Friday, March 14, 2014

Prof. Issa shivji ampa somo jaji joseph warioba, kuhusu mamlaka ya bunge maalumu la katiba.

Tangu kuundwa kwa bunge maalumu la katiba, kumekuwa na mvutano miongoni mwa wachambuzi wa masuala ya kisiasa, wanasiasa, wanaharakati na wanasheria juu ya madaraka ya bunge maalumu katika mjadala wa rasimu ya katiba. Wapo wanaodai kwamba Bunge maalumu halina mamlaka ya kubadili misingi mikuu ya rasimu huku wengine wakidai Bunge hilo ni chombo kikuu cha uwakilishi wa wananchi hivyo lina mamlaka ya kubadili hata misingi ya rasimu iliyopendekezwa na tume ya mabadiliko ya katiba kwa maslahi ya Taifa. Ifuatayo ni sehemu ya uchambuzi wa Prof. Shijvi, katika makala yake ya yenye kichwa cha habari "Dhana na maana ya Bunge Maalumu la Katiba". Ninanukuu...

Mheshimiwa Warioba katika hotuba yake aliyotoa katika mkutano wa Tanzania Centre for Democracy amejenga hoja kama ifutavyo:

"Madaraka ya Bunge Maalum yanakuwa na mipaka endapo Rasimu ya Katiba imeandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba au Chombo cha aina hiyo. Bunge Maalum linaweza kuwa huru kurekebisha baadhi ya masharti yaliyomo kwenye rasimu ya Katiba lakini si suala la kawaida Bunge Maalum kubadili hoja ya msingi. Jinsi ushirikishaji wa Wananchi unavyokuwa wa wazi na mpana ndivyo madaraka ya Bunge Maalum yanavyopungua. Mantiki ni kuzuia Bunge Maalum kunyang’anya madaraka ya Wananchi, yaani “act of popular sovereignty”. Watalaam wa masuala ya Katiba, wanaeleza kuwa madaraka ya Bunge Maalum katika mazingira haya ni kuboresha Rasimu ya Katiba. Imenukuliwa kutoka Majadiliano ya Bunge (HANSARD), Taarifa Rasmi, Mkutano wa Sita, 25 Aprili-28 Aprili, 1977, uk. 11.

… Kanuni za Bunge Maalum la Katiba sharti zizingatie kwamba Bunge Maalum, kwa mujibu wa madaraka liliyopewa chini ya kifungu cha 25(1) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, sura ya 83, ni chombo cha kuboresha masharti ya Rasimu ya Katiba.

Katika kutekeleza madaraka ya kujadili na kupitisha masharti ya kikatiba, Bunge Maalum litazingatia msingi kwamba masharti ya kikatiba ndani ya Rasimu ya Katiba ni taswira, dira na ndoto za wananchi ambazo zimeelezwa kupitia maoni ya mwananchi mmoja mmoja na makundi ya wananchi kupitia asasi, taasisi, jumuiya na makundi ya Watu wenye malengo Yanayofanana. Bunge Maalum litafanya kazi ya kuboresha masharti ya Kikatiba yaliyomo ndani ya Rasimu ya Katiba pasipo kuweka masharti mapya ambayo kwa taathira yake yanabadilisha au kufifisha masharti ya kikatiba yaliyomo kwenye rasimu ya Katiba (uk. 10-11)".

Tunaweza tukajumuisha hoja kuu za Mhe. Warioba kama ifuatavyo:

1. Madaraka ya Bunge maalum kubadilisha misingi mikuu ya rasimu au la inategemea nani aliandika rasimu. Kama Bunge lenyewe limeandika rasimu, Bunge lina madaraka hayo, lakini kama rasimu imeandaliwa na ‘Tume ya Mabadiliko ya Katiba au Chombo cha aina hiyo’, Bunge Maalum linaweza kuirekebisha na kuiboresha lakini sio kubadilisha misingi yake.

2. Hoja hii inatokana na ukweli kwamba wananchi wameshiriki kutoa maoni yao yaliyowekwa katika rasimu. Bunge likibadilisha misingi itakuwa sawa na kunyang’anya ‘madaraka ya Wananchi, yaani “act of popular sovereignty”. Hii maana yake halisi ni kwamba utoaji wa maoni mbele ya Tume ilikuwa “act of popular sovereignty” ya wananchi; maoni yao ni kielelezo cha mamlaka yao.

