TAARIFA KWA UMMA
Kama ambavyo tulitoa taarifa yetu kwa umma wa Watanzania Aprili 20 mwaka huu, kuunga mkono hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) katika kupigania maoni yanayowakilisha matakwa na maslahi ya Watanzania kwenye Rasimu ya Pili ya Katiba Mpya, ambapo tuliwataka wananchi;
- Kuungana na makundi mbalimbali katika jamii, taasisi, asasi za kiraia na watu wengine mashuhuri ambao wameamua kujitoa hadharani kusimamia maoni ya wananchi kama yalivyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya kwenye Rasimu ya Pili, kama inavyoelezwa katika katiba ya sasa, ibara ya 8 inayosema mamlaka ya kuongoza nchi yote yatatoka kwa umma/wananchi.
- Kutumia nguvu zote zilizojaa ushawishi wa hoja na mbinu halali dhidi ya njama za aina yoyote zinazofanywa kupindua na kuchakachua maoni.
- Hakuna kikundi chochote kinaweza kujitwalia mamlaka ya kwenda kinyume au kupindua maoni ya wananchi kwenye Rasimu ya Katiba Mpya, ambao ndiyo wenye hati miliki na nchi yao.
- Wananchi wa Tanzania ambao waliona mchakato wa kuandika Katiba Mpya ni fursa ya kipekee ‘kujizaa’ upya kama taifa, kwa kurekebisha na kuboresha utaifa wao kupitia mkataba halali wa ‘katiba’, wanafuatilia kwa makini mno namna ambavyo watawala wanataka kupoka na kubaka demokrasia kwenye jambo nyeti kama hili kwa manufaa ya CCM.
- BAVICHA kwa kushirikiana na vijana wengine wenye machungu na TANZANIA, tutashawishi, kuratibu na kusimamia hoja za msingi katika kuhakikisha kizazi cha sasa na vingine vijavyo, vinanufaika na matunda yatakayo andaliwa leo.
- Hatutakubali kuona Katiba Mpya inapatikana kwa ghiliba, hila na vitisho vya watawala badala ya makubaliano na maridhiano yenye nia na dhamira safi, yakiweka mbele maslahi na matakwa ya Watanzania bila kujali tofauti yoyote ile kama dini, kabila wala rangi.
Tunapenda kusema hivyo kwa sababu zimeanza kuonekana dalili za njama za wazi kabisa zinazofanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia njia mbalimbali kutaka kutengeneza hali ya taharuki na kuwatisha wananchi wasijenge hoja za kudai maoni yao yaheshimiwe kwenye kuandika Katiba Mpya ya Tanzania.
Njama hizo za kujenga hali ya hofu na kuibua sintofahamu ambazo zimekuwa zikizungumzwa na viongozi waandamizi wa chama hicho, zimeendelea kudhihirika tena baada ya chama hicho, kupitia kwa kada wake. Paul Makonda, kutoa tamko la kuhamasisha vurugu na ‘kuanzisha’ vita, kwa nia ya kuwatisha wananchi washindwe kudai katiba yao inayotaka kupokwa na CCM.
Kada huyo ambaye anajulikana ndani na nje ya chama chake kwa namna alivyo mahiri wa kutumika kwa ajili ya maslahi binafsi ya watu au wakati mwingine hata dhidi ya chama chake, kwa ajili tu ya kutetea tumbo lake, amenukuliwa leo kwenye vyombo mbalimbali vya habari, akitoa maneno ambayo kwa hakika yamezidi kuwachochea wananchi kujua kuwa CCM si chama cha siasa tena, bali genge la wabaka demokrasia.
Kupitia vyombo mbalimbali vya habari, Makonda amenukuliwa akitoa maagizo kwa vyombo vya dola na vijana wanaounda jeshi haramu la CCM (Intarahamwe), linalojulikana kwa jina la Green Guard kuanza kufanya mashambulizi dhidi ya viongozi wa UKAWA kwa sababu tu wameipiku CCM na mawakala wake, katika kujenga ushawishi kwa wananchi unaotokana na hoja zenye ushahidi wa takwimu za kitafiti na mtiririko wa mantiki katika kutetea maoni ya wananchi kwenye rasimu ya katiba.
