
Dismas Lyassa
Maisha yako yakoje? Jibu unalo mwenyewe, lakini ukweli ni kwamba kuna idadi kubwa ya watu wana maisha magumu.
Wapo waliokwenda vyuoni wakifikiri kwamba baada ya kupata ‘digrii’ yake maisha yangeweza kwenda safi, wapi bwana mambo kwa baadhi yao yamezidi kwenda kombo.
Wapo ambao kabla ya kuwa na ‘diploma’ walifikiri kwamba baada ya kuwa na elimu hiyo maisha yangeanza kuonyesha mwanga, wanashindwa kuelewa kwamba wapo watu wana digrii ya pili na mambo ni mazito.
Maisha yamejaa changamoto, wapo wengine angalau kwenye suala la uchumi wako vizuri, lakini wanapigwa na mapenzi, mtu ana gari, nyumba nzuri na kadhalika, hana amani kwa sababu tu mwenzi wake hampi amani.
Wengine wana fedha, afya ni mbaya kabisa, anaishi kwa kuzingatia masharti ya daktari, akikosea kidogo, daktari kamwambia kwamba anaweza kufa.
Kuna wanandoa, wao wenyewe wanaelewana, lakini kuna bundi limetoka nje linawavuruga, anaweza kuwa ni ndugu au hata mzazi. Je, wakati mnakutana hao ambao leo mnawapa nafasi walikuwepo?
Ni swali la msingi ambalo kila mwenye akili timamu anapaswa kulizingatia. Ni vizuri mnapokuwa kwenye uhusiano kufanya kila mnaloweza kuhakikisha uhusiano wenu unaendelea kuwa imara, si vizuri hata kidogo kuachana.
Ambao wanapaswa kuachana ni wachumba, kwamba kama watu bado hawajaoana, tayari kuna migogoro imeanza kuingia au tayari mmoja ameshaanza kuwa na uhusiano na wanawake au wanaume wengine au hata kuzaa, ni dalili kwamba akili yako haiko sawa kama utakubali kuendelea kuwa na mtu huyo.
Kuna wanawake wanakosea sana...mtu mzima lakini hana akili analazimisha mambo, mwanamme hajakutolea mahari, wewe unajipeleka kwake kuishi au kubeba mimba kwa nguvu; mwanamke mwenye akili timamu hawezi kufanya ujinga huu, mapenzi hayalazimishwi ndugu yangu, kama ‘jitu’ halieleweki, haliwezi kueleweka kwa kukubali kubeba uja uzito. Zaidi ni kwamba unaonekana unajikomba, siyo rahisi sana ukaheshimiwa katika uhusiano huo.
Nani katika nchi amepelekwa mahakamani kwa sababu hajamaliza mahari? Sijawahi kusikia, kama kweli unampenda mwanamke utafuata taratibu za kutoa kishika uchumba, kutoa mahari na kufuata taratibu zingine. Je, ungefurahi mwanao aende kuishi kwa mwanamme pasipo kufuata taratibu? Bila shaka hakuna mtu ambaye anafurahishwa na kitendo kama hicho
Maisha yanatuhitaji kupigana vilivyo na kujiheshimu, ni vigumu sana kufikiri kwamba unaweza kuwa na maisha kirahisi. Haijalishi umezaliwa katika familia ya namna gani ni lazima uangalie namna unavyoishi.
Penda kufanya kazi nyingi, kuna watu huwa wanashangaa mbona Dismas wewe ni mwandishi wa habari, lakini unafundisha utengenezaji bidhaa, unawakilisha vyuo nk, ni kweli maisha yanatuhitaji kupambana vilivyo, hata hivyo ninavyoongea haya niko safarini kuelekea Mkoa wa Mbeya, nitakuwa nikiendesha mafunzo ya utengenezaji bidhaa katika hoteli ya Kiwila kuanzia kesho hadi Machi mosi.
Maisha yanatulazimisha kuwa wabunifu, kinyume na hilo subiri kutukanwa na watoto...unamwambia mtoto mbona hunijengei nyumba, watoto wenyewe wa siku hizi, anaweza kukuliza baba kwani toka utoto hadi unazeeka kwanini ulishindwa kujenga kama unaona rahisi. Cha msingi pigana huku ukizingatia haki, kwani kinyume na hilo hatima yako haiwezi kuwa nzuri.
Maisha yanatulazimisha kuwa wabunifu, kinyume na hilo subiri kutukanwa na watoto...unamwambia mtoto mbona hunijengei nyumba, watoto wenyewe wa siku hizi, anaweza kukuliza baba kwani toka utoto hadi unazeeka kwanini ulishindwa kujenga kama unaona rahisi. Cha msingi pigana huku ukizingatia haki, kwani kinyume na hilo hatima yako haiwezi kuwa nzuri.