London, England
Fainali za Kombe la Dunia 2014 zitaanza Juni 12 hadi Julai 13 huko Brazil.
Hivi sasa zimebaki siku 73 kabla ya fainali hizo kuanza, ambapo ukibaki mwezi mmoja kabla ya kuanza.
Mtandao wa Goal.Com umezifuatilia timu zote zilizofuzu kushiriki Fainali za Kombe la Dunia 2014, umeangalia vikosi vyao na kuona udhaifu na wasiwasi wa kila kikosi. Udhaifu na wasiwasi huo ni kama ifuatavyo:
Algeria: Inakosa wachezaji wazoefu
Algeria ni timu inayoonyesha matumaini makubwa, lakini kitendo cha wachezaji wake wengi kukosa uzoefu kinaweza kuwasababishia kutolewa mapema katika fainali za dunia.
Argentina: Mabeki
Hakuna wakati, ambapo kikosi cha timu ya taifa ya Argentina kimehangaika kuwa na washambuliaji wenye kiwango cha juu, lakini mara nyingi kimekuwa kikikosa mabeki wa kiwango cha juu, hali hiyo imetokea tena mwaka huu.
Australia: Matatizo mengi
Kikosi cha Australia kina matatizo mengi. Katika safu ya ulinzi Australia haijaimarika vya kutosha, pia safu yao ya ushambuliaji inaongozwa na Tim Cahill na Joshua Kennedy ambao hawachezi katika ligi zenye ushindani mkubwa.
Ubelgiji: Beki za pembeni
Ubelgiji ina wachezaji wenye ubora katika kila nafasi, lakini wanakosa mabeki mahiri wa pembeni na kuna uwezekano mkubwa wakachezesha mabeki wanne wa kati katika Fainali za Dunia 2014.
Ubelgiji ina mabeki wa kati mahiri kama Thomas Vermaelen, Toby Alderweireld, Vincent Kompany, Daniel van Buyten na Jan Vertonghen.
Bosnia & Herzegovina: Mabeki
Inashiriki Fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza. Ina washambuliaji mahiri, viungo bora na kipa mwenye ubora. Hata hivyo ni dhaifu katika safu ya ulinzi.
Brazil: Ubunifu kutoka kiungo cha chini
Brazil huwa inapenda kutumia mfumo wa 4-2-3-1 ambao huwasaidia katika kushambulia. Hata hivyo Brazil inaonekana ina tatizo la ubunifu kwa viungo wake wa chini kwani huwa wanakosa ubunifu wa haraka wa kupeleka mipira kwa washambuliaji.
Cameroon: Safu ya ushambuliaji
Wachezaji wa Cameroon wana maumbo makubwa, wanatumia nguvu na kasi, lakini safu yao ya ushambuliaji haina makali ya kuzipita ngome za timu bora, inamtegemea zaidi Samuel Eto’o huku ikiwa haina mbadala wake.
Chile: Beki wa kati
Kocha wa Chile, Jorge Sampaoli amefanya kazi kubwa kuhakikisha anapata beki muhimu wa kati, ambapo amemchukua kiungo mkabaji wa timu hiyo, Gary Medel na kumkabidhi nafasi hiyo ya beki wa kati huku akishirikiana na Marco Gonzalez.
Colombia: Mabeki
Ukiangalia vizuri zaidi taarifa hizi za udhaifu na wasiwasi wa vikosi vitakavyoshiriki Fainali za Kombe la Dunia mwaka huu utaona timu za Amerika ya Kusini zina tatizo la safu ya ulinzi. Colombia nayo ina tatizo la safu ya ulinzi.
Costa Rica: Uwezo wa kumiliki mpira
Costa Rica inafahamika kwa kutengeneza ukuta imara, lakini tatizo kubwa la timu hii ni kushindwa kumiliki mpira kwa sababu ya aina ya mchezo wa kujilinda sana wanaoucheza.
Croatia: Siyo wazuri katika winga
Croatia ina wachezaji wenye ubora wa juu kama Mario Mandzukic, lakini wanakosa mawinga bora. Croatia ina mabeki wazuri wa pembeni na ukuta imara, lakini huku ikitegemea zaidi nyota wake wa kati Luka Modric na Ivan Rakitic.
Ecuador: Haina mpango B
Ecuador ni timu ambayo inataka kushambulia muda wote, ikikutana na timu ambayo inaweza kutuliza kasi yao inakosa mpango B na hivyo kujikuta ikihangaika.
England: Kumiliki mpira
Soka la kimataifa linataka uwezo mkubwa wa kumiliki mpira. Lakini timu ya England siyo nzuri katika kumiliki mipira kwani mchezo wao ni pasi ndefu na kasi.
Ufaransa: Washambuliaji
Ufaransa ina washambuliaji Karim Benzema, Olivier Giroud, Loic Remy na wengine wengi. Lakini ukweli ni kwamba washambuliaji wa Ufaransa hufanya vizuri katika klabu zao kuliko kwenye timu ya taifa. Wakati wa mechi za kufuzu Benzema hakufunga bao, winga Franck Ribery alifunga mabao matano.
