Wiki iliyopita niliandika katika safu hii jinsi Tanzania kama nchi nyingine za Afrika zilivyoingia mkenge katika sekta ya madini na kuishia kupoteza rasilimali hiyo kwa kile kinachoitwa uwekezaji.
Leo nitaendeleza hoja ile kwa kufafanua zaidi hali ilivyokuwa.
Kwanza ieleweke kuwa, sababu kubwa iliyowafanya wakoloni kuja Afrika kutawala, ilikuwa ni kutafuta malighafi za viwanda vyao na masoko ya bidhaa zao.
Hadi mwishoni mwa miaka 1950 na mwanzoni mwa 1960, nchi nyingi zikapata uhuru dhidi ya wakoloni.
Baada ya uhuru huo, ambao kimsingi uliridhiwa na Umoja wa Mataifa, iliamriwa kuwa kila nchi iliyo huru iwe na mamlaka na rasilimali zake. Hata hivyo, huo haukuwa mwisho wa unyonyaji wa kikoloni.
Ikumbukwe pia kwamba, tangu mwaka 1942 hadi 1945, nchi ya Uingereza iliyokuwa ikitawala dunia wakati huo, ilikuwa hoi kiuchumi kutoka na Vita Kuu ya Pili ya dunia
Vita hiyo iliyoanza mwaka 1939, ilihusisha Uingereza ikisaidiana na Ufaransa pamoja na makoloni ya Uongereza dhidi ya Ujerumani iliyokuwa ikiungwa mkono na Italia na Urusi.
Kwa upande mwingine, Japan nayo iliyokuwa ikipambana na China, ilishambulia pia upande wa Uingereza na Marekani.
Baada ya vita hiyo, Uingereza ilijikuta ikiwa hoi kiuchumi. Lakini kwa upande mwingine Marekani ambayo haikuathirika na vita hivyo, ndiyo ilikuwa inakuja juu zaidi kiuchumi.
Kwa hali hiyo, iliungana na Uingereza ili kutafuta suluhu ya kiuchumi kwa mataifa ya Ulaya, ikiwemo Uingereza.
Suluhu hiyo ilikuwa ni kuanzisha taasisi za kifedha, ambazo ni Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na baadaye Benki ya Dunia (WB). Kazi ya taasisi hizo hadi leo ni kutafuta na kuinua uchumi wa Marekani na mataifa ya Ulaya.
Kazi ya kwanza ya Benki ya Dunia ilikuwa ni kutumia mtaji wake kuyakopesha mataifa ya Ulaya ili yaimarishe uchumi wake. Lakini kwa kadiri siku zilivyokuwa zikienda waliona wazikopeshe hata nchi masikini, hasa za Afrika hata kama hazina uwezo wa kulipa. Mikopo hiyo imegeuka kuwa chambo cha kuchota rasilimali za Afrika.
Kazi nyingine ya benki hiyo ni kufanya tafiti na kutoa ushauri wa uchumi kwa dunia nzima. Lengo ni kujenga mfumo wa kuchota utajiri wa rasilimali huku ikiziacha nchi masikini zikiwa tegemezi.
Wakati huo, nchi nyingi za Afrika zilishaanza kudorora kiuchumi, licha ya kutaifisha rasilimali zilizokuwa mikononi mwa wakoloni, huku zikikabiliwa na madeni makubwa.
Ili kuyapata madini ya Afrika, Benki ya Dunia ilikuja na mkakati wa kuzikwamua kiuchumi.
Kwa mfano, mwaka 1992, Benki ya Dunia ilichapisha mkakati wa madini ya Afrika. Mkakati huo ulikuwa na lengo la kubinafsisha sekta ya madini.
Benki hiyo ilijiridhisha kuwa madini yaliyopo Afrika yalikuwa ndiyo suluhisho la uchumi wa nchi za Ulaya na Marekani kwa kushikilia asilimia nane ya madini yote ya dunia.
Hivyo ilizishauri nchi za Afrika kubinafsisha madini yake kwa sekta binafsi eti kwa sababu Serikali zimeshindwa kuyachimba
Ilishauri pia kufanyika kwa mabadiliko ya kimfumo ikiwa pamoja na ubinafsishaji na uwekezaji. Kwamba Serikali isihodhi njia kuu za uchumi, bali iziachie kampuni za kigeni zije kuwekeza.
Huo ndiyo ukawa mwanzo wa ukoloni mwingine kwa rasilimali za Afrika. Nchi za Afrika zenye utajiri wa mafuta, madini na gesi zimejikuta kwenye mzigo wa madeni ya Benki ya Dunia, huku rasilimali zake zikichotwa na kampuni za Ulaya na Marekani.
Mwaka 1996 IMF, lilianzisha mkakati wa kuzipunguzia madeni nchi za Afrika, baada ya kuombwa na nchi hizo na mashirika ya kiraia.
Yaani nchi hizo ziliiomba IMF kuziweka katika kundi la nchi masikini zaidi duniani ili zisamehewe madeni.
Nchi hizo ni pamoja na Nigeria, Sierra Leone, Gabon, Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, Liberia, Senegal, Guinea Bissau, Guinea, Burkina Faso, Burundi, Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Jamhuri ya Congo, Comoro na Ivory Coast.
Nyingine ni Ethiopia, Gambia, Ghana, Madagascar, Mali, Msumbiji, Niger, Rwanda, Senegal, Tanzania, Togo na Uganda.
Nchi hizo ambazo zina utajiri mkubwa wa madini, mafuta, gesi na maliasili nyinginezo zimeshajiingiza kwenye mtego wa Benki ya Dunia na IMF.
Kampuni za kigeni zilizoingizwa kwa baraka za taasisi hizo, zinajichotea rasilimali zinavyotaka kwa mikataba ya kilaghai. Zinaweza kugurukuta wakati zinadaiwa?
0754 897 287
src
mwananchi
src
mwananchi