Thursday, April 3, 2014

Maumivu miaka 53 ya Uhuru bila Katiba ya wananchi

KWA miaka yote ya Uhuru, Tanzania haijapata kuwa na Katiba huru iliyotokana na wananchi wenyewe:  Katiba zote, kuanzia ya Uhuru ya 1961 (Tanganyika) hadi ya 1977, zimetokana ama na ubabe wa watawala au ubabe wa chama kimoja.
Katiba tarajiwa ambayo rasimu yake imewasilishwa kwenye Bunge Maalumu la Katiba hivi karibuni, kwa vigezo vyote vya demokrasia na utawala bora, itatokana na vyote viwili – ubabe wa watawala na ubabe wa vyama.  Na kama zilivyokuwa Katiba zilizoitangulia, itakuwa Katiba ya kibabe. 
Katiba ya Uhuru ya 1961
Katiba hii, iliyojulikana pia kama “The Tanganyika (Constitution) Order in Council” kwa lugha ya Kiingereza, ilitiwa sahihi na Malkia wa Uingereza na kushushwa kwetu kama “manna”.  Iliweka muundo wa Serikali na Bunge kwa mfumo wa Serikali ya Uingereza ujulikanao kama Westminster.  Katiba hiyo haikuwa na haikutambua haki za binadamu.  Kwa hiyo, ukatili wa vyombo vya dola haukuwa na mipaka wala tiba.
Chini ya ibara ya 46 (1) ya Katiba hiyo, Gavana wa Tanganyika (Sir Richard Turnbull), ambaye aliendelea kutawala kumwakilisha Malkia wa Uingereza kwa ombi maalumu la Waziri Mkuu wa kwanza, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hadi mwaka 1962, alipewa uwezo wa kutekeleza majukumu yake atakavyo bila kulazimika kufuata ushauri wa mtu yeyote; hulka ambayo imeendelezwa chini ya ibara ya 37 ya Katiba yetu ya sasa.
Katiba hii iliwakilisha kufikia kikomo cha utawala wa Kikoloni, na sifa yake pekee ni kwamba, ilisimika uhuru na ukuu wa Bunge lenye kuwakilisha wananchi kuwa juu ya mihimili yote ya dola na kwa Bunge kusimamia Serikali.
Katiba ya Jamhuri ya 1962
Katiba hii ilipatikana kwa mapambano kati ya tabaka la Wazalendo “vibwenyenye” ndani ya chama tawala cha Tanganyika African National Union – TANU, waliotaka Mwafrika pekee ndiye ashike sawia madaraka yote ya nchi, na kwamba uraia uwe ni kwa Waafrika tu, dhidi ya matakwa ya viongozi wapya wa chama na serikali waliotaka usawa kwa wote.
Mjadala ulikuwa mkali Bungeni, huku Mwalimu Nyerere (Waziri Mkuu) akiwatuhumu wenzake kugeuka “makaburu wabaguzi wa rangi”. Ni Richard Wambura, chini ya dhana ya ukuu wa Bunge, aliyeitolea uvivu Serikali kwa matamshi makali aliposema:  “Kamwe hatukubali kutishwa kwa mtindo alioonyesha Waziri Mkuu.  Sisi ni Wajumbe wa Bunge la Wananchi wenye kuwakilisha matakwa ya Wananchi; tuna haki ya kujadili bila hofu wala woga kile tunachoamini ni kwa maslahi ya wananchi”.
Akaendelea kuonya akisema, “tabia (hii) ya Serikali ya kuwatisha Wabunge ikome mara moja humu bungeni (Soma:  Tanganyika, National Assembly Official Reports, 36th Session, Vol. V; pg. 6, 18 October 1961).
Muswada wa Uraia ulipita kwa mbinde; na kuanzia hapo, Serikali ikaingiwa hofu ya mfumo wa demokrasia aina ya Westminster na kutafuta njia ya kuwaziba midomo wabunge.
Januari 16, 1962, kiliitishwa kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya TANU kwa shinikizo la wajumbe, waliotaka Gavana aondoke ili Tanganyika iwe Jamhuri; kufutwa kwa viti vya Bunge kwa ajili ya watu wa Mataifa wasio Waafrika (minority races) na kuharakishwa kwa zoezi la kujaza nafasi zilizoshikiliwa na Wazungu ziweze kushikwa na Waafrika (Africanisation).
