Wednesday, February 19, 2014

Tujitoe sasa Shirikisho la Afrika Mashariki kabla hatujachelewa


WALIPOKUTANA kwa mara ya kwanza mjini Arusha kuanzisha mchakato wa  Shirikisho la [kisiasa] Afrika Mashariki [EAF], wakuu wa nchi tatu asilia za Afrika Mashariki – Marais Benjamin William Mkapa wa Tanzania, Yoweri Museveni wa Uganda na Mwai Kibaki wa Kenya, hawakujua kwamba, chombo walichokusudia kukianzisha kingesimama na kuanguka kabla hakijatembea kwa “degedege”, ubinafsi na unafiki wa viongozi.

Kwa mujibu wa ratiba ya utekelezaji waliyojiwekea, Shirikisho hilo lilitarajiwa kuwa limesimama na kutembea ifikapo Januari 2010; lakini ilivyo sasa, matarajio ya kufikia hatua hiyo yanafifia kwa nchi washiriki kughubikwa na mifarakano, kubaguana, kutishana na kusalitiana mithili ya ugonjwa ulioua Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Mashariki [EAC] mwaka 1977.

Kuingia kwa Rwanda na Burundi, na sasa kuvutwa na kuingia kwa Sudan Kusini katika Shirikisho hili, kumezidi kufifisha matumaini na matarajio kutokana na siasa, utamaduni na miundo mbinu ya nchi hizo kutoshabihiana na nchi tatu asilia za Afrika Mashariki kwa mambo hayo.

Ubabe, unyonyaji, nia mbaya, wivu na akili mbovu za “kibeberu” za viongozi “wababe wa vita” wa nchi za Rwanda, Uganda na Sudan Kusini, ni mambo yanayovunja moyo wa washiriki wengine wa Shirikisho tarajiwa.

Mbali na sababu hizo, ushahidi wa kihistoria unaonyesha kuwa, ni vigumu kwa nchi masikini za Kiafrika kuanzisha Shirikisho lenye mafanikio chini ya viongozi wa sasa waliosheheni kasumba za ubeberu wa kimataifa, utegemezi wa kiuchumi na kiakili. Na pia hii ndiyo changamoto kwa EAF.

Kama EAC ilishindwa sembuse EAF?

Ushirikiano wa nchi za Afrika Mashariki unaanzia mwaka 1917 kwa kuundwa Soko la pamoja kati ya Kenya na Uganda ambapo Tanganyika ilijiunga mwaka 1927.  Hata kipindi hicho na kwa hatua hiyo, Kenya ilitengeneza ziada kubwa kibiashara kuliko Tanganyika na Uganda zilizoshuhudia nakisi daima.

Haya yalikuwa ni matokeo ya uamuzi wa Kikoloni kulundika maendeleo ya viwanda nchini Kenya, kitu ambacho Wakenya walipenda kukiita “ajali ya kihistoria ya manufaa” kwa Kenya.

Huduma za pamoja [EACSO] ziliendelea kukua taratibu kipindi chote cha ukoloni, kwa kuanzia na Shirika la Reli la Afrika Mashariki [EAR] na huduma za Posta mwishoni mwa vita ya Kwanza ya Dunia, na baadaye Bodi ya Sarafu ya pamoja, Mahakama ya Rufaa, Mamlaka ya Bandari na mwisho, Shirika la Ndege [EAA].

Mwaka 1967, Mkataba wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki ulianzisha rasmi Jumuiya ya [Kiuchumi] Afrika Mashariki [iliyovunjika 1977] katika kujaribu kujenga uhusiano ulio sawa miongoni mwa nchi wanachama.

Ukweli, majaribio mengi yaliyopita ya kutaka kufikia shirikisho la kisiasa, yanaibua hatari kuu zinazokabili juhudi kama hizo kutaka kwenda zaidi ya “ushirikiano wa kiuchumi”, kuanzia na Shirikisho la Afrika Mashariki [EAF] lililoshindwa Aprili 10, 1964 ambalo lingezihusisha Kenya, Uganda, Tanganyika na Zanzibar, na baada ya kushindwa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanganyika aligeukia Muungano mdogo zaidi wa Tanganyika na Zanzibar badala yake.

Pamoja na hayo, muundo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar nao ni utata mtupu. Wakati Mkataba wa Muungano unasema ni shirikisho la kisiasa lenye serikali tatu, utekelezaji unafanyika kwa muundo [usiokuwepo] wa serikali mbili na kuzua kile kinachoitwa “Kero za Muungano”.

Watanzania wanapashwa kujiuliza swali hili la msingi kabla ya kusonga mbele kichwa kichwa: “Kama Muungano wa Tanganyika na Zanzibar pekee unatutoa jasho, Shirikisho la Afrika Mashariki je?”

