JITIHADA za Serikali katika kuhakikisha ubora wa elimu unapanda zimeanza kuzaa matunda katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne kwa mwaka 2013 ambayo yameonesha kupanda kwa kiwango cha ufaulu.
Mafanikio haya yametokana na mikakati ambayo Serikali imejiwekea katika Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa ambao una lengo la kuboresha elimu na kubadili mwenendo wa matokeo katika ngazi ya elimu ya msingi na sekondari. Katika matokeo ya mwaka 2013 kwa ujumla yanaonesha kupanda kwa asilimia ya ufaulu ikilinganishwa na matokeo ya miaka miwili iliyopita.
Kwa mwaka 2011 ufaulu ulikuwa asilimia 53.6 na kwa mwaka 2012 ufaulu ulishuka na kuwa asilimia 43.0 lakini mwaka jana ufaulu ulipanda hadi kufikia asilimia 58.25. Akizungumzia upandaji wa ufaulu huu, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa anasema taarifa zilizotolewa na Baraza la Mitihani la Tanzania zinaonesha hata katika masomo yaliyo mengi ya msingi ufaulu umepanda ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Kawambwa anasema kwa masomo ya Hisabati kwa mwaka 2012 asilimia ya ufaulu ilikuwa 12.14, kwa mwaka 2013 asilimia ya ufaulu iliongezeka kwa 5.64 na kufikia asilimia 17.78. Kwa somo la Fizikia mwaka 2012 asilimia ya ufaulu ilikuwa 43.51, mwaka 2013 imepanda na kufikia asilimia ya ufaulu 44.12 wakati kwa somo la Kemia ufaulu umeongezeka kwa asilimia 0.61 na kufanya asilimia ya ufaulu kufikia 44.12 kwa mwaka 2013.
Akielezea ulinganifu wa ufaulu kwa shule za serikali na zisizo za serikali, Dk Kawambwa anasema kwa muda mrefu kumekuwa na maoni mbalimbali kuhusu ulinganifu wa ufaulu baina ya shule za serikali na zile zisizo za Serikali. Zikipangwa kwa ubora wa ufaulu, shule zisizo za Serikali hususani za wasichana zimeonekana kuchomoza zaidi na kufanya shule 10 bora zote kuwa ni zile zisizo za Serikali.
Katika suala hili Dk Kawambwa anasema ni vema wananchi wakatambua kwamba shule hizi zinachukua wanafunzi bora ambao wanafanya vizuri zaidi katika mitihani yao ya kumaliza elimu ya msingi kutoka shule za Serikali na chache za binafsi.
“Wakati mwingine huwafanyisha mitihani ya kuchuja na kusajili wanafunzi wa kidato cha kwanza hata kabla serikali haijatangaza matokeo ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza,” anasema. Kwa upande wa shule za wananchi, Dk Kawambwa anasema sio kweli kwamba shule zote zinafanya vibaya kwani zipo shule nyingi zinazofanya vizuri katika mitihani ya kitaifa.
Anazitaja baadhi ya shule hizo kuwa ni Shule ya Sekondari Tukuyu kutwa yenye ufaulu wa asilimia 92.4, na Shule ya Sekondari Kayuki yenye ufaulu wa asilimia 96. Anasema shule ambazo bado zinafanya vibaya ni zile zenye changamoto mbalimbali kama vile upungufu wa walimu, ukosefu wa nyumba za walimu, maabara na vyumba vya madarasa.
Anasema Serikali inazifahamu changamoto hizi na tayari imeanza kuzifanyia kazi ambapo katika Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa katika sekta ya elimu mkakati mmojawapo ni ujenzi wa miundombinu ya shule.
Hata hivyo, pamoja na matokeo kuonesha kuwa hakuna shule ya serikali zikiwemo za vipaji maalum iliyoweza kushika nafasi katika shule 10 bora, ukweli ni kuwa hali ya ufaulu katika shule hizi bado ni nzuri na haipishani sana na shule nyingine zisizo za serikali zilizofanya vizuri zaidi.
Anatoa mfano kuwa wanafunzi waliopata daraja la I ni 194, II ni 99 na III ni 59 ambapo waliopata daraja IV ni 37 kwa shule za Mzumbe, Ilboru, Kibaha na Tabora Boys. Dk Kawambwa anasisitiza kwamba katika shule hizi zilizotolewa mfano hapo juu, hakuna wanafunzi waliofeli kwa daraja la sifuri.
