HASSAN Nassoro Moyo, ni kati ya waasisi wawili wa Muungano kwa upande wa Zanzibar ambao mpaka sasa bado wako hai. Mwingine ni Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi.
Moyo ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 80, ni Waziri wa kwanza wa Sheria aliyekula kiapo cha utii na uaminifu mbele ya Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano, Hayati Mwalimu Julius Nyerere Aprili 27 mwaka 1964, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Yeye ni miongoni mwa wajumbe 20 kutoka Bara na Zanzibar walioongozwa na Hayati Shekhe Thabit Kombo kuunda Katiba ya Chama Cha Mapinduzi kilichozaliwa Mwaka 1977 ambapo Katiba hiyo ilifanyiwa marekebisho kidogo na kuzaa Katiba ya Muungano inayotumika sasa na ambayo ipo katika hatua za mchakato wa marekebisho yake.
Wiki hii gazeti hili liliteta na Mzee Moyo kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kufafanua kwamba umekuja kutokana na mahusiano ya asili ya kindugu yaliyokuwepo tangu na tangu. Anasema uhusiano baina ya watu wa Tanganyika na Zanzibar ni wa kindugu na wa damu na ndio kwa sehemu kubwa uliochangia kuwepo kwa Muungano ambao sasa unaelekea miaka 50 tangu kuzaliwa kwake.
Anafafanua kwamba tangu miaka ya 1920 tayari wananchi wa pande mbili hizi za Muungano walikuwa wamejenga mahusiano makubwa ya kindugu na kibiashara ambapo wananchi wa makabila mbalimbali kutoka Bara walikuwepo Zanzibar na kinyume chake. Anayataja makabila kama Wandengereko, Wazaramo, Wamakonde na Wamanyema kwamba ni watu waliokuwa wameweka makazi yao Zanzibar miaka mingi na kujenga mahusiano makubwa ya kuoana na kuzaliana.
“Ni sawa mtu kusema kwamba Muungano wa Tangayika na Zanzibar ulikuja kwa mambo mawili makubwa... Kwanza wananchi wa pande mbili hizi walikuwa tayari wamechanganya damu na kujenga mahusiano makubwa lakini la pili ni matokeo ya mkutano wa PAFMECA (Pan-African Freedom Movement of East and Central Africa ) uliotaka bara la Afrika kuwa nchi moja,” anasema.
Pafmeca ulikuwa ni Umoja wa Vyama vya Ukombozi vya Afrika Mashariki na Kati vilivyoamini pia katika kuliunganisha Bara zima la Afrika. Mkutano wake wa kwanza kabisa ulifanyika Mwanza, Tanganyika tangu Septemba 16 hadi 18 mwaka 1958 kwa lengo la kusimamia na kushirikiana katika harakati za kulikomboa eneo la Afrika Mashariki na Kati.
Mzee Moyo anasema viongozi wawili, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Shekhe Abeid Amaan Karume walikuwa na hamasa kubwa ya kuona Bara la Afrika linaungana na kuwa nchi moja. Anasema muungano huu ni matokeo ya mikutano mbalimbali ya viongozi wa Afrika katika harakati za ukombozi wa bara hili kutoka kwa wakoloni ambapo zilikuwa na mwamko mkubwa kutoka kwa viongozi kama Kwame Nkrumah na hayati Gamal Abdul Naser wa Misri.
“Dhamira ya Bara la Afrika kuungana zinatokana na mikutano ya Pafmeca iliyofanyika katika nchi mbalimbali ikiwemo Ghana na Malawi katika miaka ya 19050 ambayo ilikuwa ikisisitiza umuhimu wa viongozi wa bara la Afrika kuungana kwa ajili ya kupambana na wakoloni,” anasema.
Hata hivyo, Mzee Moyo kwa masikitiko makubwa anasema kwamba dhamira na nia hiyo ya kuliunganisha bara zima la Afrika haikufikiwa isipokuwa Tanganyika na Zanzibar tu ndiyo zilizofikia makubaliano ya Muungano.
“Lengo na dhamira ya Bara la Afrika kuungana kwa bahati mbaya haikufikiwa isipokuwa sisi Zanzibar na Tanganyika tuliungana na kuzaliwa taifa jipya la Jamhuri ya Muungano tu ambao hadi leo tupo katika Muungano huo wa kupigiwa mfano,” anasema.
Akifafanua zaidi, Moyo anasema wakati ule wa harakati za uhuru kulikuwa na uhusiano mzuri baina ya viongozi wa vyama vya Afro Shirazi Party (ASP) na Tanganyika African National Union (Tanu) na kwamba kwa kiasi kikubwa ulichangia kuwepo kwa muungano wa Serikali mbili mara baada ya nchi hizo kupata uhuru.
Moyo anatoa mfano kwamba Hayati Mwalimu Nyerere alifanya kazi kubwa ya kuzaliwa kwa chama cha ASP na kuona kinakuwa na nguvu na uwezo wa kupambana na vyama vya upinzani vya wakati huo. “Nyerere alisaidia sana harakati za kuimarisha ASP ili iwe na nguvu za kupambana na utawala wa Sultani wa Oman,” anasema Moyo.
Moyo anampongeza Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kwa uwezo wake wa hekima na ushawishi wake mkubwa unaotokana na kukubalika katika siasa za Tanzania. Nini maoni ya Mzee Moyo kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao unafikia umri wa miaka 50 sasa?