3. Hoja hizi kuu ni kwa mujibu wa (a) ‘Wataalam wa masuala ya Katiba’; na (b) kifungu cha 25(1) cha sheria ya Mabadiliko ya. Katiba, Sura ya 83. Kutokana na hoja hizi za Mhe. Warioba, anatoa maelekezo kwamba Kanuni za Bunge Maalum zitakazotungwa na Bunge Maalum lenyewe ‘sharti zizingatie kwamba Bunge maalum … ni chombo cha kuboresha masharti ya Rasimu ya Katiba.’

UCHAMBUZI WA PROF. SHIVJI KUHUSU HOJA ZA JAJI WARIOBA NA TUME YAKE.

"1. Kuhusu madaraka ya Bunge kutegemea mchakato: Maelezo ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Sinde Warioba katika Mkutano wa Tanzania Centre for Democracy, kuhusu Tafakuri na Maridhiano kuelekea Katiba Mpya: Whitesands Hotel, Dar es Salaam, 12 Februari, 2014.

Kama nilivyoeleza hapo juu, historia ya dhana ya Bunge Maalum (constituent assembly) inasisitiza kwamba Bunge Maalum ni mwakilishi wa mamlaka (sovereignty) ya watu. Kujitungia katiba yao ni kwa mujibu wa mamlaka (sovereignty) ya watu. Kwa kuwa mamilioni ya wananchi hawawezi kukaa chini ya mti na kujadili na kuandika katiba yao, wao wanachagua wajumbe wao na wanawatuma kufanya kazi moja hii ya kuwatungia katiba. Rasimu yenyewe ya Katiba inaweza kuandikwa na kamati iliyoteuliwa na Bunge lenyewe (kama ilivyokuwa India katika kuandika katiba yao ya 1950) au rasimu inaweza kuandaliwa na kuandikwa na Tume (kama ilivyokuwa Uganda 1995). Lakini hii haibadilishi dhana na maana ya Bunge Maalum au kuweka mipaka ya madaraka ya Bunge Maalum. Katika mifano hii yote miwili, Bunge Maalum lilibadilisha mambo makubwa katika rasimu. Ukweli ni kwamba, mchakato wa Uganda haukuwa tofauti kubwa sana na mchakato wetu.

Tume ya Katiba ya Uganda chini ya Jaji Mkuu ilikusanya maoni na kuandaa rasimu pamoja na Taarifa ya uchambuzi wa kina (juzuu tatu, zaidi ya ukurasa 1000). Lakini mikono ya Bunge Maalum haikufungwa na rasimu bali Bunge lilijadili mambo mengi sana ya msingi kinyume kabisa na misingi ya rasimu. Kwa mfano, kulikuwa na sauti nzito kutoka kwa wawakilishi wa Buganda ambao walitaka muundo wa shirikisho (federal structure) badala ya muundo wa serikali moja (unitary state). Hata hivyo, hakuna yeyote katika Bunge hili – na lilikuwa na wanasheria waliobobea, akiwemo marehemu Profesa Nabudere - aliopinga kwa msingi kwamba mjadala ule ulikuwa ni batili kwa sababu ulikuwa unapinga misingi ya rasimu. Kulikuwa pia mjadala mkali kuhusu mfumo wa vyama vingi badala ya mfumo wa ‘movement system’ uliopendekezwa na Tume. Kwa hili pia, hakuna aliyepinga kwa msingi kwamba mjadala ulikuwa kinyume cha sheria au taratibu kwa sababu rasimu iliandaliwa na Tume kutokana na maoni ya wananchi. Isitoshe, pendekezo la Tume lililotokana na maoni ya wananchi kuwa na ‘National State Council’ kusuluhisha migogoro kati ya mihimili ya dola lilitupiliwa mbali na Bunge maalum, tena kwa sauti moja.

Kwa kujumuisha, ni wazi kwamba mchakato wenyewe wa kuandika rasimu ya katiba unaweza kutofautiana kutokana na hali halisi. Lakini mchakato haubadilishi mamlaka ya Bunge Maalum au kuathiri dhana yake kama chombo mahsusi cha wananchi.

