HIVI karibuni dunia imeshuhudia na kushtushwa na namna ambavyo taifa la Nigeria limekua kiuchumi barani Afrika na kufanikiwa kuipiku Afrika Kusini.
Hayo yamebainishwa katika takwimu mpya zilizotolewa za kupandisha pato la jumla la ndani linalofikia dola za Marekani zaidi ya bilioni 500, ambalo limeiwezesha nchi hiyo kuwa ya 26 kwa uchumi mkubwa duniani.
Wakitangaza hilo, wakala wa takwimu wa nchini humo walisema kuwa pato hilo limechangiwa na mafuta, mawasiliano, habari na teknolojia, biashara za mtandaoni, muziki na fillamu za Nollywood.
Nigeria haikuwa katika nafasi hiyo wakati ilipotoa mahesabu yake ya mwisho ya mwaka 1990, ambapo hawakuwa wameorodhesha sekta za muziki na filamu za Nollywood.
Kwa upande wa sekta ya filamu pekee ya Nigeria (Nollywood) inachangia pato la taifa la dola za Marekani milioni 450.
Hata kwa upande wa tasnia ya filamu nchini Afrika Kusini imekuwa ikiingiza pato la taifa linalofikia Rand bilioni 7.7
Katika hili, Tanzania inatakiwa kujifunza kitu hapa na kuhakikisha wanapitisha sera ya filamu itakayosaidia kuongeza ajira, ikiwamo ukuaji wa uchumi wa nchi.
Kwani kwa muda mrefu sasa shughuli za filamu zimekuwa zikisimamiwa na sera isiyokidhi ya Utamaduni, iliyotayarishwa na kupitishwa mwaka 1997 pamoja na sheria ya Filamu na Michezo ya kuigiza namba 4 ya mwaka 1976.
Sababu ya kutokidhi imechangiwa na kupitwa na wakati, hivyo kutokidhi baadhi ya mahitaji ya tasnia hiyo, hali inayolazimisha kutungwa kwa sera ya filamu.
Kuna mambo ambayo yanatakiwa kufanywa ili Tanzania iweze kujinufaisha na mapato ya kazi za wasanii ambapo moja ni kuangaliwa uwezekano wa kuanzisha chombo kitakachokuwa na uwezo wa kuzitangaza filamu zetu.
Chombo hicho kinatakiwa kiwe na idara za utoaji wa taarifa za upatikanaji wa fedha na kuandaa takwimu za kina ikiwamo kuzitangaza kazi hizo katika masoko mengine ya Afrika na dunia kwa jumla ili kuwezesha kuuza kazi zetu kimataifa na kuingiza fedha za kigeni.
Idara nyingine itakuwa ya kuwalazimisha wadau katika sekta ya filamu kupata mafunzo ya filamu itakayosimamia mapato yatokanayo na filamu na itakayosimamia kwa ukamilifu sheria za uharamia/wizi wa kazi za sanaa na hivyo kuwafanya watengenezaji wa kazi hizi kutokuwa na hofu ya kupoteza mapato yatokanayo na kazi zao.
Sera hiyo inatakiwa ihakikishe inaondoa matatizo makubwa yaliyo kwenye tasnia ya filamu nchini Tanzania kama vile kuhodhiwa na kundi dogo la wafanyabiashara ambalo ndilo lenye maamuzi ya mwisho ya kuamua kama filamu yake iingie sokoni au itupwe.
Katika soko kumekuwa na urasimu wa hali ya juu kwani wameweka vikwazo visivyokuwa na msingi, ambapo wameweka misimamo yao wakitaka filamu zinazokwenda sokoni lazima kuwemo na majina au sura za nyota wakubwa, kwa sababu eti ndio wanasaidia kuuza sokoni.
Wauzaji hawa wamefanikiwa katika hili kwani wamewezesha kutengeneza baadhi ya waigizaji wao ambao wakitakiwa kushiriki katika kazi za wasanii chipukizi hutoza kiasi kikubwa cha fedha kinachowakatisha tamaa chipukizi hawa.
Pindi watayarishaji wanaposhindwa kuwatumia wasanii wakubwa na kuwatumia wachanga au wasiokuwa na majina wanajikuta wakipata hasara kubwa kutokana na kujikuta wakikataliwa filamu zao kuingizwa sokoni.
Hatuwezi kuwa kama Nigeria bila ya kuwepo kwa sera bora itakayowezesha biashara hiyo kutohodhiwa na wafanyabiashara wachache wenye sauti ya kuamua kazi ya kuingia sokoni.
Ukuaji wa tasnia ya filamu popote duniani haupimwi kwa kuangalia wasanii wachache waliofanikiwa huku idadi kubwa ya wenzao wakiishi maisha duni, ila kipimo bora cha kuangalia ukuaji wa filamu ni namna ya upatikanaji wa mapato na makusanyo ya kodi ambayo kwa hapa nchini bado hali iko chini kutokana na mfumo uliopo.
Kama Tanzania itakuwa na nia ya kufikia malengo ya kupata mapato kupitia sekta ya sanaa ni lazima watengeneze sera madhubuti za kuwezesha sekta hiyo ili iweze kuchangia nchi kiuchumi
src
Tanzania Daima