Mwasisi huyo anasema hakuna mtu anayekataa Muungano katika umri uliofikia sasa wa miaka 50 isipokuwa watu wanataka mabadiliko na kuona Muungano unakuwa ni wenye tija, ukiwanufaisha zaidi wao kuliko viongozi waliopo madarakani sasa. Anasema hata Hayati Karume alipata kuwaambia wananchi kwamba faida za Muungano ni kwa wananchi wa Zanzibar kutumia fursa za kiuchumi zilizopo eneo jingine la Muungano la Tanzania Bara kufanya kazi zao na kuimarisha maisha.
Kadhalika Mzee Moyo aliyetumikia nafasi mbali mbali akiwa Waziri katika Serikali ya Muungano na mtu aliyekuwa kipenzi cha Mwalimu Nyerere, anasema Muungano uliopo sasa unatakiwa kujikita zaidi katika uchumi na maendeleo kwa pande mbili hizi za Muungano. Kwa mfano, anasema, mengi yanatakiwa kufanyika ili wananchi waweze kutumia fursa ziliopo ikiwemo kuondoshwa kwa matatizo ya ushuru wa bidhaa zinazotoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara ili kuinua vipato vyao.
“Hili tatizo limekuwa likilalamikiwa miaka mingi na wafanyabiashara wa Zanzibar wanaosafirisha bidhaa zao kwenda Tanzania Bara na kutoka nje ya nchi kwamba wanasumbuliwa na kulipa ushuru mara mbili,” anasema. Anawataka viongozi waliopo madarakani kuzifanyia kazi changamoto mbali mbali za Muungano ambazo zimegeuzwa jina na kuitwa ‘kero’ ili wananchi wa pande mbili waone faida na matunda ya Muungano.
Mzee Moyo anachukua nafasi hii pia kumpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kuchukua uamuzi wa busara kwa kuleta mchakato wa marekebisho ya katiba ambao kwa sasa umefikia hatua nzuri ya wajumbe wa Bunge la Katiba kujadili baada ya kukamilika kwa rasimu ya Katiba.
Mzee Moyo aliyehudhuria sherehe za kuzinduliwa kwa rasimu ya pili ya Katiba katika viwanja vya Karimjee Hall, ambapo rasimu ya Katiba yake alikabidhiwa mkononi na Rais Jakaya Kikwete, anasema historia itamkumbuka Rais Kikwete kwa hatua hii chanya.
“Ninampongeza kwa dhati kabisa Rais Jakaya Kikwete kwa ujasiri wake wa kutoa nafasi kwa Watanzania kujadili mchakato wa Katiba ukiwa na lengo la kupata Katiba mpya itakayokwenda na wakati na kuimarisha Muungano wetu,” anasema Mzee Moyo.
Aidha, hata katika hatua ya sasa mchakato wa Katiba ulikofikia, Mzee Moyo angetamani kuona baadhi ya watu wakishirikishwa ili kupatikana kwa Katiba bora ambapo anasema wapo wengi wenye uwezo mkubwa lakini hawajashirikishwa ipasavyo.
Mzee Moyo, kwa mfano, anamtaja aliyekuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Pius Msekwa kwamba ni ‘mtaalamu’ aliyebobea katika masuala ya Katiba na Bunge ambapo katika Bunge la kwanza la Jamhuri ya Muungano mwaka 1964 alikuwa Katibu.
“Huyu Msekwa wakati nakula kiapo pale kuwa Waziri wa Sheria alikuwa Katibu wetu wa Bunge na hata tulipounda Katiba ya mwaka 1977 tulikuwa naye kama mjumbe kutoka Bara... Kwa nini hashirikishwi katika michakato kama hii pamoja na mwenzake Bomani?” Anahoji.
Moyo ambaye ni mzaliwa wa Mkoa wa Ruvuma, Songea, mchango wake katika vuguvugu la Mapinduzi ya Zanzibar na Muungano kwa ujumla ni mkubwa sana. Mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar alishika wadhifa wa kuwa Waziri wa Nchi anayehusika na Njia za Umeme na Nishati na mara baada ya kuzaliwa kwa Muungano alichaguliwa kuwa Mbunge na Waziri wa Sheria.
Anasema baada ya kufanya kazi katika serikali ya Muungano kwa ufanisi mkubwa kama Wizara ya Sheria, Hayati Karume alimuomba kwa Nyerere kuja Zanzibar kusaidia kufanya kazi ambapo alimteua kuwa Waziri wa Kilimo. Mwaka 1977 alichaguliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, nafasi ambayo kwa miaka mingi huchaguliwa kiongozi kutoka Zanzibar kushika wadhifa yake.
Kufuatia mchango wake mkubwa na utumishi uliotukuka kwa serikali zote mbili pamoja na Chama Cha Mapinduzi, Moyo alipewa nishani ya utumishi bora na takriban marais wote wa Jamhuri ya Muungano kuanzia na Hayati Mwalimu Nyerere, Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi pamoja na Rais Jakaya Kikwete.
“Nashukuru Mungu bwana, nimebahatika kuongoza nchi yetu na kushika nafasi muhimu na nyeti kwa serikali zote mbili. Nikafanya kazi kwa utii na uaminifu mkubwa,” anasema
src
Habari Leo