Tuesday, May 20, 2014

NDOA SIYO RAHA PEKEE, JIPANGE KWA MATATIZO PIA!

 

VIJANA wengi wa sasa wanatamani kuingia kwenye ndoa wakiwa na mitazamo mbalimbali; mingi mizuri. Nasema hivyo nikimaanisha kuwa, wanaamini wakiwa kwenye ndoa, watatimiza ndoto zao za muda mrefu.
Hupiga picha kuhusu idadi ya watoto watakaozaa, namna watakavyowasomesha na jinsi ambavyo familia itakuwa yenye furaha. Kifupi wanafikiria zaidi kuhusu mambo ambayo yatawafurahisha.
Kamwe hawapati muda wa kufikiria namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha watakazokutana nazo. Hawaelewi kwamba kuna siku wanaweza kukaa wiki nzima ndani bila kuzungumza!
Je, ni kweli kwamba ndoa ni furaha tu? Hakuna huzuni? Hakuna ugomvi? Rafiki zangu, hata viongozi wa dini, wanapofungisha ndoa, husisitiza kuhusu kuvumiliana, kutunzana na kupendana kwa dhati hata katika kipindi cha shida na raha.
Msingi wa ndoa ni shida na raha. Kwa bahati mbaya, baadhi ya rafiki zetu wanapokea tofauti maneno haya, wanaamini kwa kuambiwa, humaanisha kwamba kupendana labda hata kama fedha ya kula itakosekana nyumbani, mwenzake akiumwa n.k.
Huo ni mtazamo tasa. Katika mada hii nitakufumbua, ujue nini zaidi utakutana nacho ukiwa ndani ya ndoa. Twende darasani.
WANAVYOFIKIRIA WENGI
Kama nilivyoeleza hapo juu, fikra za wengi ni tofauti. Asilimia kubwa wanafikiria zaidi kuhusu maisha mazuri yasiyo na mikwaruzano. Wanawaza kufurahia ndoa na kudhani hakuna changamoto nyingine.
Wapo wanaofikiria hata suala la tendo la ndoa.
Kwamba watakuwa huru kukutana kila siku kadiri watakavyoweza kwa kuwa wapo pamoja ndani. Hii ni mitazamo mibaya sana katika ndoa.
Ni kweli unaweza kufanya tendo la ndoa na mwenzako mara nyingi uwezavyo, lakini nani amekudanganya kwamba kila siku utaendelea kumuona kama umuonavyo leo?
Amini usiamini, zipo ndoa nyingi zinazolalamikia suala la tendo la ndoa.
Kuna ambao wanadai hawatoshelezwi huku wengine wakilalama kuwa wenzi wao hawataki kabisa kutoa unyumba. Unajua kwa nini? Ama ana mtu mwingine pembeni au amechoshwa na mapenzi ya aina moja kila siku.
WANAVYOWAZA WANAUME
Hawa fikra zao huwa kwenye suala la usafi, wanaamini wakiwa kwenye ndoa nyumba itakuwa safi, nguo zitafuliwa, kupikiwa na mambo mengine ya kifamilia.
Akili zao zinakomea hapo tu, hawawazi kuhusu migogoro na namna ya kutatua. Wanaota kuwa na maisha mazuri, kuwa na watoto na kujijengea heshima kwa jamii. Hilo tu, basi!
WANAWAKE JE?
Baadhi ya hawa ninaowazungumzia hufikiria kuhusu kuvaa vizuri, kutolewa out, kupata watoto na mengineyo. Kamwe hawana muda wa kufikiria juu ya matatizo ambayo yanaweza kutokea katika maisha ya ndoa.
Hili ni tatizo. Rafiki zangu, maisha ya ndoa hayana furaha siku zote. Kuna wakati dhoruba hutokea na kusababisha mifarakano hivyo kuhitajika umakini wa hali ya juu katika kumaliza tatizo. Si kila siku kuna amani.
TATIZO LIPO WAPI?
Kwa wale ambao wana mitazamo ambayo nimeeleza hapo juu, huwa hawana muda kwanza wa kuwachunguza wapenzi wao, lakini pia wao wenyewe kuonesha tabia zao halisi ili wenzi wao waweze kusoma kama wataweza kuendana nao.
Rafiki zangu, kwa ujumla hatutakiwi kufikiria mazuri pekee kwenye ndoa, kuna mengi ya kuvumiliana.
ISHI MAISHA YAKO HALISI
Huwezi kumjua mwenzako kama atakuwa anaishi kisanii na wewe. Sikiliza; kwa wiki mnakutana mara mbili tu, tena mnakaa kwa muda usiozidi masaa mawili, si rahisi sana kuweza kujuana tabia zenu halisi.
Pamoja na hayo, wataalamu wa mambo ya mapenzi wanashauri ili mwenzi aweze kuwa wazi zaidi kwa mwenzake ni vyema yeye akaanza kuwa wazi na kuishi maisha yake halisi kwa uwazi. Usijilazimishe kupenda kitu ambacho hukipendi. Kama kuna jambo ambalo analifanya na linakuboa, mwambie ajue ukweli.
Kwanza, uwazi wako kwake utamfanya naye awe wazi kwako. Hatakuwa na sababu ya kuigiza maisha wakati wewe unaishi maisha yako halisi.
Kila mmoja akimjua mwenzake, ndoa haiwezi kuwa na matatizo, maana kila mtu atakuwa anajua anaishi na mtu wa aina gani.
Inawezekana kabisa, mmoja wenu akaona tabia za mwenzake zimemshinda. Kama ni kweli na umegundua kwamba kuingia kwenye ndoa ni sawa na utumwa, fanya maamuzi!


