Friday, May 2, 2014

Tuache ukasuku wa Serikali mbili au tatu

 
  • Tunaweza tukawa na serikali nyingi, nchi moja
SASA ni dhahiri kwamba mchakato wa Katiba Mpya umekwama ndani ya Bunge Maalumu la Katiba. Na hakuna dalili kwamba tuna uwezo wa kutoka katika huu mkwamo.
Ni dhahiri pia kwamba waliokwamisha mchakato huu ni wabunge wa Bunge Maalumu la Katiba. Nina shaka vile vile kwamba Bunge hili, kwa muundo wake, lina uwezo wa kujitoa katika mkwamo huu.
Kwa maoni yangu Bunge hili limekwama kwa sababu kubwa mbili. Mosi, ni ukweli kwamba viongozi wetu wengi tulio nao, na ambao ndio wamejaa bungeni, ni zao la kuzuka.
Kwa namna walivyokuwa wanachangia hoja bungeni ni wazi kwamba hawa ni viongozi ambao hawakuwahi kujiandaa wala kuandaliwa kuwa viongozi.
Wamezuka tu na kujikuta wamo katika nafasi walizonazo. Hawa si watu waliowahi kupitia katika utamaduni wa mijadala angalau walipokuwa shule.
Hawana uzoefu wowote wa kupambana na hoja kinzani. Ni wazi pia kwamba wengi wa wabunge wetu ama hawaelewi au hawajaukubali utamaduni wa mfumo wa vyama vingi.
Pili, Bunge hili limekwama kwa sababu ya kujaza wanasiasa na ambao wamekaririshwa misimamo ya vyama vyao.
Ni mwendelezo ule ule wa siku zote wa kudhani kwamba katika nchi hii watu pekee wenye akili ni wanasiasa, kwa hivyo ni lazima washirikishwe katika kila jambo.
Jambo hili liliwahi kuonywa mapema na wataalamu wa kuandika Katiba. Walionya kwamba ni vizuri wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wasiwe wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kwa sababu wangehamishia utamaduni wao wa kusimamia misimamo ya vyama vyama vyao ndani ya Bunge Maalumu. Wakubwa hawakusikiliza na sasa tunavuna aibu.
Sambamba na hili, ni wazi kwamba tulifanya makosa makubwa kuruhusu jambo zito kama la Muungano liwe jambo la kisera kwa vyama vya siasa.
Matokeo yake sasa kila chama kimeibuka na msimamo wake wa kisera na wabunge wa kila upande wamekaririshwa misimamo ya vyama vyao. CCM wamekariri Serikali mbili, na wapinzani nao wamekariri Serikali tatu.
Wote wameng’ang’ania walipo. Hawasogei. Pamoja na kwamba wapinzani wanajifanya kuunga mkono maoni ya wananchi kama yalivyopendekezwa na tume, ukweli ni kwamba imekuwa bahati tu kwamba tume imekuja na maoni yanayoendana na misimamo yao.
Laiti Tume ingekuja na mapendekezo ya Serikali mbili, kwa mfano, wapinzani wangekuwa kama CCM katika kuwaporomoshea wajumbe kashfa
. Tukumbuke wapinzani waliwahi kusema kwamba Tume hii ilikuwa haina weledi wowote na baadhi yao wakataka wajumbe wake wajitoe katika tume hiyo.
Bahati nzuri akina Profesa Mwesiga Baregu wakaweka msimamo, wakaamua kuchagua nchi badala ya chama.
Ni kwamba wanasiasa wetu, wa pande zote, hawana utamaduni wa kuheshimu taaluma na wao hudhani kwamba wana akili kuliko watu wengine wasio wanasiasa. 
Sasa ni lazima tukubaliane kama nchi mambo fulani fulani yanayoashiria uhai wa nchi yasiruhusiwe kuwa sehemu ya sera za vyama vya siasa.
Haya ni lazima tuyawekee wigo kwamba ni mambo ambayo tunakubaliana kama taifa na hakuna chama cha siasa kitakachoruhusiwa kutungia sera.
