Thursday, May 29, 2014

Ni sisi wenyewe wa kujitosa au kujikomboa

 
KATIKA mfululizo huu nilieleza kiundani jinsi ambavyo siasa ya ndani ya nchi yo yote ni lazima itajionyesha katika diplomasia yake.
Siasa iliyopangiliwa vyema itazaa diplomasia iliyopangwa vyema. Misingi ya maisha ya nyumbani itajionyesha pia katika maisha yetu nje.
Imekuwa ni rai yangu kwamba diplomasia yetu imekwenda mrama. Sisemi kwamba tawala zilizoiendesha nchi yetu tangu kuondoka serikalini kwa Julius Nyerere ndizo pekee zilizopotosha diplomasia yetu. Kwa uhakika nimeandika katika makala zilizopita jinsi chini ya uongozi wake, Mwalimu aliruhusu, baadhi ya nyakati, mambo ya kipuuzi yakafanyika.
Mfano mmoja ni ule uliohusiana na Angola na jinsi Tanzania ilivyoyumba vibaya tukikaribia tarehe 11 Novemba 1975.
Ninachosema ni kwamba katika mazingira yale ya mwaka huo tunaweza kusema kwamba Mwalimu aliteleza, au aliruhusu washauri wake wamfanye ateleze, ama kwa sababu waliweza kumdanganya, ama kwa sababu yeye mwenyewe alikuwa na mitazamo iliyokuwa rahisi kumfanya akubali kuyumbishwa.
Hivi sasa tunachokishuhudia ni kwamba diplomasia yetu inakwenda hovyo, na haina mwelekeo. Nimesema katika makala zilizopita kwamba hali hii imekuwa ikiendelea, chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi, na baadaye Rais Benjamin Mkapa, halafu akafuatia Rais Jakaya Kikwete.
Wote hawa wamekuwa wakiendesha diplomasia ya hovyo kwa sababu hawakuelekea kuelewa wanatakiwa wafanye nini kwa maslahi ya Watanzania. Na msingi wa hayo ni kwamba siasa za ndani zilikwisha kuvurugwa, na leo hii bado zinaendelea kuvurugwa.
Kama nilivyosema mara kadhaa, siasa ya ndani ikiisha kuvurugwa ni lazima na siasa ya nje, yaani diplomasia, itavurugwa. Kama kuna mikanganyiko ndani ya nchi, na nje ya nchi mikanganyikao itajitokeza tu. Nitoe mifano michache.
Nchi kama Central African Republic (CAR) imekuwa katika vurugu za ndani kwa zaidi ya mwaka sasa. Raia wake wanashambuliana kwa mishingi ya itikadi za kidini, na sasa hivi ndiyo nchi inayojulikana kama nchi ya dola iliyokufa.
Ni nani anaweza kutarajia kwamba nchi kama hiyo inaweza kuwa na diplomasia inayoeleweka? Misingi ya diplomasia hiyo itakuwa ni ipi? Ni mambo gani itakayoyaunga mkono, na yapi itakayoyapinga, na kwa msingi upi?
Zipo nchi nyingi barani Afrika zinazofanana na hii, nazo zina mikanganyiko kama hiyo, ama tofauti na hiyo, lakini muhimu ni kukumbuka kwamba kwenye mikanganyiko ya nyumbani kutazaliwa mikanganyiko ya nje.
Mikanganyiko ya ndani hutokea kimsingi kwa sababu watawala wameshindwa kuwa viongozi na kuonyesha njia. Watawala hushindwa kwa sababu mbalimbali. Mojawapo ni kwamba wengi wao  si viongozi, na wala hawajawahi kuwa viongozi wa wananchi wao, au wa kitu cho chote.
Ni watu walioingia madarakani kwa sababu waliona kwamba ni nafasi ya kujineemesha, wao na familia zao, na wala hawakuwa na dhamira ya kufanya lo lote kuinua maisha ya wananchi wao, au kuwalinda dhidi ya hatari zinazowakabili.
