Monday, May 12, 2014

ALLY CHOKI:SINA MPANGO NA SIASA





, Ijumaa…



Stori: Elvan Stambuli
MWANAMUZIKI nguli katika muziki wa dansi nchini, Ally Lwambo Choki ‘Mzee wa Farasi” amesema hana mpango wa kugombea ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwakani na wala hana mpango wa kuingia katika siasa.
Mwanamuziki nguli katika muziki wa dansi nchini, Ally Lwambo Choki ‘Mzee wa Farasi”.
Choki aliyasema hayo katika mahojiano ya ana kwa ana na waandishi wa Global Publishers katika safu ya Live News Room, Ijumaa iliyopita kufuatia wananchi wa nyumbani kwao, Kibaha, Pwani kumtaka kujiingiza katika siasa na kugombea ubunge.
“Mimi siwezi kujiingiza katika siasa hata siku moja, wala sina mpango wa kugombea ubunge. Kuna watu kule kwetu Kibaha wamenishauri niingie siasa na kugombea ubunge lakini sitaki,” alisema.
Licha ya hilo, mwanamuziki huyo anayetamba kwa sasa na Bendi ya Extra Bongo akiwa mwimbaji na kiongozi, alijibu maswali ya waandishi kama ifuatavyo:
Mwandishi: Kwanza Choki hebu tueleze historia yako ya muziki kwa ufupi.
Choki: Nilianza muziki rasmi mwaka 1988 nilipojiunga na Lola Africa Band, baadaye nikajiunga na Mwenge Jazz ambapo nilidumu kwa miezi sita tu, nikahamia Bantu Group.
“Mwaka 1990 nikiwa Bantu na Hamza Kalala akiwa kiongozi tulitoa albamu ya Baba Jane. Mwaka 1991 nilitoka Bantu, nikajiunga na Legho Stars chini ya Tshimanga Kalala Asosa. Sikudumu sana nirudi Bantu ambako nako sikukaa sana, nikajiunga na Bendi ya MK Group ‘Tukunyema’.
“Mwaka 1992, nilihamia Bendi ya Washirika Stars ‘Watunjatanjata’ ambako tulitoa albamu inaitwa Gubu la Wifi. Pale tulikuwa na akina Abdul Salvado ‘Father Kidevu’ na wengine wengi.
“Ilipofika mwaka 1994 nilikwenda Nairobi, Kenya. Alikuja Muumini Mwinjuma (mwanamuziki) kunichukua na mwaka 1998 nikiwa kulekule Kenya, nilianzisha bendi inaitwa Extra Kimwa.
Mwandishi: Ulirudi mwaka gani nchini na ni kwa nini? Je, uliporudi ulijiunga na bendi gani?
Choki: Mwaka 1999 nilirudi Bongo baada ya kupata taarifa kuwa mama yangu mzazi ni mgonjwa. Niliamua nije kuwa karibu naye. Nikiwa nchini nilijiunga na The African Stars ‘Twanga Pepeta’ kwa ushauri wa Robert Hegga ‘Catapiller’ ambaye tulikuwa wote Nairobi.
“Mwaka 2000 tulitoa albamu iitwayo Jirani. Ilikuwa na nyimbo nyingi lakini Jirani ulikuwa utunzi wangu.”
Mwandishi: Ukiwa Twanga ulifanya kitu gani cha kukumbuka.
Ally Lwambo Choki ‘Mzee wa Farasi” akiwa kwenye pozi.
Choki: Kuna kipindi wanamuziki wengi walihama Twanga na kwenda kujiunga na Chuchu Sound, wengine Mchinga Sound, akiwemo Adolf Mbinga mpiga solo badala yake nikamfuata Miraji Shakashia ‘Shaka Zulu’ kushika nafasi yake na baadaye, Kizunga aliyekuja kupiga rithym gitaa.
“Baadaye tena nikawa kiongozi wa bendi tukatengeneza albamu ya Fainali Uzeeni, ikaja Ukubwa Jiwe kabla ya Chuki Binafsi. Twanga najivunia kwa sababu ni mimi ninayeongoza kwa kutunga nyimbo nyingi zilizovuma pale.
Mwandishi: Ilikuwaje ukaanzisha bendi yako?
Choki: Ni mwaka 2003 nilipoamua kuanzisha Extra Bongo. Niliona ninatakiwa kuwa na bendi yangu lakini ikatokea fitina wanamuziki wangu wakanunuliwa, nikaenda Mchinga baadaye nikarudi Twanga kisha nikajiunga na TOT ambako nilikaa kwa shida.
Mwandishi: Kwa nini unasema TOT ulikaa  kwa shida?
Choki: Niliushauri uongozi tufanye kazi kibiashara na hata kubadili jina tuite T Respect, wakakataa, wakawa wanajali zaidi kampeni za CCM.
“Mimi niliwaambia kuwa ni mtu wa vyama vyote, hivyo sikuwa tayari kuwa mwanamuziki wa kampeni wa chama kimoja. Mkataba wangu ulipokwisha niliifufua Extra Bongo mwaka 2009 na mpaka sasa namshukuru Mungu bado tupo katika ushindani.
Mwandishi: Unadhani kwa nini muziki wa dansi umeshuka kiwango?
Choki: Muziki wa dansi haujashuka kiwango isipokuwa vyombo vya habari vimeupa kisogo lakini tunatoa nyimbo nzuri na hata video nzuri.
“Pili uongozi wa bendi za muziki ni mgumu ukilinganisha na mwanamuziki wa Bongo Fleva ambapo kiongozi hana wanamuziki wengi. Hata hivyo, naamini ni wakati na kuna muda utafika muziki huu utakuwa juu.
Mwandishi: Yapo madai kuwa katika fani kuna baadhi ya wanamuziki wanatumia ndumba ili wawe maarufu, kuna ukweli na hilo?
Choki: Ushirikina upo, watu wanalogana unaweza kulogwa spika zote zikaungua kwa mpigo au ukajikuta upo jukwaani unalala tu lakini muhimu ni kufanya juhudi tu katika kazi zako.
Mwandishi:

