Saturday, May 10, 2014

Tamko la TUCTA kuhusu deni la Taifa na matumizi mabaya ya kodi


TAMKO LA SHIRIKISHO LA VYAMA VYA WAFANYAKAZI TANZANIA [TUCTA] KUHUSU DENI LA TAIFA NA MATUMIZI MABAYA YA FEDHA ZA WALIPA KODI.


Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania [TUCTA] limeshangazwa na kustushwa na deni kubwa linalowakabili Watanzania kama ilivyogunduliwa na taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali aliyoitoa Bungeni hivi karibuni.

Sisi kama tabaka la Wafanyakazi tunampongeza kwa kazi yake nzuri ambayo ndiyo iliyomfanya ateuliwe Mfanyakazi Bora katika Sherehe za Mei Mosi Mwaka 2014.

Matumizi yasiyokuwa ya lazima yanayokosa vipaumbele ndiyo yamelifikisha taifa letu katika deni hili la

Shs.21.2 Trilioni ambalo limeendelea kupanda mwaka hadi mwaka.

Kutokuwepo kwa umakini katika matumizi ya ndani ya Serikali ikiwemo manunuzi ya magari kwa pesa za Serikali na Wizara ya Viwanda na Biashara na baadaye kuandikishwa katika namba binafsi ni dalili za ufisadi na ubadhilifu wa hali ya juu, aidha matumizi ya kizembe Tanesco, Mamlaka ya Bandari, Stamico, Ngorongoro Conseration Authority, Medical Stores na Tanzania Coffee Board ni dalili za kukosekana misingi ya utawala bora. Swala la Wafanyakazi hewa limezidi kuwepo japo Waziri mwenye dhamana ya Wafanyakazi wa Umma alituahidi hapo mbeleni kwamba hili halitokuwepo tena.

Sisi kama Umoja wa Wafanyakazi tunaiomba Serikali iifanyie kazi taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu ili wale wanaohusika wachukuliwe hatua kali chini ya Sheria ya Kuhujumu Uchumi, aidha hatupendi kuona kazi nzuri ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali ikizidi kuwa mchezo wa sinema kila mwaka bila hatua zozote kuchukuliwa.

N.E. Mgaya,
KATIBU MKUU