Ujerumani: Safu ya ulinzi
Ujerumani imejiimarisha katika safu ya kiungo na ushambuliaji, lakini ina tatizo kubwa katika safu ya ulinzi kwani beki wanayemtegemea Mats Hummels amekuwa akipata majeraha mara kwa mara
Ghana: Ina upungufu kila idara isipokuwa kwenye kiungo
Ghana ina uwezo wa kuchezesha wachezaji 11, lakini wote ni wachezaji wa nafasi ya kiungo, wana wachezaji wengi wa kiungo wenye ubora wa juu, hata hivyo wana mapungufu ya uzoefu katika nafasi nyingine.
Ugiriki: Ushambuliaji
Wakati wa kuwania tiketi ya kufuzu kushiriki Fainali za Kombe la Dunia 2014, Ugiriki ilikubali kufungwa bao nne tu. Msingi wa Ugiriki ni ukuta na kumiliki mipra, lakini katika ushambuliaji inamtegemea Kostas Mitroglou tu.
Honduras: Haina nyota
Honduras ni taifa dogo, kwa kupata nafasi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia 2014 ni mafanikio makubwa sana.
Iran: Hawana stamina
Iran ina wachezaji wazuri katika safu ya ushambuliaji, lakini tatizo ni wachezaji wa Iran wanaonekana hawana stamina ya kutosha.
Italia: Inahofia majeruhi
Hali ya kukosa wachezaji wanaotakiwa kuunda kikosi cha kwanza cha timu ya Italia kwa sababu ya kuwa majeruhi ndiyo inayowaumiza.
Ivory Coast: Haina bahati
Kikosi cha Ivory Coast kinaundwa na wachezaji wengi mahiri ambao Yaya Toure, Didier Drogba, Kolo Toure, Salomon Kalou, Gervinho na wengine wengi ambao wanaweza kuwafikisha hata zaidi ya hatua ya robo fainali ila hakina bahati.
Japan: Mabeki wa kati
Kiufundi Japan ina wachezaji wengi mahiri wa kiungo, lakini ina tatizo kubwa katika safu ya ulinzi.
Mexico: Mabeki wa kati
Kocha Pablo Herrera anayeinoa Mexico ana matumaini ya kutwaa ubingwa, lakini anajua anatakiwa kuhakikisha mabeki wake wa kati wanafanya kazi yao kwa ubora wa juu.
Uholanzi: Uwezo wa kuitekeleza falsafa yao
Wachezaji wengi wa Uholanzi wapo imara katika kila idara, lakini tatizo ni falsafa ya kocha Louis van Gaal anayotaka kuitumia.
Kocha huyo anapenda mashambulizi ya timu yaanzie kupangwa nyuma.
Nigeria: Haijiamini
Kocha Stephen Keshi ana mzigo mkubwa wa kuiongoza Nigeria. Keshi amejikuta akishindwa kuelewana na mabosi wake wa Shirikisho la Soka la Nigeria (NFF) kwani amekuwa akiwaita wachezaji chipukizi na kuwaacha wakongwe, uamuzi wake huo ulimuwezesha kutwaa ubingwa wa Afrika 2013.
Ureno: Viungo wakabaji
Ukiangalia juu juu unaweza ukasema ukuta wa Ureno unaoundwa na Pepe pamoja na Bruno Alves ni imara, lakini tatizo la ukuta huu lipo kwa viungo wakabaji wake William Carvalho na Miguel Veloso.
Russia:Kucheza chini ya kiwango
Ni wazi Russia ina wachezaji wengi wazuri, lakini hii siyo mara ya kwanza kuwa na wachezaji wazuri ila tatizo la Russia ni mara kwa mara kucheza chini ya kiwango kwenye mashindano makubwa
Korea Kusini: Washambuliaji
Korea Kusini inacheza vizuri kuanzia nyuma mpaka katikati ya uwanja, lakini huwa washambuliaji wake wana tatizo la kuitumia vizuri mipira ya mwisho.
Hispania: Wasiwasi
Kuna wakati mfumo wa tiki-taka ulionekana kuinufaisha klabu ya Barcelona na timu ya taifa ya Hispania. Lakini baada ya Barcelona kufungwa 7-0 na Bayern Munich katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, pia baada ya Hispania kushindwa kuzitambia Italia na Brazil katika mechi za kombe la mabara, mfumo huo wa tiki-taka umeonekana siyo hatari tena.
Switzerland: Udhaifu wa kufunga
Switzerland ilimaliza mechi za kufuzu Fainali za Dunia 2014 huku beki wake wa kati Fabian Schar akiwa mfungaji bora wa timu, hili ni tatizo. Switzerland ipo vizuri katika safu ya ulinzi na kiungo, lakini ina tatizo katika ushambuliaji.
Uruguay: Mabeki wa pembeni
Kikosi cha Uruguay ni kati ya vikosi vinavyotarajiwa kufanya vizuri katika fainali hizi za kombe la dunia kwani kina washambuliaji bora, viungo wazuri, mabeki wa kati wa kiwango cha juu, lakini wana tatizo la mabeki wa pembeni.
Marekani:Mabao mepesi
Marekani ina wachezaji wengi wenye vipaji, lakini wana tatizo katika safu ya ulinzi. Kikosi cha Marekani kilikuwa kikikubali kufungwa mabao mepesi katika mechi za kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2014.
src
mwananchi
src
mwananchi