Friday, March 28, 2014

Ripoti ya CAG yamshtua JK! Aagiza mali zote za Serikali kurasimishwa mara moja...

 Rais aamuru mali zote za Serikali kurasimishwa- Nia ni kuwa na rekodi ya mali za Serikali na kuzuia uporaji wake

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameagiza mali zote za Serikali, zikiwemo Nyumba, kurasimishwa kwenye miliki ya Serikali kwa kutafutiwa na kupatiwa hati na nyaraka nyingine muhimu.

Rais Kikwete ametoa agizo hilo ili kuwa na rekodi sahihi ya mali za Serikali na kuzuia baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu kupora na kuchukua mali hizo, zikiwamo Nyumba, kwa sababu hazijarasimishwa na kupatiwa hati na nyaraka muhimu za kuthibitisha kuwa ni mali ya Serikali.

Rais Kikwete ambaye ametaka zoezi hilo lianze mara moja na lifanyike na kukamilishwa haraka iwezekanavyo ametoa agizo hilo leo, Ijumaa, Machi 28, 2014, wakati anazungumza na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Bwana Ludovick Utouh, baada ya kuwasilisha kwa Rais Kikwete ripoti ya hesabu za Serikali kwa Mwaka wa fedha unaoishia Juni 30,Mwaka jana, 2013, katika hafla iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam.

Rais Kikwete ametoa agizo hilo baada ya kuelezwa na Bwana Utouh kuhusu changamoto mbali mbali ambazo wataalam wa ofisi yake wamekumbana nazo katika kufanya ukaguzi wa Hesabu za Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Mashirika ya Umma na Miradi mbali mbali nchini.

Kwa jadi, tokea enzi za ukoloni, mali za Serikali hazina hati wala nyaraka rasmi za kuthibitisha umiliki wa Serikali, hali ambayo katika miaka ya karibuni imetoa mwanya kwa watu wasiokuwa waaminifu kuvamia, kudai na hata kupora mali za Serikali wakidai kuwa ni mali zao.

Katika tukio jingine lililofanyika Ikulu, Rais Kikwete amekula chakula cha mchana na wajumbe wa Umoja wa Vyama vya Kisoshalisti Duniani wa Socialiast International kwa nchi za Afrika. Wajumbe hao kutoka nchi 24 wanafanya mkutano wao wa Mwaka wa siku mbili Dar es Salaam.

Mkutano huo wa siku mbili ulioanza leo Ijumaa, unafanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere.


Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
28 Machi, 2014