- Kuishutumu Tume ya Warioba ni kutokuona mbali
MADAI kwamba Tume ya Mabadiliko ya Katiba, inayoongozwa na Jaji Joseph Sinde Warioba, haikupaswa kulitungia Bunge Maalumu la Katiba Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni farasi aliyekatika miguu.
Wala si sahihi kudai kwamba Bunge hilo lina madaraka ya kujadili na kuipitisha rasimu hiyo na wakati huo huo likapewa madaraka ya kuandika rasimu mbadala au kubadili mfumo wa rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume. Kusimamia hoja hiyo ni umbumbumbu wa Sheria kama si uhafidhina na ubinafsi kwa maslahi ya kisiasa usiozingatia ukweli na maslahi ya nchi.
Hii ni mara ya kwanza kwa nchi yetu kupitia mchakato sahihi wa Katiba ya Muungano kwa njia ya Tume huru, tofauti na nyuma ambapo Katiba zilipatikana kwa misingi ya maslahi ya kisiasa na wanasiasa chini ya “ukuu” wa Chama badala ya “ukuu” wa wananchi.
Piga-ua, na bila kujifaragua kwa lelemama na “uparanganyaji” wa kisheria, msingi wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Mkataba wa Muungano uliotiwa sahihi na waasisi wake Aprili 22, 1964 na kuridhiwa na “mabunge” ya nchi hizo wanachama Tanganyika na Zanzibar, Aprili 25, 1964 kuwa Sheria ya Muungano ya 1964. Bado ni hoja hai kwamba Mkataba huo haukupata kuridhiwa kwa upande wa Zanzibar. Iwe hivyo isiwe, si lengo la makala hii kujadili hilo.
Utaratibu wa kupata Katiba halali ya Muungano, tofauti na taratibu zilizotumika siku za nyuma na kufanya uhalali wa Katiba hizo, pamoja na iliyopo sasa, kuhojika, umefafanuliwa vyema kwenye ibara ya 7 (b) ya Mkataba wa Muungano inayosema: “Rais wa Jamhuri ya Muungano, kwa makubaliano na Makamu wa Rais ambaye pia ni Mkuu wa Serikali ya Zanzibar (a) atateua Tume kufanya Mapendekezo ya Katiba kwa ajili ya Jamhuri ya Muungano (b) Ataitisha Bunge la Katiba lenye wawakilishi kutoka Tanganyika na Zanzibar….. kwa madhumuni ya kupitia Mapendekezo ya Tume na kupitisha [to adopt] Katiba [hiyo] ya Jamhuri ya Muungano”.
Hatuna sababu ya kuparanganyika juu ya jambo hili kwa sababu utaratibu halali unaopashwa kufuatwa upo; wala hatuhitaji kushindana kwa viwango vya uhayawani kwa kumwandama Jaji Warioba kwa Tume yake kuzingatia kinachopashwa kuzingatiwa, na kana kwamba Tume hiyo ni ya Jaji Warioba pekee.
Msingi mkuu wa Muungano ni mambo ya Muungano [Union matters] na tafsiri sahihi juu ya mgawanyo wa madaraka ndani ya Muungano; bila hivyo ni kuzua “kero” za Muungano na kuparanganyika kwa Muungano.
Mambo asilia ya Muungano tangu mwaka 1964 ni kumi na moja tu, lakini yameongezeka kinyemela kinyume cha Mkataba wa Muungano kufikia 22. Mambo hayo kumi na moja kwa mujibu wa ibara ya 4 ya Mkataba wa Muungano ni: Katiba ya Muungano na Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Mambo ya Nchi za Nje, Ulinzi [sio na Usalama liliongezwa mwaka 1984], Polisi, Mamlaka juu ya hali ya hatari na Uraia.
Mengine ni Uhamiaji, Mikopo na Biashara ya Nje, Utumishi wa Umma katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Kodi ya Mapato, ushuru wa Forodha na ushuru wa Bidhaa; na mwisho, Bandari, Usafiri wa anga wa kiraia, Posta na simu za maandishi [telegraphs].
Kwa njia ya kinyemela, kama tutakavyoona hivi punde, yameongezeka yafuatayo kufikia mambo 22: Sarafu na Fedha, Leseni za Viwanda na Takwimu, Elimu ya juu, Maliasili, mafuta na gesi asilia, Baraza la Taifa la Mitihani, usafiri na usafirishaji wa anga, Utafiti, Utabiri wa hali ya hewa, Mahakama ya Rufani, na Uandikishaji [usajili?] wa Vyama vya Siasa.
Tume ya Warioba, kwa upande wake imekuja na mambo saba ambayo ni: Katiba na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano, Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano, Uraia na Uhamiaji [zimeunganishwa], Sarafu na Benki Kuu, Mambo ya Nje, Usajili wa Vyama vya siasa, na Ushuru wa Bidhaa.
