Kwa Waziri wa Mikiki na Makeke,
Uzitoni Street,
Bongo.
Mpenzi wangu,Uzitoni Street,
Bongo.
VIBAYA hivyo! Yaani wewe unaweza kukaa kimya hata mwezi bila maelezo, lakini mimi nikikosekana wiki moja tayari umeshaanza kunituhumu. Jamani.
Ama kweli kuna sheria moja kwa wanaume na sheria nyingine kwa wanawake. Uwe na subira kidogo mpenzi wangu kadhaa!
Ilikuwa hivi. MB aliamka ghafla siku moja na kuamua kwenda kijijni kumwona mama yake. Bosi bado yuko kwenye kikao dafrao huko ambako hakuna lolote zaidi ya kutafuna posho ya mipasho na BB siku hizi anaweza kukaa peke yake.
Hivyo wakati namletea supu asubuhi hata kabla hajavaa uso wake (maana Bosi asipokuwapo anaweza kuja mezani na uso uchi kabisa tehe tehe tehe. Unahesabu kila mstari! Nadhani ingekuwa Uganda wangepitisha sheria kwamba hakuna ruhusa kwenda barabarani na uso uchi maana unatisha!) ameshaanza kusema.
‘Nilimwota mama yangu usiku Hidaya. Ni vizuri kwenda kujua hali.’
Basi wakati anajipara vilivyo na kuvaa poda zake zote, mimi kazi yangu ilikuwa ni kujaza magunia ya sukari na mchele ndani ya gari, kisha safari moja kwa moja. Sikupata hata nafasi ya kuandika neno mpenzi. Na tumekaa huko karibu wiki nzima, MB akijitahidi kumaliza chakula chote alichompelekea mama yake.
Si unajua mpenzi. Mnene yuko kijijini. Mpishi wake anaye, basi watu wote walitumia hiyo nafasi ya kuja kumsalimia mke wa Bosi hasa wakati wa msosi. Na MB hakuweza kukataa ingawa najua alilalamika kichinichini, na hasa tukiwa njiani kurudi.
‘Watu wa kijijini Hidaya, hawana adabu. Wanaona kazi yetu ni kuchota pesa tu hapa mjini.’
Nilitaka kumwuliza kwani Bosi anafaya nini huko makao makuu kama si kuchota pesa tu, lakini nilijua mlipuko ungeweza kusababisha ajali. MB ni mtu tofauti sana akiwa peke yake. Bosi akiwapo utadhani mto tulivu kabisa lakini wakati Bosi hayupo hata yeye ni volkano pia.
Sasa kurudi nyumbani tukamkuta BB yuko pale na mtoto wa jirani.’
‘Kuna nini hapaMbona hayuko shuleni’
‘Ngoja mama nitakueleza.’
Hata mimi nilishangaa mpenzi maana nilijua huyu binti, pamoja na udogo wake, nadhani ana miaka 8 hivi, anasoma shule ya bweni ya wanene ya bei mbaya. ‘
‘ Imekuwaje hadi aje kwetu, tena katikati ya muhula.’
BB alifanikiwa kumbembeleza yule mtoto kisha akamgeukia mama.
‘Naomba uvumilie kidogo mama.’
‘Nivumilie niniKwa nini yupo hapa’
‘Ana matatizo mama’
‘Matatizo ganiMatatizo na wazazi’
‘Hapana mama. Ni …’
‘Basi umpeleke nyumbani. Waza …’
Ghafla yule msichana akaangua kilio hadi sote tukashtuka. BB alimbembeleza huku akimkazia mama macho.
‘Tulia, tulia. Tutakusaidia usiwe na wasiwasi.’
Kisha akamgeukia mama yake.
‘Sasa mama utanisikiliza au hautanisikiliza’
Mama akaamua kukaa.
‘Huyu ametoroka shule …’
‘Hee. We mtoto!’
Msichana alitaka kuangua kilio tena lakini BB akasema kwa sauti.
‘Mama naomba unisikilize kwanza. Kisha utasema upendavyo. Huyu ametoroka shule baada ya kupigwa sana.’
‘Shule ile. Haiwe …’
‘Mama! Tena shule hizo nyingi zinapiga sana. Unajua kwamba yule mtoto wa jirani yetu mwingine anaingia chini ya kitanda kila mwalimu akija kumpa tuition, maana anajua na kipigo mtindo mmoja’
‘Nidhamu ni muhimu!’
‘Nidhamu ya woga si nidhamu, hata kama wanakuja kufaulu mitihani. Unajua wameathirika kiasi gani kisaikolojia.’
‘Kwani tuko bungeni hapa. Hebu toa maelezo.’
