Friday, April 4, 2014

Vichwa vinavyoibeba HIP HOP TZ

MUZIKI wa Tanzania hususan wa kizazi kipya ‘Bongofleva’ unazidi kupasua anga kila kukicha kutokana na sababu kadha wa kadha, hivyo kukubalika kwa wengi.
Awali wakati vijana wa miaka 90 walipoanza kuimba muziki huo, wengi wao walionekana kama ni wahuni hasa kutokana na kwamba baadhi ya waliokuwa wakiimba kwa wakati huo walikuwa wakijihusisha na tabia za kihuni.
Pamoja na dhana hiyo, wazazi wengi walifikia hatua ya kutotaka watoto wao kujihusisha na muziki huo wakihofia wataharibikiwa katika maisha yao.
Kusimama kwa muziki huo kukasababisha kuwepo kwa aina ya muziki ambapo wapo walioimba R&B, Hiphop, Dancehall na nyinginezo ili mradi kila mmoja ahakikishe anatimiza malengo yake.
Pamoja na kuwepo kwa kila aina ya muziki katika Bongo fleva, bado muziki wa Hip hop ulionekana kuwashinda wasanii wengi wakibaki wachache akiwemo Joh Makini Ambwene Yesaya ‘AY,’ Mr II ama Sugu ambao walijikuta wakiusimamisha vizuri.
Hata hivyo, baada ya ujio wa Farid Kubanda ‘Fid Q’ katika muziki huo uliwafanya wasanii wengi waliokuwa wakiimba kujikuta katika wakati mgumu kutokana na aina ya mashairi yake.
Mbali ya kuandika, hata jinsi ambavyo Fid Q amekuwa akiishi anaonyesha jinsi gani alivyo msanii halisi wa Hip hop ukilinganisha na wasanii wengine wa muziki huo.
Kati ya nyimbo ambazo ziliweza kuliweka jina la Fid Q juu ni pamoja na Chagua Moja, Huyu na Yule, Fid Q.Com, Agosti 13, Ielewe Mitaa na Sihitaji Marafiki ambazo zimemfanya akubalike katika jamii na kuwa ndiyo alama ya Hip hop nchini.
Pamoja na mafanikio hayo ya Fid Q, pia naye ameweza kupitia changamoto  mbalimbali ikiwemo ujio wa wana-hiphop tisa ambao wanaonekana kuanza kuteka hisia za wadau wengi wa hiphop nchini.
Wasanii hao ambao wanampasua kichwa nguli huyo ni pamoja na Erick Msodoki ‘Young Killer.’
Huyu ni msanii anayetoka mkoani Mwanza aliyeingia katika muziki wa hip hop na kuufanya muziki huo kujiongezea mashabiki hasa kutokana na wimbo wake kama ‘Jana na leo’ alioshirikiana na Stamina na Quick Rocka.
Aidha, Young Killer amejikuta akiwa midomoni mwa mashabiki wa miondoko hiyo hasa baada ya wimbo wake wa ‘Dear Gambe’ kufanya vizuri katika vituo mbalimbali vya redio.
Emmanuel Elibariki ‘Ney wa Mitego’
Ukimuona tu kimuonekano ni msanii aliyeuvaa uwana- hiphop kuanzia  kimavazi na hata kujichora mwilini kama ilivyo kwa nyota wengi Ulaya wa muziki huo.
Wakati wimbo wake wa ‘Nasema Nao’ alipoutoa ilionekana kama atagombana na wasanii wengi nchini, lakini badala yake wimbo huo ulimfanya apate mashabiki wengi nchini.
Hakuishia hapo alitoa tena ‘Mwanamke hapigwi’ kitu ambacho mashabiki wengi walishangazwa na kibao hicho kwani kwa  jinsi alivyo, utadhani yeye ndiye mpigaji wa wanawake kumbe ni kati ya watu wenye huruma na kuwatetea wanawake.
Kama hiyo haitoshi, alipata mashabiki zaidi na kuwa gumzo nchini katika wimbo wake wa ‘Muziki gani’ alioimba na Diamond Platinum ambao hadi hivi sasa unafanya vizuri, kiasi cha wadau wengi wa muziki huo kuonekana kumtabiria kuwa nyota yake itang’aa zaidi.