Pamoja na kutotajwa katika nyongeza ya mambo ya Muungano, Mahakama ya Jamhuri ya Muungano [ya Rufani na ya juu], linapashwa kuwa jambo la nane la Muungano kwa vile limebainishwa vyema kwenye ibara ya 150 ya rasimu.
Kwa mapendekezo ya Tume, mambo yafuatayo ambayo hapo awali yalikuwa ya Muungano yameachwa, badala yake yatashughulikiwa na “nchi” wanachama chini ya Sheria zake: Mikopo na Biashara ya nchi za Nje; Kodi ya Mapato, Bandari na usafiri wa anga, Posta na Simu, Leseni za Viwanda na Takwimu, utafiti, Elimu ya juu na utabiri wa hali ya hewa.
Je, kwa kupunguza mambo ya Muungano kutoka 22 hadi saba, Tume ya Jaji Warioba itakuwa imefanikiwa kuuzika mzimu wa “kero za Muungano” na hofu ya Wazanzibari kutaka kumezwa na Tanganyika ambayo ndiyo Tanzania?.
Dhana ya Serikali mbili
Tumeandika mara nyingi katika safu hii kuelezea “hofu” ya Rais wa Tanganyika, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa Zanzibar kuwa karibu na Tanganyika, akibainisha hatari ya ujirani huo na jinsi Zanzibar “itakuja kutuumiza kichwa huko mbele”, kama alivyosema.
Tumeelezea pia juhudi za Mwalimu, kuanzia miaka ya mwanzo ya 1960, kutaka kuona Shirikisho la Afrika Mashariki [EAF] likiundwa ili Zanzibar imezwe ndani ya Shirikisho, na jinsi alivyoinyaka Zanzibar kuingia Muungano na Tanganyika pale EAF liliposhindwa ili mradi tu kukidhi hofu yake kwa Zanzibar kuwa mlangoni mwa Tanganyika.
Lakini hatari hiyo na “hofu” ya Mwalimu isingeweza kupata tiba kama Zanzibar ingeachwa kubakia na mamlaka na hadhi kubwa [autonomy and identity] ndani ya Muungano kama Wazanzibari walivyotaka.
Mtego ulitegwa kwa ustadi mkubwa kwa Zanzibar kuonekana inabakia kama “nchi” wakati sivyo, na Tanganyika ikifunikwa blanketi [isionekane] la Tanzania kufanya iwe ndiyo Tanzania na hapo hapo kama Tanganyika kwa maana ya kuwa ndiyo Muungano wenyewe. Na hii ndiyo dhana ya Muungano wenye Serikali mbili, kwa maana ya Zanzibar na Tanganyika – Tanzania.
Kusudio kubwa lilikuwa ni kuendelea kuongeza orodha ya mambo ya Muungano kwa njia ya amri ya Rais [Presidential Decrees] hadi Zanzibar ijikute mambo yote yamekuwa ya Muungano ikose mamlaka na hatimaye kumezwa ndani ya Muungano wenye Serikali moja.
Mtego ulivyosukwa
Mkataba wa Muungano huo wenye ibara nane tu, uliandaliwa kwa dharura, ustadi na kwa siri kubwa chini ya siku saba kufuatia kuvunjika kwa mazungumzo ya kuunda EAF. Wanasheria waliohusika kikamilifu na zoezi hili ni aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Tanganyika, Roland Brown, Mwandishi wa Sheria [Legal Draughtsman] wa Tanganyika, P. R. Ninnes Fifoot, na aliyekuwa “Solicitor General”, Mark Bomani, ambaye alinukuliwa akisisitiza “Mkataba huu uwe ni siri kubwa kabisa”.
Wakati Mwalimu alinufaika na ushauri makini wa kisheria kutoka jopo la wanasheria hao watatu, Karume kwa upande wake hakupata ushauri wowote kwa sababu ilielekezwa, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Wolfgang Dourado, apewe likizo ya dharura ya siku saba na asionekane hadi zoezi hilo liwe limekamilika.
Pia Karume hakulitaarifu Baraza lake la Mapinduzi juu ya wazo wala mchakato huo kwa vile alijua fika kwamba lingeukataa, wakati yeye aliuhitaji kujiponya kutoka kwa wahasimu wake wenye siasa za mrengo wa kushoto ndani ya ASP na Baraza waliotaka kumng’oa madarakani kwa madai ya kushindwa kusimamia na kuendeleza Mapinduzi Visiwani.