Nyerere hakutarajia mashambulizi kama hayo yaliyomkumbusha mtafaruku kama huo bungeni juu ya Muswada wa Uraia, Oktoba 1961.  Akabaini mara moja kwamba nafasi yake na ile ya TANU ilikuwa rehani; akaamua kuachia ngazi ya nafasi ya Waziri Mkuu na kumwacha Rashidi Kawawa kushika nafasi hiyo.
Tafsiri iliyozoeleka, kwamba Mwalimu aliachia ngazi kurudi kijijini kuimarisha chama si sahihi.  Ukweli unathibitishwa na gazeti maarufu la New York Times la Februari 3, 1962 (safu ya mhariri) lilipoandika:  “Inaonekana kwamba Nyerere amekumbwa na mkasa unaowapata viongozi wa Kiafrika wenye siasa baridi (wasio wanamapinduzi). Jinsi alivyobanwa upesi upesi na mawazo (shinikizo) ya wanamapinduzi mpaka akang’olewa inatisha!
Hatua hiyo ilifungua mlango kwa mchakato wa Katiba kufanya Tanganyika kuwa Jamhuri; kwani Januari 16, 1962, NEC ya TANU ilikutana na kutoa pendekezo kwa Serikali, Tanganyika iwe Jamhuri ndani ya Jumuiya ya Madola, Desemba 9, 1962.
Akiwasilisha bungeni Muswada juu ya hili, wakati huo Nyerere akiwa back-bencher bungeni, Kawawa alitaja sababu kuu mbili:  kwanza ilikuwa ni kuanzisha nafasi ya mtawala (Rais Mtendaji, Rais beberu) mwenye nguvu na uwezo wa kutenda.
Pili, kuiwezesha Serikali kuingilia kikamilifu maisha ya wananchi na sekta za kijamii na kiuchumi bila kuulizwa ulizwa au kuhojiwa; Serikali yenye mamlaka hodhi na isiyowajibika kwa chombo  chochote.
Madhumuni ya Muswada huo yalikwenda kinyume na mfumo wa Westminster unaotambua ukuu wa Bunge katika kusimamia Serikali.  Ulizaa mtawala, “Rais beberu” kwa maana ya “Imperial Presidency” asiyehojika na ambaye rasimu ya Katiba ya sasa inakusudia kumpunguzia madaraka.
Katiba hii nayo haikutokana na wananchi, bali ilitokana na kikundi cha wanasiasa uchwara ndani ya chama waliokuwa na kiu ya madaraka.  Na ili kudhibiti uhuru wa kisiasa na wa kujieleza, vyama vyote vya siasa, mbali na TANU, vilitiwa kashkashi na kutoweka; viongozi wake ama walifukuzwa nchini au walitiwa kizuizini; haki ya kusajili vyama na kuendesha mikutano ilidhibitiwa.
Muungano wa Tanzania bila Katiba
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulianzishwa kwa njia ya dharura kwa shinikizo kutoka nje.  Hapakuwa na muda wa kuandaa Katiba katika mazingira kama hayo.
Kuokoa jahazi, na ili kuupa Muungano uhalali, iliazimiwa, chini ya Mkataba wa Muungano, ibara ya (ii), (iii) na (iv), kwamba, (ibara ii): “During the period from commencement of the Union until the Constituent Assembly provided for in Article (vii) shall have met and adopted a Constitution for the United Republic (which period referred to as interim period), the Constitution of the United Republic shall be the Constitution of Tanganyika so modified to provide for the basic union matters.
Kwamba, katika kipindi cha mpito hadi Bunge la Katiba litakapoitishwa kupitisha Katiba Jamhuri ya Muungano, Katiba ya Muungano itakuwa ndiyo hiyo hiyo Katiba ya Tanganyika itakayorekebishwa kuingiza mambo ya Muungano.
Mkataba haukutaka kuingilia mambo ya Serikali za Tanganyika na Zanzibar na Sheria zake zinazosimamia mambo yasiyo ya Muungano.  Ibara ya (v) inasema: “The existing laws of Tanganyika and Zanzibar shall remain in force in their respective territories…..”;
Kwamba, kufuatia Tanganyika na Zanzibar kuungana kuunda dola moja, “Sheria za Tanganyika zilizopo na Sheria za Zanzibar (kwa mambo yasiyo ya Muungano) zitaendelea kuwa na nguvu katika nchi hizo”, kwa maana ya nchi zisizokuwa dola.