Kwa maoni yangu jambo la Muungano ni moja ya mambo hayo kwa sababu linahusu uhai wa nchi na hatupaswi kuruhusu mwanasiasa yeyote akafanyia propaganda jambo nyeti linalohusu uhai wa taifa. 
Wanaofahamu maana ya mijadala ni kwamba inabidi unapoingia katika mjadala wowote uwe huru katika kufikiri ili uweze kufungua milango ya usikivu.
Tatizo la kuingia kwenye mijadala ukiwa na msimamo wa kichama ni kwamba unakuwa umeziba ufahamu wa kutambua mantiki ya hoja kinzani na unabaki kuimba kama kasuku msimamo ambao unakuwa umekaririshwa na chama chako.
Na hiki ndicho kilichotokea ndani ya Bunge letu Maalumu. Wajumbe wa pande zote mbili za CCM na upinzani wamekaririshwa misimamo ya vyama vyao na wanaiimba kama kasuku.
Na pale hoja zao za kukaririshwa zinapoelekea kuzidiwa wanahamia kwenye kuporomosha matusi na kutoa vitisho visivyo na kichwa wala miguu, kama wale waliotishia kwenda msituni na wale waliotishia kwamba jeshi lingeingilia kati.
Hawa ni watu ambao wana dhamana kubwa lakini inaelekea hawajui wala kuthamini maana na ukubwa wa dhamana walizo nazo.
Wanaongea kama vijana wanavyopiga ‘stori’ kwenye vijiwe vya pombe za kienyeji na bado wanataka waendelee kuheshimiwa kwamba ni viongozi.
Kwa mwenendo huu ni wazi kwamba tumekwama mno kama taifa na tumekwamishwa na watu tuliowakabidhi dhamana kubwa ya kiungozi.
Sasa, kwa maoni yangu, ili tutoke hapa tunahitaji kufanya mambo mawili makubwa na magumu. Jambo la kwanza ni kwamba ni lazima tukubali kutoka nje ya sanduku ili tuweze kufikiri zaidi ya serikali mbili au tatu kwa maana kwamba tuna uwezo wa kuunda serikali zaidi ya hizi zilizopendekezwa na Rasimu ya Tume na ile Rasimu ya CCM iliyopo mafichoni.
Kwa mfano tungeweza kuiboresha Rasimu ya Tume. Badala ya kuwa na Serikali tatu kama zilivyopendekezwa, tungeamua kuwa na Serikali ya Zanzibar kama ilivyo leo na tukaunda Serikali ya Tanganyika yenye Waziri Mkuu na yenye kufuata mfumo wa kibunge.
Kwa hiyo tunapoenda kwenye uchaguzi tunachagua wabunge tu na chama kinachoshinda uchaguzi ndicho kinachotoa waziri mkuu ambaye atateuliwa na Rais wa Jamhuri.
Waziri Mkuu angeshughulikia mambo ya kawaida ya maendeleo kama vile elimu ya msingi, maji, barabara za halmashauri, kilimo, ufugaji na mengine kama hayo, wakati mambo mazito kama ardhi, elimu ya juu, kodi yakibaki kuwa shughuli za Muungano.
Kwa kufanya hivi tutakuwa tumedhibiti uwezekano wa ubabe ambao ungetokana na ukubwa wa Tanganyika.
Tungeweza kuamua vilevile kuendelea kuwa na serikali ya Zanzibar kama ilivyo lakini kwa upande wa Tanganyika tungeweza kuunda serikali kadhaa kwa mtindo wa kanda au majimbo kama ilivyo Afrika Kusini.
Serikali hizi nazo zitakuwa na mamlaka kamili katika mambo kadhaa lakini chini kidogo ya mamlaka iliyo nayo Serikali ya Zanzibar.
Hizi serikali zingeongozwa na mawaziri wakuu ambao wangeteuliwa na Rais ambaye ndiyo mkuu wa nchi na mkuu wa Serikali ya Jamhuri.
