Tuesday, May 20, 2014

ASHA BARAKA ANASUBIRI RASIMU YA KATIBA ILI AFANYE UAMUZI

.
Asha Baraka akiwa an wahariri wa…


Asha Baraka akiongea na wanahabari wa Global Publishers Ltd (hawapo pichani).
Na Elvan Stambuli
ASHA Baraka Msiilwa ni mwanasiasa kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec).
Mbali na siasa, Asha ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Aset inayomiliki Bendi ya The African Stars ‘Twanga Pepeta’.
Asha Baraka akiwa an wahariri wa Global Publishers.
Ijumaa iliyopita alitembelea ofisi za gazeti hili zilizopo Bamaga, Mwenge jijini Dar na kuzungumza na waandishi kupitia safu hii ya Live Newsroom ambapo alifafanua mambo kadhaa aliyoulizwa.
Asha alianza kwa kupigwa swali kuhusu kugombea ubunge mwakani tetesi ambazo zimeenea sana. Hata hivyo, alisema hawezi kusema chochote kuhusu hilo kwa sababu rasimu ya katiba ndiyo kwanza inajadiliwa bungeni na hajui itasemaje.
Akizungumzia safari yake ya siasa, Asha ambaye pia anajulikana kwa jina la ‘Iron Lady’ anasema:
“Nilipata ujumbe wa NEC kupitia nafasi ya Wilaya ya Uvinza (Kigoma) baada ya kuwashinda wanawake wengine 13 waliogombea. Mimi nilishika nafasi ya 10, hivyo nikapita.”
Baadhi ya maswali na majibu kati ya Asha na waandishi wa Global Publishers yalikuwa kama ifuatavyo:
Mwandishi: Tunaomba utueleze historia yako kwa kifupi.
Asha Baraka: Nilisoma Sekondari ya Tabora Girls na baadaye nikajiunga na Shirika la Bima la Taifa. Nilikuwa mdogo sana, miaka 17 tu. Pale Bima mbali ya kazi pia nilikuwa nachezea mpira.
Mwandishi: Ulikuwa unacheza michezo gani?
Asha Baraka: Nilikuwa nacheza netiboli, mpira wa kikapu na riadha na nilibahatika kucheza hadi ngazi ya taifa. Mwandishi: Uliingia lini katika siasa?
Asha Baraka: Nilijiunga na kuwa mwanachama wa CCM wakati nikiwa Shirika la Bima na tangu wakati huo nimekuwa mwaminifu kwa chama hadi leo na kuwa kiongozi wa ngazi mbalimbali wilayani hadi sasa mimi ni mjumbe wa Nec taifa.
Mwandishi: Kuwa kiongozi wa CCM na wakati huohuo unamiliki bendi, huoni kuwa unaweza kuwakimbiza wapenzi wa bendi yako wa itikadi nyingine?
Asha Baraka: Hapana! Twanga haihusiani kabisa na siasa na ndiyo maana huu ni mwaka wa tano inatumbuiza katika Ukumbi wa Bilicanas unaomilikiwa na Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe. Kwenye burudani bendi ipo tayari kupiga ikikodiwa na chama chochote cha siasa na mashabiki wetu wanajua hilo.
Mwandishi: Uliingiaje katika mambo ya muziki wa dansi?
Asha Baraka: Aliyeanza kumiliki bendi ya muziki ni kaka yangu anaitwa Ali Baraka. Alianzisha Bendi ya MK Group. Baadaye akapokewa uongozi na kaka yangu mwingine anaitwa Bakari Msii    lwa kisha nikaingia mimi.
“Awali bendi ilianza kwa kupiga katika mahoteli, wakati huo nilikuwa na wanamuziki kadhaa kama vile Nyoshi El Saadat na Mafumu Bilali Bombenga.”
AWATAJA ALIOANZA NAO TWANGA
Akizungumzia alivyoanzisha Twanga, Asha alisema:
“Baadaye nikaachana na MK Group na kuanzisha Bendi ya The African Stars nikiwa na wanamuziki kama  Banza Stone (Ramadhan Masanja), Luiza Mbutu, Adolf Mbinga, Abuu Semhando, Joseph Watuguru na wengine ambao siwakumbuki kwa sasa.
“Tuliamua kuachana na muziki wa kupiga kwenye mahotelini sasa tukaanza kupiga kwa kiingilio kwenye kumbi za kukodi.”
Mwandishi: Ushindani ulikuwaje wakati huo?
Asha Baraka: Ulikuwa mkubwa, tulikuwa tunapambana na Bendi ya Diamond Sound ‘Ikibinda Nkoi’ ya Joseph Rwegasira.
Mwandishi: Ipo dhana kwamba kwa kuwa wewe ni wa Kigoma unatumia ushirikina katika bendi na ndiyo maana kwenye ukumbi wenu wa nyumbani (Mango Garden), bendi nyingine zikipiga, zinapigia viti, hawapati wateja, unasemaje kuhusu hilo?
AKANA WATU WA KIGOMA KUWA WASHIRIKINA
Asha Baraka: Hapana, watu wa Kigoma ni wacha Mungu wawe Waislamu au Wakristo na mimi ni mmoja wapo. Wanaokosa wateja ni kutokana na muziki wao kutokidhi haja ya wapenzi wa muziki wa dansi.
Mwandishi: Unasemaje kuhusu kukimbiwa na wanamuziki, hakuathiri bendi inapotokea hivyo?
Asha Baraka: Athari ipo lakini niseme tu kwamba najivunia sana wanamuziki wanaopata maendeleo kutokana na kupitia katika mikono nyangu, wapo wengi ni zaidi ya mia moja.
“Kwa kuwa anapotoka katika bendi yangu anakwenda kutafuta maisha, huwa siwazuii. Mfano mzuri ni Charles Mbwana (Chaz Baba), nilimruhusu. Mwanamuziki yeyote akiamua kurudi huwa nampokea kwa kuwa Twanga ni kama nyumbani kwao.”
AKIRI MUZIKI WA DANSI KUDORORA
Mwandishi: Kwa nini muziki wa dansi siku hizi unadorora?
Asha Baraka: Unadorora kweli na tusipoangalia tutauua kabisa.
Bendi zote zina mifumo mipya, sebene ni zilezile hata kama mwanamuziki atatoka bendi hii kwenda nyingine nyimbo atakazoimba kule ni zilezile alizokuwa akiimba akiwa bendi aliyotoka. Mbaya zaidi siku hizi bendi nyingi zinaimba nyimbo za kukopi kitu ambacho kinaua kabisa muziki wa dansi.”
ASEMA MUZIKI HAUNA FAIDA
Mwandishi: Umefaidika na nini katika muziki wa dansi tangu uanze kujishughulisha nao?
Asha Baraka: Sijafaidika kabisa. Nyumba niliyonayo niliipata nilipokuwa Bima, shirika lilinidhamini CRDB, nikajenga. Faida kubwa katika muziki niliyoipata ni kufahamika tu ndani na nje ya nchi.
AMZUNGUMZIA ALI CHOKI
Mwandishi: Mwisho, kuna bifu kati yako na Ali Choki yule kiongozi wa Extra Bongo, huoni kuwa kuna haja ya kupatanishwa?
Asha Baraka: Mimi sijasema kibaya kwa Choki, yeye ndiye alisema akifa nisiende kumzika. Lakini sisi ni Waislamu, hilo linakatazwa na dini. Akifa kabla ya mimi nitakwenda msibani kwa kuwa najua atakuwa hajijui. Nasikitika kusema kuwa alichokisema ni tofauti na mafundisho ya Uislamu.

src
GPL