo ya Gang of Eight?
Ndugu zangu, tuambizane ukweli na ukweli ni huu: Ujangili umekuwepo miaka mingi nchini tangu enzi za Nyerere na kila mara Serikali imekuwa ikichukua hatua kukabiliana nao. Hata hivyo, hatua hizo zimeshindwa kuutokomeza kabisa uhalifu huo nchini.
Katika miaka ya karibuni hali ndiyo imezidi kuwa mbaya. Kumbukumbu zinaonyesha kuwa hata gari la Ikulu yetu (Toyota Land Cruiser) lilipata kukamatwa huko Kibiti likiwa na shehena ya pembe za ndovu baada ya kupata ajali. Si hivyo tu, hata magari ya JWTZ yamepata nayo kukamatwa yakiwa na pembe hizo!
Rais Kikwete mwenyewe, katika mahojiano ya mwishoni mwa wiki na BBC, alikiri kuwa hali ni mbaya kiasi kwamba askari wa wanyamapori waliposhindwa kuidhibiti hali hiyo aliamuru Polisi waingie, lakini nao wakashindwa, na ndipo alipoamuru JWTZ waingie (Operesheni Tokomeza).
Hata hivyo, ukweli ni kwamba mpaka operesheni hiyo iliposimamishwa, biashara hiyo haramu ya pembe za ndovu ilikuwa haijatokomezwa kabisa, na operesheni iliposimamishwa biashara ikarejea katika kasi ile ile ya mwanzo!
Sasa nirejee katika lile swali nililoliacha kiporo la ni kwa nini, pamoja na hatua zote zinazochukuliwa na Serikali, bado biashara haramu ya pembe za ndovu inashamiri Tanzania.
Jibu langu kwa ufupi ni kwamba kinachotukwaza ni kuenea kwa utamaduni wa ufisadi katika kila kona ya maisha yetu. Watanzania tunatafuta utajiri na maisha mazuri kwa njia ya mkato, na katika miaka ya karibuni tumegundua kuwa njia nzuri ya mkato ni ya ufisadi!
Tatizo hili (ufisadi) ndilo ambalo Joshua Lawrence, kwenye makala yake katika gazeti hili, aliliita “anguko la kimaadili” na “virusi vya kimfumo”.
Katika mahojiano yake na BBC, Rais Kikwete alitamka kwamba anayo majina ya majangili papa 40 nchini, na kwamba wanaongozwa na tajiri mmoja wa Arusha! Mtu unajiuliza; kama Rais ana majina hayo, mbona hatoi amri wakamatwe?
Utakumbuka pia kwamba Kikwete alishawahi kusema kuwa ana orodha ya majina ya vigogo wanaojishughulisha na biashara haramu ya madawa ya kulevya, lakini mpaka sasa hatujasikia kigogo yeyote akikamatwa! Kwa nini?
Jibu langu ni ufisadi. Yawezekana hao wanaopaswa kuwakamata vigogo hao wamo kwenye “payroll” isiyo rasmi ya mafisadi hao wa biashara hizo haramu za pembe za ndovu na madawa ya kulevya.
Lakini pia yawezekana vigogo hao wamo katika orodha ya wafadhili wa chama tawala CCM, na ndiyo sababu kuna kusitasita kuwakamata.Ni ufisadi.
Vyovyote vile, ufisadi huu haufanywi tu na vigogo wa juu wa biashara hizo bali pia umesambaa mpaka chini kwenye polisi wa kawaida, viongozi wa serikali za vijiji, wilaya na mikoa, na hata wananchi wa kawaida.
Tumefika mahali pabaya kiasi kwamba hata humo kwenye wanaounda vikosi vya hizo operesheni wamo wajumbe mafisadi ambao huvujisha siri za operesheni kwa mafisadi hao ili walipwe mapesa mengi kwa kuwasaidia wasikamatwe. Na hata wakikamatwa, wapo mahakimu walio kwenye “payroll” za mafisadi hao ambao huhakikisha hawafungwi!
Hapo ndipo tulipofikia. Ndiyo maana naamini kwamba, bila kwanza kuitokomeza kansa hii kuu ya anguko la kimaadili (ufisadi), tutaendesha operesheni za kila aina dhidi ya biashara haramu ya pembe za ndovu, lakini bado itaendelea kushamiriTanzania, na bado jina la nchi yetu duniani litaendelea kuchafuka, na haitajalisha Sunday Mail limeripoti au halikuripoti!
Na hiyo ni kwa sababu operesheni zinakuja na kupita, lakini ufisadi unaachwa ubaki. Kwa hiyo, opereshen ikimalizika na upepo ukitulia, mafisadi wanarejea tena kazini na kuendelea kuua tembo.
Naamini hicho ndicho Mchungaji Msigwa alichomaanisha katika kauli yake kwa Sunday Mail, na ndivyo pia gazeti hilo la Uingereza lilivyomaanisha katika ripoti yake.
Kwa kigezo chochote kile, huwezi kuiita ripoti yao hiyo ‘upotoshaji mkubwa na upuuzi’ kwa sababu, pamoja na yote, kuna ukweli ndani yake kama nilivyojaribu kueleza.
Tafakari.
Src –raia mwema