MUUNGANO wa Tanganyika na Zanzibar unatimiza miaka hamsini na ni jambo la kujivunia kutokana na ushirikiano wa karibu wa jamii hizi mbili kudumu katika kipindi kirefu kama hicho bila mfarakano.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo Watanzania wengi wamezaliwa na kuikuta, iliundwa rasmi Aprili 26, 1964 kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar inayojumuisha Visiwa vya Pemba na Unguja. Kikubwa kilichovutia Muungano huu ni undugu wa damu wa watu wa maeneo haya, biashara, utamaduni, lugha na mahusiano ya karibu ya kisiasa baina ya chama cha TANU na ASP.
Na kimsingi historia inaonesha kwamba nchi hizi zilikuwa moja kabla ya wakoloni kuzigawa na kuwa nchi mbili tofauti. Kabla ya uhuru wa Tanganyika, historia inaonesha kwamba Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na viongozi wengine waliokuwa wakipigania utaifa katika ukanda wa Afrika Mashariki walikuwa na matarajio ya kuwa na Muungano wa Afrika nzima baadaye.
Mwalimu Nyerere binafsi alipendelea uwepo na Muungano wa Afrika kwa kuanzia na Mashirikisho ya kikanda lakini wapo ambao walitaka muungano wa Afrika ufanyike mara moja, kama hayati Kwame Nkrumah wa Ghana.
Historia inaonesha kwamba baada ya kushauriana na viongozi mbalimbali wa iliyokuwa Jumuiya ya Wapigania Uhuru wa Afrika Mashariki na Kati (Pan- African Freedom Movement for East and Central Africa - PAFMECA), Mwalimu Nyerere alitoa tamko wakati wa mkutano wa nchi huru za Afrika uliofanyika Addis Ababa mwaka 1960 kuhusu Shirikisho la Afrika Mashariki.
“Wengi wetu tunakubaliana bila kikwazo kwamba Shirikisho la Afrika Mashariki litakuwa ni jambo zuri. Tumesema na ni kweli kwamba mipaka inayotenganisha nchi zetu imewekwa na mabeberu na sio sisi wenyewe na hivyo tusikubali itumike dhidi ya umoja wetu.”
Mwalimu alikaririwa akisema: “Lazima tuzisumbue ofisi za wakoloni kwa nia sio ya kudai uhuru wa Tanganyika, kisha Kenya na Uganda halafu Zanzibar pekee bali pia kwa nia ya kutaka uhuru wa Afrika Mashariki kama Muungano mmoja wa Kisiasa.”(Nukuu hii ilichapishwa kwenye gazeti la Tanganyika Standard, Novemba 1964).
Zipo pia taarifa zinazoonesha kwamba Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari, 1964 yalifanyika wakati Mwalimu Nyerere akiwa ameshachoshwa na kukatishwa tamaa na mazungumzo ya Shirikisho la Afrika Mashariki. Mapinduzi hayo yaliiweka madarakani Serikali ya chama cha Afro Shirazi Party (ASP) kilichokuwa na mahusiano ya karibu na Chama cha Tanganyika African National Union (TANU) kwa upande wa Tanganyika.
Hivyo Muungano wetu upo kihistoria kuhusu nchi hizi mbili, ukianzia na ukaribu, muingiliano wa kijamii, kiutamaduni, ushirikiano wa kibiashara na kubwa zaidi ni mtazamo wa awali wa Mwalimu Nyerere na Karume wa kuamini kwamba mipaka baina ya nchi hizi iliwekwa na wakoloni na siyo wazalendo.
Ushirikiano madhubuti na wa muda mrefu wa kisiasa baina ya TANU na ASP na baadaye Chama Cha Mapinduzi (CCM) vinatajwa pia kuwa sababu ya Muungano huu kudumu hadi kufikia miaka 50 sasa ukiwa haujatetereka. Hii ni sambamba, kama ambavyo imedokezwa hapo juu, na ushirikiano wa muda mrefu wa watu wa pande hizi mbili za Muungano.
Lakini kubwa ambalo pia linatajwa na wachunguzi wa mambo ya kisiasa kuhusu sababu za Muungano ni suala zima usalama baina ya nchi hizi ambao umesaidia sana katika kuimarisha uhuru wa Tanzania. Baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Morogoro waliohojiwa na mwandishi wa makala haya wameonekana kuutakia mema Muungano huku wakiorodhesha bayana faida ya Muungano na changamoto zinazohitajika kufanyiwa kazi.