Aidha, katika shule hizi zaidi ya asilimia 90 ya wanafunzi wake walipata kati ya daraja la kwanza hadi la tatu na hivyo wako kwenye kundi la wale wenye uwezekano wa kuendelea na masomo ya kidato cha tano. Aidha anasema wastani wa nusu ya wanafunzi kwenye shule hizo walipata ufaulu wa daraja la kwanza.
“Tulipofikia ni mahali pazuri kwa sababu tuko karibu kabisa na malengo tuliyojiwekea. Pamoja na kwamba kupanda kwa ufaulu katika matokeo ya mwaka huu kunaweza kuwa kumechangiwa na mambo mbalimbali, nadiriki kusema kuwa Utekelezaji wa mikakati yetu ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa umechangia kwa kiasi kikubwa kutufikisha hapa tulipo,“ anasema Dk Kawambwa.
Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now) ni miongoni mwa mkakati wa Serikali wenye dhamira ya kuimarisha mazingira ya kujifunza na kufundishia na kuhakikisha kwamba kiwango cha ubora wa elimu inayotolewa kinaongezeka.
“Wakati tunazindua mpango huu tulijiwekea malengo ya kupandisha ufaulu katika mitihani ya elimu ya msingi na sekondari kutoka asilimia 31 kwa elimu ya msingi na 43 kwa elimu ya sekondari hadi asilimia 60,” anasema Dk Kawambwa. Akielezea mikakati ya mpango huu iliyokwishanza kutekelezwa na kuonesha mafanikio, Dk Kawambwa anasema ni pamoja na ule wa upangaji wa shule kitaifa kwa kuzingatia ubora wa ufaulu wa shule katika mtihani.
Matokeo ya mwaka 2012 yalipangwa kwa makundi ya kijani, njano na nyekundu kulingana na ufaulu na kuwekwa wazi kwa jamii. Mkakati huu umeinua ari ya shule mbalimbali katika kuhakikisha zinapanda katika ufaulu. Mkakati wa pili kutekelezwa chini ya Mpango wa Matokeo Mkubwa Sasa ni Programu ya Kuboresha Uwezo wa Walimu na Wanafunzi (STEP).
Mafunzo yamekuwa yakitolewa kwa walimu. Zaidi ya Walimu 8,000 wa masomo ya Sayansi na Hisabati wamepatiwa mafunzo. Mitihani ya majaribio ilitolewa kwa wanafunzi na mada ngumu kuainishwa. Kiongozi cha Kuboresha Taaluma Shuleni kiliandaliwa na mafunzo kwa wakuu wa shule kutolewa ili kuongeza ubora wa menejimenti na utawala.
Akielezea mpango wa Serikali wa kuzitambua na kuzizawadia shule zilizofanya vizuri katika mitihani ya kitaifa, Dk Kawambwa anasema kupitia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa, serikali itatoa tuzo kwa shule zilizofanya vizuri na zile zilizoonesha maendeleo ya juu ambapo katika mwaka 2013 jumla ya shule 4,000 zikiwemo za sekondari 1,000 na za msingi 3,000 zitapewa tuzo katika maadhimisho ya wiki ya elimu yatakayofanyika katika ngazi za Wilaya, Halmashauri, Mikoa na hatimaye kitaifa kila mwaka.
Dk Kawambwa amewataka watendaji kuboresha utendaji kazi wao ili kufikia matarajio ya taifa letu ya kuwa na watu walioelimika na wenye uwezo wa kuhimili changamoto zinazotokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
“Tuache kufanya kazi kwa mazoea na badala yake tuhakikishe tunapanga mipango yetu, tunajiwekea malengo ya muda mfupi na mrefu na kubuni mikakati sahihi inayotekelezeka ambayo itatuwezesha kufikia malengo tuliyojiwekea hususan ya kuinua ubora wa elimu,” anasisitiza Dk Kawambwa.
Anatoa Mwito kwa wazazi, walezi, wanafunzi na jamii kwa ujumla kushirikiana kwa hali na mali katika kuhakikisha kuwa elimu itolewayo inakidhi viwango tarajiwa kwani jukumu la utoaji wa elimu bora nchini ni letu sote.
src
Habari Leo