Kama ilivyo kwenye sherehe za harusi, pia kwenye misiba zipo kamati mbalimbali. Kamati ya chakula, vinywaji, mapambo, muziki na usafiri.
Lakini pia kwenye misiba, ipo kamati isiyo rasmi; Nayo ni kamati ya sare. Sare za madera, khanga, vitenge, suti au fulana. Unapotokea msiba katika eneo husika, baadhi ya watu huchangamkia tenda.
Ama utasikia au kuona harakati za akinamama wanaochangisha kwa ajili ya sare. Kwa wanaopenda kuvaa madera, bei hutofautiana kulingana na kiwango cha nguo husika. Lakini kwa bei iliyozoeleka, akinamama wengi huchangia si chini ya Sh 10,000. Vivyo hivyo kwa khanga, bei yake si chini ya Sh 7,000.
Wakati mwingine, harakati hizi, hasa za uvaaji sare, zinanishawishi kujenga dhana tofauti kwamba ni sehemu ya ujasiriamali kwa baadhi ya watu kwa ajili ya kujiingizia kipato.
Hata hivyo sitaki kuchambua undani wa mambo haya maana hizi ni zama za kisasa. Ni zama za utandawazi. Ni zama za mabadiliko. Hakuna kizuizi cha kuiga na kujifunza kutoka mataifa mengine hasa yaliyoendelea.
Hizi siyo tena zama zile ambazo ilikuwa kana kwamba ni mwiko kwa mtu kwenda akiwa nadhifu msibani. Tena wenzangu akina Kalumanzila kule kijijini, walichukulia hata kuvaa viatu msibani, ni anasa. Tulikwenda peku.
Lakini sasa mambo yamebadilika. Uvaaji sare siyo tu kwenye sherehe, bali hata misibani. Tena inapofika msiba, jamii haina hiana katika kuchangia. Huitikia. Hiki ni kitendo kizuri . Ni ujamaa mzuri.
Hata hivyo natamani ushirikiano huu ungekuwa ukijitokeza pia katika ugonjwa! Jicho langu limewahi kushuhudia familia moja ambayo ndugu yao alikuwa na ugonjwa uliohitaji kufanyiwa upasuaji. Palihitajika kiasi fulani cha fedha.
Familia ililazimika kuuza sehemu ya mali yake kupata fedha za matibabu. Sina hakika kama familia iliomba msaada kwa ndugu, jamaa na majirani. Lakini wanajamii walifahamu uwepo wa mgonjwa na mahitaji ya fedha hizo.
Lakini hakuna aliyejitoa kuchangisha. Msiba unapotokea, ndipo tunashuhudia uchangishaji. Ndipo utakuta akina mama wakihamasishana kuchanga fedha za sare ya mavazi.
Hata yule ambaye wakati wa ugonjwa, hakumpelekea mgonjwa hata chungwa, siku ya msiba anakuwa tayari kutoa fedha kununua sare. Utakuta noti za wekundu zikitoka bila ubahili wowote. Hapo huwa najiuliza, mantiki ya sare hiyo ni nini?
Nakumbuka bwana mmoja aliwahi kupiga ‘stop’ sare kwenye msiba wa mkewe. Miongoni mwa hoja zake ilikuwa ni kwamba, ‘je asiye na uwezo wa kununua sare, aonekane siyo mfiwa?’ Hata hivyo yote ni mema.
Hakuna ubaya wowote wa kuvaa sare, kupamba na hata kupata burudani msibani kwani ni sehemu ya kuliwaza wafiwa. Sikatai kwamba hata kwenye msiba zipo gharama kwa ajili ya familia na waombolezaji ambao hukusanyika kuliwaza.
Ni ukweli usiopingika kwamba pia msiba una gharama zake zisizokwepeka ambazo ufumbuzi wake ni michango. Hivyo siwezi kushauri kwamba jamii iache kuchangia misiba.
Isipokuwa, ninachotaka kuhamsisha zaidi, ni jamii kujenga pia utamaduni kuchangishana kwenye ugonjwa. Vipo baadhi ya vifo ambavyo hutokana na wagonjwa kukosa matibabu yanayostahili kutokana ukosefu wa fedha.
Kama ambavyo tunashuhudia kuibuka kwa mitindo mbalimbali ikiwemo uvaaji sare msibani, basi jamii iibue mitindo mingine itakayonufaisha pia familia za wafiwa.
Badala ya kuishia kwenye kamati za chakula, mavazi na burudani, ufike wakati katika misiba, ziundwe pia kamati za kujadili ustawi wa yatima, wajane na wagane hasa anapofariki mkuu wa familia.
Haitakuwa na maana kama mwombolezaji utafurahia kuchanga fedha ya sare ya siku moja tu, na baada ya msiba, watoto wafiwa wakakosa hata nauli ya daladala ya kuwapeleka shule au familia nzima ikakosa chakula. twessige(at)yahoo.com
src
Habari Leo