Huku akiwa hajui maudhui ndani ya mkataba huo, Karume alitia sahihi akiamini ameingia Mkataba kuunda Shirikisho lenye serikali tatu – Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar na Serikali Kuu ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Dourado aliporejea, alimtonya juu ya “mchezo” ulivyochezwa ndani ya Mkataba; Karume akashtuka kiasi cha kutaka kususia sherehe za kubadilishana Hati za Muungano, mjini Dar es Salaam, Aprili 27, 1964, lakini akajipa moyo akisema: “Ulaghai huu tutaupatia dawa baadaye; kama wao [Watanganyika] hawana Serikali, si shauri yao wenyewe?”.
Ustadi wa wanasheria
Alipomwagiza Roland Brown aandae Mkataba wa Muungano, Mwalimu alielekeza Muundo uwe “kama ulivyo uhusiano kati ya Uingereza [iwe ndiyo Tanganyika] na Ireland ya Kaskazini [iwe ndiyo Zanzibar] bila mtu mwingine yeyote kujua”.
Kwa sababu Muungano huo wa dharura uliundwa bila kuwa na Katiba yake, Mkataba, chini ya ibara ya 3 ulielekeza kuwa, katika kipindi cha mpito hadi Muungano utakapopata Katiba yake ndani ya mwaka mmoja, Katiba ya Taganyika ndiyo itakuwa pia Katiba ya Jamhuri ya Muungano, kwa kurekebishwa kuingiza mambo yote ya Muungano.
Ustadi wa wanasheria hao unajionesha kwenye ibara 3 (a) na 4 ambapo, wakati ibara ya 3 (a) inalipa Bunge la Zanzibar na Rais wa Zanzibar mamlaka ya kujitawala kwa mambo yote yasiyo ya Muungano, ibara ya 4 inalipa Bunge na Rais wa Muungano mamlaka juu ya mambo yote ya Muungano na mamlaka pia kwa mambo yote yasiyo ya Muungano ndani na kwa ajili ya Tanganyika.
Ni kusema kwamba, Bunge la Muungano na Rais wa Muungano wanatawala Muungano na Tanganyika pia, wakati hawatawali Zanzibar kwa mambo yasiyo ya Muungano.
Pamoja na ustadi huu wa kuficha Muundo sahihi wa Muungano unaotakiwa/na au uliokusudiwa, ibara ya 5 ya Mkataba inaibua hoja ya Serikali tatu kwa kutamka kuwa, kuanzia siku ya Muungano na kuendelea, “Sheria za Tanganyika zilizopo na zile za Zanzibar zitabakia na nguvu na kuendelea kutumika katika nchi hizo….”.
Kwa mujibu wa kifungu cha 2 cha Sheria ya Muungano Namba 22 ya 1964, neno “Sheria zilizopo” limetafsiriwa kumaanisha “Sheria zilizoandikwa na ambazo hazijaandikwa kama zilivyokuwa kabla ya Muungano”. Ni kusema kwamba, kufuatia Muungano, Tanganyika haikufa kama ambavyo tu Zanzibar haikufutika.
Ustadi wa kuficha mambo umeoneshwa pia kwenye ibara ya 5 (b) ya Mkataba wa Muungano na kifungu cha 8 (2) cha Sheria ya Muungano, kwa kumpa Rais wa Jamhuri ya Muungano mamlaka ya kufanyia marekebisho kwa njia ya AMRI ya Rais, Katiba ya Tanganyika kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano, na Sheria za Tanganyika kwa mambo kadha wa kadha kutumika Zanzibar na kuzifuta zile za Zanzibar.
Ndiyo kusema, Katiba ya kwanza ya Muungano, ilipitishwa na kusimikwa na mtu mmoja – Rais wa Muungano ambaye alikuwa pia Mkuu wa Serikali ya Tanganyika na mtu wa upande mmoja wa Muungano - Tanganyika. Karume hakushirikishwa.
Ni Mamlaka turufu ya Mwalimu Nyerere yaliyotumika kusimika mfumo wa kisheria wa Muungano. Na kwa kutumia mamlaka hayo turufu, Mwalimu aliweza kuongeza mambo ya Muungano ki-imla hata yale ambayo hayakukusudiwa chini ya Mkataba wa Muungano ili kukidhi “hofu” yake ya kale. Na hili ndilo chimbuko kuu la kero za Muungano.
Tunafahamu, chini ya Mkataba wa Muungano, Rais hana mamlaka ya kuongeza wala kurekebisha Mambo ya Muungano kama ambavyo tu Bunge halina mamlaka hayo. Kitendo hicho kilikuwa ni ukiukaji dhahiri wa Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano na hivyo ni batili.
Karume acharuka
Kwa Karume, hilo halikumnyima usingizi. Yeye alikwishasahau juu ya Muungano tangu ulipoundwa na baada ya kugundua “ulaghai” kwenye Mkataba pamoja na utekelezaji wake kiasi kwamba, Juni 1964, miezi miwili tu tangu uundwe, alicharuka akisema “Kwangu mimi Muungano si chochote, Muungano ni kama koti tu, unalivaa inapokuwa baridi, unalivua inapokuwa joto; na vivyo hivyo likikubana”.
