Monday, April 21, 2014

Ajali ya basi yaua 20 papo hapo

Ajali ya basi yaua 20 papo hapo


Simiyu

Taarifa zinasema kuwa ajali iliyotokea katika kijiji cha Yitwimila A, kata ya Kiloleli wilayani Busega katika mkoa wa Simiyu leo hii imesababisha vifo vya watu 20 na kuacha takribani watu 40 wakiwa na majeraha, baada ya basi la Luhuye Express lililokuwa likisafiri kutoka katika mji wa Sirari, Tarime mkoani Mara likielekea Mwanza kuacha njia na kugonga nyumba kisha kupinduka.

Ajali hiyo imeelezwa kutokea saa nne adhuuri wakati basi hilo lenye namba za
usajili T410AWQ ambalo safari yake ilipangwa kufika hadi kijijini Mganza, Biharamulo huko mkoani Kagera.

Dereva wa basi hilo ameripotiwa kutoroka wakati majeruhi walipelekwa katika hospitali za Wilaya na ile ya Rufaa ya Bugando kwa matibabu zaidi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Kamishina Mwandamizi wa Polisi (SACP), Charles Mkumbo alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema basi hilo liliigonga nyumba ya marehemu, Mwalimu Lazaro Mbofu na kuibomoa yote na kisha kupinduka.

“Hadi sasa kuna maiti 10 walizopatikana katika eneo la tukio, na zaidi ya watu 30 wamejeruhiwa na kukimbizwa Bugando kwa ajili ya matibabu. Ila taarifa kamili nitaitoa baadaye juu ya watu waliokufa na waliojeruhiwa, kwa sasa nimetuma askari wa usalama barabarani kufuatilia,” amenukuliwa Mkumbo akisema.

Simiyu

Taarifa nyingine kutoka mkoani Morogoro zinasema kuwa nako basi moja limeacha njia na kupinduka katika eneo la Bwawani. Bado haijafahamika madhara yaliyosababishwa na ajali hiyo.

Morogoro

src
wavuti