Ushirikina’ unavyoenda sambamba na usasa China
Toleo la 339
19 Feb 2014
KAMA ningetoka kwenye familia ya Kichina, matambiko yangepaswa kufanyika ili kumuondolea nuksi mwanangu wa kwanza, Moukhtar, aliyezaliwa mwaka wa 2010, ambao kwa kichina unaitwa ni mwaka wa nyota Chui (Tiger).
Hapana, nimekosea. Huenda Mou, hata asingezaliwa maana wazazi wangenishauri kuwa ule si mwaka mzuri wa kuzaa mtoto, atakuja na balaa. Na ningesikiliza kwa sababu Wachina kwa asili ni wahafidhina wa kitamaduni na wazazi bado wanasikilizwa sana.
Watu waliozaliwa miaka ya Chui, ikiwemo 1938, 1950, 1962, 1974, 1986, 1998 au 2010 wanahofiwa kuwa wakatili, wagomvi na hupenda kuhoji utawala, na hivyo basi huweza kusababisha madhara kwake mwenyewe, kwa familia au mwajiri wake.
Watu hawa huwekwa mbali katika sherehe za harusi, hususan chumba cha bi harusi kwa hofu ya kuleta nuksi. Hofu dhidi ya waliozaliwa miaka ya chui haiishii katika familia, waajiri huangalia nyota ya muomba kazi na kuepuka kuajiri Chui kwa madai kuwa ni mtu mgumu kufanya naye kazi.
Inaaminika katika jamii ya Wachina kuwa mtoto aliyezaliwa mwaka wa Chui atapitia shida nyingi katika maisha yake kuliko wengine. Akiwa wa kike, ni mbaya zaidi kwani Chui wa kike hadhibitiki, ana hasira na hivyo ni nuksi kwa familia!
Kwa sababu hizo baadhi ya watu huepuka kuzaaa kipindi cha miaka ya Chui. Mwaka 2010, mwaka wa Chui aliozaliwa mwanangu Moukhtar, idadi ya watoto waliozaliwa Taiwan ambayo kiutamaduni ni sawa na China ilipungua kwa idadi ya watoto 20,000 ukilinganisha na mwaka uliotangulia. Idadi ya watoto waliozaliwa ilipungua pia China, Hongkong na nchi nyingine kama Singapore yenye wahamiaji wengi kutoka China.
Kauthar mwanangu wa pili na wa mwisho, yeye katika muktadha wa familia ya Kichina angependwa sana maana amezaliwa mwaka wa Dragon, ambao Wachina wanaamini huzaliwa watu wenye bahati, uaminifu, ujasiri, utajiri, mafanikio na vipawa tele.
Miongoni mwa wanyama 12 wanaowakilisha miaka ya Kichina, Dragon (aliye nafasi ya tano), ni mnyama pekee wa ajabu, asiyefanana na wanyama wa kawaida. Wanyama wengine 11 ni halisi wanaojulikana: panya (1), ng'ombe (2), chui (3), sungura (4), nyoka (6), farasi (7), kondoo (8), tumbili (9), kuku (10), mbwa (11) na nguruwe (12).
Dragon, kwa mujibu wa Wachina, anaweza kuogelea na kupaa, na hivyo anamaanisha maisha bila vikwazo na ni alama ya ukuu na akili. Katika China ya kale, mnyama huyu alihusishwa na mfalme. Mwaka 2000 ulikuwa wa Dragon ambapo China, Hong Kong, Taiwan kote kulikuwa na ongezeko la vizazi kwa asilimia tano.
Miaka ya Dragon ni pamoja na 1928, 1940, 1952, 1964, 1976, 1988, 2000, 2012. Baadhi ya watu maarufu waliozaliwa miaka ya Dragon ni pamoja na John Lennon (1940) mwimbaji mtunzi, mwimbaji nguli na muasisi wa kundi la The Beatles; mwanamapinduzi mzaliwa wa Argentine, Che Guevara (1928); Vladimir Putin (1952) Rais wa Urusi; Gordie Howe (1928) mmoja wa wachezaji wakubwa wa mpira wa Magongo wa zama zote.
Katika orodha hiyo wapo pia muigizaji mahiri, Russell Crowe (1964) wa Hollywood na Martin Luther King Jr. (1929) mshindi wa tuzo ya Nobel aliyeongoza harakati za kupigania haki za Weusi huko Marekani, Bruce Lee (1940) muigiaji maarufu wa filamu duniani na Deng Xiaoping (1904) kiongozi Mkuu wa China 1978 mpaka 1992 anayekumbukwa zaidi kwa kusimamia mageuzi ya nchi hiyo.
Wengine ni pamoja na Maggie Cheung (1964) ambaye ni mrembo na muigizaji mahiri mzaliwa wa Hong Kong ambaye anashikilia rekodi ya kuwa muigizaji wa kwanza kutoka Bara la Asia kushinda tuzo maarufu za filamu za Cannes Film Festival baada ya kucheza filamu ya ‘Clean (2004)’ na Waziri Mkuu wa Singapore Lee Hsien Loong: (1952) tangu 2004 ambaye pia ni mtoto mkubwa wa kiongozi muasisi wa nchi hiyo Lee Kuan Yew. Loong ana shahada ya hesabu ya daraja la kwanza kutoka Chuo Kikuu cha Cambridge.
Kwa kuwa bahati ya mtoto haiendani tu na mwaka anaozaliwa, bali hata siku na saa, inaarifiwa kuwa wapo wazazi wanaoamua kuzaa kwa operesheni ili mtoto aje siku na saa wanayoitaka!