Kwa jinsi hii, Karume alijikita pekee katika kujiimarisha Visiwani, na aliutumia Muungano kama mwavuli tu alipoona inafaa kuwadhibiti mahasimu wake.
Kiburi cha Karume dhidi ya Muungano na Nyerere kiliendelea kujionesha alipoendelea kupokea misaada ya kiuchumi na Kijeshi kutoka China, Ujerumani Mashariki na Urusi, japokuwa mambo hayo ni ya Muungano.
Pia aliendelea kudhibiti akaunti ya fedha za Kigeni na Benki pamoja na mambo ya Uhamiaji na Biashara ya nje huku akielewa ni mambo ya Muungano na ulikuwa ukiukaji wa Mkataba. Na kila alipoulizwa na Mamlaka ya juu kuhusu ukiukaji huo, siku zote alijibu kwa mkato akisema, “…..kama ni hivyo basi, tuvunje Muungano”.
Ukweli Karume hakutaka Jeshi la Ukombozi la Watu wa Zanzibar [ZPLA] kuingizwa kwenye mfumo wa Jeshi la Muungano [TPDF] na alikubali tu kwa shuruti mwaka mmoja baadaye.
Ili kuratibu mambo ya Zanzibar na kudhibiti hali, Mwalimu alimhamisha swahiba wake na Waziri pia, Bhoke Munanka, kutoka Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais [Kawawa] kwenda Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais [Karume] Visiwani kwa lengo la kutoa taarifa kuhusu mwenendo wa Karume juu ya Muungano; lakini akalazimika kumrejesha Dar es Salaam muda mfupi baadaye bila kuambua kitu.
Ukinzani na uhasama wa viongozi hawa wawili juu ya Muungano ulifikia mahali wao kutokutana au kuzungumza ana kwa ana ila kupitia wapambe wao – Bhoke Munanka kwa upande wa Nyerere na Aboud Jumbe kwa upande wa Karume.
Kuuawa kwa Karume mwaka 1972 hakukubadili hali, kwani mrithi wake, Aboud Jumbe Mwinyi, alifuata nyayo kwa kuhoji uhalali wa Muundo wa Muungano wenye Serikali mbili akitetea Muundo wa Serikali tatu kuwa ndio uliokusudiwa chini ya Mkataba wa Muungano. Kama kawaida, nguvu na ubabe uliozoeleka ukamwengua kwa kuthubutu kukanyaga “mahali patakatifu, waliposhindwa Malaika kutua”.
Hiyo ndiyo ilikuwa Zanzibar ya Karume, na ndiyo Zanzibar ya leo. Sasa Wazanzibari wana “nchi” yao, yenye Rais Mtendaji, Bunge, Mahakama, wimbo wa Taifa na ngao ya Taifa na kuacha Katiba ya Muungano ikipiga mwayo imesheheni mambo 22 ya Muungano kama pambo tu na kama ishara pia ya kubezwa yote yaliyo nje ya Mkataba wa Muungano na ubabe unaotumika.
Tunaotaka kuendelea na Muundo wa Serikali mbili tujipime, kama tuna ubavu wa kuwalazimisha Wazanzibari wabadili Katiba yao kurejea enzi za imla za ukiukaji wa Mkataba wa Muungano.
Tunafahamu, Muundo wa Serikali tatu uliopendekezwa na Tume ya Jaji Warioba ndio unaotakiwa na Wazanzibari walio wengi, badala ya Serikali mbili za wanasiasa; ikilinganishwa na wale wanaotaka Muungano uvunjwe au kuwe na Muungano wa Mkataba. Je, kupungua kwa mambo ya Muungano kutoka 22 ya sasa hadi saba, kutazika mzimu wa kero za Muungano na kuusalimisha?
Katika kujadili rasimu ya Katiba mpya, busara lazima itawale, badala ya kujaribu kuokoa “nafsi” za wahafidhina wa Vyama vya siasa na kuuangamiza Muungano wetu.

PART II
KATIKA sehemu ya kwanza ya makala haya, tuliona misingi mikuu inayopaswa kufuatwa katika kutunga Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuzingatia na kuongozwa na Mkataba wa Muungano wa 1964, ambao Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jaji Joseph Sinde Warioba imejitahidi kuzingatia.
Aidha tuliona pia kazi ya Bunge la Katiba, ambapo kwa mujibu wa Sheria ya Muungano Namba 22 ya 1964, kifungu cha 9 (1) ni “Kuridhia (rasimu) na kukubali (to ratify and adopt) Katiba ya Serikali ya Jumhuri ya Muungano”.
