- Mmoja atumia 6.7bn/-
- Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu kazini
- CCM yawasimamisha mwaka mmoja
WAKATI Chama cha Mapinduzi (CCM) kikiwasimamisha kuwania uongozi kwa mwaka mmoja wanachama wake sita wanaotajwa kuwania urais 2015, vyombo vya dola vimeanza kuchunguza fedha zinazotajwa kutumika na mmoja wa viongozi hao katika harakati zake hizo, Raia Mwema limeelezwa.
Taarifa rasmi ya CCM imeeleza kwamba chama hicho kimewawapa adhabu ya onyo kali vigogo wote sita waliohojiwa na chama hicho, adhabu ambayo inawabana kuwania nafasi yoyote ya uongozi kwa kipindi cha miezi 12, huku wakichunguzwa kama wamejirekebisha.
Taarifa za ndani ya serikali zimethibitisha kwamba tayari Kitengo cha Kudhibiti Biashara ya Fedha Haramu (Financial Intelligence Unit-FIU) kimeshaanza mchakato wa kufuatilia kiasi cha shilingi bilioni 6.7 ambazo ni matumizi ya mmoja wa wana CCM anayetafuta urais katika kipindi cha miaka miwili tu iliyopita.
Kwa mujibu wa habari hizo, FIU ambacho kiko chini ya Wizara ya Fedha kinashirikiana na vyombo vingine vya dola kama Polisi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na taasisi nyingine kwa nia ya kujiridhisha uhalali wa fedha hizo, kazi ambayo taarifa zinasema imekwishakuanza.
“TRA wanafuatilia wote anaodai (mwanasiasa huyo) wamemchangia, ili waone kama waliochanga walilipa kodi na michango inaonekana kwenye tax returns (hesabu za kodi). Waliomchangia inabidi watoe nakala za pasi zao za kusafiria, leseni zao za udereva na orodha za akaunti zao zote. Sisi hatuhusiki sana ila watu wa wanaoshughulikia money laundering (fedha haramu) wana maelekezo kufuatilia fedha alizogawa katika miaka miwili ambazo ni 6.7b/-,” alieleza mtoa habari wetu ndani ya Serikali.
Financial Intelligence Unit (FIU) Kitengo cha Kudhibiti Biashara ya Fedha Haramu kimeanzishwa chini ya sheria ya Udhibiti Biashara ya Fedha Haramu (Anti Money Laundering Act, 2006), ikiwa na jukumu la kudhibiti fedha haramu na fedha zinazotumika kufadhili ugaidi nchini. FIU ilianza kazi rasmi Septemba 2007 ikiwa na watendaji wachache wakiongozwa na Kamishna wake, Herman Kessy.
Hatua hiyo inafuatia kauli ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, wakati wa maadhimisho ya miaka 37 ya chama hicho mjini Mbeya, ambaye alisema vyombo vyote husika viwashughulikie wanaotumia fedha kusaka uongozi na kukemea wanaotangaza kuwania urais kabla ya chama kutoa ratiba ya mchakato wa kupata mgombea wa chama hicho.
Wakati hayo yakiendelea, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, amesema kwamba Kamati Kuu ya chama hicho imetoa onyo kali kwa wagombea wote sita waliohojiwa na Tume Ndogo ya Udhibiti wa Maadili, na kupelekwa kwenye Tume ya Usalama na Maadili ya chama hicho, adhabu ambayo itawalazimu kuwa chini ya uangalizi kwa miezi 12 ijayo.
Wagombea ambao walihojiwa na Kamati ya Maadili ya CCM ni pamoja na waziri mkuu wa awamu ya tatu, Frederick Sumaye, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Uhusiano na Uratibu Steven Wassira na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba.
Katika orodha hiyo pia yumo waziri mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya kampuni tata ya kufua umeme ya Richmond, Edward Lowassa, pamoja na waziri wa zamani wa Nishati na Madini, William Ngeleja.
Wiki iliyopita, baadhi ya wawania urais watarajiwa hao waliohojiwa walizungumza na waandishi wa habari wakipinga harakati za kusaka urais kwa matumizi ya fedha, harakati ambazo ziliwahi kumkera mno hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliyewahi kusema; Ikulu si mahali pa kukimbilia, ni mahali patakatifu na ukiona mtu anapakimbilia huyo anastahili kuogopwa kama ukoma.
Mmoja wa waliozunguma ni Januari Makamba, ambaye alisema urais wa kutumia fedha ili kuupata ni hatari kwa chama chao, CCM, akiungana na Membe pamoja na Sumaye. Lowassa kwa upande wake alisema mazungumzo aliyoitiwa yalilenga zaidi kuimarisha CCM kuelekea 2015.
Nape amesema kwamba adhabu hiyo ni sawa na kifungo cha nje ambacho mtuhumiwa huwa chini ya uangalizi maalumu akitakiwa kutofanya kosa lolote la ukiukaji wa maadili, vinginevyo atachukuliwa hatua kali zaidi.
Mbali ya adhabu huyo, CCM inaendelea kufuatilia mawakala na wapambe wa wawania urais hao waliotajwa kuhusika na ugawaji wa fedha na mambo mengine ya ukiukaji wa maadili, kwa lengo la kuwachukulia hatua kwa mujibu wa kanuni na taratibu za chama hicho.
“Walithibitika kuanza kampeni za kutafuta kuteuliwa kugombea urais kabla ya wakati kinyume na Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM Toleo la Februari 2010, Ibara ya 6 (7) (i).
“Wamethibitika kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya chama na baadhi yao kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya jamii. Kosa hili nalo ni kwa mujibu wa Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM,” inaeleza taarifa ya Nape kwa waandishi wa habari jana Jumanne.
Kamati Kuu ya CCM pia imewaonya viongozi na watendaji wa chama hicho kwa kuwataka kujiepusha kujihusisha na matendo ya wanaowania urais yanayovunja na kukiuka maadili ya chama na kwamba chama hicho kimewataka kuzingatia kanuni na taratibu za chama hicho.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa chama hicho mjini Dodoma wamesema kwamba uamuzi huo mwa Kamati Kuu ni muendelezo wa kuzidi kushindwa kuwachukulia hatua wanaokiuka maadili ndani ya chama hicho.
“Tuliita watu ‘magamba’ na kwamba tutavua magamba na hakuna kilichotokea, leo tunakuja na jambo jipya la kuwakaripia wote walioitwa wakati kila mmoja ana makosa yake na kwa uzito unaotofautiana. Hii kwa kweli ni ‘funika kombe mwanaharamu apite,” anasema mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kutoka mkoa mmoja wa Kanda ya Ziwa.
src-raia mwema