
Mwananchi akipima virusi vya Hepatitis B vinavyosababisha Homa ya Ini, katika Hospitali ya Rufaa Amana. Homa ya ini hivi sasa inasambaa kwa kasi kubwa ikilinganishwa na VVU. Picha na Herieth Makwetta
Watalamu wa afya nchini wameonya kuwa, kumekuwa na ongezeko la kasi la maambukizi ya Homa ya Ini, huku idadi ya wagonjwa walioathirika na ugonjwa huo wakizidi kuongezeka.Takwimu zilizotolewa na benki kuu ya damu nchini, zimeeleza kuwa kati ya asilimia 100 ya damu inayokusanywa kwa mwaka, asilimia 0.6 hukutwa na virusi vya Ukimwi (VVU), huku asilimia saba ikikutwa na maambukizi ya homa ya ini ‘Hepatitis B (HBV) hivyo kufanya ugonjwa huo kuwa tishio jipya nchini.
Hata hivyo, wamesema kasi itaongezeka zaidi kutokana na vyanzo vya maambukizi kuwa rahisi na visivyoepukika kirahisi hasa maeneo yenye msongamano wa watu. Majimaji, mate, zinaa, jasho vimetajwa kuwa vyanzo vikuu vya maambukizi ya kirusi hicho, kinachosambaza ugonjwa huo.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Amana, Dk Meshack Shimwela, anasema ongezeko ni kubwa ukilinganisha na Virusi vya Ukimwi na kumekuwa na ongezeko kubwa la wagonjwa wanaougua homa ya ini miaka ya hivi karibuni, ukilinganisha na miaka ya nyuma Tumeanza rasmi kampeni hii ya kutokomeza Homa ya Ini kutokana na namna inavyoathiri watu wengi hivi sasa. Wengi wanadhani kwamba tatizo hili linawapata watu wenye tabia hatarishi pekee, la hasha! Mfano jijini Dar es Salaam kuna msongamano mkubwa wa watu, pia foleni. Watu mpo kwenye daladala mnagusana, joto linasababisha jasho. Ni rahisi kuambukizana,” anasema Shimwela.
Dk Shimwela anatoa wito kwa Watanzania wote kujitokeza kupima, ili kujua kama wana maambukizi ya virusi hivyo ili waanze kupatiwa matibabu ya kurefusha maisha au kupewa chanjo iwapo hawajapata maambukizi.
“Kuna njia mbili, moja ni kupewa matibabu ya kurefusha maisha au kupewa chanjo kwa wale wote waliokutwa hawana maambukizi. Bila kufanya hivyo unaweza ukajikuta unapata maambukizi, ilhali ungepima awali ungepewa chanjo ya kirusi hicho hatari,” anasema Shimwela.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Grace Magembe anasema ugonjwa wa homa ya ini unakuwa tishio jipya kuwahi kutokea nchini, tangu virusi vya Ukimwi miaka 25 iliyopita.
“Tulipambana sana na Ukimwi miaka 25 nyuma, tumefanikiwa lakini wakati tunahakikisha kutokomeza kabisa, limeibuka ugonjwa sugu wa Homa ya Ini ambao unakua kwa kasi kubwa. Hatuna budi kuhakikisha kwamba tunatokomeza na kujikinga,” anasema.
Magembe anasema uelewa wa Watanzania wengi bado upo chini, ukizingatia homa hiyo inaambukizwa kwa njia rahisi ukilinganisha na Ukimwi.Tunakumbana na changamoto nyingi sana katika ugonjwa huu, kwani mtu mwenye maambukizi hana dalili zozote, anaishi na maambukizi haya kwa muda mrefu kabla ya kuanza kupata madhara. Ifahamike wazi kwamba ugonjwa huu unaambukizwa kwa majimaji, mate, damu na jasho,” anasema Magembe.
Dalili za Homa ya Ini
Anazitaja dalili kuu za mgonjwa wa Homa ya Ini kuwa ni: Homa kali, manjano katika ulimi, ngozi na macho na pia hutapika sana.
“Mgonjwa wa homa ya ini anapata homa za mara kwa mara kama ilivyo kwa mgonjwa wa Ukimwi, lakini huyu yeye anapata dalili za moja kwa moja zinazomtambulisha. Mwili wake kuwa na manjano, kutapika na homa kali ni moja ya dalili za mgonjwa wa homa ya ini,” anasema Magembe.
Anabainisha kuwa homa ya ini husababisha saratani ya ini na wakati mwingine kusababisha ini kuharibika kabisa.
“Ini kuharibika ni moja ya dalili za ugonjwa huu, mara nyingi wengi hujikuta wakipata saratani ya ini na haya ndiyo matokeo ya homa hii. Wataalamu mbalimbali wamekuwa wakitoa huduma hii kwa watoto waliozaliwa kuanzia mwaka 2008 mpaka hivi sasa, hivyo kuna kila sababu ya watu wote waliozaliwa chini ya umri huo kupima ili kujua afya zao,” anasema.