NATAMANI kuona maisha ya kimapenzi ya vijana wa sasa yakiwa hayana migogoro. Ni furaha yangu kuona vijana wakifanikiwa katika kazi zao na maisha yao kwa ujumla.
Maisha bora au utaratibu mzuri wa maisha unatokana na uhusiano mwema wa mhusika na mwenzake.Aliyegombana na mpenzi wake usiku uliopita, siku yake huwa nzito sana kazini. Kila anachokifanya hukumbuka ugomvi wa usiku ulivyokuwa.
Kama mtu ataondoka nyumbani akiwa hana maelewano na familia yake, ni wazi kwamba siku yake itatawaliwa na giza. Hata kama atajitahidi kuficha, lakini itafikia mahali atashindwa. Kazi inahitaji utulivu.
Ndivyo ilivyo katika maisha, lazima upate mwenzi sahihi ambaye atakupa furaha badala ya mateso. Hapa ndipo tunapojadili jambo moja kubwa na muhimu sana; amani na furaha ya ndoa.
Wiki iliyopita nilisema tatizo ni kwamba, kuna watu ambao wanaishi maisha ya kuigiza na si maisha yao halisi. Hapo ndipo kwenye tatizo.
Sasa tuendelee...
ELEZA MATATIZO
Katika kuishi kwako maisha yako halisi, mwenzako naye atakuwa kama wewe. Hiyo ni hatua nzuri maana itakuwa rahisi kwako kugundua tabia za mwenzako. Hapo utazijua nzuri na mbaya.
Acha kulea matatizo, bila kujali jinsi, mwambie mpenzi wako tabia ambazo hazikufurahishi.
Ili aweze kubadilika kwa urahisi zaidi, unatakiwa kumwambia kwa utaratibu, lakini pia umpe sababu za wewe kukataa tabia zake hizo.
Akiendelea nazo kuwa mkali, wakati mwingine ukali unasaidia. Kwa kukemea, kama ni kweli anakupenda na anahitaji uhusiano wenu uendelee, basi lazima atabadilika. Akifanya hivyo itakuwa vizuri zaidi kwako, maana utakuwa na uhakika angalau kwa asilimia chache kwamba mpenzi wako anakusikiliza.
WENGINE NI TABIA ZA ASILI
Lazima ufahamu kwamba wakati unapambana na tabia za mpenzi wako zisizokupendeza, zipo tabia nyingine ni za asili. Hazibadiliki. Sasa hapo lazima uwe makini kwa mambo mawili; mosi, zitakuathiri?
Pili, ni tabia zitakazokugombanisha na jamii? Maana kuna tabia nyingine zinavumilika, lakini je, hazitaleta athari kwa majirani zenu watarajiwa? Haya ni mambo ya kutafakari kabla ya kuingia kwenye ndoa.
Mathalani kuna baadhi ya watu wana viburi au dharau za kuzaliwa! Hata umfanyeje, habadiliki. Unaweza kumwuliza kitu akanyamaza. Ni tabia ya kiburi, lakini kwa sababu amezaliwa akiwa na tabia hiyo, hawezi kuiacha. Sasa hapo lazima ujiulize, utawezana naye?
Utaweza kumvumilia na kiburi chake kwa maisha yenu yote? Huu ni mfano tu rafiki zangu, zipo tabia nyingi za asili, ambazo kwa nafasi yako unaweza kuzichunguza kwa mpenzi wako kabla ya kuchukua uamuzi mzito wa kuingia kwenye ndoa.
KUWA MKWELI
Ukweli ni silaha, ni haki na siku zote humfanya mtu awe huru. Kama kuna jambo ambalo hujalipenda kwa mpenzi wako, haraka mwambie. Acha kukaa na vitu moyoni. Si utaratibu mzuri.
Hata kama nguo zake hazikufurahishi mwambie ukweli atabadilika. Kama anakupenda atakusikiliza. Kwani anamfurahisha nani huko barabarani zaidi yako? Kuwa mkweli.
KUHUSU KAZI
Suala la kazi kwa baadhi ya wanandoa huwa ni tatizo. Utakuta mwanaume amemkuta binti anafanya kazi, wamependana na kufunga ndoa. Ghafla anamwambia mwenzake aache kazi!
Ndoa nyingi hasa changa huingia kwenye mgogoro huu.
Kwangu mimi, wanandoa wote kufanya kazi ni bora zaidi, maana ile maana ya usaidizi wa mwanamke inakuwa imekamilika. Kwa maisha ya sasa mama kukaa nyumbani siyo jambo zuri.
Hata hivyo, ili kuepusha matatizo, suala hili ni vyema mkajadiliana mapema. Kaa na mwenzako, mwulize ana mawazo gani kuhusu kazi baada ya ndoa.
Anzisha huu mjadala na mwisho muwe na majibu yenye usawa. Mkubaliane kwa pamoja. Hii itakusaidia maana mgogoro huu utakuwa umeisha kabla hata ya ndoa yenu.
Wiki ijayo nitakuwa hapa katika sehemu ya mwisho ya mada hii



src
GPL