BUNGE Maalum la Katiba ni chombo pekee chenye idadi kubwa ya wanawake waliopo kwenye nafasi ya juu ya kutoa maamuzi mazito kwa mustakabali wa Taifa.
Pamoja na wingi wa wanawake hao, hadi sasa wanaume wanaongoza kwa kuwasha vipaza sauti na kutoa maoni huku wengine wakitumia nafasi hiyo vibaya kwa lengo la kukwamisha kwa makusudi au kuchelewesha kazi za bunge hilo.
Wananchi wanashangazwa na ukimya wa wanawake waliobahatika kuingia kwenye Bunge hilo la kihistoria.
Uzoefu unaonesha kuwa wanaharakati hao wangekuwa nje ya Bunge wangekuwa wameshatoa tamko kulaani upotevu wa muda unaopotea katika malumbano yasio na tija kwa Taifa wakati gharama za Bunge hilo zinatokana na fedha za walipa kodi.
Huenda wanaharakati hao wamepitiwa na usingizi mzito wakati wakisoma mazingira ya Bunge. Hivyo tunaamini watazinduka na kuchangia mijadala ya Bunge hilo Maalum la Katiba ili kuhakikisha Katiba ijayo itakuwa na mashiko kwa ustawi waTaifa, kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni.
Wanawake waliopo Bunge Maalum la Katiba wanapaswa kuhakikisha Katiba itanufaisha watu wote ili kujenga Taifa imara. Wanawake Bunge la Katiba wasiogope wala kusita kuunga mkono maoni mazuri yenye manufaa kwaTaifa kutokana na hofu kwamba wakifanya hivyo watakuwa wameunga mkono kundi au chama fulani.
Watanzania wanataka Katiba yenye mfumo wa siasa utakaoboresha demokrasia ili viongozi waweze kuwajibika au kuwajibishwa kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Tunahitaji Katiba itakayokuwa mhimili madhubuti katika vyombo vya kusimamia haki na sheria sio Katiba itakayotoa mwanya wa kusambaratisha umoja wetu na kutoa fursa kwa vibaraka au wenye uchu wa madaraka kupenyeza maslahi yao binafsi.
Katiba mpya inapaswa kupunguza bajeti ya kugharimia shughuli za utawala na kuongeza bajeti ya uzalishaji mali.
src
Habari Leo