Ndio kusema tunaweza tukawa na majimbo au kanda kati ya tano hadi saba kwa Tanganyika, kila kanda ikiwa na watu kati ya milioni mbili hadi tano, ambayo ndiyo idadi ya watu katika nchi nyingi za Ulaya zinazotupa misaada.
Kisha tunakuwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano itakayokuwa na mamlaka kwenye mambo makubwa kadhaa lakini zaidi ya yale yaliyopendekezwa katika Rasimu ya Tume.
Kimsingi Serikali ya Muungano lazima iwe na fursa ya kushughulikia mambo kadhaa yanayohusu maendeleo ya wananchi, vinginevyo ni Serikali ambayo itakuwa haina mvuto kwa wananchi wa kawaida.
Serikali ya majimbo au kanda ndio imekuwa sera ya CHADEMA kwa muda mrefu, lakini sijui ni kitu gani kimewapata na sasa hakuna anayeongelea tena jambo hili wakati mimi nadhani ndio ilikuwa wakati mwafaka wa kulipigania.
Tukishaandika Katiba mpya hakuna chama cha siasa kitakachokuwa na uhalali wa kuibuka na sera kuhusu mambo nyeti kama haya.
Mapendekezo yanaweza yakawepo mengi. Muhimu ni kwamba lazima tuwe wabunifu na tutoke katika sanduku. Tatizo ni kwamba huwezi kuwa mbunifu kama umekaririshwa msimamo wa kivyama kama kasuku.
Ndio maana siamini kwamba hili Bunge la Katiba lililojaa misimamo ya kukaririshwa lina uwezo wa kutuandikia katiba mpya.
Jambo la pili kuhusu namna ya kutoka katika huu mkwamo ni kuangalia uwezekano wa kisheria wa kulivunja Bunge Maalumu la Katiba na kuliunda upya.
Tukiamua kuliunda upya Bunge hili kuna haja ya kuzingatia mambo kadhaa ya msingi. La kwanza, pengine kuna haja ya kuacha kuwajumuisha wabunge wa sasa katika bunge hili.
Nchi nyingi zilizoandika Katiba Mpya kwa mtindo wa Bunge la Katiba hazikujumuisha wabunge wa kawaida. Jambo la pili ni kuangalia uwezekano wa kutunga sheria itakayowapiga marufuku wale wote wanaowania kugombea katika uchaguzi mkuu ujao ili kuepuka mgongano wa maslahi.
Kuna nchi kadhaa ambazo zilifanya hili kwa kutambua uwezekano wa mgongano wa kimaslahi kwa sababu wajumbe ambao wanawania uongozi katika uchaguzi ujao watafanya kazi kubwa ya kujiuza watakapokuwa bungeni.
Ni kwa sababu hii wanasiasa wetu waling’ang’ania kwamba lazima Bunge lionyeshwe ‘live’ ili waonekana kwa wapiga kura. Tunahitaji wajumbe wa Bunge la Katiba ambao hawana haja ya kuonekana wanapotoa michango yao ili wafanye kazi yao kwa utulivu bila mbwembwe.
Bado tuna nafasi ya kujikwamua kwenye mkwamo. Cha msingi ni dhamira na nia. Rais Kikwete bado ana nafasi ya kulinda heshima yake. Auvae tena ujasiri kama alivyofanya awali kwa kuanzisha mchakato huu bila chama chake kutaka.
Namshauri amuagize Mwanasheria Mkuu apeleke marekebisho ya sheria katika Bunge la Bajeti linaloanza ili, pamoja na mambo mengine, apate nguvu ya kulivunja Bunge Maalumu la Katiba.
Muundo wa Bunge Maalumu jipya lazima uzingatie kupunguza wanasiasa ili wasiwe zaidi ya theluthi moja na kwamba wale wote wenye nia ya kugombea katika uchaguzi mkuu ujao wapigwe marufuku kuwa wajumbe wa Bunge Maalumu.

Kitila Mkumbo
src
Raia mwema