TANGU Bunge Maalum la Katiba mpya, lilipoanza vikao vyake, kumekuwa na makundi mbalimbali, wakiwemo, wasomi, wanasiasa, wanaharakati, vijana kwa wazee yakijadili Katiba hiyo.
Kila kundi limekuwa likijaribu kushawishi Watanzania, kuhusu mambo wanayoyataka katika Katiba hiyo mpya. Katika rasimu masuala mengi yamebainishwa kuwemo kwenye Katiba.
Lakini makundi hayo yote yamekuwa yakijipambanua kwenye eneo moja pekee la mfumo wa Serikali ngapi, ndio unafaa utambuliwe na Katiba hiyo.
Kwa kweli hoja hiyo ndio imekuwa mjadala mkubwa, kiasi cha wajumbe wenyewe wa Bunge hilo maalum la Katiba kulumbana huku kila mmoja akivutia upande wake. Malumbano hayo yamesababisha makundi hayo kufikia hatua ya kuitana wasaliti.
Lakini, pamoja na hali hiyo, Rais Jakaya Kikwete hivi karibuni wakati anazindua rasmi Bunge hilo, alibainisha wazi msimamo wake kuwa jambo la msingi ni kwa wajumbe hao, kuungana na kusimama kama Watanzania na kutengeneza Katiba yenye manufaa na itakayodumu hadi kizazi kijacho.
Katika hotuba yake, Rais Kikwete aligusia mifumo tofauti ya Serikali ikiwemo serikali moja, mbili na tatu.
Alieleza faida na hasara za kila mfumo huku msisitizo wake ukiwa ni kwa wajumbe hao, kuchambua mifumo hiyo na iwapo watapendekeza mmojawapo, wahakikishe kuwa unatekelezeka kwa faida ya Watanzania.
Pia, alisisitizia juu ya mfumo wa serikali mbili, kwa kuwa tayari umekuwepo na unafahamika, hivyo ni rahisi kukabiliana na changamoto zake.
Alibainisha wazi kuwa iwapo Watanzania wanahitaji mfumo mwingine wa serikali, kama vile serikali tatu, lazima faida, hasara na changamoto zake zibainishwe, kwa kuwa Tanzania haina uzoefu na mfumo huo.
Lakini, pamoja na hotuba hiyo, kumeibuka mijadala na makundi mbalimbali huku wengine wakitafsiri vibaya hotuba hiyo, wakidai Rais Kikwete ameegemea upande mmoja wa serikali mbili na kusisitiza kuwa mfumo wa serikali tatu hautekelezeki, jambo ambalo si la kweli.
Kana kwamba hiyo haitoshi, Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ambao unaundwa na wajumbe wa Bunge hilo wapinzani, umetangaza kufanya ziara mbalimbali kueleza hila za CCM, kuhodhi mchakato wa Katiba mpya.
Jambo la msingi, si kuwachanganya kwa sasa Watanzania, wajumbe hao wa Bunge Maalum wanapaswa kutumia fursa waliyonayo kupitia Bunge hilo, kuchambua mifumo hiyo, kama alivyopendekeza Rais Kikwete na kuwaridhisha wanaopingana nao.
Huu si wakati wa makundi, kuwekeana uhasama na kusemeana kwa wananchi. Makundi yakiendelea kufanya hivyo, muda wa Bunge hilo, utaendelea kupotea na kazi maalum ya kupitia vipengele vya rasimu hiyo ili kupatikana Katiba mpya, haitafanyika ipasavyo.
Ni wazi kuwa kila upande, una hoja nzito kuhusu mfumo wa Serikali wanaoutaka hivyo ni vyema zikatumika njia za busara kuhakikisha kuwa kila anayetetea hoja yake, anaiwasilisha vyema kwa wajumbe wenzake na kushawishi na si kuunda makundi au kutengeneza uhasama miongoni mwa Watanzania.
Ikumbukwe kuwa kinachotafutwa hapa ni Katiba, itakayosimamia na kutatua matatizo ya muda mrefu ya Watanzania, Katiba ambayo itatekelezwa na kudumu kizazi hadi kizazi, hivyo ni vyema mawazo ya kila mtu yaheshimiwe na si kunyoosheana vidole.
Hilo linawezekana, iwapo wajumbe wa Bunge hilo, wataaminiana na kupeana nafasi na kubwa zaidi kusikilizana, kwani wakiendelea na makundi na kulumbana, upo uwezekano mkubwa muda wa kujadili vipengele hivyo, ukapita bila Katiba kupatikana.
Watanzania kwa sasa macho na masikio yao yapo Dodoma. Hakuna anayetaka kuona nani anasimamia wapi wala msimamo wake ni upi. Watu wote wanachotaka ni Katiba mpya, itakayomaliza kero zao na si kuona fedha za wananchi na muda muafaka uliopangwa, unapotea bure.
src
Habari Leo