Wednesday, March 12, 2014

Kutana na Rais ajaye wa Msumbiji: Filipe Nyussi

 
Filipe Nyussi
USIJALI kama hujapata kumsikia Filipe Nyussi. Watu wa Msumbiji walio wengi pia hawajui mengi kuhusu mtu huyu. Hivyo ni wakati muafaka wa kuanza kumfahamu.
Labda mambo yaende ndivyo sivyo, na ingawa mjane wa Samora Machel, rais wa kwanza wa nchi hiyo na rais wa kwanza wa nchi hiyo, Graca Machel  hakufurahi,  Nyussi  atakuwa Rais ajae wa Msumbiji.
Jumamosi iliyopita na karibu na alfajiri ya siku iliyofuata ya Jumapili, vigogo wa chama tawala, Frelimo, walikutana Matola, karibu na Maputo, kufanya uamuzi mkubwa.
Vigogo hao wa Kamati Kuu ya Frelimo, walikuwa na jukumu la kumchagua rais mpya wa chama hicho, ambaye kwa asilimia kubwa, ndiye atakayekuwa Rais ajaye wa Msumbiji.
Rais wa sasa wa Msumbiji,  Armando Guebuza, anamalizia muhula wake wa pili wa uongozi. Kama katiba ya nchi hiyo inavyosema, ni lazima aondoke kwenye uongozi licha ya kuwa chama hicho kina wabunge wengi bungeni ambao wanaweza kubadilisha katiba kumuwezesha aendelee na ngwe nyingine.
Kwa jambo kama hili linalotokea Msumbiji, zamani barani Afrika ingekuwa ni vigumu kufanyika. Lakini sasa linawezekana, na hiyo imefanya  bara hilo sasa kuwa na marais wachache wanaokaa madarakani kwa muda mrefu.  Uchaguzi Mkuu wa Msumbiji umepangwa kufanyika Oktoba maka huu.
Frelimo ni chama chenye uzoefu mkubwa wa uchaguzi. Rekodi yake nzuri ya vita ya wenyewe kwa wenyewe, uzoefu mkubwa wa masuala ya uchaguzi na ukweli kwamba kipo madarakani hivi sasa, mambo hayo yote yanafanya kiwe na nafasi nzuri ya kushinda.
Chama hicho kimekuwa kikiongeza viti bungeni kila uchaguzi unapofanyika  tokea kumalizika kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe katika miaka ya mwanzoni mwa 1990.
Mwaka 2009 kilishinda viti 191 kati ya viti 250 vilivyopo bungeni. Kimsingi, umaarufu wa Frelimo unafanya mgombea wa urais wa chama hicho kuwa na uhakika wa asilimia kubwa kuwa kiongozi wa nchi.
Uhaikika huo unakuwa mkubwa licha ya kuwapo kwa upinzani kutoka kwa maadui zao wa zamani wa vita ya wenyewe kwa wenyewe, Renamo, na chama kipya cha siasa cha Democratic Movement of Mozambique (MDM).
Lakini mkutano huo wa Kamati Kuu ya Frelimo ulikuwa mgumu kutabirika. Kama vilivyo karibu vyama vyote vilivyopata kuonja utamu wa mfumo wa chama kimoja,  siasa na ushindani hasa katika vyama hivyo iko ndani kwa ndani.
Makundi mawili yaliibuka wakati wa maandalizi ya mkutano huo. Kundi moja lilikuwa liko bega kwa bega na Rais anayemaliza muda wake, Guebuza na jingine linalowakilisha vigogo wa zamani, aliyepata kuwa rais wa nchi hiyo, Joaquim Chissano na Graca Machel.
“Ushindani ndani ya Frelimo ni jambo zuri,” anasema  mwanazuoni, Elisabete Azevedo-Harman na kuongeza:  “Hali ya sintofahamu iliyokuwapo wiki kadhaa kabla ya mkutano na orodha iliyowasilishwa katika dakika ya mwisho inaonyesha ya kuwa kuna demokrasia ndani ya chama hicho.
“ Chama hicho pia kilionyesha ya kuwa bado kina tabia ya kuhoji uongozi, tabia ambayo imekuwa ikioneka kila mara kinapofanya uchaguzi.”
Mwaka 2013  ilionekana kama tabia hiyo ingekoma wakati Guebuza alipoonekana kuwa na sauti kubwa katika siasa za chama hicho.
Lakini mchakato uliofanyika  wa kumpata Nyussi unaonyesha ya kuwa hakuna mtu anayeonekana kuwa mmiliki wa chama hicho.“Hiki ni kitu kizuri kwa uimarishaji wa chama,” anasema ,” anasema Azevedo-Harman.