Kwa tafsiri hii, wanaosema Zanzibar ni nchi isiyo dola hawajakosea; lakini swali la kujiuliza ni je, Tanganyika ilikwenda wapi baada ya kudumu kwa jina tu bila matendo hadi mwaka 1965?
Katiba ya 1965
Kuteuliwa kwa Tume ya kupendekeza Katiba ya chama kimoja mwaka 1963 chini ya Rashidi Kawawa, kulidhihirisha kiu ya kikundi cha wanasiasa uchwara kudhibiti demokrasia. 
Kati ya hadidu za rejea kwa Tume ilisomeka hivi:  “Ili kuondoa utata na kutoelewana, inasisitizwa kwamba, si jukumu la Tume kufikiria Tanganyika iwe ya chama kimoja au hapana, maana tayari uamuzi ulikwishachukuliwa na chama.  Kazi pekee ya Tume ni kusema tu ni aina gani ya Taifa la chama kimoja tuwe kwa kuzingatia maadili ya Taifa letu na kwa misingi niliyokwishaelekeza ifuatwe” (Soma: Report of the Presidential Commission on Establishment of a Democratic One Party State para 8, pg. 2).
Tume ya Rais ilikamilisha taarifa yake na kuwasilisha kwenye kikao cha pamoja cha NEC za TANU na Afro-Shirazi Party (ASP) Mei 3, 1963.  Maamuzi ya kikao hicho ndiyo yaliyoelekeza kutungwa kwa Katiba ya muda ya Muungano ya 1965 kufanya nchi kuwa ya chama kimoja.
Chini ya ibara ya 3 (3) ya Katiba hiyo, iliagizwa kuwa, shughuli zote za kisiasa (na za Serikali) nchini, zitafanyika chini ya na mamlaka ya chama pekee cha TANU.
Hapa tena, hapakuwa na ushirikishwaji wa wananchi kupata Katiba wanayotaka.  Kazi hii ilifanywa na vyama vya siasa ambavyo wanachama wake hawakufikia hata theluthi ya Watanzania, licha ya kwamba vyama vya siasa sio jambo la Muungano kuweza kugusa mambo ya Muungano.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya 1977
Katiba ya 1977 inasimama kwenye mafiga matatu iliyorithi kutoka Katiba ya 1962 na ya 1965 ambayo ni:  Kwanza, rais beberu (imperial presidency) asiyeambilika; pili, muundo wa serikali mbili; na tatu, serikali ya chama kimoja.
Kuingia kwa mfumo wa Vyama vingi vya Siasa mwaka 1992 na marekebisho yaliyofanyika hakujaiondolea Katiba harufu ya mafiga hayo.
Tume ya kupendekeza Katiba ilikuwa ya watu 20, wote kutoka CCM; na ni Tume hiyo hiyo iliyopendekeza kuunganishwa kwa TANU na ASP kuunda CCM.
Mapendekezo yaliwasilishwa kwenye kikao cha siri cha NEC.  Siku Tume hiyo ya Katiba ilipoteuliwa, ndiyo siku hiyo Bunge la Katiba (Constituent Assembly) ambalo wajumbe wake walikuwa wabunge wote wa Bunge la Muungano bila mwananchi hata mmoja lilipoteuliwa.
Mapendekezo ya Tume/NEC yaliwasilishwa kwenye Bunge la kawaida, Aprili 25, 1977 na kujadiliwa kwa muda chini ya saa mbili kutokana na kile kiongozi wa shughuli za serikali bungeni, Makamu wa Pili wa Rais, Rashidi Kawawa, alisema “Maamuzi ya NEC hayajadiliwi”. Alisema, “Kwa kuwa mapendekezo haya yamekwisharidhiwa na NEC, Bunge hili halina mamlaka ya kwenda kinyume na kile kilichoridhiwa na NEC isipokuwa kupitisha tu”.