Kala Jeremiah
Hakuna aliyeshangaa baada ya kutwaa tuzo tatu za Kili Music kutokana na nyimbo za ‘Karibu Dar’ aliomshirikisha Ben Paul na ‘Dear God’, ambazo zimemfanya kukubalika zaidi katika medani hiyo.
Kabla ya kutoa nyimbo hizo, Kala alitoa wimbo wa ‘Ningekuwa Rais’, ambao ulifanya vizuri lakini si katika kiwango cha juu ukilinganisha na nyimbo hizo zilizompa tuzo tatu.
Nyimbo nyingine ambazo zilimtambulisha Kala ni pamoja na ‘Waambieni,’ ‘Wimbo wa Taifa’ na ‘Wizi Mtupu.’
Emmanuel Simwinga ‘Izzo Business’
Ni msanii ambaye pamoja na kuwa na kipaji cha kuandika mashairi lakini nyota inaonekana bado haijaanza kung’aa kama anavyotaka mwenyewe.
Nyimbo zake za ‘Utarudishwa Mbeya’ alioshirikiana na Bele 9 na ‘Love me’ alioshirikiana na Barnaba na Shaa licha ya kufanya vizuri lakini bado hajawa midomoni mwa mashabiki wengi wa muziki huo.
Sharif Thabit ‘Darasa’
Kama ilivyo kwa Izzo Business, Darasa ana kipaji cha kuandika na kuimba lakini inawezekana hajapata promosheni ya kutosha ndiyo maana jina lake halijajulikana.
Lakini, wimbo wake wa ‘Sikati Tamaa’ alioshirikiana na Ben Paul, ukiusikiliza ni lazima utataka kumjua zaidi.
Wimbo huo pia aliutoa kwa mara ya pili akishirikiana na Godzilla na Joh Makini na kumfanya kujitangaza zaidi.
Kabla ya Sikati tamaa remix, Darasa alitoa wimbo wa Njia Panda akishirikiana na Diamond.
Godzilla
Nathubutu kumuita 50 Cent wa Tanzania kwa jinsi anavyoimba na kwenda na midundo hana tofauti na mwanamuziki huyo wa Marekani.
Kitakachokufanya uwatofautishe ni lugha wanazotumia lakini kama Godzilla akiamua kuimba Kiingereza ukimsikia kwa mara ya kwanza utafikiria ni 50 Cent.
Nyimbo zake za ‘Zaidi ya Hapo’ na ‘Milele’ zilimtambulisha vizuri zaidi huku akiitwa jina la Rais wa Salasala kutokana na nyimbo zake nyingi hata alizoshirikishwa kulinadi eneo hilo analoishi.
Ukiachana na hilo, Godzilla aliamua kuanzisha lebo yake iliyojulikana Godzilla inc.
Wasanii hao pia wapo wengine kama Stamina, Nick Mbishi na Roma Mkatoliki ambao pia wanafanya vizuri katika medani hiyo na kufanya kuwepo na ushindani wa kweli.
Nyimbo za ‘Ushauri Nasaha’ na ‘Kabwela’ ndizo zilizomtangaza vizuri Stamina huku ‘Gumzo la jiji’ iliyoimbwa na Nick Mbishi pia ilimuweka vizuri licha ya kuwa alishashirikishwa katika nyimbo nyingi za wasanii wengine.
Roma Mkatoliki yeye tangu atoe wimbo wake wa  ‘2030’ ambao umemfanya kuwa juu na kujikuta akipata shoo mbalimbali ndani na nje ya nchi, amejikuta anakaa midomoni mwa wadau wengi wa muziki huo.
Wapo wana-hiphop wengi tu ukiachana na waliotajwa hapo juu lakini hao ndio ambao hata ukiamshwa usingizini ukiambiwa utaje wanamuziki wa miondoko hiyo nina uhakika watano kati yao watakuwepo.
Uwezo wao wa kuimba na kutunga vitu vinavyoelezea maisha halisi ya Mtanzania ndiyo sababu kubwa inayowafanya wazidi kupata wafuasi na si mashabiki kama wenyewe wanavyopenda kusema.

src
TD