Mohammed Matokeo ni mwanasiasa na mchambuzi wa mambo ya kisiasa anayesema kwamba suala la Muungano ni muhimu kwamba hata mataifa makubwa duniani yameungana kutokana na umuhimu wa kushirikiana. Matokeo anasema mbali na suala la usalama kwa pande hizi za muungano, Muungano uliopo ambao unatimiza miaka 50, umekuwa na faida pia za kijamii ikiwa ni pamoja na kifamilia za pande hizi mbili kuoleana.
Pia anataja faida za mambo ya kibiashara kwani watu wa pande mbili za Muungano wamewekeza vitegauchumi vyao na wanafaidika. “Muungano wetu umejenga udugu wa kifamilia. Mpemba ameoa mwanamke wa Kinyakyusa huko Mbeya, na Mnyakyusa ameoa mwanamke wa Kiunguja. Ujenzi wa familia unafanya undugu wa damu uliosababishwa na Muungano,” anasema Matokeo.
Hata hivyo, kwa maoni yake anasema wananchi wa kawaida wa pande zote mbili za muungano hawana matatizo kubwa na Muungano wala muundo wake isipokuwa mengi yanakuzwa na viongozi na watawala. Anashauri kuwa ili Muungano uweze kudumu na kuleta faida zaidi kwa wananchi wa pande mbili hizo mambo ya msingi ya kuimarisha Muungano yawekwe wazi ili kuondoa shaka ya kila upande.
“Maoni yangu ni kwamba Muungano uwepo na ulindwe kwa nguvu zote kwa kuwa una faida nyingi lakini kikubwa ni kuangalia mfumo wa muundo wake,” anasema. Kuhusu serikali tatu anasema ni kama huwa zipo ndani ya Muungano wa sasa, “Kwani kwa kule Zanzibar ipo Serikali ya Mapinduzi na Bara ipo Serikali ya Tawala za Mikoa ya Serikali za Mitaa (Tamisemi) ambayo shughuli zake ni kwa Bara pekee.”
Matokeo anasema suala la idadi ya serikali linaweza kwake lisiwe hoja sana ingawa anaunga mkono serikali tatu, isipokuwa la muhimu ni kuyapatia ufumbuzi malalamiko mbalimbali ya pande zote mbili za muungano. Matokeo anaamini kwamba ili kudumisha Muungano kwa kipindi kingine cha miaka 50 au zaidi, marekebisho makubwa ya Katiba ya sasa yanahitajika ikiwa ni pamoja na kurudisha nafasi ya Makamu wa Rais kuwa ni Rais wa Zanzibar.
Angependa kuona Katiba ya Jamhuri ya Muungano ikitamka kwamba Waziri Kiongozi wa Zanzibar ni Naibu Waziri Mkuu huku pia Waziri Mkuu akiwa na uwezo wa kushughulika hata mambo ya Zanzibar sawia na Naibu wake.
Hata hivyo Matokeo bado anajawa na hofu juu ya Muundo wa Serikali tatu, kwamba upande mmoja wa muungano, hususan Bara, unaweza kujiona ndio unachangia zaidi na kutaka kujitenga ama Serikali ya Muungano inayochangiwa na washirika ikaonekana kama boya lisilo na maana na hatimaye nchi moja kuweza kujitenga kwa ushawishi wa mataifa ya nje na kusababisha Muungano kuvunjika.
“Hili suala linahitaji kuaminiana sana kwa viongozi wa Serikali hizo tatu na kama kiongozi mmoja akiwa si muadilifu na mwenye uchu wa madaraka Serikali tatu haitabaki salama, itaparaganyika,” anasema Matokeo. “Serikali tatu inayopendekezwa ina faida na hasara zake. Viongozi wasipoaminiana ni rahisi kujitenga,” anasema Matokeo.
Mkazi mwingine wa Manispaa ya Morogoro, Shaaban Vigulo, anasema Muungano bado unafaida kubwa na ni vyema ukaendelea kuenziwa na kudumishwa. “Siwezi kusema hakuna faida katika Muungano, zipo nyingi na kubwa. Watu wa Bara na Visiwani wameingiliana kijamii, kibiashara, kielimu na hata mambo ya utamaduni na kuoana,” anasema
src
Habari Leo
Monday, March 24, 2014
Home »
MAKALA
» KUELEKEA SHEREHE ZA MIAKA 50 YA MUUNGANO: Muungano ni tunu tangu enzi za kusaka uhuru, lazima uenziwe
KUELEKEA SHEREHE ZA MIAKA 50 YA MUUNGANO: Muungano ni tunu tangu enzi za kusaka uhuru, lazima uenziwe
10:54 PM MAKALA