Mchakato wa Katiba mpya 2014
Mchakato wa Katiba mpya unaoendelea sasa, tofauti na michakato ya Katiba zote zilizotangulia, umefuata taratibu zote zinazotakiwa katika kupata Katiba ya Muungano kwa mujibu wa ibara ya 7 ya Mkataba wa Muungano wa Aprili 22, 1964 inayosema:
“The President of the United Republic in agreement with the Vice-President who is head of the Executive in Zanzibar shall: (a) Appoint a Commission to make proposal for Constitution for the United Republic. (b) Summon a Constituent Assembly composed of Representatives from Tanganyika and from Zanzibar …… for the purpose of considering the proposals of the Commission aforesaid and to adopt a Constitution for the United Republic”.
Kwamba, Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa makubaliano na Makamu wa Rais ambaye pia ni Mkuu wa Serikali ya Zanzibar: (a) Atateua Tume ya kuandaa rasimu ya Katiba kwa ajili ya Jamhuri ya Muungano (b) Ataitisha Bunge la Katiba lenye wawakilishi kutoka Tanganyika na kutoka Zanzibar……. kwa ajili ya kujadili Rasimu ya Tume na kukubali (adopt) na kuridhia Katiba kwa ajili ya Jamhuri ya Muungano.
Ingawa neno kuridhia Katiba halijitokezi sana katika ibara hiyo ya Mkataba wa Muungano, lakini sharti hilo limewekwa wazi kwenye Sheria ya Muungano Namba 22 ya 1964, kifungu cha 9 (1) kuwa, “A Constituent Assembly summoned in accordance with the Articles of Union shall have power to ratify and adopt a Constitution for the Government of the United Republic to make provision consequential on, and supplemental to, the new Constitution and to make other provision as the constituent Assembly think fit”.
Kwamba, “Bunge la Katiba lililoitishwa kwa mujibu wa Mkataba wa Muungano, litakuwa na mamlaka yasiyohojika ya kuridhia rasimu na kukubali Katiba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano, kuongeza matakwa ya ziada kwa Katiba mpya litakavyoona inafaa”.
Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano hazitaji nani atateua wajumbe wa Bunge la Katiba, ingawa katika mchakato unaoendelea wajumbe wameteuliwa na Rais wa Jamhuri, ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa chama tawala – CCM, hatua ambayo imezua malalamiko mengi kwamba huenda akatumia ushawishi wake kuhakikisha kwamba chama chake kinahodhi agenda na mchakato, kama ilivyotokea kwa Katiba za 1962, 1965 na 1977.
Akifungua Bunge la Katiba mjini Dodoma, Machi 21, 2014, Rais Jakaya Kikwete aliiponda hadharani Tume ya Katiba aliyoiteua yeye mwenyewe kwamba mapendekezo mengi yaliyotolewa na Tume hiyo hayafai na kuelezea kile alichosema “Sisi katika Chama cha Mapinduzi tunaamini……”
Rais aliendelea kusema kwamba, baadhi ya mapendekezo ya Tume hatayavumilia na kwamba wanaotaka yatekelezwe wasubiri aondoke madarakani.
Kwa kauli hii kutoka kwa kiti cha “Imperial Presidency” na Mwenyekiti wa chama tawala, je, si kwamba “ubabe” wa michakato ya Katiba za 1962, 1965 na 1977 unajirudia?  Na kwa maelekezo hayo, wabunge wa Bunge la Katiba wanasubiri nini Dodoma kwa kuwa tayari kazi ya kutunga Katiba wamekwishafanyiwa kwa marekebisho yaliyoagizwa na kuelekezwa na uongozi wa nchi?
Mchakato huu ulianza vizuri, na kwa Rais, baada ya kupokea Rasimu ya Tume, kuwaasa wananchi kujiandaa “kisaikolojia” kupokea muundo wowote wa Serikali utakaopendekezwa na Tume kutokana na maoni ya wananchi.
Umma wa Kitanzania unashindwa kufahamu alikotokea “dumuzi” anayelitafuna Bunge la Katiba kwa sasa.  Lakini kwa hali ilivyo, Katiba itakayotokana na kupuuzwa kwa mapendekezo ya Tume iliyokusanya maoni ya wananchi haiwezi kuwa ya kidemokrasia; itakosa uhalali wa kijamii na kisiasa (socio-political legitimacy) na muda si mrefu inaweza kuzua machafuko tusiyoweza kutarajia
- src
Raia mwema