Monday, April 14, 2014

NANI ATABADILI MIOYO YETU?





NIMSHUKURU sana Mungu, mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kukutana tena leo, wakati mamia ya ndugu zetu wakiwa mahospitalini wakishindana na vifo, lakini sisi tu wazima. Kama ninavyosisitiza wakati wote, hatuko hivi tulivyo kwa sababu ya ujanja wetu, bali uhai na uzima wetu upo mikononi mwake yeye aliye juu.
Kuna baadhi ya vitu vinatokea katika jamii yetu ambavyo ni vigumu sana kuamini kama kweli sisi tunaishi hivi kwa sababu ya mazingira magumu au kwa vile tumemsahau Mungu. Tumekuwa na roho ya ajabu, ya kikatili isiyofanana kabisa na sifa kubwa ya ukarimu, undugu na mshikamano unaosifika nje ya nchi yetu.
Kinachonifanya niseme hivi, ni ongezeko na vitendo visivyo vya kibinadamu vinavyoendelea kutokea nchini, hasa katika kipindi hiki ambacho kuna jinamizi kubwa la ajali mfululizo. Vitendo vya watu kukimbilia kuwapora majeruhi wa ajali badala ya kuwasaidia.
Ni jambo linalosikitisha sana kiasi cha kutuondolea kabisa sifa yetu nzuri ya miaka mingi ya huruma. Sina uhakika kama wanaofanya vitendo hivi wanajaribu kupiga picha na kujigeuza wao ndiyo wale waathirika wa ajali na jinsi gani wanavyojisikia, wanapowaona Watanzania wenzao, wakiwavua viatu, saa, wakichukua simu, wakichukua fedha na mali zao mbalimbali na kutokomea bila kuwapa msaada?
Hili ni jambo la kinyama kuliko unyama wenyewe unavyokuwa kwa sababu wakati mwingine majeruhi huhitaji msaada wa haraka, lakini kuna Watanzania wenzetu wanakimbilia kwanza kukusanya mali.
Ipo simulizi moja ya kusikitisha sana niliyowahi kuisikia, kuwa vijana wa kihuni, hasa jijini Dar es Salaam, huwaua majeruhi wa ajali nyakati za usiku, endapo ajali hiyo itatokea katika eneo ambalo halina watu.
Ni kwamba mtu anapopata ajali usiku, kwa mfano katika eneo lisilo na watu, wakati akiwa  peke yake au na mtu na wote wamejeruhiwa, wanachofanya waliokimbilia  ni kuwamalizia na baada ya hapo huchukua vitu vyote na kuondoka navyo.
Ndugu zangu, fedha au mali havina thamani yoyote mbele ya Mungu. Utafanya kila kitu hapa duniani, lakini kama mtu hakuwekeza kwa Mwenyezi Mungu, siku ya hukumu kila mmoja atalipia matendo yake.
Inasikitisha sana kwamba mtu akipata ajali, anapoona watu wanakimbilia eneo hilo, huanza kupatwa na hofu zaidi badala ya faraja, kwani anaodhani wanakuja kumuokoa, kumbe wanakuja kummaliza.
Niwaombe ndugu zangu Watanzania, kama zamani tulikuwa watu wema tuliopendana, tulioshirikiana na kusaidiana kwenye matatizo, basi hata sasa tunaweza kufanya hivyo.
Huenda kuna shetani alipita hapa katikati yetu, akabadili mioyo yetu na kutupandikiza ukatili huu, sasa umefika wakati wa kumkataa, kwa sababu tunachowafanyia ndugu zetu wanaopata ajali ni ukatili wa kutisha!
Hakuna mtu anayeweza kumaliza matatizo au shida zake kwa kuwapora majeruhi wa ajali. Mtu huyo anachokifanya ni kujiongezea dhambi na kuahirisha shida yake kwa muda mfupi. Hata kama utapata shilingi milioni 100 kwa mtu aliyefariki au kuumia katika ajali, bado huwezi kutajirika kwa sababu huwezi kupata baraka.
Utafanya matanuzi na kununua vitu vya gharama ambavyo baadaye utaviuza na kuishiwa, wakati roho ya marehemu itakapokuwa ikikulilia.Ni lazima tujifunze kumuogopa Mungu. Kama inaonekana jambo hili ni gumu kwa kizazi chetu cha sasa, basi angalau wazazi waanze kuwafundisha watoto wetu faida za kumtukuza Mungu, kwani atawasaidia kuyatambua na kuyakimbia maovu.
Pengine hii inatokana pia na watu kuchoshwa na maisha magumu yanayosababishwa na baadhi ya viongozi wetu wanaoshindwa kuwajibika ipasavyo.
Nao pia wanapaswa kupewa lawama hizi na hii iwasaidie pia kutambua kuwa kushindwa kwao kuwajibika katika maeneo yao kunachangia kumomonyoka huku kwa maadili na kupandikiza roho za kinyama kwa Watanzania wenzao.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

src
GPL