Monday, March 31, 2014

Zitto Kabwe:India after Gandhi na India since independence

 
Kama kuna Nchi ya kujifunza kuhusu kuandika Katiba na kuelewa mchakato mzima ni India. “ikiwa na Ibara 395 na Nyongeza 12 Katiba ya India inaweza kuwa ndio Katiba ndefu kuliko zote duniani” anaandika bwana Guha katika Kitabu cha ‘India after Ghandhi’.
“ilikuwa ni saa tano kamili asubuhi tarehe 9 Desemba mwaka 1946, Bunge Maalumu la Katiba la India lilianza mkutano wake wa kwanza. Kwa namna yeyote ile suala la Uhuru wa India sasa lilikuwa ni suala la tarehe tu na sio suala la mjadala tena” wanaandika mabwana Chandra, Mukherjee M na Mukerjee A katika Kitabu cha ‘India since Independence’. Hivi ni vitabu viwili ambavyo wanasiasa na wachunguzi wa mambo wa Tanzania wanapaswa kuvisoma ili kurutubisha mchakato wa kuandika Katiba ya Tanzania. Mambo mengi yanayojadiliwa sasa wenzetu wameyapitia na kama wazungu wapendavyo kusema “dont reinvent the wheel’ tunaweza kujifunza na kuweka mafunzo hayo katika mazingira yetu na kupata Katiba bora. Mambo ya Katiba utayakuta sura ya 6 ya ‘India after Gandhi’ na sura ya 4 ya ‘India since Independence’.
Ilichukua miaka mitatu kuandika Katiba ya India katika ngazi ya Bunge la Katiba, mikutano kumi na moja ya Bunge hilo na jumla ya siku zilizotumika ni Mia moja Sitini na Tano. Sehemu kubwa sana ya kazi ya uandishi ilifanywa na Kamati mbalimbali na kukusanywa na Kamati ya Uandishi iliyokuwa chini ya Mwanasheria maarufu kutoka daraja la chini (untouchables) bwana B. M. Ambedkar. Mengi yanayoonekana kusumbua mchakato wa Tanzania yaliisumbua sana India. Mengine ambayo Tanzania hayana shida nayo kama suala la lugha, yaliisumbua India. Lugha gani itumike kuzungumza ndani ya Bunge maalumu na Katiba iandikwe jwa lugha gani ilizua mjadala kuliko jambo lingine lolote. “Tarehe 10 Disemba 1946 wakati kanuni za Bunge zinaandaliwa bwana R V Dhulekar kutoka United Provinces alileta marekebisho ya kanuni na kuanza kuongea lugha ya Hindustani ambapo Mwenyekiti alimsimamisha ili aongee Kiingereza. Yeye akajibu “ Wasiojua Hindustani hawana haki ya kuwepo India” ameandika bwana Guha. Ilimchukua Jawaharlal Nehru kusimama ndipo mjumbe huyo akakubali kukaa chini baada ya kuanza kufoka kwa sauti kubwa kusisitiza kwamba lugha ya Hindustani ndio inapaswa kuzungumzwa nchini India.
Wale wanaodhani migomo ni tatizo wakisoma vitabu hivi wataona namna Chama cha Muslims League kilivyoamua kususia Bunge Maalumu la Katiba wakitaka India igawanywe kuwa Nchi mbili huru, moja ya Waislamu na nyingine ya Wahindu. “mkutano wa kwanza ulipoanza chama cha Muslims League kiligomea kushiriki na tarehe 13 Disemba Nehru alitoa hoja ya ‘Madhumuni na Sababu’ ambayo iliahirishwa ili kusubiri Muslims League washiriki, hawakushiriki. Ilipofika Mkutano wa tatu tayari mpango wa Waingereza kuigawa India kuwa Nchi ya India na Nchi ya Pakistani ukawa umetimia na hapakuwa na shida tena ya kuwasubiri Muslims League” anaandika Chandra na wenzake.