...Choki akipozi na baadhi ya wana Global.
Umejitoa katika mashindano ya Kilimanjaro Music Awards, unaweza kusema sababu?
Choki: Nisingependa sana kuzungumzia hilo kwa sababu simo, niliachana nao baada ya albamu tuliyotoa nikiwa Twanga ya Mtaa wa Kwanza kushinda na Wimbo Bora kuwa Mtaa wa Kwanza kushinda lakini mtunzi wakasema eti ni Aset Club, nilichukia na kujitoa kwa kujua kuwa hapo kuna jambo.
Mwandishi: Unamzungumziaje marehemu mzee Muhidin Maalim Gurumo?
Choki: Alikuwa mwalimu na mtu anayesikiliza ushauri. Binafsi nilifanya naye kazi nyingi. Tuliwahi kutoa albamu yenye nyimbo zake tatu na zangu tatu na ilifanya vizuri sana na tulipata fedha nyingi mpaka kila ninapokutana naye akawa anasema ‘nakushukuru sana kijana.’
Mwandishi: Nini siri ya mafanikio yako?
Choki: Ni juhudi tu, sinywi pombe, niliacha mwaka 1994, wala sivuti sigara, nina nyumba, gari na watoto sita, namshukuru Mungu.
Mwandishi: Nini kilikufanya uache kunywa pombe?
Choki: Siku moja nilikunywa sana pombe, kesho yake nikaamka na ulevi na tulikuwa na shoo mchana. Nilitakiwa nipige dramsi na kuimba, kwa kweli nilipata tabu sana na nikaapa kwamba sitakunywa tena pombe, ikawa mwisho siku hiyo.
Mwandishi: Nakushukuru sana kwa kuja ofisini kwetu Choki.
Choki: Na mimi nawashukuru sana Global Publishers kwani magazeti haya yamenifanya nifanye vizuri katika albamu yangu ya Mtenda niliyoizindua katika Ukumbi wa Dar Live mwaka huu


src
GPL