Ingawa kisiasa, Bunge Maalum lililochaguliwa moja kwa moja na wananchi linakuwa na uhalali zaidi na hadhi ya juu kabisa, katika hali halisi, kutokana na uwiano wa nguvu za kitabaka na makundi katika jamii, wanaoingia katika Bunge Maalum wanaweza wakapatikana kwa njia mbalimbali, ikiwemo kuteuliwa, kama tutakavyoona hivi punde. Hata hivyo, bila kujali nani ni wajumbe wa Bunge la Katiba, kisheria dhana na hadhi ya Bunge Maalum haibadiliki. Angalia Ben Nwabueza, Constitutional Democracy in Africa, vol. 1, Ibadan: Spectrum Books, uk. 195-198. Angalia pia Mahendra P. Singh, V. N. Shukla’s Constitution of India, 9th edn. Lucknow: Eastern Book, uk. A- 24- A-25. Angalia David Mukholi (1995) Uganda’s Fourth Constitution: History, Politics and Law, Kampala: Fountaion Publishers, uk. 49)

2. Kuhusu ushirkishaji wa watu kutoa maoni: Hoja hii ya Mhe. Warioba kwa kweli ni kuhalalisha pendekezo la Tume la serikali tatu, ambalo ni msingi mkuu wa rasimu. Hoja ni kwamba pendekezo hili limetokana na wananchi wenyewe. Niseme tu, kwanza, pamoja na kazi nzito iliyofanya na Tume, pamoja na kukusanya maoni ya wananchi, hii haitoshi kunyang’anya wananchi mamlaka yao ambayo wanayadhihirisha kupitia Bunge Maalum. Tume kamwe haiwezi kuwa na hadhi sawa au zaidi ya Bunge Maalum. Tume sio mwakilishi wa wananchi, wala haikuchaguliwa na wananchi, wala sio chombo cha kufanya maamuzi. Tume inatoa mapendekezo. Mapendekezo yanaweza kukubaliwa au kutupiliwa mbali.

Kama kweli jukumu la Bunge Maalum ni kuboresha tu au kurekebisha tu mapendekezo bila kubadili misingi yake, basi hatukuwa na haja ya kuwa na Bunge lenyewe. Mapendekezo ya Tume yangeenda moja kwa moja kwa wananchi kupigiwa kura ya maoni.

Pili, ukiangalia kwa makini takwimu zilizotolewa na Tume yenyewe, wala sio sahihi kusema kwamba wananchi walio wengi walitaka serikali tatu. Kwa jumla, waliotoa maoni mbele ya Tume ni watu 351,664 (ang. Jedwali 3, uk. 9 ). Kati ya hao, 47,820 tu (asimilia 14) ndiyo waligusia muundo wa muungano. Asilimia 86 hawakuzungumzia muundo wa muungano kwa maana yoyote - ya serikali moja, mbili, tatu au muungano wa mkataba. Wao walikuwa na mambo tofauti kabisa kuhusu maisha yao. Isitoshe, kati ya waliogusia muundo, asilimia 30 walitaka serikali mbili, asilimia 37 walipendekeza serikali tatu, na asilimia 25 walitaka muungano wa mkataba; asilimia nane walitaka serikali moja.

Kwa hivyo, waliopendekeza serikali tatu ni theluthi moja tu ya waliogusia muundo wa muungano, na ni asilimia 5 tu ya waliotoa maoni. Waliotaka serikali mbili na muungano wa mkataba ni asilimia 55, yaani zaidi ya nusu ya waliotoa maoni juu ya muundo wa muungano. Hata ukichanganya waliotaka serikali moja na serikali mbili ni asilimia 38, inazidi kidogo wale waliotaka serikali tatu. Kwa takwimu hizi za Tume yenyewe, utasema je kwamba serikali tatu ni chaguo la wananchi na ni ‘taswira, dira na ndoto za wananchi’?
Sidhani kuna haja ya kusema zaidi juu ya hoja hii: haina mshiko wala ushahidi wa maana.