Ingawaje hatufanani sana, na mpaka sasa hakuna chama kilichogomea mchakato wa kuandika Katiba ya Tanzania, mazingira ya India na Pakistani na baadaye Bangladeshi (awali Bangladesh ilikuwa sehemu ya Pakistan ikiitwa East Pakistani mpaka mwaka 1975 ilipopigana vita kutaka kuwa Nchi huru) yanaweza kutokea Tanganyika na Zanzibar (Unguja na Pemba). Historia huwa ina tabia ya kujirudia.
Mjadala mkubwa Tanzania ni muundo wa Muungano ambapo baadhi wanataka Serikali mbili (ya Muungano na ya Zanzibar), wengine Serikali tatu (ya Muungano, Tanganyika na Zanzibar) na hata wengine ndani ya hizo Serikali tatu wakitaka Serikali ya Muungano kuwa na nguvu sana kuliko zile za Washirika. Mchakato wa kuandika Katiba ya India nao ulikuwa na mjadala mkali sana kuhusu Shirikisho au Serikali Kuu imara (Federal or Unitary). “Katiba ya India imegawanya mamlaka katika sehemu tatu: Mambo ya Muungano, mambo ya Washirika (states) na mambo ya pamoja (concurrent)…… hata hivyo wajumbe wenye kutaka mamlaka zaidi kwa washirika walikuja juu kupinga kiasi cha mjumbe mmoja kusema ‘washirika watakuwa ombaomba kwa Serikali Kuu’. Mjumbe mwingine alijibu wenzake ‘Mamlaka makubwa yataifanya Serikali ya Muungano kuwa imara na kuweza kupanga na kusimamia maendeleo ya Nchi nzima’. Ambedkar akasema ‘tunataka Serikali imara ya Muungano’ na mwingine akasema ‘Shirikisho lenye Serikali ya Muungano yenye nguvu iwezekanavyo’” ameandika Guha. Chandra na wenzake wamemnukuu Ambedkar akisema “Muungano wa Washirika unatakiwa zaidi kuliko Shirikisho la Washirika”. India leo ni ‘Unitary’ lakini Majimbo yake (States) zina uhuru mkubwa wa kuamua mambo yao. Tanzania inaweza kuwa na Muungano wa Serikali Tatu bila ya kuwa Shirikisho na Serikali za Washirika zikawa na madaraka ya kutosha kuendesha mambo yao ilhali Serikali ya Muungano ina Mamlaka kamili ya kuendesha Nchi.
Jambo moja kubwa tunajifunza kutoka mchakato wa kuandika Katiba ya India kutokana na vitabu hivi viwili ni namna ambavyo mwafaka ulikuwa unajengwa ili kutimiza malengo. Mchakato ulifanyika kukiwa na chama kimoja chenye nguvu, chama cha Congress, kiasi cha wapinzani kuona labda Congress watahodhi Katiba. Hata hivyo walihakikisha kila wakati kuna maridhiano au mwafaka kati ya wengi na wachache.
Nehru, Kiongozi wa Congress hakuwa mwongeaji sana isipokuwa tu pale ilipohitajika na kwa hotuba za masuala maalumu. Kulikuwa na Rajendra Prasad aliyefanya kazi ya ziada kuendesha mikutano na vikao vyote vya Bunge Maalumu. “Wahindi wanajulikana kwa kuongea zaidi kuliko kusikiliza” bwana Guha anaandika “Prasad alihakikisha vikao havisimami na kutoa haki ya kila mtu kuongea”. Kulikuwa na B R Ambedkar ambaye alikuwa mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi na alihakikisha mawazo na dhana ngumu zinawekwa katika lugha inayoeleweka katika Katiba. Nadhani mtu muhimu kuliko wote, kwa maoni yangu, alikuwa Bwana Vallabhbhai Patel ‘alifanya kazi kubwa ya kutayarisha rasimu za awali, alihakikisha anajenga maridhiano miongoni mwa wajumbe walikuwa wanapingana vikali kwa hoja. Kuna wakati alikuwa anawachukua wajumbe wakorofi kwa matembezi ya asubuhi na hata kunywa nao chai ili kuleta mwafaka’. Katiba ni Mwafaka wa Taifa, Ni Nani Vallabhbbhai Patel katika Bunge Maalumu la Katiba Tanzania?
RaiaTanzania, March 31, 2014