Tuliona pia aina ya muundo uliokusudiwa na jinsi, kwa kutumia wanasheria wa nchi za Magharibi (Roland Brown, Fifoot), matakwa ya Mkataba huo yalivyopindishwa kwa kufifisha “uhuru” (autonomy) na sura au utambulisho (identity) wa Zanzibar uliokusudiwa chini ya Mkataba, na hivyo kumfanya Rais wa Kwanza wa Zanzibar, hayati Abeid Amani Karume acharuke kutaka kususia Muungano.
Sababu kubwa ni kwamba, Karume alitia sahihi Mkataba wa Muungano (kwa kutegeshewa?) bila kujua maudhui na yaliyokuwamo kwenye Mkataba. Upo ushahidi kwamba, aliwaonesha Mkataba huo baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Mapinduzi baada ya kueleweshwa vyema na Dounado kuhusu yaliyokuwamo nao hawakuridhika; kisha akasema, “Kama hamuutaki (Mkataba huu), nitaurudisha kwake (Nyerere)”. Licha ya kutoridhiwa na Baraza hakupata kuurudisha.
Na baada ya kubaini jinsi alivyochengwa kufikia Muungano na utekelezaji kinyume na alivyotarajia, Karume alitupilia mbali kila kitu na kuwa mtu wa kujihami daima dhidi ya Muungano kutaka kufifisha mamlaka yake. Aliitawala Zanzibar kama “nchi huru” kwa ndani, hata kwa mambo yaliyopaswa kushughulikiwa na Muungano. Kilichoibuka ni Kero za Muungano ambazo zimedumu hadi leo.
Niharakishe kusema hapa kwamba, uhasama wa viongozi hawa wawili ulisababisha uteuzi wa Tume ya Katiba na Bunge la Katiba lililopaswa kuitishwa ndani ya mwaka mmoja kupitisha Katiba ya Muungano lisiteuliwe “hadi wakati mwingine mwafaka”.
Bunge hilo, kwa mujibu wa Mkataba, ndilo hili linaloendelea hivi sasa Mjini Dodoma. Ni kusema kwamba, kwa miaka 50 ya Muungano, Tanzania imetawaliwa kwa Katiba zilizopatikana kwa taratibu zisizozingatia matakwa ya Muungano.
Kero ni nyingi, lakini kero ya kwanza ya Muungano ilikuwa Mei 19, 1964 wakati aliyekuwa Waziri wa Biashara na Viwanda wa Muungano, Kassim Hanga, alipohudhuria Baraza la Huduma za pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACSO) mjini Nairobi kama Mwakilishi wa Tanzania.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, iliyosomwa na mteule wake, aliyekuwa Rais wa Kenya wa wakati huo, Jomo Kenyatta, hakuficha furaha yake kwamba, “kufuatia Muungano wa Tanzania, Zanzibar haitashiriki tena kama “Mtazamaji” (Observer) bali kama Tanzania”.
Ikumbukwe kuwa, kuanzia miaka ya 1963, wakati Mwalimu Nyerere akipigia chepuo kuundwa kwa Shirikisho la Afrika Mashariki hadi liliposhindwa Aprili 10, 1964, Zanzibar ilihudhuria vikao hivyo kama mwalikwa mtazamaji.
Hanga akagutuka, na usiku huo akampigia simu Karume kumjulisha hilo. Kwa hasira, Karume akamwagiza Hanga kurejea Zanzibar (sio Dar es Salaam iliyomtuma) mara moja kwa kile kilichoitwa “Zanzibar haikuhitaji EACSO”, na kuacha mkutano ukiendelea.
Pigo kubwa la pili kwa Muungano kwa mkono wa Karume ni pale alipopitisha (Amri) Sheria (Decree) kufanya ASP kuwa Chama pekee chenye mamlaka ya juu kuliko vyombo na taasisi zote Visiwani. Hiyo ilikuwa Mei 11, 1965 miezi, miwili tu kabla Tanzania kuwa nchi ya Chama kimoja. Chini ya amri hiyo, Chama cha ASP kiliunganika na Serikali kuwa ndicho Serikali na Serikali kuwa ndiyo ASP.
Chini ya amri hii pia, Karume alianzisha idara saba ambazo ni Jeshi, Polisi, Usalama, Vijana, Wafanyakazi, Wanawake na Wakulima, zikiongozwa na Wakuu wa Idara wa kuteuliwa na yeye mwenyewe, kwa kushauriana na Baraza la Mapinduzi.
Lengo lilikuwa ni kuhamisha kwa staili yake, mamlaka ya vyombo vya ulinzi Visiwani kama Jeshi, Polisi na “Usalama”, kutoka kwenye Muungano kuwa ndani ya mamlaka ya Wazanzibari.
Na ndivyo ilivyokuwa kwa Mahakama, pale Zanzibar ilipoanzisha muundo wake wa Mahakama na kujitoa kwenye Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki, na baadaye hukumu za “Mahakama” za Kizanzibari kutokatiwa rufaa kwenye Mahakama Kuu ya Tanzania. Kwa baadhi ya “hukumu”, Karume mwenyewe alikuwa na mamlaka ya mwisho.
