Kila Mjumbe ana cha kuzungumza juu ya kikao cha Bunge la Katiba kilichovunjwa, kutokana na zogo lililozuka bungeni siku ambayo Jaji Joseph Warioba alilazimika kuahirisha kuwasilisha Rasimu ya Pili ya Katiba kwa wajumbe wa bunge hilo.
Wabunge waliopata nafasi ya kuzungumzia tukio hilo ni Mbunge Viti Maalumu (CCM) katika Bunge la Jamhuri ya Muungano ambaye pia ni Mke wa Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta.
Anapozungumza na gazeti hili nje ya Ukumbi wa Bunge mjini Dodoma, muda mfupi baada ya kikao kuvunjika, Margaret Sitta anasema mpaka wakati huo, hakuwa akielewa kiini cha kilichotokea.
“Suala la Warioba kuwasilisha rasimu lilizungumzwa kwenye kikao cha Bunge kilichofanyika asubuhi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali akaeleza na kutengua kanuni kwamba la kwanza litakuwa la pili na la pili litakuja baadaye, sijui nini kimetokea,” Mama Sitta anaeleza.
Mama Sitta anaamini ikiwa tatizo ni matumizi
Mama Sitta anaamini ikiwa tatizo ni matumizi ya kanuni, ingetakiwa asimame mbunge mmoja, lakini walisimama wengi hali aliyoielezea kuwa siyo ya kawaida ingawa alibainisha kuwa anaamini yangeisha tu.
Dk. Seif Rashid ambaye ni Mbunge wa Rufiji (CCM) na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, anaona zogo lililotokea bungeni kuwa ni matokeo ya uelewa duni wa mfumo wa utawala bora, unaowakabili baadhi ya wanasiasa nchini.
“Utawala bora unaelekeza kufanya kinachowezekana na kisichowezekana kufanyika kuachwa ili kifanywe wakati mwingine. Hakuna maana ya kusababisha uvunjifu wa kikao muhimu kama hiki kwa hoja zisizokuwa na athari kwa Mchakato wa Kuunda Katiba tunaoendelea nao,” anaeleza Dk. Seif.
Dk. Seif anasema rasimu inayowasilishwa na Jaji Warioba siyo mpya kwa Mtanzania yeyote aliye makini kwa kinachoendelea nchini, hususan wabunge wa Bunge hilo.
Anasema dhana hiyo inatokana na rasimu hiyo kukabidhiwa mara ya kwanza kwa Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk. Mohammed Shein, Desemba 30, mwaka jana, kabla haijasambazwa kwa wananchi kupitia njia tofauti.
Anasema ni hoja isiyo na mashiko, kudai kuwa muda wa zaidi ya saa 2:30 hautoshi kwa Jaji Warioba kuwasilisha rasimu hiyo bungeni, kama inavyoelekezwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2012, Sura Na. 83 kwa maana anaamini kila mtu anafahamu kilichomo.
Dk. Seif pia haafikiani na madai kwamba Jaji Warioba kuwasilisha rasimu kabla ya Rais Kikwete kuhutubia Bunge, kutaathiri mijadala ya Bunge wakati wa kuboresha rasimu hiyo Sababu za Dk. Seif kuamini hivyo anazitaja kuwa kwanza Rais Kikwete anatarajiwa kuhutubia bungeni akiwa kiongozi mkuu wa nchi na siyo vinginevyo. Akataka ikumbukwe kuwa kiongozi huyo ndiye mwasisi wa mchakato wa Katiba, unaoendelea nchini
Anasema madai kwamba Rais Kikwete akihutubia Bunge baada ya kuwasilishwa Rasimu ya Pili bungeni, itakuwa sawa na kumfanya kuwa sehemu ya Bunge hilo, kwa maelezo kwamba kwa namna moja au nyingine katika mazungumzo yake anaweza kujikuta akichangia maboresho ya rasimu husika; hayana mashiko.
Anarejea kanuni zinazoongoza Bunge hilo kwamba zinaruhusu kualika mtaalamu yeyote kutoa ufafanuzi juu ya suala litakaloonekana na kuafikiana kuwa linahitaji ufafanuzi na kuhoji kama nao kwa hatua hiyo watakuwa wamekuwa sehemu ya Bunge hilo.
“Dai hili halina msingi wowote, kwa mfano mimi ni muumini wa Dini ya Kiislamu na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, nikialikwa kuhudhuria na kuzungumza kwenye shughuli ya kijamii inayofanywa na wenye imani ya Kikristu, nitakuwa Mkristu? Tukio hili linadhihirisha uduni wa uelewa katika suala zima la utawala bora,” alieleza Dk. Seif.
Profesa Costa Ricky Mahalu, ambaye alikuwa akiongoza Kamati ya Kuboresha Rasimu ya Kanuni za Bunge Maalumu, zinazodaiwa kuvunjwa na mwenyekiti wa Bunge hilo, Sitta anasema hakuna kanuni iliyovunjwa.
“Ibara ya 85 (4) (d) mwenyekiti anapewa mamlaka ya kuongeza orodha yoyote ambayo haikuwapo kwenye mpangilio wa shughuli za bunge na pia anayo mamlaka ya kutumia busara yake, kuamua mambo kulingana na atakavyoona inafaa,” anaeleza Profesa Mahalu.
src
mwananchi
src
mwananchi