3. Kuhusu maoni ya wataalam wa kikatiba: Mhe. Warioba anadai kwamba watalaam wa masuala ya kikatiba wanaunga mkono kwamba Bunge Maalum lina mipaka ikiwa mchakato umefuata kuwa na Tume kuandaa rasimu. Bahati mbaya Mheshimiwa hakutaja majina yao wala kunukuu maandishi yao. Kwa hivyo ni vigumu kujua hao watalaam ni nani na walisema nini na katika muktadha gani.

4. Kuhusu kifungu cha 25(1) ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba: Takwimu na jedwali zote zinatokana na Takwimu za Ukusanyaji wa maoni ya Wananchi kuhusu Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Disemba, 2013.

Inadaiwa na Mhe. Warioba na wengine kwamba kifungu cha 25(1) cha sheria ya mabadiliko ya katiba kimeweka mipaka ya madaraka ya Bunge Maalum. Kifungu hiki kwa lugha ya Kiswahili kinasema: “25(1) Bunge Maalum litakuwa na mamlaka ya kujadili na kupitisha masharti ya katiba inayopendekezwa … . “ Kwa mujibu wa kifungu hiki Bunge Maalum lina uwezo wa (1) kujadili; na (2) kupitisha. Kifungu hiki hakisemi kwamba baada ya kujadili masharti ya rasimu, Bunge halina mamlaka ya kuyabadili. Yaani maana sahihi ni kwamba baada ya kujadili Bunge (a) linaweza kupitisha masharti haya kama yalivyo; au (b) kubadili, na kuyapitisha mabadiliko. Hakuna popote pale neno ‘kuboresha’ limetumika. Kama kweli nia ilikuwa ni kulipa Bunge mamlaka ya kuboresha au kurekebisha tu sheria ingesema hivyo. Kuna mantiki gani ya kujadili kama huna uwezo wa kuibadili au hata kuitupilia mbali?

Kifungu 25(1) cha Kiingereza kimeweka jambo wazi zaidi: The Constituent Assembly shall have and exercise powers to make provisions for the New Constitution of the United Republic of Tanzania … .

Maana ya ibara hii ni wazi kabisa. Bunge Maalum ndiyo chombo kinacho weka masharti ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano. Inaelekea tafsiri ya Kiswahili ni mbaya lakini mantiki yake ni ileile ya yale inayoelezwa katika kifungu cha Kiingereza.

Kwa kuhitimisha, ni wazi kabisa kwamba sheria ya mabadiliko ya katiba haikuweka mipaka ya mamlaka ya Bunge Maalum kama invyodaiwa. Na isingeweza kufanya hivyo kwa sababu sheria yenyewe ilipitishwa na Bunge la Kawaida, tena sio kwa theluthi mbili, ambayo ingeipa sheria ya mabadiliko hadhi ya sheria ya kikatiba (constitutional act). Na hatimaye pendekezo (proposed constitution) la Bunge Maalum halirudi kwa Bunge la Kawaida bali linapelekwa moja kwa moja kwa wananchi kupigiwa kura ya maoni. Kwa hivyo, wananchi watapigia kura zao juu ya pendekezo la Bunge Maalum na sio rasimu ya Tume. Rasimu ya Tume itakuwa na nafasi ya kihistoria tu, sio ya nguvu za kisheria.

Nafasi ya Bunge Maalum ni ya kipekee kabisa katika mchakato wa kutunga katiba mpya. Nafasi yake ni nzito kuliko ile ya Tume na muhimu kuliko kura ya maoni. Hii ni kwa sababu Bunge Maalum ndiyo chombo cha kufanya maamuzi mazito, sio Tume. Bunge ndiyo litapitia rasimu ibara kwa ibara, kufanya uchambuzi, kutathmini athari zake kwa Taifa, kuhakikisha kwamba hakuna migongano katika ibara, kuangalia kwa undani mfumo na muundo unaopendekezwa unatekelezeka au hapana na, muhimu kuliko yote, mfumo unaopendekezwa utaimarisha utulivu na amani na umoja wa nchi (national and territorial integrity) au utazaa vurugu, migogoro na hatimaye maangamizo ya nchi"
src
JF



Click image for larger version.   Name: ImageUploadedByJamiiForums1394820157.398025.jpg  Views: 0  Size: 49.2 KB  ID: 144893Click image for larger version.   Name: ImageUploadedByJamiiForums1394820226.895633.jpg  Views: 0  Size: 96.0 KB  ID: 144894