Graca Machel alifanya kila lijnalowezekana kuhakikisha ya kuwa Guebuza hakiburuzi chama hicho kufuata matakwa yake binafsi. Licha ya kuwa yeye pia ni mjane Nelson Mandela wa Afrika Kusini, Graca anashiriki kikamilifu katika siasa za  nchi aliyozaliwa ya Msumbiji.
Kuwapo kwake kulikuwa muhimu mno siku ya mkutano wa Kamati Kuu ya Frelimo. Hotuba yake ilisisimua hasa aliposisitiza kuwapo kwa ushindani wenye maana. Muda mfupi kabla ya mkutano huo, washirika wa Guebuza walijaribu kuuteka mkutano huo uende kama wanavyotaka wao.
Majina matatu, yote yakiwa yametoka kwenye kambi yao yaliwasilishwa ili wapigiwe kura kumpata rais mpya wa Frelimo. Chissano na Graca Machel walifanikiwa kuongeza majina mawili kufanya Kamati Kuu ichague kati ya hao watano walioteuliwa.
Hata hivyo, juhudi za Chissano na Graca zilishindwa kuzaa matunda kwani kambi ya rais anayeondoka madarakani bado ilikuwa na nguvu.
Waziri wa Ulinzi, Filipe Nyussi kutoka katika kambi hiyo aliibuka mshindi kwa kuwapita wapinzani wake kwa mbali. Huo ulikuwa ni ushindi wa dhahiri kwa Guebuza kwani Nyussi ni mmoja wa wafuasi wake wakubwa.
“Kilichotokea ni kile kinachotokea mara zote Msumbiji. Rais anayeondoka madarakani kuwa bado mwenye nguvu kutokana na mtu anayechukua nafasi yake kuonekana dhahiri kwamba  ndiye aliyemjenga.
Hali ingekuwa tofauti kama mshindi angekuwa Luisa Diogo ambaye aliungwa mkono na Chissano na Graca Machel. Diogo ndiye aliyekuwa wa pili nyuma ya Nyussi hata kura zilipopigwa kwa mara ya pili. Mwanamama Diogo alipata kuwa waziri mkuu.
Joseph Hanlon, mhadhiri mwandamizi katika Chuo Kikuu Huria cha Uingereza na mtaalam wa siasa za Msumbiji anasema: “Nyussi hajulikani sana ndani ya chama na hata kwa wananchi. Si tu yuko karibu na Guebuza, lakini kupanda kwake kisiasa kumetokana na juhudi za kipekee za kiongozi huyo anayeondoka madarakani kutokana na jinsi alivyomjenga. Katika hali hiyo, uongozi wake akichaguliwa kuwa Rais wa Msumbiji utategemea kwa kiasi kikubwa ushauri wa Guebuza”.
Nyussi ni mwanasiasa ambaye hakutarajiwa kwamba ataikwaa nafasi hiyo pamoja na ukweli kwamba amekuwa Waziri wa Ulinzi tokea mwaka 2008, kwa kawaida nafasi hiyo ni ya juu.
Kabla ya kuwa Wazii wa Ulinzi alikuwa meneja wa Shirika la Reli linalomilikiwa na Serikali.  Huko ndiko walikofahamiana na Guebuza (Guebuza aliwahi kuwa waziri wa Usafirishaji hivyo Nyussi alikuwa chini yake kwani Shirika la Reli lilikuwa chini ya wizara hiyo).
“Ni vigumu kuitabiri visheni ya kisiasa ya Nyussi wala mwelekeo wake wa madaraka kwa sababu hakuna anayemfahamu nchini. Hata hivyo, kuna mambo mawili  kuhusu yeye yanayojitokeza. Kwanza ni ujana. Akiwa na umri wa miaka 55 anatoka katika kizazi kingine kulinganisha na viongozi wote waliopita wa Msumbiji.
“Nyussi ni mdogo kwa Guebuza kwa miongo miwili. Hili kwa vyovyote litampatia maksi katika kujinadi. Jambo la pili ni asili yake. Nyussi anatoka kaskazini mwa jimbo la Cabo Delgado na anakuwa kiongozi wa kwanza wa Frelimo kutoka kaskazini.
“ Ingawa Cabo Delgado ni ngome kubwa ya Frelimo, eneo la kaskazini la Msumbiji siku zote limekuwa ndiyo chanzo cha upinzani kwa chama tawala. Ni jambo la kujivunia kwamba Frelimo kwa mara ya kwanza imepata mgombea kutoka kaskazini,” anasema Azevedo-Harman.
