Saturday, March 1, 2014

Dodoma ni usanii na utalii tu !!!

Februari 18 mwaka huu  Bunge Maalumu la Katiba lilianza mjini Dodoma, likiwa na kazi kubwa ya kuipitia Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa lengo la kuiboresha na kuipitisha, kabla wananchi hawajaipigia kura kuikubali au kuikataa.

Bunge hilo linaundwa na Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar na wajumbe 201 wa kuteuliwa na kufanya idadi yao kufikia 629.

Kwa muda wa siku 13 tangu kuanza kwa Bunge hilo kazi kubwa ilikuwa ni kuandaa na kujadili rasimu ya kanuni. Kanuni hizo ndizo ambazo zitatumika kuliendesha Bunge hilo.

Mimi ni miongoni mwa wananchi wanaofuatilia vikao vya Bunge hilo kwa makini, lakini tabia na kauli zinazotolewa na baadhi ya wajumbe wake zinaonyesha jinsi walivyo wabinafsi.

Siku ambayo Rais Jakaya Kikwete alitangaza majina ya wajumbe 201, wapo wananchi walioponda uteuzi huo, lakini binafsi nilijua kipimo cha walioteuliwa kwa Watanzania ni hoja watakazokuwa wakitoa katika vikao vya bunge hilo.
Nilijua wazi kuwa hata wale wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wale wa Baraza la Wawakilishi, wataweka uzalendo mbele na kuacha masilahi ya vyama wanavyotoka.

Lakini imekuwa tofauti. Baadhi ya wajumbe hao wamedhihirisha kuwa wapo mjini Dodoma kwa ajili ya kulamba posho na kutetea masilahi ya vyama vyao vya siasa.

Wengi wamesahau kuwa wamechaguliwa na kuteuliwa kwa ajili ya kuwawakilisha Watanzania milioni 43 ndani ya Bunge hilo.

Baadhi yao badala ya kujadili masuala ya msingi wamekomalia nyongeza ya posho kwa madai kuwa wanayolipwa sasa ya Sh300,000 kwa siku, ni kiduchu na haitoshi kwa sababu gharama za maisha mjini Dodoma zimepanda.

Wanapendekeza kulipwa Sh500,000

Lakini nyumba za kulala wageni hapa Dodoma zinapangishwa kwa kati ya Sh20,000 hadi 80,000, chakula cha kawaida Sh6,000, kukodi teksi ni kati ya Sh3,000 hadi 6,000 sasa nyongeza hiyo ya posho ni kwa ajili ya nini?

Wapo waliokuja na familia zao, ndugu na jamaa, madereva na mambo chungu mzima. Huo msafara wa kazi gani?
Katika uchangiaji wa  masuala mbalimbali baadhi ya wajumbe hao wamekosa aibu kabisa. Wamediriki kuwasha vipaza sauti tena wakati wenzao au mwenyekiti wa muda wa Bunge hilo, Ameir Panju Kificho  akizungumza,  na kupaza sauti wakitaka kupewa karatasi za kusaini ili kulipwa posho. Hicho ndicho kilichowapeleka Dodoma kweli?

Wajumbe hawa wamesahau kabisa kuwa Bunge hilo ni la kihistoria na nchi yetu haijawahi kuwa na bunge kama hili tangu tupate uhuru 1961.

Ukiacha wapenda posho, wapo wanaoibuka asubuhi na kusaini kisha kuingia mtaani na kuwaona tena ni mpaka mchana au jioni.  Hawana habari kabisa na kinachoendelea wao kikubwa ni posho tu.

Wengine walionyeshana ubabe kuhusu suala la kura za siri au za wazi wakati wa kupiga kura kupitisha Rasimu ya Katiba.

 Najua kuwa kila chama kina msimamo wake, lakini pamoja na msimamo huo ni lazima kutakuwa na wanachama wanaokwenda kinyume na jambo hilo.

Nchi yetu imekuwa muumini wa kupiga kura ya siri ambayo hupigwa siyo tu katika uchaguzi mkuu bali katika masuala mbalimbali ya kupitisha hoja fulani.
Cha kushangaza baadhi ya wajumbe ambao ni wanachama na wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walikuwa wakilazimisha upigaji wa  kura ya wazi, kwa maana ya kila mtu kusimama na kusema anampigia kura nani kati ya waliojitokeza kugombea.

Katika hili ni mjumbe gani kutoka chama hicho atayekubali kupiga kura ya wazi na kupingana na maelezo au msimamo wa chama chake.

Kama ikiwa ni kura ya siri wajumbe hao wanaweza kwenda kinyume na chama chao na hakuna wa kuwahukumu.

Sijui wanahofia nini kwa sababu hata Chadema au makundi mengine ndani ya Bunge hilo yana wajumbe  wanaounga mkono muundo wa Serikali tatu, wapo baadhi wanaopingana na mfumo huo. Inakuwaje makundi hayo yanakuwa kimya lakini CCM wanashupalia kura ya wazi, kuna jambo hapo!

Suala la kura ya wazi linashinikizwa lipite ili litumike hadi wakati wa kupitisha rasimu hiyo baada ya kujadiliwa na kuboreshwa.

Hilo likifanikiwa maana yake ni kwamba hata kama rasimu hiyo itakuwa imechakachuliwa itapita tu
Nasema hivyo kwa sababu mjumbe yeyote wa CCM atakayepinga katika zoezi la upigaji kura wa wazi mwaka 2015 atapigwa chini kugombea ubunge na wale wanaojipambanua kuutaka urais ndiyo kabisa watakuwa wamejitoa wenyewe.

Wengine wamekuwa vinara kwa kutengeneza mazingira ya kugombea uenyekiti wa kudumu wa Bunge hilo, huku kundi kubwa likiwa nyuma yao kuwaunga mkono. Makundi ya wanaoutaka urais 2015 nayo hayako nyuma.

Sioni mantiki ya wajumbe hawa kukomalia mambo hayo niliyoyaeleza hapo juu, kikubwa ni kujikita katika hoja za msingi na kuhakikisha kuwa inapatikana Katiba ya wananchi na siyo ya kundi fulani la Watanzania.
                           
   src-mwananchi