Thursday, March 20, 2014

Suala la ushoga tutaweza vipi kulikwepa kuzungumzia?

 
Siku chache zilizopita Rais Jakaya Kikwete alihojiwa na Mtangazaji wa Shirika la Kimataifa la Utangazaji la CNN akiwa London ambako alikwenda kuhudhuria mkutano unaohusu kupambana na ujangili.
Baada ya kuzungumzia masuala ya ujangili na jinsi ambavyo Tanzania inajitahidi kupambana nao mtangazaji huyo Christiane Amanpour alimchomekea Rais Kikwete suala kuhusiana na msimamo wa Tanzania katika kufuta sheria zenye kukataza vitendo vya kishoga (mapenzi ya kingono kwa watu wa jinsia moja).
Swali la mwanamama huyo lilikuwa linalenga kummulika Rais Kikwete kama mtego ili wajue msimamo wa Tanzania ni upi kuhusiana na suala hilo na zaidi ya yote suala la ndoa za mashoga.
Swali la Amanpour lilijengwa kutoka katika dhana kuwa nchi kadhawakadha za Magharibi zimekuwa zikitupilia mbali sheria kandamizi dhidi ya mashoga na nyingine zimefikia hata kuhalalisha kile kinachoitwa “ndoa za mashoga”.
Marekani yenyewe japo katika serikali ya shirikisho ndoa bado inatambulika rasmi kama ni ya mwanamume na mwanamke, katika serikali kadhaa za majimbo (zinazounda Shirikisho la Marekani) zimetammbua kile kinachoitwa “haki za mashoga”.
Amanpour alitaka kujua hasa Serikali ya Tanzania inaelekea vipi katika kutambua haki za mashoga kama sehemu ya kile alichokiona ni mwamko wa haki za kiraia duniani.
Jibu la Rais Kikwete kimsingi lilikuwa na sehemu mbili. Sehemu ya kwanza alikanusha kwa maneno machache tu madai ya Amanpour kuwa mashoga katika Tanzania wanateswa na kukamatwa na kufungwa kwa sababu hiyo au hata kuuawa. Lakini sehemu ya pili ni jibu ambalo ndio msingi wa swali langu katika mada hii.
Rais Kikwete aliulizwa moja kwa moja kama yeye mwenyewe anaona wakati umefika wa kufutilia mbali sheria zinazoharamisha vitendo vya kishoga na vyenye kutoa adhabu kali kwa wahusika. Rais Kikwete alisema I can’t say that at this time yaani “siwezi kusema hivyo sasa hivi”. Kwa maneno mengine ‘wakati wake haujafika bado’.
Tunapo elekea katika kuandika Katiba mpya naamini mojawapo ya changamoto za wabunge (sielewi kwa nini wanaitwa Wajumbe wa Bunge!) ni kujaribu kupatanisha vipengele mbalimbali vya rasimu ya Katiba na masuala haya ya haki za mashoga?
Maswali yanayohusiana na hilo yanahitaji kujibiwa kwani hayakwepeki hata kama yanatufanya tujisikie vibaya na kuwa na kichefuchefu. Ni maswali ambayo yatahitaji majibu na kama hatutatafuta majibu sasa ni wazi huko mbele tutalazimishwa kuyatafuta.
Tunaweza kujikuta tunatumia njia ya Uganda na Nigeria – kupitisha sheria kali dhidi ya vitendo vya ushoga tukiamini kwa kufanya hivyo tutakuwa tunawatisha watu kutofanya vitendo hivi. Hata hivyo, sote tunajua kuwa sheria peke yake na hata adhabu havijawahi kutosha kuwafanya watu wasifanye matendo mabaya.
Kama  sheria dhidi ya kuua ingekuwa inaweza kuzuia watu wasiue, watu wangekuwa hawauani; hili ni kweli pia katika masuala ya wizi, ufujaji wa mali ya umma n.k.  Na ukweli kuwa sheria tayari zipo dhidi ya vitendo hivi na tena zina adhabu kali tu lakini zimechangia vipi kupunguza vitendo hivi au hata kuwafanya watu waache?
Labda hoja inaweza kutolewa kuwa sheria hizi hazijasimamiwa vizuri na hivyo watu wanaona kana kwamba vitendo hivi vya kishoga vimevumiliwa katika jamii. Labda ianze ‘kamatakamata’ kama ile ya Operesheni Tokomeza ambapo watu wote wanaojulikana kuwa wanahusika na vitendo hivi wanatiwa pingu na kufikishwa mahakamani. Je, ni kweli tunataka hili?
