Monday, March 17, 2014

UHAMIAJI UNATAKIWA KUFIKIRI ZIADI




MWENYEZI Mungu, mwingi wa rehema ni wa kushukuriwa sana kwa kila jambo tunalolitenda hapa duniani. Kwa mara nyingine ameendelea kutenda miaujiza yake na leo hii tunakutana tena kwenye safu yetu maridhawa.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, yalitokea mambo mengi, yakiwemo uchaguzi wa Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, kitu ambacho sasa kimefungua rasmi shughuli za chombo hicho kitakachofanya kazi kwa muda wa siku 70 ili kutuletea Katiba Mpya ya Tanzania.
Kama nilivyosema, pamoja na kutokea kwa habari nyingi, lakini iliyonivutia zaidi, ilikuwa ni ile ya Idara ya Uhamiaji nchini, kutangaza ongezeko la bei kwa wahitaji wapya wa hati za kusafiria na wale waliopoteza, ikiwa ni mojawapo ya mikakati yake kuhakikisha inadhibiti upotevu na matumizi mabaya ya pasipoti zetu.
Msemaji Mkuu wa Idara hiyo, Abbas Irovya aliwaambia waandishi wa habari kuwa wamebaini upotevu wa kutisha wa hati za kusafiria, kwani  jumla ya hati za kusafiria 1932 ziliripotiwa kupotea katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2010 hadi mwaka jana.
Irovya anawatuhumu baadhi ya Watanzania wasio waaminifu kuwa wanauza pasipoti hizo kwa watu wa mataifa mengine, ambao wanazitumia kwa malengo yasiyo mazuri, yakiwemo ya kihalifu.
Kama mojawapo ya njia za kudhibiti hali hiyo, kuanzia sasa, watu watakaohitaji pasipoti mpya, watatakiwa kulipa kiasi cha shilingi laki moja (100,000) na wale waliopoteza, nao watalazimika kujikamua kiasi cha shilingi laki mbili (200,000) ili waweze kuipata upya.
Napenda kuwapa pongezi zangu nyingi Uhamiaji kwa kufikiri juu ya kudhibiti jambo hili, ambalo kwa kweli limekuwa likitoa taswira mbaya ya nchi yetu, hasa kwa kuwa nyingi ya pasipoti zinazopotea, hufikia katika mikono ya wahalifu, ambao hutekeleza vitendo vyao na kuonekana kuwa vimefanywa na Watanzania.
Ingawa ni kweli pia kama walivyosema Uhamiaji, kwamba baadhi ya Watanzania wenzetu huziuza hati hizi kwa watu wenye nia ovu.
Lakini hata hivyo, juhudi hizi naziona kama zina mushkeli, kwa sababu chanzo kikubwa cha upotevu wa hati za kusafiria, ni idara yenyewe, hivyo mtu wa kwanza kuangaliwa na kuwekewa mikakati, ni wafanyakazi wa idara hii.
Ingawa ni vigumu kuwa na ushahidi wa kuthibitisha hili kwa asilimia mia moja, lakini ule wa mazingira unaonyesha kuwa baadhi ya wafanyakazi, hasa wanaojihusisha na utoaji wa hati, ndiyo wamekuwa chimbuko la uuzwaji na upotevu wa hati hizi za kusafiria.
Pamoja na ukweli kwamba hati hizi zinaweza kughushiwa, lakini baadhi ya watumishi wamekuwa wasuka mipango wakubwa wa kuzitoa kwa watu wasio Watanzania, tena kwa kuwaelekeza na kuwajazia baadhi ya vitu muhimu.
Badala ya Uhamiaji kuongeza bei ya kupata hati, ingeanza kwanza na mambo yaliyo ndani yake, ikiwa ni pamoja na ubora wa pasipoti hizo ili kuzuia watu kuweza kuzidurufu. Lakini pia suala la kuziondoa kwenye mzunguko hati hizo kila zinaporipotiwa kupotea, kwani hilo litasababisha wanaozitumia kukamatwa wanapokutwanazo.
Lakini kuongeza bei ya pasipoti ni kutowatendea haki wananchi, kwani kuwa nazo ni haki yao ya msingi. Baadhi ya watu wanahitaji pasi hizo kutokana na kutakiwa kwenda nje ya nchi kwa matatizo ya kiafya au shida zingine maalum, hivyo kumfanya atoe fedha zaidi ni kumpa adhabu kwa kosa ambalo siyo lake.
Wanaopoteza hati hizi makusudi au wanaozihitaji kwa malengo mengine wadhibitiwe, fedha zilizoongezeka ni kichekesho. Hizi siyo hela kwa watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya, magaidi au wahalifu wa aina yoyote, sana watakaoumia ni raia walalahoi.
Ongezeko hili la bei hakika linawaumiza watu ambao hawahusiki na mbaya zaidi, ni kauli kwamba waombaji watatakiwa kusubiri miezi sita kabla ya kupata hati hizo, je hiyo ni haki? Nimalizie kwa kusisitiza kuwa Idara ya Uhamiaji ijiangalie yenyewe kwanza kabla ya kutoa adhabu kwa wasiostahili lakini Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe afikirie upya uamuzi huu unaoumiza watu wengi bila sababu ya msingi na asingoje kelele za Watanzania.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.