Hili si tatizo la Tanzania pekee. Afrika nzima imejaa watu kama hawa. Wanakumbukwa kwamba walipitapita katika maeneo ya nchi zao wakiahidi hili na lile. Wakati mwingine ahadi hazikuwa na sababu yo yote; wangeweza wakajikalia kimya juu ya ahadi (wasiahidi lo lote) na bado wakapata kura walizozitaka.
Tatizo wakati mwingine ni kwamba wanasiasa uchwara  huamini kwamba mchezo wa siasa maana yake ni kutoa ahadi ambazo unajua tangu awali kwamba hazitekelezeki. Kwa maneno mengine, kuna imani iliyojengeka kwamba siasa ni kusema uongo.
Katika ngwe hii inayoanza wiki hii ninayo nia ya kurejea masuala makuu ya siasa zetu na uchumi wetu, na jinsi ambavyo tumekuwa tukienenda katika nyanja hizi. Kusema kweli, napenda kuchunguza ni jinsi gani tunajenga mahusiano baina ya maeneo na sehemu mbalimbali katika nchi yetu kwa njia ambazo zinahatarisha uhai na usalama wa Taifa letu.
Ili kuyajadili masuala haya, bila shaka itanilazimu kuangalia kwa undani iwapo bado tunaendelea na juhudi za kujenga utaifa au tunababaisha ujengaji wa miundombinu ya unyonyaji ambayo umuhimu wake wa kweli ni kwa waporaji wa nje na wasaidizi wao wa ndani katika uporaji wa rasilimali za nchi na watu wake.   
Haitawezekana kujadili masuala haya bila kuzungumzia kashafa tuliyoishuhudia katika kile kilichoitwa mchakato wa kuandika katiba mpya kwa ajili ya nchi yetu. Kashfa ambayo imewaacha watu wengi wakijiuliza iwapo kile tulichokishuhudia ndiyo hali halisi ya nchi yetu, na iwapo uozo uliotugubika umefikia viwango vya kutisha kama vile tulivyovishuhudia kwenye televisheni na kwenye redio.
Nia yangu ni kuibua mjadala mpana wa hali juu ya hali ya nchi yetu, na kuufanya mjadala huo kuwa wa kudumu. Hatuwezi kujiwekea ukomo wa kufikiri na kusemezana kuhusu nchi yetu na kisha tukataraji kwamba tutakuwa salama.
Najua kwamba hali yetu ya sasa, na hasa tukiangalia kile tulichokiona na kukisikia wakati wa mijadala ya Dodoma, inatoa taswira ya watu waliodidimia katika upuuzi na ujinga kiasi kwamba labda waletewe mwokozi kutoka kwa Mwenyezi Mungu ndipo wataweza kupona. Mimi siamini hivyo.
Naamini kwamba ukombozi wetu u mikononi mwetu, na kwamba jinsi ambavyo tutafanya kazi kwa weledi ndivyo tutakavyopata ahueni katika maswahibu tunayoelekea kukumbana nayo leo.
Kinyume chake, jinsi ambavyo tutaendeleza upuuzi na ujinga, kama tunavyofanya leo, ndivyo tutakavyozidi kudidimia katika lindi la upuuzi na ujinga, hatima yetu ikiwa ni kuwa kama nchi hizo ambazo nimekuwa nikizijadili.
Najua kwamba tumezoea kujisalimisha au kujipatia manufaa kwa kutoa rushwa ili tuepukane na majukumu yetu, ama tuchaguliwe, ama tupate tenda bila kuistahili, na kadhalika. Bahati mbaya kwa watoa na wapokea rushwa, rushwa ya kumuhonga Mwenyezi Mungu ili atuepushe na athari za upuuzi wetu, bado haijajulikana ni mapesa kiasi gani.
  src
Raia mwema
Rai ya Jenerali