Jukumu la kusuluhisha migogoro kati ya mahitaji binafsi ya nchi wanachama na matakwa ya kikanda lilianza kwa kuundwa Umoja wa Watawala Afrika Mashariki – “The East African High Commission” [EAHC] baada ya Vita ya Pili ya Dunia, ukihusisha magavana wa nchi tatu za Afrika Mashariki pamoja na mtawala wa Zanzibar kama mwalikwa na Umoja wa Huduma za pamoja Afrika Mashariki - “The East African Common Service Organization” [EACSO].

Nchi zote tatu, tofauti na nchi za EAF la sasa, zilikuwa chini ya nguvu unganishi [uniting force] moja yenye mamlaka ya mwisho – Uingereza, ambayo kupitia Katibu wake wa Makoloni, ilikuwa na uamuzi wa mwisho kama magavana hao watatu [sasa Marais wa Nchi za Afrika Mashariki] hawakukubaliana juu ya jambo lolote.

Phillip Mitchell, Gavana wa Kenya ambaye pia ndiye alikuwa Mwenyekiti wa kwanza wa EAHC, alipendelea mtizamo wa kikanda na aliwahi kusikika, kama anavyonukuliwa katika kitabu cha Thomas Frank “East African Unity Through Law” – uk. 58, akisema: “Wakati hakuna hata nchi moja kati ya nchi tatu za Afrika Mashariki iliyokubali kuunda shirikisho kati yake na nyingine mbili, EAHC yenyewe ni mamlaka ya kishirikisho ingawaje nchi tatu hizi hazipendi kukiri hivyo”.

Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa wazo la Shirikisho Afrika Mashariki kuwekwa hadharani kwa kupigiwa debe.  Uwezekano wa kuundwa kwa EAF wakati huo ulikuwa mkubwa kuliko sasa kutokana na kuwapo nguvu-unganishi [Katibu wa Makoloni] ila kwa sababu tu nchi hizo zilipata uhuru mapema kabla mchakato haujashika kasi.

Hivi sasa, nchi za Afrika Mashariki [na viongozi wake] hazina nguvu – unganishi itakiwayo ambapo kila kiongozi ni “kambale mwenye sharubu” ndani ya kidimbwi chake. Je, tutarajie nini kwa juhudi za kuunda EAF chini ya “ubabe” na “ukambale” huu?

Kuingia kwa Burundi na Rwanda ni baraka au janga?  Na hii lugha ya mgawanyiko kati ya “walio tayari” [kwa Shirikisho] – “Coalition of the Willing” na “Wasio tayari” inatoka wapi?  Nazo chokochoko za Rwanda za “mtafutano” kwa Tanzania zinatoka wapi?  Iko wapi nguvu – unganishi kuweza kurekebisha haya ili Shirikisho liendelee?

Tumesema ilikuwa rahisi kuunda Shirikisho enzi za ukoloni kuliko leo kwa sababu kulikuwa na nguvu – unganishi.  Wakati kilichoongoza enzi hizo ilikuwa “nguvu ya kitawala”, na mamlaka ya kuelekeza kitakiwacho, kinachoongoza leo ni “utashi wa kisiasa”  usio na nguvu kuweza kudhibiti ukiukaji.

Ndiyo maana sasa tumeanza kuamini kwamba, Kwame Nkrumah hakukosea pale alipopendekeza mwaka 1960 kuwa, iwe sharti kuu tangulizi [condition precedent] kwamba, ili nchi ya Kiafrika ipate uhuru, lazima kwanza ikubali kuwa mwanachama wa Shirikisho la Afrika, kama ambavyo tu ilivyokuwa lazima kwa nchi zilizotawaliwa na Uingereza kuwa wanachama wa Jumuiya ya Madola chini ya Malkia wa Uingereza.

Mwanzo mbaya

Dalili za mwanzo mbaya kwa EAF zilianza kujionyesha pale Rwanda na Burundi zilipojiunga, pale Rais wa Rwanda, Paul Kagame, alipolalamika kubaguliwa [kwa kujihisi?] kwamba Tanzania, Kenya na Uganda zinawaona [Rwanda na Burundi] kama nchi “zilizolaaniwa na zenye kuleta migogoro na mgawanyiko”, huku Mwai Kibaki [Kenya] akidai wazi wazi kwamba muda ulikuwa haujawadia kwa Wanyarwanda na Warundi kuongoza EAF.

Kagame akang’aka akisema: “Ni upumbavu [uzuzu] mtupu! Huwezi ukawa na wanachama wa Shirikisho ambapo haki zinatolewa kwa msingi wa madaraja andamizi [seniority], lakini wakati wa kulipa ada wote mnalipa sawa”.Kisha akaendelea kusema: “Shirikisho lazima life, na hakika litakufa umma ukijua kwamba Rwanda na Burundi wanabaguliwa”. 

