Sunday, March 30, 2014

Kanuni zimetumia siku 40, rasimu je?

BUNGE Maalumu la Katiba limetumia siku 40 kwa wajumbe wake kutengeneza kanuni za kuwaongoza.
Kama muda hautaongezwa ina maana Bunge hilo limebakiza siku 30 ili kutimiza siku 70 zilizowekwa kwa mujibu wa sheria kwa wajumbe hao kuwa wameandika katiba mpya ambayo itapelekwa kwa wananchi kupigiwa kura ya maoni.
Bunge hili lilianza kukutana tangu Februari 18, mwaka huu, huku likitawaliwa na matukio ya hapa na pale ambayo mengi yanaleta hasira kwa wananchi.
Mosi, wananchi wengi wanaona kama wajumbe wametumia muda mrefu kutengeneza kanuni hizo ili kuhalalisha nyongeza ya siku 20 badala ya 70 kwa lengo la kunogesha posho yao.
Pili, wako wanaoamini kwamba uteuzi wa wajumbe ulikosewa kwa kuingiza wanasiasa wengi, hivyo kutumia bunge hilo kuendesha mivutano ya kisiasa badala ya kujikita kufanya kazi iliyowaweka Dodoma.
Tatu, wako wenye fikra kwamba serikali ya CCM haina dhamira ya dhati ya kukamilisha mchakato huo, na kwa sababu hiyo wanaamini kuwa hata kasoro nyingi zinazojitokeza zinaletwa makusudi ili katiba mpya isiandikike.
Nne, wananchi wengine wanaamini kwamba vyama vya upinzani vinataka kukwamisha mchakato huo kwa makusudi ili kutumia mtaji huo kuidhoofisha CCM kwenye Uchaguzi Mkuu ujao 2015.
Mawazo yote haya ni sahihi,  vilevile si sahihi kwa upande mwingine. Ni kweli mchakato wa kuandaa kanuni umetumia muda mrefu lakini tukijilinganisha na mataifa yaliyopitia mchakato kama huu, sisi wajumbe wetu wamejitahidi.
Kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya Katiba, mabunge mengine maalumu ya katiba katika nchi nyingine yametumia miezi mitatu mpaka sita kuandaa kanuni hizo.
Usahihi katika hili ni kwamba upotevu wa muda unasababishwa na wajumbe wengi kufanya propaganda za kutafuta umaarufu badala ya kujielekeza kujadili hoja iliyopo mezani.
Laiti wajumbe wetu wa Bunge la katiba wangeacha propaganda na kujikita kwenye hoja, wanaweza kumaliza kazi ya kuijadili rasimu hata kabla ya siku 70.
Propaganda ninazozimaanisha ni minyukano isiyokwisha, kupindisha mambo yaliyokubaliwa awali na kutoheshimiana kwa baadhi ya wajumbe kujiona wao ndio bora kuliko wengine.
Mathalani Bunge hilo awali lilipitisha kanuni zake nyingine na kuziacha mbili za 37 na 38 zinazohusu kura ya uamuzi. Lakini ndani ya muda mfupi ukatumia ujanja wa kuitengua kanuni ya 7 (1) (g) (h) ili kumleta Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba kabla ya Rais Jakaya Kikwete.
Suala hili lilipoteza muda wa Bunge kufanya kazi kwani makundi yalianza mivutano isiyokwisha japo mingine ilikuwa na mantiki ndani yake.
Kwa mfano; unaweza kujiuliza kama kanuni zilikuwa zimekwishapigwa teke na kumleta Jaji Warioba wa kwanza ni kwanini zikafanywa hila kwa kutaka kumpangia muda mfupi wa saa moja na baadaye saa mbili awasilishe ripoti ya rasimu yake?
Hapa ndipo nakubaliana na hoja ya kundi la wananchi wanaoamini kwamba CCM haina dhamira ya dhati ya kuandika katiba mpya.
Kwa sababu muda wa siku mbili uliopotea bila Bunge kufanya kazi lazima utafidiwa kwa kodi za wafuja jasho.
Katika propaganda hizo hizo za kupoteza muda, Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta, alishindwa kutumia wadhifa wake kumweka sawa Rais Kikwete ili ajielekeze kwenye masuala ya jumla wakati akihutubia bunge hilo, badala yake wote wakakazana kumkejeli Jaji Warioba.
Kilichofuata baada ya hapo zilipotea tena siku mbili bila Bunge kufanya kazi zake, makundi yakivutana kujadali na kuweka misimamo ya kujibu mashambulizi kwa walioanza kupindua rasimu ya Warioba ambayo kimsingi ndio mawazo ya wananchi.
Kwa kifupi hili ni Bunge la kupoteza muda kwa masuala ambayo yangeweza kuepukika endapo kuna dhamira ya dhati kwa watawala katika kuendesha mchakato.
Watu wazima na akili zao timamu, wanakutana na kushauriana kupendekeza marekebisha kanuni kwa sababu tu ya kutafuta urahisi wa kuweza kupenyeza masilahi yao kirahisi bila kujali suala hilo litazua mtafaruku.
Hili nalo limejitokeza, Bunge likaahirishwa mara mbili ndipo hoja hiyo ikaondolewa huku muda ukiwa umepoteza bila wajumbe kufanya kazi.
Wiki hii imehitishwa kwa kupoteza muda mwingine wa siku mbili za wajumbe kurushiana madongo, matusi mazito na vijembe vya kisiasa chini ya kivuli kilichoitwa kujadili aina gani ya kura itumike kuamua.
Narudia kusema kuwa inachekesha kuona watu wazima wanatumia siku nzima, mate yakiwatoka mdomoni hadi kutaka kukunjana eti wanabishania kura ya siri na wazi kwa kuzungumza tu.
Naamini suala hili hata wangepewa watoto wa chekechea kuliamua, wametumia dakika zisizozidi 10 kwa kuafikiana ipigwe kura ya siri kisha watazame matokeo yameamua nini.
Utashangaa kuona Bunge lenye wasomi wa kila aina, hawataki kufikiria njia nyepesi kama hiyo na ilipotokea mmoja wao akashauri hivyo anazomewa. Hii kama si kupoteza muda tule posho, katiba hakuna tusemeje? Tafakari

src
Tanzania DAIMA