Ni vizuri pia kufahamu ya kuwa Cabo Delgado ni sehemu ambayo gesi asilia imegundulika kuwapo.
Licha ya kuwa Nyussi ana mambo mengi yatakayompatia nafasi nzuri ya kushinda, bado atahitajika kufanya kampeni ya nguvu.
Chama kipya cha upinzani cha MDM chenye vijana wengi, kimeonyesha kuwa kiko makini kwa kufanikiwa kufanya mambo kadhaa ambayo yaliiletea taabu Frelimo.
Chama hicho kilifanikiwa kushinda chaguzi kadhaa za majimbo ya mjini dhidi ya Frelimo katika chaguzi ndogo. Kimejipatia umaarufu makubwa katika maeneo yote ya mjini.
Hata hivyo, licha ya umaarufu huo wa maeneo ya mjini, chama hicho kipya kinafahamu fika kwamba kwenye nafasi ya Urais hakiwezi kufua dafu.
Hivyo kitakazania kupata viti vya kutosha bungeni ili kukipokonya chama tawala ushindi wa theluthi mbili ambao Frelimo kinajivunia bungeni.
 Nyussi atajitahidi hilo lisifanyike ingawa kwa demokrasia yenye afya, uwiano mzuri kati ya chama tawala na upinzani ni jambo jema  kwa maslahi ya nchi.
Chama kingine cha kukiangalia ni Renamo. Kutokana na kuvunjika kwake moyo kwa kupata mafanikio kiduchu katika zama hizi za demokrasia, kimetishia kurejea tena kwenye uadui.
Baada ya tishio hilo, chama tawala kilikaa pamoja na uongozi wa Renamo ambao walikubali kushiriki katika uchaguzi.
Hata hivyo, kumekuwapona matukio ya fujo ambayo yanahusishwa na Renamo yaliyofanyika Februari 24 mwaka huu.
“Hii inatia shaka kama Renamo iliyoko Maputo na Renamo iliyoko msituni ni kitu kimoja au chama hicho kina matawi mawili kila tawi likiwa na maslahi yake,”anasema  Weimer.
Filipe Jacinto Nyussi alizaliwa miaka 55 iliyopita (Februari 9, 1959) Namau, Wilaya ya Mueda, Jimbo la Cabo Delgado. Ni Mmakonde kama walivyo wengi wa wakazi wa Jimbo hilo. Ni mhandisi makanika aliyesomea taaluma hiyo nchini Czechoslovakia, na amepata pia kusomea utawala Chuo Kikuu cha Manchester, Uingereza. Amepata mafunzo mbalimbali ya utawala nchini India, Afrika Kusini, Swaziland na Marekani.
Kabla ya kuteuliwa kuwa waziri na Rais Guebuza, Machi 27, 2008, alikuwa akifanya kazi katika shirika la Bandari na Reli alikofikia nafasi ya kuwa Mtendaji Mkuu mwaka 1995 na hatimaye kuingia katika Bodi ya shirika mwaka 2007.
Kati ya mwaka 1993 na 2002 alikuwa rais wa Klabu ya Soka ya Ferroviario ya Nampula (Clube Ferroviário de Nampula),  klabu ya daraja la kwanza iliyoko Nampula. Yeye ni mhadhiri pia wa chuo kikuu.
Kuingia kwake Wizara ya Ulinzi kulimwondoa  aliyekuwa waziri Tobias Joaquim Dai ambaye taarifa zimekuwa zikiashiria kwamba aliondolewa kama alama ya kuwajibishwa kutokana na tukio la mlipuko katika ghala la silala la Malhazine mjini Maputo, ulioua watu zaidi ya 100 na kuharibu makazi 14,000.
Uchunguzi wa serikali wa chazo cha ajali hiyo ulisema kulikuwa na uzembe huku Dai akishutumiwa kwamba hakuchukua hatua za haraka kuepusha maafa hayo.
Septemba 2012 Nyussi alichaguliwa kuingia kwenye Kamati Kuu ya Frelimo, wakati wa kikao cha 10 cha Kongresi ya chama hicho.
Alitangazwa Machi 1, 2014 kuwa mgombea wa Frelimo baada ya ushindi katika kura ambazo katika raundi ya kwanza hazikutoa mshindi akiwa amepata asilimia 46, nyingi kwa mbali, kuliko mshindi wa pili Diogo, lakini ambazo zilikuwa chini ya nusu ya idadi inayotakiwa mshindi apate.
Alimshinda Diogo kwa asilimia 68 kwa 31 katika raundi ya pili baada ya kuwa wamebaki wagombea wawili.
 src
raia mwema