Kauli hiyo ya Makonda ya kuwaagiza vijana wa Green Guard wajipange kufanya mashambulizi bila shaka kwa nia ya kuteka, kujeruhi, kutesa na hata kuua, ambayo imepata baraka za viongozi wakuu wa chama chake (ref. Gazeti la Mwananchi, Jumanne, Aprili 22, 2016, Toleo Na. 5022, uk. 3, aya ya 9), imedhihirisha mambo mengi ambayo BAVICHA tumekuwa tukisema kuwa CCM kinahusika;
Wamedhihirisha tuliyoyasema- Interahamwe;
Interahamwe ni kikundi cha kijeshi kilichokuwa kinatumiwa na watawala kupambana kwa nguvu na kukandamiza demokrasia na wapinzani wa kisiasa wa serikali nchini Rwanda hadi kusababisha mauaji ya kimbari nchini humo. CCM nao wanapitia katika hali hiyo hiyo ya kulazimika kutumia vikundi haramu vya kijeshi ambavyo vinalindwa na dola, kushambulia watu wanaosimamia maslahi na matakwa ya wananchi.
Kauli ya Makonda ambayo Jeshi la Polisi nchini kupitia kwa msemaji wake, Advera Senzo limesema eti halina taarifa nayo, imedhihirisha kwa ushahidi kuwa kikundi cha ulinzi cha Green Guard huwa kinatumika kushambulia, kupiga watu, kuteka, kutesa na hata kuua kama ambavyo kimefanya mara kadhaa hususan wakati wa chaguzi ndogo.
Pia kauli hiyo imedhihirisha kile ambacho wananchi wamekuwa wakihoji kulikoni ukimya wa serikali na vyombo vyake katika matukio mbalimbali ya utesaji, utekaji nyara kwa nia ya kuua, ambavyo watu mbalimbali ndani ya jamii wamekuwa wakifanyiwa hususan wanapokuwa na mtizamo au maoni tofauti na watawala.
Upo ushahidi wa wazi, ukiwemo wa viapo, kuwa Green Guard ambao CCM wamewaagiza kushambulia viongozi wa UKAWA wamekuwa wakihusika katika matukio ya njama za kutesa, kuteka na kuua watu, kwa kutumia njia mbalimbali, ikiwemo silaha na sumu, suala ambalo mara kadhaa chama hicho kimekuwa kikikanusha, lakini hatimaye kimedhihirisha.
Na kauli hiyo ya CCM ya kuagiza Green Guard kushambulia watu, ikithibitishwa zaidi na matendo ya kikundi hicho, imesaidia kufafanua kauli iliyotolewa bungeni na mjumbe wa UKAWA, Prof. Ibrahim Lipumba, kuwa chama hicho kimegeuka kuwa Intarahamwe.
Makonda ni mtu wa aina gani
Kama kauli ya Makonda isingekuwa na baraka za CCM na watawala, tungewaomba Watanzania wampuuze kwa upuuzi wake unaomthibitisha kuwa yeye ni mpuuzi.
Anajulikana kwa umahiri wake wa kutanguliza tumbo lake na kulinda maslahi ya wakubwa wanaomtumia kwenye makundi ya ndani ya CCM. Akiwa chuoni Moshi pia mara kadhaa ametumika na watu wan je ya chama hicho ili akihujumu chama chake, CCM.
Itakumbukwa kwamba wakati wa uchaguzi mkuu wa chama hicho mwaka jana, alikuwa Makonda huyu huyu ambaye aliandika mambo mengi akionesha namna ambavyo chama hicho kinanuka kwa rushwa na kimekubuhu kwa ubakaji wa demokrasia.
Lakini kwa sababu siku zote amekuwa akitanguliza tumbo lake mbele kabla ya kitu kingine na wenzake wanamjua, hao hao aliowaita wala rushwa na wabaka demokrasia, wakampachika cheo hicho alichonacho sasa ndani ya UVCCM ambacho kimemfanya ale matapishi yake, sasa eti anawaita ni wazalendo, badala ya genge la wahuni kama alivyoonesha yeye mwenyewe.
Itakumbukwa pia, kwamba ni kijana huyu huyu akiwa pamoja na viongozi wengine waandamizi wa CCM, akiwemo Samuel Sitta, Harrison Mwakyembe, Nape Nnauye na wengine, waliwahi kuunda chama cha CCJ, wakisema CCM ni chama kinachokufa na hawawezi tena kuwa wanachama wa chama kisichosimamia misingi yake.
Tunaweza kusema mambo mengi kwa namna tunavyomjua kijana huyu, lakini itoshe kusema kuwa tangu tulipomtangaza Nape Nnauye kuwa ni Vuvuzela namba moja ndani ya CCM, hatukuwahi kujua kuwa mwingine anayemfuatia kwa ukaribu ni Paul Makonda.
Tunahitimisha kwa kutoa angalizo na onyo kwa vijana CCM wasidiriki kutekeleza hayo maagizo ya kuwashambulia viongozi wa UKAWA, tuko tayari kusimama na kuwalinda viongozi wetu.
Imetolewa leo Aprili 22, 2014, Dar es salaam na
Daniel Naftal
Afisa Utawala na Fedha
Baraza la Vijana CHADEMA (BAVICHA)