
Ukweli ni kwamba kuna umuhimu mkubwa wa wale waliofanikiwa katika maisha kuwakumbuka na kuwasaidia wasiojiweza lakini kwa wale wazima, wenye afya na nguvu za kutosha hawastahili kusaidiwa bali wanatakiwa kutumia vile walivyojaaliwa na Mungu kuhakikisha wanaendesha maisha yao bila kuwa tegemezi.
Wengi wa waliobahatika kuwa na mafanikio walichagua mafanikio, waliuchukia sana umaskini kiasi cha kulazimika kupambana vilivyo ili kuhakikisha wanaondokana na maisha duni na ya utegemezi.
Hiyo inaonesha kwamba kila mtu kama atachagua mafanikio na kuchukia maisha ya utegemezi anayo nafasi ya kubadili maisha yake na kuondokana na maisha duni.
Hata maandiko matakatifu yanaeleza kwamba miongoni mwa yale yanayomchukiza Mungu ni pamoja na kitendo cha mtu ambaye ana uwezo wa kutafuta na akapata kwa kufanya kazi na kujikimu mahitaji yake lakini kabweteka na kutegemea msaada kutoka kwa wengine.
Wapo watu huko mtaani ambao eti kwa sababu mmoja kati ya ndugu zao ana uwezo kifedha basi hawataki kabisa kujishughulisha huku wakiweka akilini kwamba ‘flani yupo, atanisaidia.’
Ni sawa, mtu yeyote kama anao uwezo ana haki ya kusaidia ndugu zake pale inapobidi lakini si vibaya kwanza wewe ukajiuliza, umejisaidiaje kwa nguvu na akili ulizopewa na Mungu na umeshindwa wapi?
Usikae tu ukabweteka na kutegemea fulani atakusaidia, fahamu na huyo fulani ana majukumu yake.
Si kwamba kwa sababu ana uwezo basi kila siku atakuwa akiangalia nani ana tatizo amsaidie, kuna kipindi atakuwa hana uwezo wa kukusaidia, je utaishije kama wewe mwenyewe hujajiwekea msingi imara wa maisha yako?
Waliobahatika kuwa katika nafasi nzuri kimaisha ni mashahidi wa usumbufu wanaoupata kutoka kwa watu wa karibu yao ambao hawataki kujituma kufanya chochote katika maisha yao.
Wao wanategemea tu kusaidiwa licha ya kwamba wakiamua kujituma kwa bidii wanaweza kuondokana na hali duni waliyo nayo.
Tusijaribu kuutengeneza ugumu kwenye maisha. Kwani hao ambao maisha yao ni mazuri wana akili ya aina gani? Je, wao wana vichwa viwili na mikono minne? Hapana! Naamini ni watu wa kawaida tu kama mimi na wewe.
Kikubwa ambacho kimewafanya waishi maisha hayo ni kuuchukia umaskini.
Anza leo kuchukia maisha ya kupiga mizinga watu, ona aibu! Pambana kutafuta maisha yako na hata pale utakapokuwa umekwama, watu watakusaidia. Unatakiwa uanze kujisaidia mwenyewe kabla hujafikia hatua ya kusaidiwa.
Kwa kumalizia nishauri tu kwamba, ukitaka kufanikiwa katika maisha chukulia mafanikio ya wengine kama changamoto kwako. Unapoona mwenzako kafanikiwa, kaa chini na uumize kichwa. Jiulize kama wengine wanakula bata kwa nini wewe uishi maisha ya kuungaunga?
Wapo wanaosema wamejaribu lakini wameshindwa, sawa lakini kumbuka hakuna kushindwa wala kukata tamaa katika kutafuta maisha mazuri. Hivyo kuwa tayari kupambana mpaka siku unaingia kaburini.