Kadhalika, kwa imani kuwa nyota za wazazi pia huchangia bahati ya mtoto, wazazi huwauliza watabiri, kutokana na nyota za wawili hao (mume na mke), je, ni mujarabu kupata mtoto mwaka huo. Ikiwa jibu ni hapana wazazi huahirisha kutafuta mtoto.
Mwaka mpya wa Kichina ulioanza Januari 31, 2014 ni mwaka wa farasi, utafuatiwa na mwaka wa kondoo, kisha mwaka wa tumbili, kuku, mbwa, nguruwe, panya, ng’ombe, chui, sungura, dragon – mzunguko huendelea hivyo.
Kwa mara ya kwanza, mwaka huu nimeshuhudia sherehe za mwaka mpya wa Kichina nikiwa hapa Shanghai. Sherehe za mwaka mpya ni sherehe muhimu zaidi katika taifa hili. Kwa kawaida mwaka mpya wa Kichina huingia kipindi cha mwishoni mwa Januari au mwanzoni mwa Februari na kusherehekewa kwa siku 15 na kukutana na sikukuu nyingine ijulikanayo kama Sikukuu ya Mwanga.
Katika kipindi cha sherehe za mwaka mpya ofisi na biashara hufungwa na watu wengi hurudi makwao walikotokea kuungana na familia. Ukipanda treni au mabasi na kadhalika ukitembea mjini unaona kabisa kumepwaya.
Wachina wanapenda sana kupiga baruti kuadhimisha sherehe yoyote, hata ikiwa ya kifamilia, lakini siku za sherehe ya mwaka mpya mgonjwa wa moyo hawezi kuhimili kelele za baruti.
Katika kuadhimisha, watu wazima pia huwapa watoto zawadi ya fedha katika bahasha nyekundu, kuashiria kufukuza ubaya na kuleta bahati. Kadhalika, alama ya bahati ijulikanayo kama ‘fu’ huning’inizwa mlango mkubwa wa nyumba ili kuvuta bahati. Vilevile, kabla ya siku yenyewe ya mwaka mpya nyumba hupamba kiubunifu kwa kutumia vipande vya karatasi vyekundu vilivyoandikwa maombi yao katika mwaka mpya.
Ukiacha katika sherehe za mwaka mpya, Wachina wana vipengele vingine vingi vya imani za kishirikina, kama sehemu ya utamaduni wao.
Kuna namba za bahati, mfano Na. 8 na za balaa mfano Na 4. Nyumba zenye namba za balaa huepukwa, kadhalika, desturi hizo hutumika katika kuchagua namba za gari au simu. Kuna usomaji wa alama za uso na mikono ambapo madaktari wa kisasa wa Kichina hutumia elimu hii kuwasaidia kujua tabia za wagonjwa wao.
Kadhalika, kuna vijiimani vya kawaida kama usijenge nyumba kuelekea kaskazini utapata balaa, usifagie siku ya mwaka mpya utafukuza baraka, haifai kuoa mtu aliyekuzidi au uliyemzidi miaka 3 au 6, ukila tambi usiikate kwani huongeza umri, mbwa akilia muda mrefu usiku kuna mtu kafa au ukimpiga mtu na fagio unapata balaa.
Kwa imani hizi za kishirikina (kwa maana hazijathibitika kisayansi) jamii ya Wachina inakuwa jamii ya aina ya pekee iliyoweza kuchanganya usasa, unaotokana na mendeleo ya sayansi na maendeleo kwa upande mmoja na utamaduni kwa upande mwingine, tena kwa ufanisi mkubwa.
Katika Afrika yetu mara nyingi utamaduni umeonekana kuwa ni kikwazo cha usasa na maendeleo. Karibuni nilikutana na rafiki yangu mmoja Mzambia, tulijadili sana kuhusu hali ya Afrika na jinsi tunavyoshindwa kujikwamua kutoka katika lindi la umaskini, ujinga na maradhi. Ndugu huyu wa Kizambia anaamini kuwa utamaduni wetu kwa kiasi kikubwa ni kikwazo cha maendeleo.
Huenda kuna ukweli katika hili. Lakini tusisahau mchango wa uongozi wa taifa la China, chini ya uongozi wa Chama cha Kikomunisti cha nchi hiyo katika kuweka sera sahihi na nidhamu katika uendeshaji wa nchi, jambo ambalo Waafrika tumeshindwa.
Nikirudi kwa Chui na Dragon, kwa mwanangu Moukhtar, na wengine waliozaliwa mwaka wa Chui wasikate tamaa. Maana ni hao hao watabiri wa Kichina wanaotuambia kuwa waliozaliwa miaka ya Chui huwa waandishi wazuri, wanamuziki mahiri, waigizaji matata, wajasiriamali wenye mafanikio na wanasiasa machachari.
Zaidi ya hayo, unajua nini? Taiwan nchi ambayo wazazi walikimbia kuzaa mwaka wa chui 2010, mwaka wa mwanangu Moukhtar, mwaka huohuo 2010 ilikuwa ikitawaliwa na rais na makamu wa rais waliozaliwa mwaka wa Chui.
Rais, Ma Ying-jeou, aliyetawala nchi hiyo tangu mwaka 2008 yungali madarakani. Makamu wake wa rais, Chui mwenzake, aliyeanza naye awamu ya kwanza Vincent Siew alistaafu mwaka 2012. Wawili hao walifanya kazi nzuri kabisa jambo linalothibitisha kuwa hizi ni imani tu zisizo na mashiko yoyote