MWANZONI nilisema kwamba diplomasia ya nchi yo yote ile lazima itakuwa ni kielelezo cha siasa za ndani, jinsi watu wa nchi husika wanavyoishi na kuhusiana, jinsi walivyopangilia shughuli zao za uzalishaji na mgawanyo wa mazao yao, jinsi wanavyotarajia kuishi katika zama za mbele, na jinsi ambavyo wangependa kuhusiana na majirani zao na watu wa mataifa mengine kwa ujumla.
Kwa maana hiyo, diplomasia inakuwa ni siasa ya nje ambayo ni mwangwi wa siasa ya ndani. Inapotokea kwamba siasa za ndani ni za ubabe na ‘mwenye nguvu mpishe’ na siasa za nje pia zitakuwa ni za ubabe vivyo hivyo. Sisi kama Watanganyika na baadaye Watanzania tulikuwa tumekubali siasa ya ndani iliyosimama juu ya misingi ya usawa wa binadamu wote, usawa na haki kwa wote.
Wako watu ambao hawataki kujua, lakini ni msingi huo uliotufanya tujitoe mhanga kuungana na Waafrika wenzetu waliokuwa bado chini ya utawala wa kikoloni. Jukumu la ukombozi tulilikubali kuwa ni letu kwa sababu tulisema kwamba iwapo kuna sentimita ya Afrika ambayo bado iko chini ya utawala wa mkoloni sisi hatuwezi kudai kwamba tuko huru.
Falsafa hiyo ndiyo iliyotupa nguvu kubwa kutufanya tushirikiane na wenzetu (si kuwasaidia kama wanavyosema wasiojua maana halisi ya ukombozi) kulikomboa bara hili. Zilikuwapo nchi nyingine huru katika bara hili lakini kwa sababu ya siasa zake za ndani za ‘mwenye nguvu mpishe’ hazikuonekana sana katika mapambano haya. Kwao makaburu walikuwa ni wenzao, hata kama walikuwa tofauti kidogo.
Na hapa ningependa tuelewane. Imekuwapo tabia ya kusema ‘tuliwakomboa hawa’. Ni uongo. Hatukumkomboa mtu hata mmoja, bali tulishirikiana na wenzetu katika kuutokomeza ukoloni ambao ulikuwa ni mwiba kwetu pia. Na pili, tusije tukaamini kwamba sote, kwa sababu ni Watanzania, basi sote tulishiriki katika harakati hizo. Walikuwapo Watanzania waliomaini kwamba juhudi za Mwalimu Nyerere katika ukombozi zilikuwa zinatupotezea muda na rasilimali.
Hadi leo wapo watu wanaomini kwamba umasikini wetu umetokana na rasilimali ‘tulizopoteza’ katika harakati za ukombozi. Wengi miongoni mwa watawala wetu wenye umri kama wangu ama chini kidogo wala hawakujua nini kilikuwa kinaendelea Kusini mwa Afrika, achilia mbali Guinea Bissau na Cape Verde. Leo wanaweza kutamba kwa kusema ‘tuliwakomboa’ lakini ukweli ni kwamba walikuwa mbali sana na ukombozi wanaouzungumzia leo.
Ni mantiki ile ile: Wale waliotetea siasa ya ndani iliyojali utu, usawa na haki ni hao hao waliotetea ukombozi barani Afrika na duniani kote. Ndio wale wale waliosimama kuitetea Vietnam dhidi ya ‘mwenye nguvu mpishe’ ya Marekani, na ndio hao hao waliosimama kuitetea Palestina dhidi ya ‘mwenye nguvu mpishe’ ya Israeli. Haishangazi, basi, kwamba watetezi wa haki ndani ndio watetezi wa haki nje pia.
Ushahidi upo. Tulipoanza kuachana na misingi ya haki katika siasa za ndani, na tukaingia katika unyang’au tuliokuwa tukiwasema nao ndugu zetu wa Kenya, siasa zetu za nje zikawa ni za kinyang’au. Tukaachana na utetezi wa wanyonge, tukawa watetezi wa madhalimu. Tukaacha mshikamano wetu wa jadi, tukawa ni watetezi wa kile kilichoitwa ‘utandawazi.’
Kama wanafunzi dhaifu wa historia, tukauchukulia utandawazi kama falsafa mpya yenye maslahi kwetu. Wakuu wetu wakavutwa, wakapandishwa ndani ya ndege, wakapelekwa huku na huko, wakaenda wakiimba ‘utandawazi’. Siasa mpya ya nje ya nchi yetu, ndiyo kusema diplomasia yetu, ikawa ni ‘utandawazi.’
‘Utandawazi,’ kwa ye yote anayejua historia kidogo tu, tumekuwa nao tangu enzi na enzi. Ukoloni ulikuwa ni sehemu ya utandawazi. Utumwa ulikuwa ni sehemu ya utandawazi. Safari ya Mtaliano Marco Polo kwenda China ilikuwa ni sehemu ya utandawazi. Safari za Mtaliano Christopher Columbus kwenda Marekani zilikuwa ni sehemu ya Utandawazi.
Nilisema wakati huo kwamba hata katika misahafu mbalimbali tunaupata utandawazi, kama vile Kain alivyolaaniwa na kupelekwa kuishi ughaibuni kwa kosa la kumuua ndugu yake, na Bwana Mkubwa akamtia alama kwenye paji la uso ili atakakokwenda watu wa huko wamtambue.
Ama Bwana Yesu alipopelekwa na wazazi wake kutafuta salama nchini Misri. Ama Quraan iliposema ‘tafuteni elimu hadi China.’ Yote haya ni uthibitisho tosha kwamba hakuna jipya katika utandawazi isipokuwa msukumo mpya na ari mpya ya mabeberu kutuweka chini yao, na teknolojia mpya wanayoitumia kwa malengo hayo wakati sisi tunazalisha Waafrika mamilioni wanaomaliza shule na ‘Division 0’.
Niliuliza wakati huo: Kama kweli dunia hii imekuwa ni kijiji cha ulimwengu, je sisi tunajikuta wapi katika mipangilio ya kijiji hicho? Tumepangiwa maskani yetu yawe wapi katika kijiji hicho na majukumu yetu ni yapi? Je, katika kijiji hicho Afrika ndiyo ofisi kuu ya utawala wa kijiji chetu? Je, sisi tumo ndani ya maabara ya kijiji tukifanya utafiti wa mbinu mpya za kuinua uzalishaji?
Je, Afrika ni maktaba ambamo watoto na watu wazima wanajisomea ili kuongeza ujuzi wao au kujiburudisha kwa hadithi tamu? Je, katika mipangilio ya kijiji hicho sisi ndio wazalishaji wa chakula cha kulisha kijiji kizima?
Ama, niliuliza, Afrika ndiko unapatikana msalani wa kijiji hicho, ambako kila mwanakijiji ana uhuru wa kwenda kujisaidia baada ya kuwa amekula na kushiba? Sikupata jibu kutoka kwa wakuu wetu waliokuwa wakibadilisha ndege kwa ndege, wakikimbilia wapi sijui, kueneza injili ya ‘utandawazi’ na ‘kijiji cha dunia’.
Muda uliopotea katika kazi hii ya bure kwetu ni mwingi, na kilichopatikana hakijulikani isipokuwa mwendelezo wa kile kilichoelezwa na rafiki yangu marehemu Chachage Seithy Chachage ‘collective imbecilisation.’
src
raia mwema