Jambo lingine lililotikisa Muungano wakati wa Karume, lakini akashindwa kwa kunaswa kwa “mtego” wa kisheria, lilihusu mambo ya Benki na Fedha.
Wakati wa enzi za ukoloni, nchi za Tanganyika, Kenya, Uganda na Zanzibar ziliunda, kwa njia ya hisa, Taasisi ya sarafu Afrika Mashariki (East African Currency Board) – EACB, iliyosimamia “sarafu” chini ya usimamizi wa Waziri wa Makoloni wa Uingereza.
Nchi wanachama zilistahili gawio la faida na haki ya kukopa kutoka EACB. Baada ya uhuru, usimamizi wa EACB uliwekwa mikononi mwa serikali za kila nchi zilizowakilishwa EACB, ikiwamo Zanzibar.
Lakini kwa Zanzibar, hata hivyo, Muungano kati yake na Tanganyika kuwa “nchi moja” kulibadili mambo kufanya kutokuwa na uwakilishi EACB. Japokuwa jambo ya fedha na mabenki hayakuwa ya Muungano, kama ambavyo pia Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha wa wakati ule, D. Namfua alivyokiri, katika barua yake kwa utawala wa nchi, Kumb. TYC/46/01/502 ya Juni 9, 1964, kwamba “Zanzibar ingeweza kushiriki kwa mwavuli wa “Ushirikiano wa kimataifa”, lakini Namfua hakuelewa kwamba kwa sababu Mambo ya Nje lilikuwa jambo la Muungano, na Zanzibar haikuwa Taifa licha ya kuwa “nchi” isiyo dola, isingeweza kushiriki.
Kufuatia kushindwa kwa juhudi za kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki, nchi zote tatu, isipokuwa Zanzibar ambayo sasa ilikuwa “Tanzania”, ziliamua kuanzisha Benki Kuu na sarafu zake.
Hapo, mgogoro wa ndani ukazuka juu ya mambo matatu: Kwanza, kama Zanzibar ilistahili kupokea na kunufaika na hisa zake za EACB baada ya kuvunjika kwa EACB; pili, nafasi na wajibu wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) tarajiwa kwa mambo ya Fedha ya Zanzibar. Na tatu, nini kingezuia Zanzibar kuanzisha Benki Kuu na sarafu yake, ikizingatiwa kwamba mambo hayo hayakuwa ya Muungano?
Wakati maswali haya yakiwa bado hayajapata majibu, Karume alianza mchakato wa kuanzisha Benki Kuu ya Watu wa Zanzibar yenye mamlaka na udhibiti wa akiba ya fedha ya Zanzibar.
Na kwa kasi ya pekee, akahamisha akiba ya paundi za Uingereza 700,000 kutoka Benki Grindlays ya Uingereza kwenda Benki Norodony Moscow, tawi la London, ili fedha hiyo isiweze kufikiwa na Benki za Uingereza, nchi ambayo ilikuwa nyuma ya (hila za) Muungano, wala zisinyakuliwe na Serikali ya Muungano.
Karume ategeshewa
Kwa hili, na kutokana na ukweli kwamba Fedha halikuwa jambo la Muungano, hoja ya Zanzibar ilikuwa na mantiki nzito. Lakini Serikali ya Muungano haikutaka kuona Zanziabar ikiwa na Benki yake. Hapo tena, magwiji wa sheria wa Mwalimu Nyerere, wakiongozwa na Roland Brown, aliyepata kuandaa Mkataba na Sheria tata ya Muungano yenye makengeza ya nyoka mwenye sumu kali, wakaingia kazini kudhibiti mbio za Karume.
Ukaandaliwa Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba ya Muda, kufanya Sarafu, fedha za Kigeni na udhibiti wa ubadilishanaji fedha, kuwa mambo ya Muungano, na kuwasilishwa Bungeni Juni 10, 1965, na kupitishwa siku hiyo hiyo.
Kana kwamba alikuwa ametegeshewa ajikaange mwenyewe, Karume, wakati huo akiwa Kaimu Rais wa Jamhuri ya Muungano wakati Mwalimu akiwa nje ya nchi, alipewa Muswada huo uliopitishwa na Bunge na kuutia sahihi siku hiyo hiyo kuwa Sheria Namba 21 ya 1965, na kuanza kutumika siku hiyo hiyo.
Kama ambavyo alivyotia sahihi Mkataba wa Muungano mwaka 1964 bila kujua alichokuwa akitilia sahihi, vivyo hivyo safari hii tena, Karume hakujua nini alichokuwa akitilia sahihi. Hata wabunge wa Bunge la Muungano kutoka Zanzibar hawakubaini madhara kwa Zanzibar, kwa kile walichokuwa wakipitisha.