Mfarakano wa viongozi hao hivi karibuni juu ya jambo dogo tu kama vile maudhui ya Wimbo wa Shirikisho, unaonyesha kushindwa kwa utashi wa kisiasa kuhusu Shirikisho. Wakati Rais Jakaya Kikwete alilalamika kwamba wimbo huo una ladha ya “Kikristo” mno na hivyo unatakiwa uwekwe kwenye mzania urekebishwe, Yoweri Museveni kwa upande wake alilalamika akisema umepoa, na kwamba lazima uzingatie wimbi la mapinduzi ya kidemokrasia, uwe wa kimapinduzi na wenye mdundo wa nguvu kuonyesha harakati.

Mwai Kibaki yeye hakuwa na maoni; wakati Kagame na Pierre Nkrunzinza [Burundi] walikubali kucheza kwa mdundo wowote unaokubalika, kwa sababu hawakuwa sehemu ya mchakato wa wimbo huo ulipotungwa.

Lakini pamoja na hayo, leo, mdundo na harakati hasi za Marais Kagame na Museveni zinaonekana kushabihiana kuleta mwanzo mbaya kwa Shirikisho, kama tutakavyoona hivi punde.

Wababe wa vita ndani ya EAF?

Museveni, Kagame, na sasa Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir ni wababe wa vita ndani ya Shirikisho la Afrika Mashariki.  Wakati madhumuni ya ushirikiano wowote ni pamoja na kutatua migogoro kwa njia ya amani, wao ni vita na chokochoko kama sehemu ya mazoezi ya umwagaji damu.

Museveni na Kagame walimpindua Laurent Kabila wa DRC, na kuna maswali mengi kuliko majibu juu ya kifo cha mwasisi wa Taifa la Sudan Kusini, Kanali John Garang aliyekufa kwa “ajali ya ndege” – Chopa ya Uganda ikiendeshwa na Kanali wa Jeshi la Uganda.

Majeshi ya Museveni yanapigana mahali pengi – yapo Somalia, Jamhuri ya Afrika ya Kati [CAR], DRC na sasa Sudani Kusini, yakipigana bega kwa bega na majeshi ya Kagane huko DRC na Sudan Kusini.

Ndege za kivita za kisasa za kikosi M23 cha Kagame zinahifadhiwa Juba, Sudan Kusini, na Jeshi la nchi hiyo linafunzwa na Kagame.  Hatuna hakika, kwamba choko choko za Kagame za mara kwa mara na zisizo na msingi kwa Tanzania, huenda ni sehemu ya kujitanua kwa ubabe wa Kagame na mwenzake Museveni, Afrika Mashariki.

Tunafahamu, vita ya sasa kati ya DRC na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Kagame na Museveni ni matokeo ya kikao kijulikanacho kama “Pembe Tatu” kilichofanyika mjini Gisenyi, Rwanda miaka miwili iliyopita kabla ya maasi, kati ya Kagame, Museveni na Jenerali Bosco Taganda kama sehemu ya maandalizi ya kile wanachokiita “Kuhalalisha na Kupanua Himaya ya Wahima” kwa lengo la kuitawala Afrika Mashariki.

Kwenye kikao hicho, lilipitishwa Azimio la kumega Kilometa 120 ndani ya ardhi ya DRC kutoka mipaka ya nchi hiyo ili ipoteze maziwa manne – Ziwa Albert, Ziwa Edward, Ziwa Kivu na Ziwa Tanganyika. 

Hatutashangaa kufahamu kesho kwamba, chokochoko za Kagame kwa Tanzania ni sehemu ya mpango wa upanuzi wa himaya hiyo, na amezidi kujivunia uimara wa intelijensia yake kiasi kwamba eti anafahamu hata rangi ya shuka za Ikulu ya Dar es Salaam.

Kung’ang’ania madarakani kwa Rais Museveni wa Uganda akidai hadi amehakikisha EAF limeundwa na yeye kuwa Rais wa kwanza, kama anavyojinasibu katika kitabu chake, “Sowing the Mustard Seeds”, huenda ni sehemu ya mkakati wa wababe hao wawili wa vita kutekeleza ndoto yao.

Muungano wa walio tayari

Kutengwa kwa Tanzania na Burundi katika mambo kadhaa makuu ya EAF na nchi za Rwanda, Uganda, Kenya na Sudan Kusini kuna harufu ya “Pembe Tatu”, ambapo Kenya imeingizwa kichwa kichwa bila kujua.  Chambo?  Sudan Kusini.