Wapo wanaoweza kujibu kwa haraka kuwa hilo ndilo njia sahihi kama inavyotokea  kwenye baadhi ya nchi ambako mashoga wanaadhibiwa vikali hata kuuawa! Lakini katika suala hili la ushoga wakati mwingine tunawazungumzia zaidi wale watu (kwa wanaume) ambao wanaonekana kuwa na tabia za kike na kujifanya ni wanawake (japo wanaume) au wale wanawake ambao wanaanzisha mahusiano na wanawake wengine kama vile waoni wanaume.
Lakini vipi kwa wale ambao hawajioneshi kama ni watu wa jinsia tofauti; watu ambao wana ndoa zao na wengine wana familia zao lakini bado wanafanya vitendo hivi ambavyo vinaonekana ni kinyume cha maumbile, dini na hata tamaduni?
Jibu la Rais Kikwete halikutosha; kwamba ‘wakati haujafika’ si jibu  lililojaa fikara na inaonekana ni kana kwamba Rais Kikwete hajawahi kufikiria jambo hili kwa kina. Na si yeye tu, wengi wetu hawajawahi kufanya mjadala wa kiakili kuhusiana na hili kwa sababu linahusiana na tabia chafu, ya kidhambi kiasi kwamba hata watu wenye akili kulizungumzia haiwezekani. Lakini kutolizungumzia au kulijadili hakuondoi ukweli kwamba mambo haya yapo!
Bahati mbaya sana yapo kwenye ofisi, yapo kwenye shule, yapo mitaani na yapo hata kwa wanasiasa! Leo hii sidhani kuna mtu – hasa mijini humu – ambaye hajui angalau mtu mmoja ambaye ni shoga!
Tena wengine ni watu ambao tumewakubali, tu na waona kwenye TV, tunapata huduma zao (kama ni kupamba nyumba au vitu vingine) na tunawajua kuwa ni mashoga? Je, tungependa watu hawa wakamatwe na kufungwa au hata kuuawa? Je, tuwatafutie adhabu gani ya kuwafanya waache vitendo hivi?
Je, inawezekana kabisa kuondoa vitendo hivi kwa kutumia nguvu au sheria kali? Kama vitendo  hivi vingeweza kuondolewa kwa namna hii duniani visingekuwepo kabisa. Je, tuendelee kuvifumbia macho kana kwamba havipo kabisa?
Ninaamini nimefungua mjadala wa watu kuweza kuzungumza na kujadiliana na hasa huko kwenye Bunge la Katiba. Ukisoma rasimu ya Katiba mpya utaona kuwa inatoa ulinzi mkubwa kwa raia na kuwahakikishia usalama wao.
Kuna ibara kadha wa kadha ambazo zinataja haki na ulinzi huo kwa “kila mtu” au “kila raia” au “kila mwanamke” n.k.
Swali kubwa ambalo litahitaji kujibiwa na wabunge wetu hawa na viongozi wetu na labda na kila mmoja wetu ni je, haki hizi ambazo tunataka kuziweka katika Katiba mpya zinawalinda wote isipokuwa mashoga? Au tuweke katika Katiba mpya kipengele mahsusi ambacho kitatambua tu suala la ndoa na familia kama ni suala la watu wa jinsia tofauti na hivyo kuondoa uwezekano wa mashoga kutaka kuja kufungia ndoa Tanzania?
Je, tukifanya hivyo tutakuwa tumefanya sahihi au tunaamua kuwaachia Watanzania wa vizazi vijavyo waje kuamua kama wao katika wakati wao wanaona kuwa mashoga si tishio katika jamii?
Lakini katika kufikia maamuzi hayo imani zetu za kidini na maadili yetu tutaviwe kawapi? Je, tunaweza kweli kuwa waumini wazuri wa dini zetu huku tukikubali au  kubariki vitendo hivi kwa misingi ya ‘haki za raia’ na “haki za binadamu’ kama Christiane Amanpour alivyojaribu kumseti Kikwete? Lakini kwani tunatunga Katiba mpya ya kidini?
Au tusijadili tuache liwalo na liwe? Au hili si suala la kusumbua vichwa vyetu kwani ni suala la utamaduni wa Nchi za Magharibi kama Rais Kikwete alivyosema?
-