Dodoma. Watanzania wametakiwa kutokuwa na hofu kuhusu mchakato wa Katiba Mpya unaoendelea hivi sasa Bungeni Dodoma, kwani Katiba hiyo itapatikana.
Akifungua kikao cha Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma leo, Mwenyekiti wa baraza hilo, Samuel Sitta amesisitiza kuwa kwa njia moja ama nyingine, mchakato huo wa Katiba lazima ufanikishwe.
“Mimi naamini Mungu anaipenda Tanzania, na nina hakika kwa njia moja au nyingine tutatunga Katiba Mpya,” amesema Sitta.
Baadhi ya wawakilishi pia walitumia fursa zao Bungeni hapa leo kuwasihi wajumbe toka kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) walosusia vikao warejee Bungeni, wakiwakumbusha kuwa wana wajibu wa kuhakikisha wananchi wanapata Katiba inayolinda maslahi yao.
“Sisi kama wanasiasa, ambao siku zote tumekuwa ndio watetezi wa wananchi, itakuwa ni ajabu sana…[kama] sisi tutaingia mitini, tukaacha tu [mchakato wa Katiba] ukaishia hivi hivi,” amebainishia mwakilishi wa Vyama vya Siasa Bungeni hapa, Rashid Mtuta.
“Tutakuwa tunawasaliti.”
Mjumbe mwingine anayewakilisha Vyama vya Wakulima, Hamisi Dambaya, amesisitiza kuwa Bunge hilo litakuwa “limewakosea sana” Watanzania kama litaondoka bila kutengeneza Katiba Mpya.
“Tutumie zaidi hoja ya kufanya maridhiano katika kuhakikisha kwamba hili Bunge linamalizika kwa Katiba Mpya kupatikana.”
Aliongeza: “Hakuna sababu ya msingi kwa vyama vya siasa kukimbia katika meza ya maridhiano.”
Dambaya amedai kuwa Watanzania watakuwa hawajatendewa haki kama wajumbe “watatoka ndani ya Bunge na kuanza kufanya shughuli hizi za kutengeneza Katiba nje ya Bunge.”
src
mwananchi
src
mwananchi