Baada ya kutia sahihi Muswada huo na kurejea Zanzibar, alielezwa na Dourado jinsi sheria aliyotia sahihi ilivyokuwa na athari kubwa kwa maslahi ya Zanzibar, na kwamba asingefanya lolote kwa sababu ilikwishakuwa sheria.
Bila kujali yaliyotokea, Karume aliendelea na mchakato wa kuanzisha Benki ya Watu wa Zanzibar kwa kuteua Tume ya Benki ya kupendekeza Muundo na Mamlaka ya Benki, iweze kufanya kazi za Benki Kuu na kutambuliwa hivyo na Sheria za Muungano.
Kuanzishwa kwa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) mwaka 1966 kulimkata ngebe Karume na mbio za kuanzisha Benki ya watu wa Zanzibar. Wazanzibari walilowa, pale Nyerere, kwa mamlaka aliyopewa chini ya ibara ya 5 (b) ya Mkataba wa Muungano, na kifungu cha 8 (2) cha Sheria ya Muungano kama tulivyoona mwanzo, alipotoa Amri kwamba, Sheria ya Tanganyika ya Benki na Fedha za Kigeni (Cap 139) itumike pia Zanzibar.
Hoja za Wazanzibari zikaendelea kupata majibu ya uhakika. Katika waraka wake kwa uongozi wa Zanzibar, Kumb. TYC.46/01 wa Machi 22, 1966; aliyekuwa Waziri wa Fedha wa wakati huo, Amir Habib Jamal, alisema yote kwamba, kuanzia wakati huo, “ ni Gavana wa BOT pekee ndiye atakuwa kwenye Bodi ya EACB, na Zanzibar haitawakilishwa”.
Pili, kwamba mgawo wa rasilimali na mtaji, na au faida iliyopatikana kutokana na Tanganyika na Zanzibar kuwekeza katika EACB italipwa Serikali ya Tanzania. Tatu, kwamba, michango yote pamoja na riba iliyolimbikizwa na Zanzibar italipwa na Hazina ya Tanzania.
Nne, kwamba, baada ya EACB kuvunjwa na mali kugawanywa, mali ambazo vinginevyo zingekwenda Zanzibar, zitachukuliwa na Serikali ya Muungano. Tano, ilifanywa marufuku kwa Zanzibar kuanzisha Benki Kuu, lakini ikaruhusiwa kuanzisha Benki ya kawaida kwa Sheria za Zanzibar, mradi tu benki hiyo isifanye kazi zilizo mahsusi kwa Benki Kuu.
Zanzibar haikamatiki
Ilikuwa rahisi kuidhibiti Zanzibar enzi za udikteta wa chama kimoja na “hekima” za ‘mkono wa chuma’ za Mwalimu Nyerere na umbumbumbu wetu, kuliko enzi hizi za “uamsho” (re-awakening), demokrasia, sayansi na teknolojia.
Ni ujinga kuficha Mkataba wa Muungano kwa kuwaambia wanaouhitaji kwamba haupo, na eti kwamba wanaotaka kuona nakala yake waende Umoja wa Mataifa ulikohifadhiwa!
Kwa ujumla, kiburi na kejeli za hayati Karume kwa Muungano zilikuwa za msingi kama tunavyobaini sasa kutokana na lundo la kero za Muungano mbele yetu. Pamoja na udikteta wake, lakini kama kuna kitu Wazanzibari kinachofanya wamheshimu na kumtukuza mwasisi huyo wa Taifa la Zanzibar na Muungano, ni Uzanzibari na ungangari wake wa kutotaka kuburuzwa kwa mambo yaasiyo ya Muungano.
Wasomi na Serikali mbili au tatu
Wasomi wa Sheria, Sayansi ya Jamii na Siasa wanaelewa fika kwamba Muungano uliokusudiwa ni wa Shirikisho, lakinii kwa kujipendekeza kwa wanasiasa na kutojiamini, wakati mwingine wanakubali kusaliti taaluma zao kusimamia serikali mbili; huku ukweli na historia ukiwasuta.
Profesa wa Sheria, B.P. Srivastava, katika “The Constitution of the United Republic of Tanzania – Some Salient Features, some Riddles” (East Africa Law Review – 1981 – 83), anabainisha Muundo sahihi wa Muungano kwa kusema, “Jamhuri ya Muungano iliyokusudiwa ni ya muundo wa pembe tatu, ambapo Tanganyika na Zanzibar zinaunda kona mbili za kitako, na Jamhuri ya Muungano inaunda kizingia (vortex)”.