Tunafahamu, wanufaikaji wakubwa wa Uhuru wa Sudan Kusini wamekuwa ni wale wafanyabiashara, wawekezaji na watafuta ajira kutoka Kenya na Uganda ambao wamefurika huko kwa maelfu kuanzia hapo.  Hii ni neema na kutua mzigo kwa Kenya na Uganda zinazokabiliwa na tatizo la ongezeko kubwa la wasomi wasio na ajira kufuatia viongozi wa Kenya kunyakua na kuhodhi ardhi na kuwaacha wananchi bila kipande cha ardhi kuweza kukidhi maisha.

Na baada ya “nyang’au” hao kupigwa ‘stopu’ na Tanzania kwamba ardhi si jambo la Shirikisho, walizira na kuisusia nchi yetu kwamba haijawa tayari kwa Shirikisho na kufunga fungate ya ajabu ajabu na Sudan Kusini.  Tungesinzia ardhi yetu leo ingekuwa mikononi mwa wasaka makazi mapya kutoka Kenya, Uganda na Rwanda!

Wakati wa mapigano kati ya majeshi ya Salva Kiir na yale ya Riek Machar kwa mgogoro wa ndani ya Sudan Kusini, Uganda na Kenya zilipeleka majeshi kwa madai ya kuwalinda na kuwaondoa raia wake waliozingirwa Juba.

Haukupita muda ikabainika kuwa majeshi ya Uganda na Rwanda, yalikuwa yakipigana bega kwa bega na majeshi ya Salva Kiir dhidi ya majeshi ya Riek Machar, huku Museveni akimpa Machar siku nne kuacha mapigano, vinginevyo apigwe na kutokomezwa.

Kushiriki kwa Uganda na Kenya kwenye mapigano nchini Sudan Kusini kunaonyesha nchi hizo zina maslahi makubwa katika nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa mafuta na ambayo ukubwa wake ni mara mbili ya nchi hizo za Afrika Mashariki.

Kenya ingependa jeshi lake lishiriki kikamilifu katika mapigano hayo chini ya “Umoja wa walio tayari” ila kwa vita iliyojiingiza Somalia ambayo imeipunguzia nguvu za kijeshi kuweza kuingia vita mpya. 

Kwa yote hayo, Sudan Kusini sasa ni tatizo la Usalama kikanda kama tu ilivyo DRC, kwa sababu ya mamlaka ya EAF kuhodhiwa na wababe wa vita – Rwanda na Uganda.

Kinachofanywa na wababe hawa wawili wa vita – Kagame na Museveni, ni ubeberu wa wazi wazi dhidi ya majirani zao kwa agenda ya siri ya kupanua himaya.  Kwa utamaduni kama huu, EAF haliwezi kujengwa kwa utashi wa kivita na upanuzi wa himaya, badala ya utashi wa kisiasa ambao ni dhahiri haupo.

Njia salama ni kujitoa

Watanzania hatujasahau jinsi Jumuiya ya Afrika Mashariki [EAC] ilivyovunjika kwa karaha kubwa Februari 5, 1977 [siku ya kuzaliwa kwa CCM] kwa kukosekana utashi wa kisiasa, kama inavyothibitishwa na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Kenya, Charles Njonjo aliyesema kwa furaha: “Jana usiku [5/2/1977], nilikunywa glasi tano za mvinyo [champagne] kwa kuvunjika kwa EAC na glasi zingine tano za pombe kali [whisky] kwa kifo cha Serikali ya Tanzania kisichoepukika”.

Na mapema mwaka 2006 wakati viongozi wa Afrika Mashariki wakiendeleza mchakato wa EAF, Njonjo huyo huyo alisikika akilaani akisema: “Nakerwa mno na juhudi zinazofanywa na wakuu wa nchi za Afrika Mashariki za kufufua EAC.  Kwa muda wote sijaamini wala sitaamini kwamba ni nia njema kuwa na Jumuiya……. Unatarajia nini kutoka nchi kama Tanzania, Uganda na Kenya ambazo uchumi wake ni shagharabaghara kufanya mambo yaende?”

Bado kina Njonjo wapo na sasa, wababe wa vita tunao miongoni mwetu.  Na hii inauweka ushiriki na uwamo wa nchi yetu katika EAF hatarini, ikizingatiwa madhumuni yaliyofichika ya Kenya, Uganda na Rwanda na uwezekano wa migogoro inayoweza kuibuka katika nchi yoyote mwanachama ambapo badala ya kutarajia suluhu za kiungwana, sasa tutarajie vita vya kibeberu na upanuzi wa himaya. 

Historia itupe somo na kutufumbua macho juu ya viongozi wanaopeleka majeshi nje ya mipaka ya nchi zao kwa sababu zisizofahamika.  Na kwa sababu sisi sio taifa la vita na umwagaji damu, njia salama kuepuka aibu na karaha za 1977 ni kujitoa sawia katika EAF kabla hatujachelewa.

Src –raia mwema