
Mpendwa msomaji wangu, nadhani unafahamu kwamba wengi wetu hasa wale ambao wako katika maisha ya ndoa wanatarajia kitu kimoja ambacho kinaweza kuongeza furaha na amani, nacho si kingine bali ni mtoto.
Kwa kawaida haijalishi ni mtoto wa jinsia gani licha ya kwamba, kuna baadhi ya wazazi wanaosema; ‘Nikipata mtoto wa kiume nitafurahi sana’. Wengine watakuambia wanataka watoto wa kike ili mradi kila mmoja ana chaguo lake.
Swali ni je, mara baada ya kupata mtoto uliyekuwa ukimuota, uko tayari kumpa malezi yanayostahili ili aje kuwa mzazi bora hapo baadaye?
Kuna baadhi ya wazazi huwa na ndoto ya kupata watoto katika maisha yao ya ndoa, lakini suala la kuwalea linakuwa zito kiasi cha kusababisha watoto wengine kuzagaa mitaani huku baadhi yao wakionekana kuwa na tabia zisizostahili.
Hii yote inatokana na wazazi kushindwa kutambua wajibu wao kwa watoto wao. Wanadhani wakishawazaa basi tena kinachofuta ni kutafuta mtoto mwingine bila kujua huyu wanamuandaa vipi kuja kuishi maisha mazuri baadaye.
Kimsingi unapopata mtoto unatakiwa kuhakikisha unamlea katika mazingira mazuri yenye mwelekeo wa kumfanya kuja kuwa mzazi bora na jamii inayomzunguka imuige.
Nadiriki kusema hivyo kwa sababu wengi unaowaona wamefanikiwa katika maisha yao ni lazima kwa namna moja ama nyingine wazazi wao wamechangia.
Ni kweli wapo ambao wamepambana wenyewe katika kusaka mafanikio lakini ni ukweli usiopingika kwamba, mwanga waliopata toka kwa wazazi ndio uliochangia kwa kiasi kikubwa kufanikiwa.
Kuna mambo ya msingi sana ambayo mzazi anatakiwa kuhakikisha mwanaye anayapata kuanzia utotoni, mambo ambayo yanaweza kuja kumfanya kuwa na maisha mazuri na mfano bora wa kuigwa. Waswahili wanasema; ‘Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo.’
ELIMU SAHIHI
Nilishawahi kuzungumza katika moja ya makala zangu zilizopita kuhusu mambo ya msingi ambayo mzazi anatakiwa kuyazingatia pindi anapofikiria juu ya elimu kwa mtoto wake.
Hakuna asiyejua kwamba elimu ni ufunguo wa maisha, hivyo mzazi anatakiwa kuhakikisha anafanya kadri awezavyo, kwa kuuza maandazi ama kufanya vibarua ili aweze kumpatia mwanaye elimu ya kutosha na bora.
Hiyo itamfanya aweze kuja kuyaendesha maisha yake vizuri baadaye na asije kuwalaumu wazazi kwa kuwa na maisha mabaya kutokana na kushindwa kumpatia elimu inayostahili.
KUJIAMINI!
Kitu ambacho wazazi wengi wanakosea kwa watoto wao bila kujua kwamba kitakuja kuwaathiri hata watakapokuja kuwa wakubwa, ni kuwajengea mazingira ya kuwa wanyonge, wanaojihisi hawawezi.
Suala la kujiamini ni la msingi sana kwa kila binadamu ili aweze kufanikiwa katika maisha yake na kujiamini huko kunajengeka kuanzia utotoni.
Mtoto anatakiwa apewe uhuru wa kueleza hisia zake na kusikilizwa pale anapodhani anastahili kuzungumza mbele ya wazazi wake. Ajifunze kupitia kufanya makosa, asiadhibiwe kwa makosa ambayo huenda yanamjenga kiakili.
Kwa mfano, unapomkuta mwanao anawasha taa ya umeme, ujue anafanya hivyo baada ya kuona wakubwa wakiwasha, hivyo naye anataka kuiga, siyo mbaya licha ya kwamba ni hatari.
Itaendelea wiki ijayo.
src
GPL