Naye gwiji la Sheria na Mwanasheria Mkuu wa kwanza wa Zanzibar huru, ambaye mwaka 1964, kwa uelewa wake wa Sheria, alitupwa nje kila mara wakati wa mchakato wa Muungano, Wolfgang Dourado, katika andiko lake “The Consolidation of the Union: A basic Re-appraisal” (mada kwenye Semina ya Chama cha Wanasheria cha Tanganyika, 1983) anasema: “Watu wengi, wakiwamo viongozi wa Chama na Serikali, wanashindwa kufahamu kwamba, Serikali ya Muungano yenye kutekeleza mamlaka juu ya mambo ya Muungano kwa eneo lote la Muungano, ni serikali tofauti na ile ya Muungano inayotekeleza mamlaka kwa mambo yasiyo ya Muungano kwa ajili ya na ndani ya Tanganyika.
“Kwa mantiki hii, kuna serikali tatu, kwa maana ya Serikali ya Muungano inayotekeleza pia mambo ya Tanganyika yasiyo ya Muungano, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano kwa ajili ya Mambo ya Muungano”.
Profesa Issa Shivji, gwiji lingine la sheria nchini, ambaye siku za karibuni ameonekana kujichanganya kwa kutetea Muundo wa Serikali mbili, anakiri Muungano wetu ni wa Shirikisho lenye serikali tatu.
Katika kitabu chake, “The Legal Foundations of the Union (uk. 37 na 39) anasema: “Wakati Wazanzibari wako chini ya Serikali mbili – Serikali Kuu ya Muungano na Serikali ya kikanda ya Zanzibar kama ilivyo kwa Shirikisho lolote lile, Watanganyika wao wako chini ya Serikali moja; lakini ni sehemu tu ya serikali.
Kwa kuziweka pande zote pamoja, na kwa kuitazama Sheria ya Muungano ilivyo, nawasilisha kwa uhakika kwamba, msingi wa kishirikisho unaotawala Sheria ya Muungano wetu ni aina ya Katiba ya Shirikisho”.
Akimnukuu aliyekuwa Jaji Mkuu wa India, Sikri, katika kesi ya Kesavananda, Shivji anasema: “Yatakuwa marekebisho haramu, kama yatafanyika (na yaliyofanyika), kubadili msingi, muundo au maudhui muhimu ya Katiba (Mkataba wa Muungano) kuhusu yafuatayo: Ukuu wa Katiba (Mkataba wa Muungano), Jamhuri na udemokrasia wa Serikali, Katiba isiyo ya kidini, mgawanyo wa madaraka kati ya Bunge, Utawala na Mahakama; na mwisho, Muundo wa kishirikisho wa Katiba”.
Anasema: “Muundo wa Serikali ya kishirikisho unaoainishwa katika kifungu cha 5 cha Sheria ya Muungano, ndio msingi mkuu wa watu wa Tanganyika na Zanzibar kuungana…. Kamwe, upande mmoja wa Muungano hauna mamlaka kubadili mgawanyo wa madaraka na Msingi wa Muungano, na kwamba kitendo kama hicho ni batili”.
Shivji anamaliza kwa kupigilia msumari (uk 45) akisema:” Kuongezwa kwa mambo ya Muungano kulikofanywa kwa AMRI ya Rais na Bunge, ni kitendo haramu cha kubaka madaraka na kudhalilisha msingi mkuu wa Muungano; ni kinyume cha msingi unaotawala mfumo wa Shirikisho kuweza kubomoa msingi wa Muungano”.
Wazanzibari wasaliti wa Muungano?
Mengi yamesemwa juu ya Zanzibar kuwa na Katiba yake inayotambua, pamoja na mambo mengine makuu, Zanzibar kujitambua kama nchi yenye mipaka kamili, na kwamba nchi hiyo ni miongoni mwa nchi mbili (iko wapi ya pili?) zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Na kwa mujibu wa ibara ya 132 ya Katiba hiyo, Sheria za Muungano zilizopitishwa na Bunge la Muungano sharti zijadiliwe na kuridhiwa na Baraza la wawakilishi kama njia ya kukomesha tabia iliyozoeleka ya kupanua orodha ya mambo ya Muungano.
Yote haya ni kwa Zanzibar kutaka kuona Zanzibar na Tanganyika zinakuwa “nchi” zenye mamlaka kamili kwa mambo yasiyo ya Muungano. Kwa hilo hatuwezi kuwabandua, piga-ua, hata kama ni kwa kura ya wazi au ya siri.
Kwa mtazamo wa juu juu, huu unaweza kuonekana kama usaliti wa Wazanzibari kwa Muungano, lakini kilichofanyika na wanachofanya ndio ukweli wenyewe, kwamba Muungano wetu ni wa kishirikisho na hauwezi kubadilika maadam Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano zipo na zinataka hivyo. Mengine yote na kinyume cha hayo ni uhafidhina wa kisiasa usiopenda kutambua na kukiri ukweli.
- src
Joseph Mihangwa
raia mwema