Walio kwenye hatari ya maambukizi
Dk Magembe anawataja wafanyakazi wa kwenye maabara, hospitalini, nyumba za kulala wageni, machangudoa, wahudumu wa baa na wanafunzi wa vyuo au wanaoishi kwenye mikusanyiko mikubwa, kuwa wapo kwenye hatari zaidi ya kupata maambukizi hayo.
“Kampeni hii inahusisha watu wanaoishi kwenye mikusanyiko ya watu wengi, lakini pia watu wanaofanya shughuli au kazi hatarishi. Mkoa wetu wa Dar es Salaam, tumeanza kwa kuwapima na kuwapa chanjo wafanyakazi wa Hospitali ya Amana. Zaidi ya wafanyakazi 200 kati ya 350 wamekwishapimwa na kupewa chanjo kwa wale waliokutwa hawana maambukizi,” anasema Magembe na kubainisha kwamba zoezi hilo linaendelea katika hospitali nyingine.
Anatoa wito kwa waajiri wote kuhakikisha wanatoa huduma ya kupima na chanjo kwa wafanyakazi wao, wanaofanya kazi hatarishi kama njia mojawapo ya kuwakinga na gonjwa hilo.
Takwimu kutoka Damu Salama
Mkurugenzi wa Damu Salama, Dk. Festo Nkya anasema takwimu zao zinaonyesha kupanda kwa homa ya ini, huku maambukizi ya virusi vya Ukimwi yakipungua.
“Kwa mwaka Damu Salama, tunakusanya jumla ya chupa 170,000 za damu, lakini baada ya vipimo tumekuwa tukimwaga damu yenye maambukizi, inaonyesha homa ya ini inakua zaidi kuliko Ukimwi. Lakini tumegundua kwamba hakuna uhamasishaji kuhusu tatizo hili,” anasema Nkya.
Anasema kufuatia tatizo hilo, mpango wa damu salama utafanya marekebisho katika dodoso la wachangiaji damu pamoja na miongozo ya kuratibu VVU NA VVI.Tupo katika hatua za kuboresha madodoso, lakini pia tutaendeleza kampeni hii, ili kuhakikisha kizazi kitakachokuwepo miaka 18 ijayo, kiwe hakina maambukizi ya virusi vya homa ya ini,” anasema.
Walengwa wa mpango huo
Mwanzilishi wa kampeni hizi, Eric Shigongo anasema Hospitali ya Amana kwa kushirikiana na Global Publishers imeanzisha kampeni hiyo maalumu itakayosaidia kutoa elimu, kupima na kutoa chanjo kwa wale ambao bado hawajaathirika na kwa makundi maalum.
“Homa ya Ini ni ugonjwa hatari sana, unaua zaidi ya watu milioni moja kwa mwaka, huku ikiwaacha watu bilioni mbili wakiwa na maambukizi ya ugonjwa huo. Tumeamua kutokomeza homa ya ini hapa nchini. Walengwa wa mpango huu ni Watanzania wote, lakini kuna makundi maalumu ambayo ndiyo yataangaliwa zaidi wakiwamo: Wanafunzi, wafanyakazi kwenye maabara, hospitalini, nyumba za kulala wageni, machangudoa, wahudumu wa baa na wanafunzi wa vyuo au wanaoishi kwenye mikusanyiko mikubwa,” anasema
Shigongo anasema watu watakaopewa huduma hiyo bure ni machangudoa na wafanyakazi katika nyumba za kulala wageni, huku kampeni hiyo ikitarajiwa kufikia kilele Julai 28, mwaka huu.
Kauli ya Serikali
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki, anasema, wanafunzi na wafanyakazi hospitalini watapewa kipaumbele katika mpango huo utakaotekelezwa mwaka huu.
“Homa ya ini ni ugonjwa hatari mno, hivyo tutaanza kwa kuwashughulikia wanafunzi wote wa shule za sekondari na msingi, kwani watoto waliofanikiwa kupata chanjo hii ni wale waliozaliwa kuanzia mwaka 2008.
Katika hili pia tutaangalia watumishi katika hospitali zetu na ninaagiza hili lifanyike, Amana wamekwishapimwa na kuchanjwa hivyo naagiza Temeke, Mwananyamala na Muhimbili wafanye hivyo, kisha hospitali binafsi na wao pia,” anasema Meck Sadiki.
Anasema mpango huo ni endelevu na kuwataka wananchi mbalimbali kufika katika vituo vya afya kwa ajili ya vipimo.
“Maambukizi ya homa ya ini ni makubwa hivi sasa kuliko Ukimwi na watu walio katika hatari ya kuambukizwa ni watu wa maabara na wafanyakazi wa hospitalini, pia ninawasihi watu wote kufika katika vituo vya afya ili kupata uhakika wa afya zao.”