‘Basi wikiendi iliyopita, ilikuwa siku ya wazazi kuwatembelea. Wakati wanataka kuondoka, Sofia alilia sana maana hapendi anavyotishwa na kupigwa pale na alikuwa na hamu ya nyumbani. Sasa wakati analia akapita mwalimu mmoja. Badala ya kuonyesha ubaba, alipenda zaidi ubabe … we mtoto nyamaza ama sivyo nitakupiga kesho! … mwisho ikabidi mama aondoke na mwalimu kweli alitimiza azma yake kesho yake mpaka Sofia aliamua kukimbia. Kapanda basi na kafikia hapa.’
Mama alijaribu kujilainisha kidogo.
‘Pole sana, Sofia, sasa kwa nini usiende nyumbani.’
‘Baba atanipiga.’
‘Hawezi kukupiga.;
‘Atanipiga mama. Nikimwambia kuhusu shule anasema ni lazima nijifunze nidhamu. Kazi yangu ni kuchezacheza tu. Lakini nasoma kwa nguvu zote mama.’
‘Najua, najua mwanangu, lakini lazima uende nyumbani. Ngoja sisi tukisindikize. Tutamwelezea baba yako.’
Basi baada ya kubembeleza mara kibao na kuahidi kwenda na BB pia, Sofia alikubali. Walikaa huko muda mrefu. Baadaye BB aliniambia kwamba baba kweli alikuja juu na alitaka kumchapa mwanaye lakini BB alisimama katikati.’
‘Mimi nampeleka kwenye shule ambayo iko ndani ya kumi bora ya taifa kisha anatoroka. Ngoja nimfunze adabu.’
‘Lakini baba huoni kwamba ametoroka kwa sababu mwalimu amempa adhabu bila adabu’
‘We mtoto huna adabu na wewe. Hebu nipishe.’
Lakini, kwa mujibu wa BB, hata MB aliingilia kati.
‘Chonde, chonde baba, huoni mtoto anavyotetemeka. Na ameumia. Kweli ni kazi ya shule kuwaumiza watoto wetu.’
‘Wajue maisha ni magumu. Hakuna huruma.’
Basi baada ya mabishano mengi sana, hatimaye baba alitulia kidogo na mama alimkumbatia mwanaye hivyo MB na mwanaye waliweza kurudi. Lakini BB alikuwa bado kavaa sura ya hasira kabisa.
‘Unaona mamaHata mimi niko katika shule kumi bora lakini hatuchapwi. Angalia Sofia, alikuwa mcheshi, mchangamfu, mtundu, alifurahia shule, na masomo, na maisha, sasa hana hamu kabisa. Elimu bora ni ile inayobomoa ucheshi na ubunifuBasi sote tupelekwe jeshi tu.’
MB akacheka.
‘Ndiyo maana ya JKT mwanangu.’
‘Ohoo usinikumbushe hilo mama. Lazima niongee na baba. Wizara ya Mashule inashikia bango kila kipengele cha sheria kwa ajili ya shule binafsi, kwa nini haikagui hiyo piaKupiga hivyo ni mwiko kulingana na sheria ya elimu. Kwanza mwalimu wa kiume haruhusiwi kumchapa mtoto wa kike, pili lazima asaini kitabu na mambo mengine chungu mbovu. Wakague shule na kuhakikisha sheria zinafuatwa.’
‘Mbona hazifuatwi katika shule za serikali.’
‘Mmmh! Hakuna sheria yoyote inayofuatwa katika shule za serikali. Zimekuwa yatima tu, huku serikali ikikumbatia shule nyingine. Sasa ihakikishe kwamba sheria hizi zinafuatwa.’
‘Lakini unajua wazazi wengi wanapenda watoto wao wachapwe. Tazama yule baba.’
BB akatingisha kichwa.
‘Ni kweli mama, nawashangaa. Wanataka watoto wao watoke shule kama misukuleWote ni wasomi hawasomi mambo ya ukuaji wa mtotoHawaoni watoto wao wanvyobadilikaAu kwa kuwa walichapwa sana walipokuwa shuleni wanataka kulipiza kisasi kwa watoto wao.’
MB akacheka.
‘We mwanangu kweli unastahili kuchapwa na wewe. Unatuchamba na kutuchambua wazee namna hii’
BB alitabasamu.
‘Kwa hiyo unataka niwe msukule na mimi’
Basi mjadala uliahirishwa hadi kurudi kwa mbangi wa katiba. Lakini hata mimi nashangaa mpenzi. Sidhani kama wale wanafaulu kwa sababu ya kuchapwa. Wana vitabu nyumbani, wanatembea na kuona mengi, wanaweza kuingia intaneti na kuwasiliana na watu na kujifunza mengi, wanakutana na Kiingereza kila mahali. Si kwa sababu ya kupigwa. Hebu fikiria mtoto anaingia uvunguni kwa woga wa mwalimu wake. Hatari kabisa.
Akupendaye daima … ila uthubutu kunipiga tehe tehe tehe,
Hidaya
raia mwema